Kwanini ndege ya kijeshi ya Nigeria iliivamia Burkina Faso, Traore kujibu mapigo?

Chanzo cha picha, NAF
Siku ya Jumatatu jioni, muungano wa Sahelian AES (Muungano wa Mataifa ya Sahel), unaojumuisha Burkina Faso, Mali na Niger, ulitoa taarifa kulaani kile ilichoeleza kama ukiukaji haramu wa anga yake uliofanywa na ndege ya kijeshi ya Nigeria.
Imeripotiwa kuwa ndege ya kijeshi ya Nigeria C-130 ilitua siku ya Jumatatu katika mji wa Bobo Dioulasso nchini Burkina Faso.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na AES, hatua ya ndege ya Nigeria ilikiuka kanuni za kimataifa na inachukuliwa kuwa "ukiukaji wa uhuru wake".
Muda mfupi baadaye, hata hivyo, mamlaka ya Nigeria ilitoa taarifa yao wenyewe, ikidai kwamba "kufeli kwa mitambo kumeilazimisha ndege kutua Burkina Faso".
Tangazo hili linakuja siku moja baada ya Nigeria kutangaza kuwa imetuma kikosi nchini Benin, ambako ndege yake ilikuwa imezuia jaribio la mapinduzi.
Uhusiano kati ya nchi za Sahel (Niger, Mali na Burkina Faso) umekuwa mbaya tangu mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea katika nchi hizi.
Juhudi zote za Nigeria na jumuiya ya maendeleo ya Afrika Magharibi kuona nchi hizi zikirejea katika utawala wa kidemokrasia hadi sasa zimeambulia patupu.
Hali hii ilipelekea nchi husika kutangaza kujitoa kutoka ECOWAS na kuunda kambi ya AES Sahel.
Hili ndilo lililochochea taarifa iliyochapishwa na nchi za Saheli baada ya kutua kwa ndege ya kijeshi ya Nigeria huko Burkina Faso, ambayo ilizua uvumi kwamba mzozo kati ya pande hizo mbili unaweza kuwa sababu.
"Tuko katika hali ya hatari" - Burkina Faso
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Taarifa ya nchi za ECOWAS imefichua kuwa uchunguzi wa mamlaka ya Burkinabe ulithibitisha kuwa ndege hiyo ya Nigeria C130 iliingia nchini bila kibali na ilikuwa imebeba watu 11 wakiwemo wafanyakazi wawili na wanajeshi tisa.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burkina Faso, Emile Zerbo, alisisitiza zaidi kwamba ndege hiyo ilikiuka sheria za anga ya nchi yake kwa kuruka bila idhini.
AES ilieleza tukio hilo kuwa ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa na kusema kwamba uwezo wote wa ulinzi wa anga umewekwa katika hali ya tahadhari, kwa idhini ya kukamata ndege yoyote iliyothubutu kuingia bila kibali.
Shirika hilo lilionya kuwa litachukua hatua dhidi ya ndege yoyote inayokiuka anga ya nchi katika eneo hilo bila kibali, kwa kuitungua.
Kauli hii inajiri siku chache baada ya Nigeria kuthibitisha kuwa imetuma ndege za kivita na wanajeshi kusaidia serikali ya Benin kuzima jaribio la mapinduzi nchini humo.
Nchi za ESA, ambazo ni Burkina Faso, Mali na Niger, ambazo zimeondoka ECOWAS, zinaweza kuwa na wasiwasi hasa kuhusu hatua mpya za kiusalama katika kanda, hasa kwa vile ECOWAS hapo awali ilitishia kuingilia kijeshi nchini Niger kufuatia mapinduzi ya 2023.
Nchi hizi tatu, chini ya utawala wa kijeshi, zinakabiliwa na mzozo wa muda mrefu wa usalama ambao umewasumbua kwa miaka mingi.
Kwa nini ndege hii ilitua Burkina Faso?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka ya Nigeria imesema kuwa ndege ya kijeshi ya NAF C-130 iliyotua kwa dharura nchini Burkina Faso ilikuwa katika safari ya kusafirisha mizigo kuelekea Ureno ilipolazimika kutua kutokana na hitilafu ya mitambo.
Katika taarifa, Jeshi la Wanahewa la Nigeria (NAF) lilisema kuwa ndege hiyo ilipaa kutoka Lagos, lakini marubani waligundua tatizo la kiufundi ambalo liliwalazimu kutua kwa dharura katika uwanja wa ndege wa Bobo-Dioulasso, ulio karibu zaidi.
Taarifa hiyo inabainisha: "Wanajeshi wetu wako salama na wako salama na walipokelewa kwa heshima na mamlaka ya Burkina Faso."
"Maandalizi yanaendelea kutekeleza majukumu waliyokabidhiwa. Jeshi hilo linashukuru kwa msaada walioupata na tunawahakikishia wananchi kuwa litaendelea kuheshimu itifaki za kiutendaji na hatua za kiusalama, sambamba na kuhakikisha ustawi wa wanajeshi wake katika utendaji wa kazi za ulinzi wa taifa," ilisema taarifa hiyo.
Kwa nini habari hii ni tofauti ?
Taarifa iliyotolewa na mamlaka ya Nigeria inatofautiana na ile ya serikali ya kijeshi ya Burkina Faso na shirika la AES linalodai kuwa ndege hiyo ya Nigeria iliingia katika anga ya nchi hiyo bila kibali, tukio lililopelekea kukamatwa kwa wanajeshi hao na kukamatwa kwa ndege hiyo nchini humo.
ESA ilielezea tukio hilo kama "ukiukaji wa anga yake na uhuru wa nchi wanachama wake." Ilisema kuwa kutua huko kumefanywa kwa kupuuza sheria ya kimataifa ya usafiri wa anga.
Kukamatwa kwa wanajeshi hao wa Nigeria na kukamatwa kwa ndege hiyo kunaonyesha jinsi AES inavyotaka kuthibitisha mamlaka yake juu ya anga katika utaratibu mpya inaojaribu kuanzisha.
Sasa kwa vile ESA imeamuru nchi wanachama wake kuangusha ndege yoyote ambayo inakiuka sheria zake, kile ambacho kingezingatiwa kuwa ukiukaji wa kawaida wa kiufundi kinaweza kuzidisha mzozo mkubwa.
Kwa Nigeria, hali hii inaweza kutatiza uhusiano wake na majirani zake wa Saheli, kuvuruga usafiri wa anga wa kikanda na kuathiri jukumu lake katika mapambano dhidi ya ugaidi.
Lockheed C-130 Hercules ni nini?
Jeshi la Anga la Nigeria lina ndege ya Lockheed C-130 Hercules, ambayo huitumia kusafirisha vifaa vya kijeshi au wanajeshi.
Hii ni mojawapo ya ndege muhimu zaidi za jeshi, kuwezesha usafirishaji wa zana za kijeshi au za kibinadamu, au askari, ndani na nje ya Nigeria.
C-130 Hercules ni ndege ya kijeshi yenye injini nne ya muundo wa Marekani, iliyoundwa ili iweze kutua na kupaa kutoka uwanjani, hata ikiwa si uwanja wa ndege uliotayarishwa mahususi.
Mbali na kusafirisha mizigo, ndege hii inaweza kutumika kwa ajili ya misheni nyingine, kama vile vita vya angani, kujaza mafuta ndani ya ndege za kivita, utafutaji na uokoaji, na utafiti wa kisayansi.
Hii ndio ndege ambayo nchi nyingi hutegemea kusafirisha zana za kijeshi kote ulimwenguni.












