Tunachofahamu kuhusu mwanajeshi wa Marekani anayezuiliwa Korea Kaskazini kufikia sasa

Chanzo cha picha, EPA
Mwanajeshi wa Marekani anazuiliwa nchini Korea Kaskazini baada ya kuvuka mpaka kutoka Korea Kusini bila kibali, jeshi la Marekani limethibitisha.
Tukio hilo linajiri wakati kuna mvutano hasa na Kaskazini, mojawapo ya mataifa yaliyojitenga zaidi duniani. Marekani inawaomba raia wake wasiende huko.
Katika taarifa hii tunaangazia kile tunachojua kuhusu tukio hilo kufikia sasa.
Nini kilitokea mpakani?
Mwanajeshi Travis King, 23, alivuka kutoka Korea Kusini hadi Kaskazini baada ya kuzuru mpaka wa Eneo lisilo na Jeshi (DMZ).
Wakati huo alikuwa akisindikizwa kurudi Marekani, iliripotiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu, lakini anaonekana kuwapa wasindikizaji wake karatasi ya forodha kwenye Uwanja wa Ndege wa Incheon badala ya kupanda ndege.
Kisha alitoka nje ya kituo hadi kwenye mpaka wa umbali wa kilomita 54 (maili 34).
Shahidi aliyeshuhudia tukio hilo katika ziara hiyo ya mpakani alisema alimsikia askari huyo akicheka kwa sauti kubwa kabla ya kukimbia.
Kamandi ya Umoja wa Mataifa, ambayo inaendesha DMZ, ilisema inaamini kuwa mwanajeshi huyo sasa yuko chini ya ulinzi wa Korea Kaskazini.
Kamanda wa Marekani wa ngazi ya juu alisema hakuna mawasiliano yoyote na mwanajeshi huyo na tukio hilo linachunguzwa na Jeshi la Marekani Korea.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amesema wasiwasi mkubwa wa Pentagon ni kwa ajili ya ustawi wa mwanajeshi huyo.
Tunajua nini kuhusu askari huyo?
Travis King amekuwa akihudumu katika Jeshi la Marekani tangu Januari 2021. Ni mtaalamu wa upelelezi - awali alipewa kitengo cha Kitengo cha kwanza cha Kivita cha jeshi kwa zamu na jeshi la Marekani nchini Korea Kusini.
Alikuwa akikabiliwa na hatua za kinidhamu baada ya kushikiliwa nchini Korea Kusini kwa tuhuma za kushambulia, kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, likiwanukuu maafisa wa Marekani.
Wiki moja iliyopita, alipelekwa hadi Camp Humphreys - kambi ya jeshi huko Korea Kusini - kwa ajili ya kurejeshwa nyumbani.
Afisa wa ulinzi wa Marekani alithibitisha kuwa Pte King alikuwa akitakiwa kusafiri hadi Fort Bliss huko Texas ambako alipaswa kutengwa kiutawala na jeshi.
Afisa wa ulinzi alisema mwanajeshi huyo "alivuka mpaka" kwa makusudi.
Kwa nini tukio hili ni gumu sana kwa Marekani?
Mvutano unaoongezeka kwenye rasi ya Korea umekuwa kipaumbele zaidi cha sera za kigeni kwa utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden.
Tukio hilo lilitokea siku ambayo manowari ya makombora ya nyuklia ya Marekani iliwasili katika bandari ya Busan nchini Korea Kusini - Hatua inayoonekana kuwa maonyesho ya nguvu za kijeshi za Marekani ambazo zilikewara Wakorea Kaskazini.
Hatua hiyo ilikuwa jibu la Marekani kwa majaribio zaidi ya 100 ya makombora mapya ya Korea Kaskazini katika miaka michache iliyopita.
Mwanajeshi huyo anaweza kuwa chambo mpya itakayotumiwa na Korea Kaskazini dhidi ya Marekani.
Ni nini kilifanyika kwa Wamarekani waliozuiliwa na Korea Kaskazini hapo awali?
Raia wa Marekani wamezuiliwa Korea Kaskazini mara kadhaa tangu mwaka 1996. Walijumuisha watalii, wasomi na waandishi wa habari.
Mnamo Julai 2017, serikali ya Marekani ilipiga marufuku raia wa Marekani kuzuru nchi hiyo - hatua ambayo tangu wakati huo imerefushwa hadi Agosti mwaka huu.
Wafungwa wa Marekani wamekuwa wakikabiliwa kikatili katika magereza ya Korea Kaskazini.
Mnamo 2018, Kaskazini ilimwachilia mwanafunzi wa chuo kikuu wa Marekani, Otto Warmbier, ambaye alikuwa amefungwa kwa kuiba ishara ya hoteli. Alirudi Marekani akiwa hana fahamu na baadaye akafariki.














