Bangladesh inavyoshuhudia ongezeko kubwa la vifo vitokanavyo na radi

Chanzo cha picha, Mamun
Siku ambayo alifikiria kuwa angesherehekea harusi yake, Mamun aliwazika jamaa zake 16.
Walikuwa wameuawa na radi wakiwa njiani kuelekea kwenye sherehe.
Wakiwa wamevalia sari na suti zao nzuri zaidi, wanafamilia wake walipanda mashua ili kuungana na Mamun, dhoruba kali ilipopiga. Mvua iliponyesha, mashua ilisogea na wakajificha chini ya bati kwenye ukingo wa mto, walipogongwa.
Bangladesh, ambayo inakabiliwa na hali mbaya ya hewa na dhoruba kali, inakabiliwa na wastani wa vifo 300 vinavyotokana na radi kila mwaka, kwa mujibu wa UN.
Hiyo inalinganishwa na chini ya 20 kila mwaka nchini Marekani, ambayo ina karibu mara mbili ya idadi ya watu.
Ni mzigo mzito kwa taifa la Asia Kusini, na kwa wengi kama Mamun, ambaye anazungumza kwa mara ya kwanza kuhusu kile kilichotokea siku hiyo mnamo Agosti 2021.
Mvulana huyo mwenye umri wa miaka 21 alikuwa akijiandaa nyumbani kwa wakwe zake katika eneo la Shibganj kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo, aliposikia sauti ya radi dakika chache kabla ya kupata habari hiyo ya kumuumiza.
Alikimbilia kwa familia yake, ambapo alikutana na eneo lenye fujo na hali ya kuchanganyikiwa.
"Baadhi ya watu walikuwa wakikumbatia miili," Mamun anakumbuka, "waliojeruhiwa walikuwa wakilia kwa uchungu... watoto walikuwa wakipiga kelele. Nilikuwa nimepoteza. Sikuweza hata kuamua niende kwa nani kwanza."

Chanzo cha picha, Mamun
Mamun alipoteza baba yake, babu, binamu, wajomba na shangazi zake. Mama yake hakuwa kwenye mashua na alinusurika kushambuliwa na radi.
"Nilipopata maiti ya baba yangu nilibubujikwa na machozi tu. Nilishtuka sana nikaugua," Mamun anasema.
Baadaye jioni hiyo, mazishi ya jamaa zake yalifanyika, karamu ya harusi ambayo walikusudiwa kufurahia badala yake iligawanywa kwa wasio na makazi.
Mamun baadaye alioa, lakini anasema hasherehekei ukumbusho wa harusi yake kwani inasababisha kumbukumbu chungu. "Baada ya tukio hilo la kusikitisha, sasa ninaogopa sana mvua na radi."
Radi ni muuaji mkubwa nchini Bangladesh, na kupoteza maisha zaidi kila mwaka kuliko mafuriko.

Chanzo cha picha, SALMAN SAEED
Idadi ya vifo vilivyoripotiwa kutokana na radi pia imeongezeka kwa kasi, kutoka kadhaa tu kwa mwaka katika miaka ya 1990.
Nasa, Umoja wa Mataifa na serikali ya Bangladesh wanataja kuongezeka kwa dhoruba kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kama sababu ya kuongezeka kwa matukio mabaya.
"Ongezeko la joto duniani, mabadiliko ya mazingira, mifumo ya maisha yote ni sababu za kuongezeka kwa vifo kutokana na radi," Md Mijanur Rahman, mkurugenzi mkuu wa kitengo cha kudhibiti majanga cha Bangladesh, aliiambia BBC.
Huo ndio uzito, kwamba serikali imeongeza majanga ya radi katika orodha rasmi ya majanga ya asili ambayo nchi inayakabili ambayo ni pamoja na mafuriko, vimbunga, matetemeko ya ardhi na ukame.
Wengi wa waathiriwa wa radi ni wakulima, ambao wanaathiriwa na hali ya hewa wanapofanya kazi mashambani kupitia miezi ya mvua ya masika katika majira ya masika na kiangazi.

Chanzo cha picha, SALMAN SAEED
Shati inayoning'inia kwenye uzio uliochakaa, inayotazama uwanja katika eneo la Satkhira nchini Bangladesh ni ukumbusho wa kuhuzunisha wa mmoja wa waathiriwa.
Siku chache tu zilizopita, shati hilo lilikuwa limevaliwa na Abdullah alipokuwa akienda kwenye mashamba makubwa ya mpunga kufanya kazi yake ya siku.
Sasa, ikiwa juu ya kizuizi cha mbao, shati inapigwa na kuharibika, kingo zilizoungua zinaonesha ambapo radi iliacha alama mwezi Mei mwaka huu.
Mke wa Abdullah, Rehana, alinipeleka shambani kunieleza kilichotokea siku alipofiwa na mume wake.
Kulikuwa na jua kali wakati Abdullah na kikundi cha wakulima walikwenda kuvuna mpunga. Kufikia alasiri dhoruba kali ilianza, na radi ikampiga mumewe.
"Baadhi ya wakulima wengine walimleta kwenye duka hili lililo kando ya barabara," Rehana anasema, akionesha kibanda kidogo kando ya njia. "Wakati huo alikuwa tayari amekufa."

Chanzo cha picha, SALMAN SAEED
Huko nyumbani kwa Rehana, mchele aliovuna Abdullah siku moja kabla upo kwenye marundo nje ya nyumba ndogo ya chumba kimoja.
Wenzi hao walikuwa wamechukua mkopo hivi karibuni ili kujenga chumba cha pili ili kupanua nyumba yao ya kawaida.
Ndani, mtoto wa kiume wa wanandoa hao Masood, mwenye umri wa miaka 14, anasoma kitabu.Rehana anahofia kuwa atasalia na deni maishani mwake na anashangaa atalipia vipi masomo yake.
“Hofu ilinishika sana hivi kwamba sasa nikiona mawingu angani, sithubutu hata kumruhusu mwanangu atoke nje,” anasema huku akibubujikwa na machozi.

Chanzo cha picha, SALMAN SAEED
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Radi ni wasiwasi unaoongezeka katika nchi nyingine pia ikiwa ni pamoja na nchi jirani ya India ambayo pia imeona kuongezeka kwa idadi matukio ya radi katika miaka ya hivi karibuni, lakini kupungua kwa idadi ya vifo kutokana na jitihada zinazofanywa.
Kuna juhudi nchini Bangladesh kufanya zaidi kupunguza idadi ya vifo kutokana na radi.
Wanaharakati wanasema miti mirefu zaidi inahitaji kupandwa katika maeneo ya vijijini ili kukabiliana na athari za mashambulizi, hasa katika maeneo ambayo yamebeba mzigo mkubwa wa ukataji miti.
Pia wanatoa wito kwa mpango mkubwa wa kujenga vibanda, ili wakulima waweze kupata makazi salama, na mifumo mipana ya tahadhari ya mapema ili kuwatahadharisha watu kuhusu dhoruba zinazoweza kutokea.
Changamoto moja ni mawasiliano duni na ukosefu wa matumizi ya simu katika maeneo ambayo watu wako hatarini zaidi.
Ukosefu wa ufahamu pia ni changamoto. Wengi nchini hawatambui jinsi radi inavyoweza kuwa hatari.
Mkulima Ripon Hossen, ambaye alikuwa pamoja na Abdullah siku aliyopoteza maisha hakuwahi kufikiria jinsi radi ingeonekana kwa karibu, hadi ilipopiga.

Chanzo cha picha, SALMAN SAEED
"Kulikuwa na sauti kubwa, na kisha nikaona taa nyingi zinazowaka," alikumbuka. "Ilikuwa kama diski ya moto imetuangukia. Nilihisi mshtuko mkubwa wa radi na nikaanguka chini.
"Baada ya muda, nilifungua macho yangu na nikaona kwamba Abdullah amekufa."
Ripon haamini kuwa alinusurika. Anasema anaogopa kufanya kazi katika maeneo ya wazi, lakini katika eneo hili la kilimo duni kilimo ndicho chanzo pekee cha mapato kwake.
"Mimi hulia kila ninapomfikiria rafiki yangu Abdullah," anasema.
"Ninapofumba macho usiku, kumbukumbu zote za siku hiyo hurudi kama kumbukumbu ya nyuma. Siwezi kujifariji."












