Venezuela yaishutumu Marekani kwa 'unyang'anyi mkubwa'
Hatua ya Washington ya kukamata meli mbili za mafuta za Venezuela ilikuwa "mbaya zaidi kuliko uharamia," balozi wa Venezuela katika Umoja wa Mataifa alisema.
Muhtasari
- Mzozo wa Ukraine: Zelensky atoa maelezo ya mpango mpya wa amani
- Wanaharakati wa mitandao ya kijamii wa Uingereza miongoni mwa watano walionyimwa viza ya Marekani
- Makumi ya watu wakamatwa katika msako dhidi ya uhalifu wa mtandaoni Ghana
- Venezuela yaishutumu Marekani kwa 'unyang'anyi mkubwa'
- Wanavijiji wa mpakani wametekwa nyara na kupelekwa Urusi - Ukraine
- Umoja wa Kijeshi wa Sahel wazindua kituo cha TV cha pamoja na benki ya uwekezaji
- Trump alisafiri kwa ndege ya Epstein zaidi ya ilivyofikiriwa awali - mwendesha mashtaka
- Wataalamu wa UN waitaka Iran isitishe hukumu ya kifo dhidi ya mwanaharakati mwanamke
- Mtangazaji wa Uingereza ashtakiwa kwa makosa mapya ya unyanyasaji wa kingono
- Mkuu wa jeshi Libya afariki katika ajali ya ndege Uturuki
- Ukraine yapoteza mji wa mashariki uliokumbwa na vita
Moja kwa moja
Na Asha Juma & Ambia Hirsi
Mzozo wa Ukraine: Zelensky atoa maelezo ya mpango mpya wa amani

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky Volodymyr Zelensky wa Ukraine ametoa maelezo ya mpango mpya wa amani unaoipatia Urusi uwezekano wa kuwaondoa wanajeshi wa Ukraine mashariki na kuundwa kwa eneo lisilo na wanajeshi.
Akielezea kwa kina mpango huo wenye vipengele 20 uliokubaliwa na wajumbe wa Marekani na Ukraine huko Florida mwishoni mwa juma, Zelensky alisema Urusi itajibu Jumatano mara tu Marekani itakapozungumza nao.
Akiuelezea mpango huo kama "mfumo mkuu wa kumaliza vita", alisema ulipendekeza hakikisho la usalama kutoka kwa Marekani, Nato na Ulaya kwa ajili ya kukabiliana na uratibu wa kijeshi ikiwa Urusi itaivamia tena Ukraine.
Juu ya swali kuu la Donbas mashariki mwa Ukraine, Zelensky alisema kuwa na "eneo huru la kiuchumi" chaguoni jambo linalowezekana.
Aliwaambia waandishi wa habari kwamba kwa vile Ukraine inapinga kujitoa, wapatanishi wa Marekani wanapanga kuanzisha eneo lisilo na kijeshi au eneo huru la kiuchumi.
Eneo lolote ambalo wanajeshi wa Ukraine watajiondoa linapaswa kuchungwa na Ukraine, alisisitiza.
"Afua ni mbili," Zelensky alisema, "vita vitanaendelea, au uamuzi ufikiwe kuhusu maeneo yote ya kiuchumi."
Soma pia:
Wanaharakati wa mitandao ya kijamii wa Uingereza miongoni mwa watano walionyimwa viza ya Marekani

Chanzo cha picha, Alamy
Maelezo ya picha, Clare Melford na Imran Ahmed, ambao wamekuwa wakifanya kampeni dhidi ya matamshi ya chuki na habari potofu mtandaoni, wamepigwa marufuku kuingia Marekani. Wanaharakati wawili wa mitandao ya kijamii wa Uingereza ni miongoni mwa watu watano walionyimwa viza vya Marekani baada ya Wizara ya Mambo ya Nje kuwashutumu kwa kutaka "kulazimisha" majukwaa ya teknolojia ya Kimarekani kukandamiza uhuru wa kujieleza.
Imran Ahmed, mshauri wa zamani wa Kazi ambaye sasa anaongoza Kituo cha Kukabiliana na Chuki ya Kidijitali (CCDH), na Clare Melford, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Disinformation Index (GDI), walitanjwa kuwa "wanaharakati wenye itikadi kali" na utawala wa Trump na kupigwa marufuku kuingia Marekani.
Kamishna wa zamani wa Ufaransa wa Umoja wa Ulaya na watu wawili wakuu katika shirika la kupinga chuki la mtandaoni lenye makao yake nchini Ujerumani pia walinyimwa viza.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameongoza viongozi wa Ulaya kulaani hatua hiyo, akiitaja kuwa ni ya "kutisha".
Makumi ya watu wakamatwa katika msako dhidi ya uhalifu wa mtandaoni Ghana

Maafisa nchini Ghana wanasema wamewakamata watu 48 wanaoshukiwa kwa kuhusika na uhalifu wa mtandaoni katika eneo la Dawhenya viungani mwa mji wa Accra.
Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Kidijitali na Ubunifu wa Ghana, Sam George, alisema kukamatwa kwa watu hao kulifuatia operesheni ya usiku iliyoongozwa na Mamlaka ya Usalama wa Mtandao ya nchi hiyo, kwa ushirikiana na Huduma ya Polisi ya Ghana.
Katika taarifa yake siku ya Jumatano, alisema "Waliokamatwa wanaaminika kuwa raia wa Nigeria, kulingana na mahojiano ya awali, ambayo yanajumuisha wanaume 46 na wanawake wawili".
Maafisa wanasema washukiwa hao wanahusishwa na uhalifu mkubwa unaofanywa mtandaoni, ikiwa ni pamoja na ulaghai wa mapenzi, ulaghai wa uwekezaji mtandaoni, mipango ya uigaji na biashara haramu ya dhahabu mtandaoni.
Bidhaa zilizopatikana wakati wa operesheni hiyo zilijumuisha vipakatalishi, simu za mkononi na vifaa vya intaneti.
Bw George alisema Ghana itaendelea kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni, na kuongeza: "Tutaendelea kuwasaka wahalifu wa mtandao bila kukoma."
Kukamatwa kwa watu hao kunakuja siku chache baada ya Mamlaka ya Usalama wa Mtandao ya Ghana kuwashikilia raia 32 wa Nigeria wanaoshukiwa kufanya uhalifu wa mtandaoni wakati wa operesheni huko Kasoa-Tuba, karibu na Kasoa katika Mkoa wa Kati.
Pia unaweza kusoma:
Venezuela yaishutumu Marekani kwa 'unyang'anyi mkubwa'

Chanzo cha picha, Getty Images
Venezuela imeishutumu Marekani kwa "unyang'anyi mkubwa" katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York.
Hatua ya Washington ya kukamata meli mbili za mafuta za Venezuela ilikuwa "mbaya zaidi kuliko uharamia," balozi wa Venezuela katika Umoja wa Mataifa alisema.
Kikao hicho cha dharura kiliitishwa kujadili hatua ya kukamatwa kwa meli hizo za mafuta, katika pwani ya Venezuela mapema mwezi huu.
Marekani pia imesema kuwa inafuatilia meli ya tatu ya mafuta ya Venezuela.
Rais Trump amemshutumu Rais wa Venezuela Nicolas Maduro kwa kuendekeza biashara ya dawa za kulevya na kusema magenge yamekuwa yakiendesha shughuli hizo bila kuadhibiwa kwa muda mrefu sana.
Mnamo Desemba16, Trump aliamuru kuzuiliwa kwa meli zote za mafuta za Venezuela zilizowekewa vikwazo.
Rais wa Marekani amesema Marekani itayahifadhi au kuyauza mafuta ghafi ambayo imechukua, pamoja na meli zenyewe.
Marekani imekuwa ikiimarisha uwepo wake wa kijeshi katika Bahari ya Pasifiki na Caribbean katika miezi ya hivi karibuni, ikituma wanajeshi 15,000 na meli za kubeba ndege na meli za kivita katika eneo hilo.
Maelzo zaidi:
Wanavijiji wa mpakani wametekwa nyara na kupelekwa Urusi - Ukraine

Chanzo cha picha, Francisco Richart/SOPA Images/LightRocket
Wakazi 52 wa kijiji cha Hrabovske nchini Ukraine wamepelekwa Urusi baada ya vikosi vya nchi hiyo kuvamizi kijiji hicho cha mpakani, mamlaka mjini Kyiv zinasema.
Wanajeshi 13 wa Ukraine pia walikamatwa mpakani katika eneo la kaskazini mashariki mwa Sumy.
Shambulio hilo lililifanyika usiku wa Jumamosi, wakati wanajeshi 100 wa Urusi waliposhambulia kijiji hicho, alisema Viktor Trehubov, msemaji wa Kikosi Kazi cha Pamoja cha Kijeshi cha Ukraine.
Raia hao walikusanywa kanisani na baadaye kuvushwa mpaka hadi Urusi, aliiambia BBC.
Ni nadra sana kwa vikosi vya wavamizi kuwachukua raia na kuwapeleka Urusi kabla ya kuwekwa kwa misngi thabiti ya usimamizi katika eneo linalokaliwa kimabavu, aliongeza.
Mpaka sasa Urusi haijatoa tamko lolote kuhusiana na hatma ya wakzi hao wa Hrabovske, lakini ripoti kutoka Ukraine zinaonyesha kuwa huenda walipelekwa Belgorod, kituo kikuu cha kikanda takriban maili 50 (kilomita 80) ndani ya Urusi.
"Mama ya marafiki zangu amepelekwa huko. Hakuna njia ya kuwasiliana naye," alisema Volodymyr Bitsak, mjumbe wa baraza la mkoa wa Sumy.
"Najua, wamepelekwa katika jiji la Belgorod na wanazuiliwa mahali pasipojulikana."
Soma zaidi:
Umoja wa Kijeshi wa Sahel wazindua kituo cha TV cha pamoja na benki ya uwekezaji

Chanzo cha picha, Getty Images
Mkutano wa pili wa kila mwaka wa Muungano wa Nchi za Sahel (AES), uliofanyika katika mji mkuu wa Mali, Bamako, umemalizika kwa wito wa umoja, kuzinduliwa kwa kituo kipya cha televisheni cha kikanda na mipango ya benki ya pamoja ya uwekezaji.
Viongozi wa muungano huo wenye wanachama watatu walisema kituo kipya cha Televisheni cha AES kitasaidia kukabiliana na taarifa potofu na kuipa eneo hilo sauti yake.
Pia walitangaza kuundwa kwa benki ya ushirika ya uwekezaji ili kuimarisha uhuru wa kiuchumi.
Waziri Mkuu wa Niger, Ali Mahaman Lamine Zeine, amesema kubuniwa kwa benki hiyo "ni sehemu ya maono mapya ya kijiografia.
Aliongeza kuwa nchi hizo tatu "zitaunganisha rasilimali, njia na mikakati ili kutoa eneo la AES miundombinu muhimu kwa maendeleo yake".
Mkutano huo uliimarisha ujumbe mzito kuhusu "uhuru", Kanali Assimi Goïta wa Mali, Kapteni wa Burkina Faso Ibrahim Traoré na Jenerali Abdourahamane Tchiani wa Niger wakiahidi kufanya kazi pamoja kushughulikia vitisho vya usalama vinavyowakabili.
Nchi hizo tatu, zilizo chini ya utawala wa kijeshi, zimejiondoa kutoka kwenye jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi, Ecowas, na kuunga mkono Urusi kama mshirika wa kimaendeleo.
Maelezo zaidi:
Ashtakiwa kwa kumpa mke wake wa zamani dawa za kulevya na kumbaka

Chanzo cha picha, Pracedo
Diwani wa zamani amefikishwa mahakamani akishtakiwa kwa mfululizo wa makosa ya kingono dhidi ya mke wake wa zamani kwa kipindi cha miaka 13.
Philip Young anashtakiwa kwa makosa 56, ikiwa ni pamoja na makosa mengi ya ubakaji na kumpa dawa za kulevya mke wake wa zamani Joanne Young, ambaye ameondoa haki yake ya kisheria ya kutotajwa jina.
Akifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Swindon mapema, mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 49 - ambaye zamani alikuwa akiishi Swindon lakini sasa anaishi Amberley Road huko Enfield - alithibitisha jina lake na anwani yake. Hakuomba msamaha.
Wanaume wengine watano walioshtakiwa kwa makosa ya kingono dhidi ya Bi Young, mwenye umri wa miaka 48, walifika katika mahakama hiyo hiyo, huku wawili wakikana mashtaka yote.
Congo yasitisha usindikaji wa shaba na kobalti kuzuia usafirishaji haramu wa madini

Chanzo cha picha, Reuters
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imesitisha usindikaji wa madini ya shaba na kobalti, kulingana na amri iliyoonekana na Reuters, katika juhudi za kuboresha uwazi na kuzuia usafirishaji haramu wa madini.
Congo, muuzaji mkuu wa kobalti duniani anayechangia karibu 70% ya uzalishaji wa kimataifa, imekuwa ikipambana kwa miongo kadhaa na uchimbaji haramu wa madini ambao huathiri mapato ya taifa.
Amri hiyo, iliyoandikwa Desemba 19 na kusainiwa na waziri wa madini Louis Watum Kabamba, inaamuru viwanda vyote vinavyosindika na kuuza shaba na kobalti kusitisha shughuli hiyo na kuthibitisha asili ya madini yanayotumika.
Tume itaundwa kuhakikisha utekelezaji wa amri hiyo na kufuatiliaji uhalali wa madini yanayotumika, hati hiyo ilisema.
Pia unaweza kusoma:
Kamishna wa zamani wa EU na wengine wanyimwa viza na Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema itawanyima viza watu watano, akiwemo kamishna wa zamani wa EU, kwa kutaka "kulazimisha" majukwaa ya mitandao ya kijamii ya Marekani kukandamiza mitazamo wanayopinga.
"Wanaharakati hawa wenye msimamo mkali na mashirika yasiyo ya kiserikali wameendeleza ukandamizaji unaofanywa na mataifa ya kigeni - katika kila kisa wakiwalenga wazungumzaji na makampuni ya Marekani," Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio alisema katika taarifa
Thierry Breton, aliyekuwa mdhibiti mkuu wa teknolojia katika Tume ya Ulaya, alisema kwamba "kuna njama" ya ukandamizaji inayoendelea.
Breton alielezewa na Idara ya Mambo ya Nje kama "mpangaji" wa Sheria ya Huduma za Kidijitali za EU (DSA), ambayo inalazimisha udhibiti wa maudhui kwenye makampuni ya mitandao ya kijamii.
Breton ametofautiana na Elon Musk, mtu tajiri zaidi duniani na mmiliki wa X, kuhusu wajibu wa kufuata sheria za EU.
Hivi majuzi Tume ya Ulaya ilitoza faini mtandao wa X ya €120m (£105m) kwa sababu ya beji zake za bluu kwa watumiaji wake - faini ya kwanza chini ya sheria za digitali za EU.
Ilisema mfumo huo ulikuwa "wa udanganyifu" kwa sababu kampuni hiyo haikuwa "ikithibitisha watumiaji kwa njia ya msingi yenye kuonyesha umuhimu wa hatua hiyo".
Akijibu, tovuti ya Musk ilizuia Tume kutengeneza matangazo kwenye jukwaa lake.
Kwa upande wake, Breton aliandika kwenye mtandao wa X: "Kwa marafiki zetu wa Marekani: Udhibiti sio kile munachofikiria."
Pia unaweza kusoma:
Trump alisafiri kwa ndege ya Epstein zaidi ya ilivyofikiriwa awali - mwendesha mashtaka

Chanzo cha picha, Davidoff Studios/Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump aliorodheshwa kama abiria kwenye ndege ya kibinafsi ya mhalifu wa kingono marehemu Jeffrey Epstein mara nane kati ya 1993 na 1996, barua pepe mpya iliyotolewa na Idara ya Sheria ya Marekani (DOJ) inasema.
"Donald Trump alisafiri kwa ndege ya kibinafsi ya Epstein mara nyingi zaidi kuliko ilivyofikiriwa hapo awali," inasomeka barua pepe ya Januari 7, 2020 kutoka kwa wakili msaidizi wa Marekani.
Jina la Trump kwenye rekodi ya safari ya ndege halionyeshi makosa yoyote yaliyofanyika. Mnamo 2024, Trump aliandika: "Sikuwahi kusafiri kwa Ndege ya Epstein" na kukanusha kufanya makosa yoyote kuhusiana na Epstein.
Idara ya Sheria inasema baadhi ya faili zilizotolewa Jumanne "zina madai yasiyo ya kweli na ya kusisimua" dhidi ya Trump.
Trump alikuwa rafiki wa Epstein kwa miaka mingi, lakini rais huyo amesema walitofautiana yapata mwaka 2004 - miaka kabla ya Epstein kukamatwa kwa mara ya kwanza.
Toleo la hivi karibuni la hati - zenye kurasa zaidi ya 30,000 - ni sehemu ya faili zinazoitwa za Epstein ambazo Idara ya sheria ilitakiwa kisheria kuzichapisha zote kufikia Ijumaa iliyopita.
Epstein alifariki katika chumba cha gereza cha New York mwaka wa 2019 alipokuwa akisubiri kesi yake kuhusu mashtaka ya biashara haramu ya ngono.
Soma zaidi:
UN yaitaka Iran kusitisha hukumu ya kifo dhidi ya mwanaharakati mwanamke

Chanzo cha picha, X
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa na wanawake 400 mashuhuri wameitaka Iran isitishe hukumu ya kifo dhidi ya Zahra Tabari, mhandisi wa umeme mwenye umri wa miaka 67 na mwanaharakati wa haki za wanawake.
Bi Tabari alikamatwa mnamo mwezi Aprili na kushtakiwa kwa kushirikiana na kundi la upinzani lililopigwa marufuku, Shirika la Mujahidina la Watu wa Iran (PMOI), kulingana na familia yake.
Mnamo mwezi Oktoba, Tabari alihukumiwa kifo kwa "uasi wa kutumia silaha" na Mahakama moja huko Rasht baada ya kesi kusikilizwa kwa njia ya video iliyodumu chini ya dakika 10.
Familia yake ilisema uamuzi huo ulitokana na ushahidi mdogo sana na usioaminika: kipande cha kitambaa chenye maneno "Mwanamke, Upinzani, Uhuru", na ujumbe wa sauti ambao haujachapishwa.
Mamlaka ya Iran bado haijatoa maoni kuhusu kesi hiyo.
Takriban watu wengine 51 wanajulikana kukabiliwa na adhabu ya kifo nchini Iran baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya usalama wa taifa ikiwemo uasi wa kutumia silaha, pamoja na "uadui dhidi ya Mungu", "ufisadi" na ujasusi, kulingana na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.
Bi Tabari alikamatwa wakati wa uvamizi nyumbani kwake bila kibali cha mahakama, na alihojiwa kwa mwezi mmoja huku akizuiliwa katika kifungo cha peke yake na kushinikizwa kukiri kuchukua silaha dhidi ya serikali na kuwa mwanachama wa kundi la upinzani, kulingana na wataalamu.
Bi Tabari alikataliwa kupata wakili aliyemchagua na aliwakilishwa na wakili aliyeteuliwa na mahakama, walisema, wakiongeza kwamba hukumu yake ya kifo ilitolewa mara baada ya kusikilizwa kwa kesi.
Soma zaidi:
Mtangazaji wa Uingereza ashtakiwa kwa makosa mapya ya unyanyasaji wa kingono

Chanzo cha picha, Reuters
Russell Brand ameshtakiwa kwa makosa mengine mawili ikiwemo shtaka moja la ubakaji, Polisi wa Jiji Kuu la Uingereza wamesema.
Katika taarifa mpya, jeshi la polisi lilisema Huduma ya Mashtaka ya Kitaifa (CPS) imeidhinisha shtaka la ziada la ubakaji na shtaka la unyanyasaji wa kingono kuhusu wanawake wengine wawili.
Mtangazaji, mchekeshaji na mwigizaji huyo, hapo awali alikanusha mashtaka matano ikiwemo makosa mawili ya ubakaji, makosa mawili ya unyanyasaji wa kingono na kosa moja la unyanyasaji usio wa kingono kwa wanawake wanne.
Bw. Brand, mwenye umri wa miaka 50, anatarajiwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Westminster tarehe 20 Januari 2026 kuhusiana na mashtaka hayo mawili mapya.
Mkuu wa jeshi Libya afariki katika ajali ya ndege Uturuki

Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images
Waziri mkuu wa Libya amesema, mkuu wa jeshi la Libya ameuawa katika ajali ya ndege nchini Uturuki.
Jenerali Mohammed Ali Ahmed al-Haddad na wengine wanne walikuwa ndani ya ndege aina ya Falcon 50 iliyokuwa ikitoka mji mkuu wa Uturuki, Ankara, Jumanne jioni.
Katika chapisho kwenye mtandao wa X, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki Ali Yerlikaya alisema mawasiliano na ndege hiyo ya biashara yalipotea saa 20:52 saa za eneo (17:52 GMT) – takriban dakika 42 baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege wa Ankara.
Ndege hiyo iliyokuwa ikielekea Tripoli ilikuwa imetoa ombi la kutua kwa dharura kabla ya mawasiliano kupotea.
Mabaki ya ndege hiyo baadaye yalipatikana kusini-magharibi mwa Ankara, na uchunguzi sasa unaendelea kuhusu kilichosababisha ajali hiyo.
Pia unaweza kusoma:
Ukraine yapoteza mji wa mashariki uliokumbwa na vita

Chanzo cha picha, Reuters
Wanajeshi wa Ukraine wamejiondoa kutoka mji wa mashariki wa Siversk uliokumbwa na vita, huku Urusi ikiendelea kusonga mbele taratibu.
Jeshi la Ukraine lilisema Jumanne kwamba lilichukua hatua hiyo "kuokoa maisha ya wanajeshi wetu na uwezo wa kupigana wa vitengo", na kuongeza kwamba vikosi vya Urusi " vina faidika pakubwa na nguvu kazi".
Kutekwa kwa mji wa Siversk kunaileta Urusi karibu na miji ya mwisho iliyosalia ambayo ni "ngome ya ukanda" wa Sloviansk na Kramatorsk ambayo bado iko mikononi mwa Ukraine katika eneo la viwanda la Donetsk.
Mapema siku hiyo, maafisa walisema watu watatu - akiwemo mtoto mdogo - waliuawa katika shambulio kubwa la ndege zisizo na rubani za Urusi usiku kucha na makombora dhidi ya Ukraine.
Urusi ilianzisha uvamizi kamili dhidi ya Ukraine mnamo Februari 2022, na kwa sasa inadhibiti takriban 20% ya eneo la Ukraine.
Katika taarifa, jeshi la Ukraine lilisema wanajeshi wa Urusi wanaendelea na "vitendo vya mashambulizi" katika eneo la Siversk "licha ya kupata hasara kubwa".
Iliongeza kwamba "vikosi vya ulinzi vya Ukraine vilikuwa vimemchosha adui wakati wa mapigano ya Siversk".
Kabla ya uvamizi wa Urusi, Siversk ilikuwa na watu wapatao 11,000.
Wiki mbili zilizopita Urusi ilikuwa tayari imeripoti udhibiti wa mji huo - lakini Ukraine ilikana madai hayo wakati huo.
Siversk imeangamizwa kama mji katika kipindi cha miezi mingi ya mapigano makali.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 24/12/2025.
