Wafungwa wa kivita wa Korea Kusini walivyotelekezwa kwa miongo kadhaa Korea Kaskazini

 Lee Dae-bong alivuka mto na kuingia China kutoroka Korea Kaskazini baada ya nusu karne kama mfungwa wa vita

Akiwa na umri wa miaka 92, Lee Dae-bong hafurahii haswa kuamka kitandani. Ameishi maisha ya kutosha. Anaporekebisha nguo yake ya kulalia , mkono wake wa kushoto unaonesha vidole vitatu vilivyokosekana.

Jeraha lake si matokeo ya vita alivyopigana, lakini miaka 54 iliyofuata alilazimika kuhangaika katika mgodi wa makaa ya mawe wa Korea Kaskazini.

Mwanajeshi huyo wa zamani wa Korea Kusini alikamatwa wakati wa Vita vya Korea na wanajeshi wa China, waliokuwa wakipigana pamoja na Korea Kaskazini. Ilikuwa tarehe 28 Juni 1953; siku ya kwanza ya vita vya Arrowhead Hill, na chini ya mwezi mmoja kabla ya silaha kukomesha miaka mitatu ya kikatili ya mapigano.

Watu wa kikosi chake, waliuawa siku hiyo. Yeye na manusura wengine wawili walipokuwa wakipakiwa kwenye treni ya mizigo, alidhani walikuwa wakielekea nyumbani Korea Kusini, lakini treni hiyo ilielekea Kaskazini, hadi mgodi wa makaa wa mawe wa Aoji, ambako alitumia muda mwingi wa maisha yake. Familia yake iliambiwa ameuawa katika mapigano.

Kati ya wanajeshi 50,000 na 80,000 wa Korea Kusini walitekwa nyara nchini Korea Kaskazini baada ya Vita vya Korea kumalizika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yaligawanya peninsula hiyo.

Mkataba wa amani haukuwahi kufuatwa, na wafungwa hawajawahi kurudishwa. Bw. Lee alikuwa mmoja wa wachache sana ambao walifanikiwa kupanga njama yake ya kutoroka.

Ni 80 tu kati ya makumi ya maelfu ya wanajeshi wa Korea Kusini waliokuwa wameshikiliwa Kaskazini walifanikiwa kurejea nyumbani

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa miongo kadhaa, licha ya mapigano kadhaa, makubaliano ya kusitisha mapigano kwa kiasi kikubwa yamefanyika, na kufanya huu kuwa usitishaji mrefu zaidi katika historia.

Lakini kukosekana kwa amani kumeleta madhara katika maisha ya Bw Lee, pamoja na wafungwa wenzake na familia zao. Huku Korea Kaskazini na Kusini zikiadhimisha miaka 70 tangu kusainiwa kwa makubaliano hayo, hadithi zao ni ukumbusho kwamba Vita vya Korea havijaisha.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa miaka ya kwanza ya kifungo chake Bw Lee alilazimika kufanya kazi kwa wiki moja katika mgodi wa makaa ya mawe ikifuatiwa na wiki moja akisoma itikadi za Korea Kaskazini, hadi, mwaka wa 1956, yeye na wafungwa wengine walipokonywa vyeo vyao vya kijeshi na kuambiwa waoe na kujiingiza katika jamii.

Lakini wao, na familia zao mpya, waliteuliwa kama watu waliotengwa na kuwekwa chini kabisa ya mfumo mkali wa tabaka la kijamii wa Korea Kaskazini.

Kuchimba makaa ya mawe, siku baada ya siku, kwa zaidi ya miaka 50 ilikuwa kazi ya kustaajabisha, lakini ilikuwa taharuki ya majeraha na kifo ambayo Bw Lee anasema ilikuwa ngumu zaidi kustahimili.

Siku moja mkono wake ulinaswa kwenye mashine ya kuchakata makaa, lakini upotevu wa vidole vyake ulionekana kuwa mdogo, kwani alishuhudia marafiki mbalimbali wakipoteza maisha katika mfululizo wa milipuko ya gesi ya methane.

"Tulitoa vijana wetu wote kwenye mgodi huo wa makaa ya mawe, tukisubiri na kuhofia kifo kisicho na maana wakati wowote," anasema. "Nilikumbuka sana nyumbani, haswa familia yangu. Hata wanyama wanapokaribia kufa wanarudi kwenye mapango yao."

Lee Dae-bong alilazimika kufanya kazi ngumu ya mikono katika migodi ya makaa ya mawe ya Korea Kaskazini na kupoteza vidole vitatu.

Huku Korea Kaskazini na Kusini zikiashiria amani iliyopo kwenye rasi hiyo, wengi wa wafungwa wa vita na familia zao wanalaumu pande zote mbili kwa mateso yao.

Marais mbalimbali wa Korea Kusini wamekutana na viongozi wa Korea Kaskazini, lakini ajenda ya kurejea kwao ilikuwa duni.

Kaskazini, baada ya kuachilia wafungwa 8,000 pekee, imekataa kukiri kuwa kuna wengine zaidi.

Katika mkutano wa kilele mwaka 2000 kati ya rais wa wakati huo wa Korea Kusini, Kim Dae-jung, na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-il, suala hilo hata halikutajwa.

Huu ndio wakati Lee Dae-bong anasema alipoteza matumaini yote, akigundua njia pekee ambayo angewahi kurudi nyumbani ni ikiwa angetoroka.

Siku tatu baada ya mwanae wa pekee kuuawa katika ajali ya mgodini, huku mkewe akiwa amefariki kwa muda mrefu, Bw.Lee alianza safari yake. Sasa akiwa na umri wa miaka 77, alivuka mto kwa siri hadi China, maji hayo yalimfika shingoni.

Yeye ni mmoja wa wafungwa 80 waliotoroka na kurejea nyumbani Korea Kusini, na ni watoro 13 pekee ambao bado wako hai.

Makumi ya maelfu ya wafungwa waliosalia waliachwa waangamie migodini. Ni wachache, kama wapo, bado wako hai, ingawa watoto wao wamebaki.

Chae Ah-in alikuwa na umri wa miaka sita baba yake alipouawa katika mlipuko wa gesi kwenye mgodi wa Korea Kaskazini. Muda si muda dada zake wakubwa walitumwa kufanya kazi mahali hapo.

Akiwa bado shuleni, alipigwa na kuonewa sana. Hakuweza kuelewa kwa nini familia yake 'ililaaniwa'. Baadaye tu, aliposikia dada zake wakinong’ona, ndipo alipojua kwamba baba yake alikuwa mwanajeshi wa Korea Kusini.

"Kwa muda mrefu nilimchukia," anasimulia, kutoka nyumbani kwake viungani mwa Seoul, ambako aliwasili mwaka wa 2010. "Nilimlaumu sana kwa kutufanya sote kuteseka."

Akiwa na umri wa miaka 28, Bi Chae pia alichagua kutoroka maisha yake yenye uchungu nchini Korea Kaskazini, na kuvuka kwanza hadi China, ambako aliishi kwa miaka 10. Ni hadi alipowasili Korea Kusini ndipo alipogundua kuwa baba yake alikuwa shujaa.

“Sasa ninamheshimu na ninajitahidi sana kumkumbuka,” asema. "Ninahisi tofauti na waasi wengine wa Korea Kaskazini, kwa sababu mimi ni binti mwenye fahari wa shujaa wa vita wa Korea Kusini."

Lakini Bi Chae hatambuliwi na serikali ya Korea Kusini kama binti wa mkongwe aliyejitolea maisha yake kwa ajili ya nchi yake.

Wafungwa wa vita (POWs) ambao hawakuwahi kufika nyumbani wanawekwa alama kama waliopotea, wanaodhaniwa kuwa wamekufa, na hawaheshimiwi kama mashujaa wa vita.

"Korea Kusini ipo leo kutokana na watu kama baba yangu, lakini mateso yetu bado hayajatatuliwa," anasema, akitaka wote wawili watambuliwe jinsi walivyo.

Ndugu wa wafungwa kwa miaka mingi wamekuwa wakidai wapendwa wao warudishwe nyumbani na watambuliwe kuwa mashujaa wa vita.

Chanzo cha picha, Getty Images

Takriban watoto 280 wameweza kutoroka na kufika Korea Kusini. Mwingine ni Son Myeong-hwa, mwenyekiti wa Jumuiya ya Familia ya wafungwa wa kivita wa Vita vya Korea, ambaye anapigana kwa niaba yao.

"Watoto katika Korea Kaskazini waliteseka kutokana na maumivu ya hatia na chama, na bado hapa Korea Kusini hatukubaliwi. Tunataka kupewa heshima sawa na ambayo familia za maveterani wengine walioanguka hupokea," alisema.

Serikali ya Korea Kusini ilituambia haina mpango wa kubadilisha uainishaji wake wa maveterani.

Kufikia wakati Lee Dae-bong alipofika nyumbani, tayari mzee, wazazi wake na kaka yake walikuwa wamekufa. Ijapokuwa Korea Kusini ilikuwa imebadilika zaidi ya kutambuliwa, dada yake mdogo alimpeleka kwenye ardhi ya mji wake wa kale.

Bw Lee anakumbuka jinsi marafiki zake waliokuwa wakifa huko Korea Kaskazini wangewasihi watoto wao siku moja wawazike katika miji yao. Matakwa yao bado hayajatekelezwa. Na kukosekana kwa amani kati ya Korea Kaskazini na Kusini kumeziacha familia hizi zikihangaika kutafuta amani yao wenyewe.

Lee Dae-bong na Chae Ah-in bado wana ndoto ya Kaskazini na Kusini kuunganishwa tena.

Bi Chae anataka kuleta mwili wa babake kuupumzisha nchini Korea Kusini.

Kwa Korea Kaskazini na Kusini, amani na kuunganishwa bado ni lengo lililowekwa rasmi. Lakini miaka 70 tangu mapigano ya silaha, ndoto hii inahisi kuwa mbali zaidi.