Sri Lanka: Waandamanaji ‘’watakaa ikulu mpaka viongozi waondoke’’

Waandamanaji walivamia nyumba ya rais wa Sri Lanka huko Colombo na kuchoma moto nyumba ya Waziri Mkuu
Maelezo ya picha, Waandamanaji walivamia nyumba ya rais wa Sri Lanka huko Colombo na kuchoma moto nyumba ya Waziri Mkuu

Waandamanaji wamesema wataendelea kukalia makazi ya rais na mawaziri wakuu wa Sri Lanka mpaka viongozi wote wawili watakapojiuzulu rasmi.

Rais Gotabaya Rajapaksa alisema atajiuzulu tarehe 13 Julai, kulingana na tangazo lililotolewa na spika wa bunge siku ya Jumamosi.

Lakini rais mwenyewe hajaonekana au kutoa taarifa kwa umma.

Vyanzo vya kijeshi vimeiambia BBC kwamba kwa sasa yuko kwenye meli ya Wanamaji katika maji ya Sri Lanka.

Kaka yake, Waziri Mkuu wa zamani Mahinda Rajapaksa, yuko kwenye kambi ya wanamaji nchini humo, duru zinasema.

Maelfu walifika Colombo Jumamosi wakimtaka ajiuzulu baada ya miezi kadhaa ya maandamano.

Rais amelaumiwa kwa usimamizi mbaya wa uchumi wa nchi, ambao umesababisha uhaba wa chakula, mafuta na dawa kwa miezi kadhaa.

Waziri Mkuu wa sasa Ranil Wickremesinghe pia alisema atajiuzulu kufuatia maandamano ya Jumamosi, ambapo makazi yake ya binafsi yalichomwa moto.

Lakini waandamanaji wanasalia na mashaka kuhusu nia ya viongozi hao.

Waandamanaji wengi walishangazwa na fahari ya jumba hilo

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Waandamanaji wengi walishangazwa na fahari ya jumba hilo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Waandamanaji wengi walishangazwa na fahari ya ikulu "Mapambano yetu hayajaisha," kiongozi wa maandamano ya wanafunzi Lahiru Weerasekara alisema, akinukuliwa na AFP.

"Hatutaacha mapambano haya hadi [Rais Rajapaksa] aondoke," alisema.

"Siku chache zijazo zitakuwa nyakati za mashaka sana kuona kitakachotokea kisiasa," mchambuzi wa masuala ya kisiasa na wakili wa haki za binadamu Bhavani Fonseka aliiambia Reuters, akiongeza kuwa itakuwa ya kuvutia kuona kama viongozi hao "wanajiuzulu".

Viongozi wa kisiasa walifanya mikutano zaidi kujadili ubadilishanaji wa madaraka siku ya Jumapili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, alisema kuwa serikali yoyote mpya inahitaji kuzingatia mara moja utulivu wa muda mrefu wa kiuchumi.

Spika wa bunge la Sri Lanka aliambia kipindi cha BBC World Service Newshour kwamba serikali mpya ya mseto lazima iundwe ndani ya wiki moja baada ya rais kujiuzulu rasmi.

Mahinda Yapa Abeywardena, ambaye ni mwanachama wa chama tawala cha rais, alilaumu zaidi Covid-19 kwa shida za kiuchumi zinazokumba nchi.

"Janga la Covid limesababisha uharibifu nchini kiuchumi kwa hivyo tulilazimika kutumia pesa zetu zote kwa chanjo," alisema.

Sri Lanka: Ya Misingi

  • Sri Lanka ni taifa la kisiwa kutoka kusini mwa India: Ilipata uhuru kutoka kwa utawala wa Uingereza mwaka 1948. Wasinhala, Watamil na Waislam – ambao wanachangia 99% ya wakazi milioni 22 wa nchi hiyo.
  • Kina kaka wa familia moja imetawala nchi hiyo kwa miaka mingi: Mahinda Rajapaksa alikua shujaa kati ya Wasinhali walio wengi mwaka wa 2009 wakati serikali yake ilipowashinda waasi wanaotaka kujitenga wa Kitamil baada ya miaka mingi ya vita vikali na vya umwagaji damu vya wenyewe kwa wenyewe.
  • Kaka yake Gotabaya, ambaye alikuwa waziri wa ulinzi wakati huo, ndiye rais wa sasa lakini anasema anajiuzulu.
  • Sasa msukosuko wa kiuchumi umesababisha ghadhabu mitaani: Kupanda kwa mfumuko wa bei kumesababisha baadhi ya vyakula, dawa na mafuta kukosekana, kuna uhaba wa umeme na watu wa kawaida wameingia mitaani kwa hasira huku wengi wakilaumu familia ya Rajapaksa na serikali yao kwa hali hiyo.

Makumi ya watu walijeruhiwa katika maandamano ya Jumamosi.

Msemaji wa hospitali kuu ya Colombo aliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumamosi kwamba watu watatu wametibiwa majeraha ya risasi.

Waandamanaji waliingia ndani ya ikulu huku wakiimba nyimbo na kupeperusha bendera ya taifa siku ya Jumamosi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Waandamanaji waliingia ndani ya ikulu huku wakiimba nyimbo na kupeperusha bendera ya taifa siku ya Jumamosi

Matukio ya ajabu ya Jumamosi yalionekana kuwa kilele cha miezi mingi ya maandamano ya amani nchini Sri Lanka.

Umati mkubwa wa watu ulikusanyika kwenye makazi rasmi ya Rais Rajapaksa, wakiimba kauli mbiu na kupeperusha bendera ya taifa kabla ya kuvunja vizuizi na kuingia ndani ya ikulu.

Video za mtandaoni zilionesha watu wakirandaranda ndani ya nyumba hiyo na kuogelea kwenye kidimbwi cha rais, huku wengine wakimwaga vilivyokuwemo kwenye droo ya kuhifadhi vitu, kuokota vitu vya rais na kutumia bafu lake la kifahari.

Tofauti kati ya anasa ya jumba hilo na miezi ya taabu iliyovumiliwa na watu milioni 22 wa nchi hiyo ilijitokeza kwa waandamanaji.

"Wakati nchi nzima inakabiliwa na matatizo kama haya watu wamekuja hapa kutoa shinikizo hilo. Unapoona anasa katika nyumba hii ni dhahiri kwamba hawana muda wa kufanya kazi kwa ajili ya nchi," Chanuka Jayasuriya aliiambia Reuters.

Bw Rajapaksa aliondoka katika makao yake rasmi siku ya Ijumaa kama tahadhari ya usalama kabla ya maandamano yaliyopangwa, vyanzo viwili vya wizara ya ulinzi vilisema, kulingana na Reuters.

Ingawa ni makazi rasmi ya Bw Rajapaksa, kwa kawaida hulala katika nyumba tofauti iliyo karibu.

Watu hucheza kadi katika makazi rasmi ya waziri mkuu wa Sri Lanka siku ya Jumapili

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Watu wakicheza karata katika makazi rasmi ya waziri mkuu wa Sri Lanka siku ya Jumapili