Tunajua nini kuhusu binti ya Kim Jong-un?

.

Chanzo cha picha, KCNA via Reuters

Maelezo ya picha, Kim Jong un na bintinye

Bintiye kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un ameonekana hadharani kwa mara ya pili ndani ya wiki moja, na hivyo kuibua uvumi kuwa anaweza kumrithi baba yake .

Lakini vyombo vya habari vya nchi hiyo havijafichua jina au umri wa msichana huyo na vilimtaja tu kama mtoto "mpendwa zaidi" au "mpendwa" wa kiongozi huyo.

Chombo cha habari cha serikali ya Korea Kaskazini KCNA kiliripoti Jumapili kwamba Kim na bintiye walikutana na wanajeshi, wanasayansi na wengine waliohusika katika kurusha kombora la Hwasong-17 mwezi huu.

Picha za hivi punde za KCNA hazikuwa na tarehe lakini ilisema kwamba Kim na bintiye walipata umati "umejaa shauku na furaha isiyo na kikomo" huku wakionyesha "utukufu wa juu na heshima kubwa kwake".

Kwa hivyo tunajua nini kuhusu binti huyu wa Kim Jong-un?

.

Chanzo cha picha, KCNA via Reuters

Maelezo ya picha, Rais wa Korea kaskazini Kim jong Un na bintiye

Alitajwa kwa mara ya kwanza mnamo 2013

Kim Jong-un anaongoza mojawapo ya taifa la siri zaidi duniani, na ni machache sana yanayojulikana kuhusu maisha yake binafsi.

Mnamo Julai 2012, Korea Kaskazini ilithibitisha kuwa Ri Sol-ju alikuwa mke wa Kim, mwezi mmoja baada ya kuonekana naye hadharani.

Tangu wakati huo, vyombo vya habari vya Korea Kusini vimekisia kwamba wawili hao wana watoto watatu.

Mnamo Septemba 2013, mchezaji mstaafu wa mpira wa vikapu wa Marekani, Dennis Rodman, ambaye alikuwa Korea Kaskazini wakati huo kwenye "ziara ya diplomasia ya vikapu," alinukuliwa katika gazeti la Uingereza The Guardian akisema kwamba "Kim alikuwa na mtoto wa kike."

"Nilimshika mtoto wao Ju-ae na kuongea na [mke wa Bw Kim] pia. Yeye ni baba mzuri na ana familia nzuri," Rodman aliambia gazeti hilo.

Lakini hakukuwa na jibu rasmi au uthibitisho kutoka kwa Korea Kaskazini juu ya maoni ya Rodman.

.

Chanzo cha picha, KCNA via Reuters

Muonekano wa kwanza mnamo 2022

Mnamo tarehe 19 Novemba 2022, KCNA ilichapisha picha kadhaa za baba na binti huyo kwa mara ya kwanza, kuthibitisha ripoti za uvumi za muda mrefu za kuwepo kwake.

Vyombo vya habari vya serikali viliripoti kwamba wawili hao walikuwa wakizungumza na maafisa, wakikagua makombora na kutazama kurushwa kwa kombora la masafa marefu kutoka kwenye ukumbi wa kutazama siku moja kabla.

Lakini hakukuwa na undani wa jina au umri wa msichana katika ripoti hiyo.

"Kufichuliwa kwa bintiye Kim Jong-un kumewavutia wachambuzi wa Korea Kaskazini zaidi ya habari kwamba imefanikiwa kurusha kombora lake lenye nguvu zaidi linaloweza kufika Marekani," mwandishi wa BBC Seoul Jean Mackenzie alisema.

"Je, hii ina maana kwamba amechaguliwa kuwa mrithi wa Kim Jong-un na siku moja atakuwa akiiongoza Korea Kaskazini?"

Muonekano wa pili mnamo 2022

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Na wiki moja tu baada ya picha za kwanza za baba na binti huyo kutolewa, KCNA ilichapisha seti nyingine ya picha za wawili hao Jumapili.

Tena, bila kutaja umri au jina lake, lakini wakati huu alielezewa kuwa mtoto "mpendwa zaidi" au "thamani" wa kiongozi.

"Hakika hii inashangaza. Picha ya Kim Ju Ae akiwa amesimama pamoja na babake huku akiadhimishwa na mafundi na wanasayansi waliohusika katika uzinduzi wa hivi punde wa ICBM ingeunga mkono wazo kwamba huu ni mwanzo wa yeye kuwekwa kama mrithi anayetarajiwa," Marekani. Mtandao wa habari wa NBC ukimnukuu Ankit Panda, mtaalamu wa Shirika la Carnegie Endowment for International Peace.

Baadhi ya wachambuzi, hata hivyo, wametahadharisha kuwa ni mapema mno kusema kama yeye ni mrithi.

Chun Su-jin, mwandishi wa Korea Kusini wa kitabu kuhusu viongozi wanawake wa Korea Kaskazini, alinukuliwa katika ripoti ya Reuters kwamba nafasi ya wasomi wa Korea Kaskazini kumkaribisha bintiye Kim kama mtawala inakaribia sifuri.

"Haiko tayari kumkaribisha kiongozi wa jinsia nyingine," alisema. "[Kim] anaandaa tu onyesho kwamba yeye ni baba mwenye upendo, si tu dikteta katili ambaye anarusha makombora."

"Nchini Korea Kaskazini, jinsia bado ni muhimu kuwa kiongozi," alisema Hyun In-ae, mtoro wa Korea Kaskazini ambaye sasa anafanya kazi katika Taasisi ya Ewha ya Mafunzo ya Kuunganisha huko Seoul.

Iwe binti wa Kim ndiye mrithi au la, tayari kuna mwanamke mmoja katika serikali ambaye amevutia kimataifa kwa miaka kadhaa.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Dadake kim mwenye uwezo mkubwa

Kim Yo-jong: Dada mwenye uwezo mkubwa

Wakati uvumi ulipoibuka mnamo 2020 juu ya afya ya Kim Jong-un, dada yake, Kim Yo-jong alionekana kama mtu anayeweza kuchukua nafasi ya familia hadi mmoja wa watoto wa Kim atakapokuwa na umri wa kutosha.

Kim Yo-jong amekuwa akishikilia nafasi ya juu katika serikali kwa muda. Hivi majuzi ametoa vitisho vya matusi kwa Korea Kusini juu ya vikwazo.

Lakini ni dhahiri kwamba kuonekana kwa bintiye Kim Jong-un kumezua maswali zaidi kutoka kwa ulimwengu, kama mwandishi wa BBC Jean Mackenzie anavyoeleza.

"Kwanini umuoneshe sasa? Bado ni mdogo sana. Ikiwa anamuandaa kuchukua madaraka, hii inaweza kumaanisha kuwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 38 ana matatizo ya kiafya? Afya yake ni suala la uvumi mwingi, kama inavyoonekana kuwa hatari kubwa kwa utulivu wa serikali."

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kim jong un na dadake pamoja na bintiye