'Hapana inamaanisha hapana' - Wanawake wa Iran wanaoandamana kupinga hijab ya lazima

Wanawake walishiriki picha zao mitandaoni bila kufunika vichwa vyao
Maelezo ya picha, Maandamano ya hijab Iran

Wanawake nchini Iran wamekuwa wakiandamana kupinga sheria kali za hijab za nchi hiyo kwa kuvua vazi hilo hadharani na kuweka picha zao katika mitandao ya kijamii.

"Hakuna Hijab ya lazima!Leo niliendesha gari hadi kazini bila kuvalia hijab kichwani ili kupinga sheria hiyo! Ndoto yetu ni kuwa huru kuamua cha kuvaa," mwanamke mmoja wa Iran alisema katika kanda ya video iliyochapishwa mtandaoni.

Wanaharakati wa kutetea haki wametoa wito kwa wanawake kote nchini humo kuweka mtandaoni video zinawaonesha wakiwa wametoa hijab hadharani kuendana na Julai 12 ambayo ni Siku ya Kitaifa ya Hijabu na Usafi katika kalenda rasmi ya Iran.

Makumi ya wanawake waliitikia wito huo, licha ya hatari ya kukamatwa kwa kitendo hiki cha uasi wa kiraia, ambacho ni kinyume na sheria za nchi kuhusu "mavazi ya Kiislamu".

Kuvua hijab
Maelezo ya picha, Baadhi ya video zilionyesha wanawake wakivua hijab zao

Wanawake katika sehemu mbalimbali za nchi walirekodi video za selfie kutoka kwenye bustani, mitaa ya jiji na hata ufukweni, wakijionyesha bila hijabu zao, wengine wakiwa wamevaliamavazi ya kiangazi na kaptula.

Katika video moja iliyoshirikishwa mtandaoni na maelfu ya watu, mwanamke anaweza kuonekana akitembea kando ya barabara ya maji, kabla ya kuvua hijab yake, kuiacha ianguke chini, na kisha kuikanyaga na kuondoka.

Siku hiyo hiyo, mamlaka iliandaa mikutano ya hadhara kwa wanawake waliovalia hijabu kusherehekea "ulinzi wake wa Kiislamu". Televisheni ya Taifa ilipeperusha sherehe ya "Hijabu na Usafi", iliyojumuisha maonyesho ya kina mama waliovalia majoho marefu meupe na hijabu za kijani katika rangi za kitaifa.

 Sherehe ya Hijabu na Usafi ulioungwa mkono na serikali

Chanzo cha picha, Tasnim News Agency

Maelezo ya picha, Sherehe ya Hijabu na Usafi ulioungwa mkono na serikali

Wakati huo huo, kwenye mitandao ya kijamii ya Kiajemi hashtag ya kampeni hiyo ambayo inatafsiriwa kwa Kiajemi kama: "Hapana inamaanisha hapana, wakati huu hapana kwa hijab ya lazima", ilisambaa haraka haraka, ikikuzwa na wanaharakati, pamoja na baadhi ya waandishi wa habari na wanasiasa wa upinzani.

Baadhi ya wanawake waliwakemea wanaume walio madarakani ambao wanawajibikia kuwawekea mipaka ya uhuru wao wa kibinafsi.

"Mnatuona tu kama kwama watu wa kunatumikia heshima yenu, kama mali yenu! Mnatuona kama wanadamu dhaifu na wasio na uwezo wowote. Munatulazimisha kufunika vichwa vyetu kulingana na hali mbaya na ukosefu wen wa usalama," mwanamke kutoka kaskazini mwa Iran alisema katika video iliyotumwa kwa BBC Idhaa ya Kiajemi, huku akivua hijabu yake mbele ya kamera.

Wanawake watano walioweka video zao mitabndaoni kama sehemu ya kampeni hiyo ya hivi punde wamekamatwa, BBC Idhaa ya Kiajemi inaripoti.

Vida Movahed (pichani), nyota wa vuguvugu la maandamano kama hayo mnamo 2018, alitumikia kifungo cha miezi kadhaa gerezani.
Maelezo ya picha, Vida Movahed (pichani), nyota wa vuguvugu la maandamano kama hayo mnamo 2018, alitumikia kifungo cha miezi kadhaa gerezani.

Iran imeshuhudia kampeni kadhaa kama hayo katika miaka ya hivi karibuni chini ya hashtag akam vile #UhuruWangu na #JumatanoNyeupe, na wanawake wanaopigania haki ya kuamua mavazi yao.

Lakini ukandamizaji wa hivi majuzi wa "polisi wa maadili" wa Iran dhidi ya wanawake wanaodaiwa kutofuata kanuni za mavazi umesababisha wapinzani wa sera hiyo kutaka kuchukuliwa hatua.

 Polisi wa maadili wanaweza kuwakamata wanawake kwa kutovaa "hijab sahihi"

Chanzo cha picha, ISNA

Maelezo ya picha, Polisi wa maadili wanaweza kuwakamata wanawake kwa kutovaa "hijab sahihi"

Tangu mapinduzi ya Kiislamu ya 1979 nchini Iran, wanawake wametakiwa kisheria kuvaa mavazi ya kujisitiri ya "Kiislamu".

Kiutendaji, hii ina maana kwamba wanawake lazima wavae chador, vazi linalofunika mwili mzima, au hijab na nguo inayofunika mikono yao.

Baadhi ya wanaume wa Iran pia wamekuwa wakiunga mkono kampeni hiyo kwenye mitandao ya kijamii, wakionekana kwenye video pamoja na wanawake wanaoandamana.

Picha inayoonyesha ukuta wa msikiti mmoja mjini Tehran iliyochorwa ujumbe: "Mkate, kazi, uhuru, vazi nalotaka" ilisambazwa sana mtandaoni, ikirejelea mzozo wa kiuchumi wa nchi hiyo pamoja na sheria ya hijab.

ukuta wa msikiti mmoja mjini Tehran iliyochorwa ujumbe: "Mkate, kazi, uhuru, vazi la kujitolea"
Maelezo ya picha, Ukuta wa msikiti mmoja mjini Tehran iliandikwa ujumbe: "Mkate, kazi, uhuru, vazi unalotaka"

Mkuu wa mahakama ya Iran, Gholamhossein Mohseni Ajeei, ameashiria kuwa mataifa ya kigeni yanahusika na kampeni hiyo, akiyaagiza mashirika ya kijasusi kutafuta "mikono nyuma ya pazia uchi".

Rais Ebrahim Raisi pia ameahidi kukabiliana na "kukuza ufisadi uliopangwa katika jamii ya Kiislamu", akimaanisha moja kwa moja kwenye kampeni hiyo. Lakini wanawake wengi wameazimia kuendelea na maandamano yao licha ya vitisho hivyo.

"Unaweza kutukamata, lakini huwezi kusimamisha kampeni yetu," alisema mwanamke mmoja kwenye video iliyowekwa kwenye mtandao wa kijamii. "Hatuna cha kupoteza. Tulipoteza uhuru wetu miaka iliyopita, na tunadai urejeshwe."