Kuanguka kwa Yoon Suk Yeol: Rais 'mtata' wa Korea Kusini mwenye jazba na msukumo wa kijeshi

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Jean Mackenzie
- Nafasi, Seoul correspondent
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Ijumaa ya April 4, 2025, Mahakama ya Kikatiba ya Korea Kusini iliamua kuwa Rais Yoon Suk Yeol alitumia vibaya mamlaka kwa kutangaza sheria ya kijeshi mwezi Desemba, na hivyo akafutwa kazi rasmi kwenye nafasi ya urais.
Uamuzi huu ulikuwa wa kihistoria kwani ni mara ya kwanza kwa rais wa taifa hilo kuondolewa madarakani kwa jaribio la mapinduzi ya kijeshi katika zama za kisasa.
Kabla ya tukio hilo, Korea Kusini ilikuwa ikiheshimiwa kama taifa lenye demokrasia imara, maendeleo ya kiteknolojia na utamaduni unaovutia duniani kote. Hakukuwa na dalili kuwa rais wake angechukua hatua kali za kijeshi dhidi ya taasisi za kiraia.
Alikuwa anawaza nini?
Tangazo la Yoon la kutaka jeshi kuchukua udhibiti wa serikali liliwashangaza raia wengi, na pia viongozi wa kimataifa. Dunia ilishangazwa na rais wa nchi ya kidemokrasia kutangaza hali ya kijeshi kana kwamba Korea Kusini ilikuwa vitani.
Ingawa alifuta tangazo hilo ndani ya saa sita, athari za kisiasa na kijamii zilikuwa tayari zimetokea. Uamuzi huo ulimwangusha Yoon kisiasa na kuvuruga taswira ya nchi hiyo kimataifa.
Tabia ya Yoon: Ushindi Kwanza
Yoon alijulikana tangu akiwa mdogo kama mtu aliyejikita kwenye kushinda kwa gharama yoyote. Rafiki yake wa utotoni, Chulwoo Lee, anasema kuwa Yoon hakuwa tu mrefu na mwenye nguvu darasani, bali pia alikuwa na maamuzi ya haraka na msimamo mkali kwa jambo analoamini kuwa ni sahihi.
Akiwa mwanafunzi, alionesha tabia ya kusimamia haki, hata kama haikuwa katika muktadha wa kisiasa. Alimkemea polisi hadharani walipokuwa wakimhoji msichana – tukio lililoacha alama kwa waliomshuhudia. Hii ilionesha jinsi ambavyo hasira yake haikuwa ya kificho bali ya ghafla na ya moja kwa moja.

Katika miaka ya 1980, wakati dikteta Chun Doo-hwan alipoitawala Korea Kusini kwa sheria ya kijeshi, wanafunzi wengi waliandamana mitaani. Lakini Yoon hakuwa miongoni mwao –akionekana zaidi kujali sheria na siasa za heshima badala ya harakati za mabadiliko. Hili lilimtofautisha na wenzake wa wakati huo.
Hata hivyo, ndani yake kulikuwepo mchanganyiko wa msimamo mkali kwa haki na kutopenda kusikiliza wengine. Kwa walio karibu naye, huu ulikuwa mwelekeo ambao ungekuja kugharimu siasa zake baadaye.

Alikuwa Mwendesha mashtaka asiyeogopa na kutishwa
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kazi ya Yoon kama mwendesha mashtaka ndiyo ilimtambulisha kwa umma kama mtu jasiri, asiye na woga, na mwenye msimamo thabiti. Alijizolea umaarufu mkubwa mwaka 2013 alipoanzisha uchunguzi dhidi ya idara ya ujasusi ya nchi, kinyume na maagizo ya wakubwa wake.
Hatua hiyo ilimsimamisha kazi, lakini ilimpatia sifa kama shujaa wa sheria.
Wakati alipokuwa anatoa ushahidi mbele ya bunge, alitamka kwa ujasiri: "Siwajibiki kwa mtu yeyote zaidi ya sheria." Kauli hii ilimpa heshima kwa Wakoresha wengi waliotamani kuona uwajibikaji katika utumishi wa umma.
Mwaka 2018, Yoon aliandika historia nyingine kwa kumfungulia mashtaka na kisha kumtia hatiani Rais wa zamani Park Geun-hye, ambaye alihukumiwa kwa ufisadi. Hii ilimletea sifa kutoka kwa wanamageuzi na upande wa kushoto kisiasa.
Lakini kadri muda ulivyopita, rafiki zake walianza kuona kuwa uchunguzi wake ulianza kuwa wa kulipiza kisasi badala ya kutafuta haki. Alipoonywa na rafiki yake wa karibu Chulwoo Lee, alikasirika sana na kuvunja urafiki wao. Tabia ya kutokubali kukosolewa ikawa wazi zaidi.
Kupanda Kisiasa na Kuteleza
Baada ya kutimuliwa kutoka nafasi ya mwendesha mashtaka mkuu, Yoon aligeukia siasa – jambo lililoonekana kuwa gumu kutokana na ukosefu wake wa mtandao wa kisiasa. Alikubali kuwania urais kupitia chama cha kihafidhina cha People Power Party.
Waliomteua walijua alikuwa mtu wa msimamo mkali, lakini walimchagua kwa sababu waliona ana nafasi kubwa ya kushinda dhidi ya wapinzani wao. Hata hivyo, matatizo yaliibuka mara tu kampeni zilipoanza – Yoon alikataa ushauri na kufanya maamuzi kwa misingi ya mazungumzo ya pombe na marafiki wa karibu badala ya wataalamu wa siasa.
Baada ya kushinda uteuzi wa chama, siasa zake zilienda mbali zaidi upande wa kulia. Alianza kusikiliza zaidi sauti za wanahabari na wanasiasa wenye misimamo mikali, waliomweleza kuwa upinzani unahusiana na Korea Kaskazini. Akilini mwake, alijenga picha ya adui mkubwa anayepaswa kushughulikiwa kwa nguvu zote.

Chanzo cha picha, Getty Images
Watu wa karibu naye walihuzunika kuona jinsi ambavyo Yoon aliyekuwa na msimamo wa haki aligeuka kuwa kiongozi wa siasa za hofu, shaka, na chuki. Alijiondoa kabisa kutoka kwa marafiki wa zamani waliomshauri kuwa rais wa umoja.
Utawala wa Kimwendawazimu
Alipoingia madarakani, Yoon alileta mtindo wa kazi wa ofisi ya mwendesha mashtaka – akaamini kuwa anaweza kutawala kwa kushinikiza kila jambo. Alikataa kushirikiana na kiongozi wa upinzani, akimchukulia kama mhalifu badala ya mshindani wa kisiasa.
Washauri wake waliomshauri awe mpatanishi walifukuzwa au walijiondoa, na aliwazunguka kwa watu waliomkubali tu. Utamaduni wa kusema ukweli ulififia, na ofisi ya rais ikageuka kuwa eneo la woga na kukubali kila anachotaka kiongozi.
Alijifanya kama hahitaji kukubalika na wananchi, jambo lililomuathiri vibaya kisiasa. Mke wake aliingia kwenye kashfa ya zawadi za kifahari, lakini Yoon alikataa kuomba msamaha. Hali hii ilizidi kuchochea hasira ya umma dhidi ya serikali yake.
Katika uchaguzi wa wabunge, chama chake kilipoteza viti vingi na upinzani ukapata nguvu mpya. Lakini Yoon hakujifunza kutokana na hali hiyo – aliamini bado anaweza kutumia amri za rais kutekeleza ajenda yake, bila bunge.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mpango wa Sheria ya Kijeshi na Kuanguka

Chanzo cha picha, Getty Images
Hatua ya Yoon kutangaza sheria ya kijeshi ilifikiwa baada ya kuona upinzani unazidi kushika kasi, na bunge kuendelea kumzuia kisera. Alianza kuamini nadharia kuwa wapinzani wake walikuwa na ushawishi wa kifalsafa kutoka Korea Kaskazini, ingawa hakuwa na ushahidi.
Kwa msaada wa vyanzo vya mitandao ya kihafidhina, Yoon aliamini kuwa alikuwa katika vita vya kulinda taifa dhidi ya marxisim na upinzani unaodhamiria kuiangamiza Korea Kusini. Alifananisha wapinzani wake na chama cha kikomunisti cha China.
Mwishowe, Desemba 3, alitangaza hali ya kijeshi. Hatua hiyo iliwashangaza wote, hata watu wake wa karibu. Wananchi walimiminika mitaani kupinga, jeshi likakataa kutii amri hiyo, na bunge likachukua hatua za haraka kisheria.
Baada ya saa chache, Yoon alilazimika kufuta agizo hilo. Lakini uharibifu wa kisiasa ulikuwa tayari umetokea. Mahakama ya Katiba ilimhukumu kwa kutumia vibaya mamlaka, na kumvua urais milele.















