Wataalamu wasema usambazaji chakula Gaza unaimarika lakini 100,000 bado wako katika 'hali mbaya'
Chanzo cha picha, Reuters
Wataalamu wanaoungwa mkono na Umoja wa
Mataifa wanasema kumekuwa na maboresho katika lishe na usambazaji wa chakula
huko Gaza tangu kusitisha mapigano, lakini watu 100,000 bado wamekabiliana na "hali
mbaya" katika kipindi cha mwezi uliopita.
Mnamo Agosti, Taasisi inayoshughulikia ualama
wa chakula (IPC) ambayo inafuatilia na kuainisha changamoto zinazohusiana na
njaa duniani ilisema kwamba watu nusu milioni - karibu robo ya idadi ya watu wa
Gaza - waliishi katika maeneo yanayokumbwa na njaa.
Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya
kibinadamu yameweza kuongeza chakula kinachoingia Gaza tangu kusitisha mapigano
kati ya Israel na Hamas mwezi Oktoba.
Wizara ya mambo ya nje ya Israeli ilisema
ripoti ya IPC "ilipotoshwa kimakusudi" na "haiakisi ukweli
katika Ukanda wa Gaza".
Uhuru wa Ukraine na Poland unawezesha uhuru kote Ulaya Mashariki – Zelensky
Chanzo cha picha, EPA
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amekuwa
Warsaw leo akimtembelea rais mpya wa Poland, Karol Nawrocki.
Anasema safari hiyo "inafungua hatua
mpya, yenye maana zaidi" ya mahusiano kati ya nchi hizo.
"Mahusiano si kati ya majirani tu,
bali kati ya sehemu mbili za Ulaya ambazo bila hivyo kusingekuwa na uhuru na
usalama wa kuaminika katika sehemu yetu yote ya Ulaya," anaandika kwenye
chapisho lake katika mtandao wa X.
Anasema alijadili usalama wa Ulaya na
Nawrocki, pamoja na vita nchini Ukraine.
"Uhuru wa Ukraine na uhuru wa Poland
ndio msingi unaowezesha kila taifa katika sehemu yetu ya Ulaya kuishi kwa uhuru
- bila utawala wa Moscow," Zelensky anasema.
"Ndiyo maana ni muhimu tushirikiane,
tusaidiane, na kuratibu juhudi zetu za kutetea Ulaya na mataifa yetu."
Madai ya Putin kuhusu uwanja wa vita "hayana uthibitisho wa ukweli - Mkuu wa jeshi la Uingereza
Maelezo ya picha, Sir Richard Knighton asema mafanikio ya Urusi katika uwanja wa vita ni ya polepole
Putin alieleza alipokuwa akianza mkutano
wake na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yanayodaiwa na Urusi katika uwanja
wa vita, akidai kwamba vikosi vya Ukraine vilikuwa vikirudishwa nyuma katika
mstari mzima wa mbele na havikupata "mafanikio yoyote".
Mkuu wa jeshi la Ulinzi la Uingereza
anasema madai ya Urusi ya kuchukua maeneo makubwa ya Mashariki mwa Ukraine ni
"upuuzi".
Sir Richard Knighton amerejea hivi karibuni
kutoka kutembelea wanajeshi wa Ukraine karibu na mstari wa mbele.
Akizungumza na BBC huko Kyiv, anasema
maendeleo ya vikosi vya Urusi yamekuwa ya taratibu.
“Nimeona takwimu
zinazoonyesha hali halisi ilivyo na Ukraine inaendelea kupigana kwa nguvu dhidi
ya uchokozi wa Urusi na inaendelea kusababisha hasara kubwa, kwa hivyo madai
ambayo Putin anasema hayathibitishwi na ukweli uliopo kwenye eneo la mapambano,”
Knighton anasema.
Shambulio la nyuki laua wanafunzi wawili, na kujeruhi nchini Ghana
Chanzo cha picha, Meha Kumar/ Save the Elephants
Familia mbili zinaomboleza kufiwa na watoto
wao katika shambulio la nyuki Kusini mashariki mwa Ghana siku ya Jumatano.
Watoto wawili walio chini ya umri wa miaka
10 waliuawa na wengine kujeruhiwa baada ya kundi la nyuki kuteremka kwenye
shule ya msingi ya Evangelical Presbyterian katika wilaya ya Anloga katika mkoa
wa Volta, walipokuwa wakijiandaa kwa likizo.
Inaaminika nyuki hao walichokozwa baada ya watoto
hao kurusha mawe kwenye mzinga wao
uliokuwa mtini walipokuwa wakicheza mpira wa miguu.
Mwalimu Mkuu Thywill Deynu aliambia vyombo
vya habari nchini humo "nyuki waliwashambulia wanafunzi wa chekechea
zaidi, kwa sababu hawakuweza kutoroka kujiokoa."
"Tuliita huduma ya zimamoto kutoka
wilaya ya Anloga kudhibiti hali hiyo," Citinewsroom ilinukuu.
Maafisa wa afya katika hospitali ya
serikali ya Manispaa ya Keta wanasema kati ya wanafunzi wanne waliokimbilia
kituoni, wawili kati yao walipoteza maisha.
"Tuliangalia hali ya wale
waliofikishwa kwenye kitengo chetu cha dharura na baada ya kufanyiwa upasuaji, wawili walikuwa
mahututi," Dkt. Fiifi Agyemang, afisa wa matibabu hospitalini alisema.
Aliongeza "mmoja wa watoto hayuko
hatarini sasa na tulimtoa mtoto mwingine ambaye alikuwa na nafuu Alhamisi."
Mama wa mmoja wa marehemu (mtoto wa miaka
minne) Mawuko Kumeko alishtuka na kuhuzunika alisema "Sijawahi kupata
maumivu ya aina hii, ninawezaje kupona?"
"Nilimpeleka mtoto wangu shuleni na
kuondoka kwenda sokoni na ndugu yake mdogo lakini nikarudi kusikia mwanangu
ameshambuliwa na nyuki."
Familia nyingine iliyopoteza binti yao wa
miaka tisa tayari inajiandaa kuzika.
"Kuumwa na nyuki kwa kawaida
husababisha hali inayoitwa kitaalamu anaphylaxis hasa mtu anapokuwa na
mzio," mtaalamu wa matibabu Dkt. Andrews Baha aliiambia BBC.
Hili ni shambulio la tatu la nyuki
kurekodiwa katika wiki moja kote Ghana.
Mnamo Desemba 13, nyuki walimshambulia na
kumuua mkulima huko Kusini-mashariki mwa Ghana katika wilaya ya Akatsi
Kaskazini.
Viongozi wa Magharibi wanaifanya Urusi kuwa adui - Putin
Chanzo cha picha, Reuters
Mhariri wa BBC jijini Moscow, Steve
Rosenberg, amemuuliza rais Vladimir Putin swali katika mkutano wa kila mwaka wa
waandishi wa habari wa rais wa Urusi.
Je, unaandaa mustakabali gani kwa Urusi na
raia wake? Rosenberg anauliza. Je, kutakuwa na operesheni mpya maalum za
kijeshi?
Putin anatoa jibu kwa kina, ambapo anatetea
mfumo wa kisiasa wa Urusi, anaibua kesi ya hivi karibuni ya "upotoshaji wa
taarifa", na anarejelea suala la Donald Trump dhidi ya BBC.
Kiongozi huyo wa Urusi pia anawashutumu
viongozi wa magharibi kwa "hila chafu", na anasema kwamba nchi
wanachama wa Nato zinaendelea na hili kupitia taarifa kwamba zinajiandaa kukabiliana
na Urusi.
"Je, kweli tutashambulia Ulaya? Huu ni
upuuzi," anaongeza. "Wanaunda taswira ya uadui na wanaifanya Urusi
kuwa adui."
Anaendelea kusema kwamba Urusi iko tayari kushirikiana
na nchi kama Marekani na Uingereza "lakini kwa usawa" kwa
"heshima inayostahili" kwa kila mmoja.
Polisi wasema mshukiwa wa ufyatuaji risasi wa Chuo Kikuu cha Brown apatikana amekufa
Chanzo cha picha, Providence Police/Handout via Reuters
Mshukiwa wa shambulio la risasi la wiki
iliyopita katika Chuo Kikuu cha Brown amepatikana amekufa katika huko
Salem, New Hampshire kufuatia msako wa siku sita ulioendeshwa katika majimbo kadhaa nchini Marekani, polisi
wanasema.
Walimtambua mshukiwa huyo kama Claudio
Neves Valente, 48, raia wa Ureno ambaye alisoma katika chuo kikuu huko
Providence, Rhode Island, takriban miaka 25 iliyopita.
Mkuu wa polisi wa Providence Oscar Perez
alisema ushahidi wa video na vielelezo kutoka kwa umma viliwaongoza wachunguzi
hadi eneo la kukodisha gari ambapo walipata jina la mshukiwa na kumfananisha na
mtu waliomlenga.
Maafisa walisema pia wanaamini Valente
alimuua profesa wa Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts (MIT) siku mbili
baada ya shambulio la risasi la Desemba 13 dhidi ya Brown.
Nigeria yaiomba radhi Burkina Faso baada ya ndege yake ya kijeshi kuingia bila idhini, na wanajeshi 11 kuzuiliwa
Chanzo cha picha, Nigeria’s foreign affairs ministry
Waziri wa masuala ya
kigeni wa Nigeria, Yusuf Tuggar, ameomba radhi rasmi kwa Burkina Faso kufuatia
kuingia bila idhini kwa ndege ya kijeshi ya Nigeria katika anga ya Burkina
Faso, tukio lililosababisha kuzuiliwa kwa wanajeshi 11 wa Nigeria.
Msemaji wa Tuggar
aliambia BBC kuwa wanajeshi hao waliokuwa wakizuiliwa wameachiwa huru na
wanatarajiwa kurejea Nigeria, ingawa hakufafanua ni lini.
Kwa mujibu wa Jeshi la
anga la Nigeria, ndege hiyo ilikuwa ikielekea Ureno ilipopata hitilafu ya
kiufundi na kulazimika kutua Burkina Faso.
Kutua huko bila idhini
kulisababisha mvutano wa kidiplomasia na muungano wa nchi za Sahel (AES),
unaojumuisha Burkina Faso pamoja na majirani zake Mali na Niger.
Katika taarifa yake,
AES ilielezea tukio hilo kama “kitendo kisicho cha kirafiki” na kusema kuwa
majeshi ya anga ya nchi wanachama yamewekwa katika hali ya tahadhari ya juu
kabisa na yameruhusiwa “kuangamiza ndege yoyote” itakayobainika Kwenda kinyume cha anga ya shirikisho hilo.
Nchi tatu wanachama wa
AES, ambazo zote zinaongozwa na serikali za kijeshi, zimejiondoa katika jumuiya
ya kikanda ya Afrika Magharibi, Ecowas, na zimeanza kuimarisha uhusiano wao na
Urusi, huku wanachama wengi wa Ecowas wakiendelea kuwa washirika wa mataifa ya magharibi.
Tuggar aliongoza
ujumbe wa ngazi ya juu kwenda katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou,
siku ya Jumatano, kujadili tukio hilo na kiongozi wa kijeshi, Ibrahim Traoré.
Putin aonyesha kutokuwa tayari kufanya maridhiano kuhusu vita vya Ukraine
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Rais Putin akiwa katik amkutano na waandishi wa habari
Mkutano na waandishi
wa habari wa Rais Vladimir Putin umeanza kwa hoja zilezile anazotumia mara kwa
mara kuhalalisha vita dhidi ya Ukraine.
Ametaja tena kile anachokiita “mapinduzi” ya
mwaka 2014, yaliyomwondoa madarakani rais mwenye mwelekeo wa Urusi, Viktor
Yanukovych, na kuishutumu Ukraine kwa madai ya “kuchochea vita”.
Kwa mujibu wa rais Putin,
matukio hayo ndiyo chanzo cha hali ya sasa ya mgogoro.
Putin pia amesema kuwa
Ukraine “inakataa kumaliza mgogoro huu kwa njia za amani” na haiko tayari
kujadili masuala ya mipaka au kutoa ardhi.
“Chanzo kilichosababisha mgogoro huu lazima kishughulikiwe”, akionesha tena
kutokuwa tayari kufanya maridhiano.
Kauli hii inaashiria msimamo wa Urusi
kwamba sababu ilizotaja ndizo zilizochangia uvamizi wa kijeshi
mwaka 2022.
Rais huyo wa Urusi anafanya mkutano wake wa mwisho wa mwaka kwa njia ya simu na waandishi wa habari.
Tukio la mwaka huu litakuwa na mseto wa mambo ambapo Putin atajibu maswali ya waandishi wa habari, pamoja na maswali
yaliyowasilishwa na umma kwa ujumla katika wiki za hivi karibuni.
Kremlin imesema karibu
maswali milioni tatu yalitumwa katika ofisi ya rais Putin na kwamba yote yameshughulikiwa
kwa karibu.
BBC imepiga kambi
katika ukumbi ambapo tukio hilo litafanyika karibu na Kremlin.
Wafanyakazi wengi wa
televisheni za nchini Urusi wanaonekana
wakifanya matangazo ya moja kwa moja.
Kwa Vladimir Putin
inatoa nafasi ya kutangaza mtazamo wake kwa
ulimwengu na kujipambanua kama baba wa taifa anayetatua matatizo ya Warusi
(zaidi ya watu milioni mbili wametuma maswali kwa kiongozi wa
Kremlin).
Vurugu zazuka Bangladesh baada ya kifo cha kiongozi wa maandamano ya vijana
Chanzo cha picha, Getty Images
Vurugu zimezuka nchini Bangladesh kufuatia kifo cha Sharif Osman Hadi, kiongozi maarufu wa harakati za vijana zilizomtoa madarakani Waziri Mkuu wa zamani, Sheikh Hasina.
Hadi alipigwa risasi na washambuliaji waliovaa barakoa alipokuwa akitoka msikitini mjini Dhaka wiki iliyopita na alifariki kutokana na majeraha Alhamisi ya Desemba 19,2025 akiendelea kupata matibabu Singapore.
Shambulio hilo lilitokea siku moja baada ya mamlaka za Bangladesh kutangaza tarehe ya uchaguzi wa kwanza tangu mapinduzi ya 2024, ambapo Hadi alikuwa anapanga kushiriki kama mgombea huru.
Baada ya kusambaa kwa habari za kifo chake, mamia ya wafuasi wake walikusanyika katika uwanja mjini mji mkuu kuandamana.
Baadaye, waandamanaji waliharibu ofisi za magazeti maarufu ya Bangladeshi, The Daily Star na Prothom Alo, huku jengo moja likiwashwa moto.
Afisa mmoja wa polisi alisema: “Mamia ya watu wamekusanyika hapa na kufanya shambulio hilo.”
Vikosi vya usalama vilitumwa eneo hilo, huku wafanyakazi wa zima moto wakiokoa waandishi wa habari waliokuwa wamefungwa ndani ya jengo.
Hadi, mwenye umri wa miaka 32, alikuwa kiongozi mkuu wa kundi la maandamano ya wanafunzi la Inqilab Mancha na alikuwa mkosoaji makini wa India, ambako Hasina bado yupo uhamishoni kwa hiari yake.
Vyama vya kisiasa vya Bangladesh vimeomboleza kifo chake na kuwataka wanasiasa wa mpito kuwaleta wahalifu mahakamani.
Mshindi wa tuzo ya Nobel, Muhammad Yunus, ambaye anaongoza serikali ya mpito, alieleza kifo cha Hadi kuwa “pungufu isiyoweza kurekebishwa kwa taifa.” Aliongeza: “Maendeleo ya nchi kuelekea demokrasia hayawezi kusitishwa kwa hofu, hadaa au damu.”
Serikali ya mpito ilitangaza Jumamosi kama siku ya maombolezo ya kitaifa.
Yunus pia alisema shambulio hilo lilikuwa limepangwa mapema na lengo la wahalifu lilikuwa kuharibu uchaguzi.
Alisisitiza kuwa vurugu yoyote inayolenga kuvuruga uchaguzi haitakubalika na kwamba tukio hilo ni tatizo linalotia wasi wasi katika siasa za nchi. Uchunguzi unaendelea na baadhi ya watu wamekamatwa kuhusiana na shambulio hilo.
Hasina alikimbilia India mnamo 5 Agosti mwaka jana, kufuatia wiki za maandamano yaliyoongozwa na wanafunzi, ikimalizia utawala wa miaka 15 wa kidikteta.
Mnamo Novemba, alihukumiwa kifo kwa uhalifu dhidi ya binadamu baada ya kupatikana na hatia ya kuruhusu nguvu za kikatili kutumika dhidi ya waandamanaji, kati yao 1,400 wakifariki wakati wa machafuko.
'Kuna uwezekano Mwezi umeundwa kwa jibini kuliko kometi kuwa chombo cha Aliens'- Wanasayansi
Nyota aina ya Kimondo yaani Comet ambayo ni kitu cha tatu kinachojulikana kati ya nyota kuingia kwenye mfumo wa sayari inakaribia zaidi Dunia.
3I- Atlas iligunduliwa kwa mara ya kwanza mnamo Julai mwaka huu na tangu wakati huo imetoa mkia unaong'aa wa vumbi na gesi ilivyokuwa ikipashwa na Jua.
Wanasayansi wanasema hakuna ushahidi kuwa ni kitu chochote zaidi ya kimondo, licha ya nadharia maarufu kwamba ni uchunguzi uliotumwa na wageni yani aliens.
Wanaastronomia wanachunguza kitu hicho cha miaka bilioni nane ili kujifunza zaidi kuhusu historia ya galaksi yetu kabla ya kutoweka.
Hata kwa karibu zaidi, bado iko zaidi ya kilomita milioni mia mbili na sabini kutoka kwa Dunia.
Trump na wapatanishi kukutana kujadili awamu ya pili ya kumaliza vita Gaza
Chanzo cha picha, Khames Alrefi/Anadolu via Getty Images
Rais wa Marekani, Donald Trump, na mwakilishi wake maalumu, Steve Wittkopf, watakutana Ijumaa ya Desemba 19, 2025 na maafisa wa Qatar, Misri na Uturuki huko Miami, Florida, kujadili hatua ya pili ya makubaliano ya kumaliza vita katika Ukanda wa Gaza.
Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani, alisema mkutano huo utaandaa mpango kamili wa kuhamia hatua ya pili ya makubaliano na kuunda utawala wa kiraia wa Palestina haraka iwezekanavyo.
Akiwa Washington, Al Thani alisema amekubaliana na Katibu wa Jimbo la Marekani, Marco Rubio, kuongeza juhudi kufanikisha hatua hiyo, kwa kuwa hali ya sasa inahatarisha makubaliano kila siku.
Hali ya kibinadamu Ukanda wa Ghaza inazidi kuwa mbaya kutokana na baridi kali.
Wizara ya Afya inayosimamiwa na Hamas ilitangaza kifo cha mtoto wa mwezi mmoja, Saeed Asaad Abdeen, kutokana na baridi kali katika eneo la Al-Mawasi, magharibi mwa Khan Younis. Idadi ya vifo kutokana na baridi na mabadiliko ya hali ya hewa imefikia 13.
Kina mama wanaonyonyesha wanakabiliwa na hali mbaya, wakiwa hawana blanketi wala sehemu salama za kuwakinga watoto wao wachanga. Mama mmoja aliiambia BBC: “Mtoto wangu alizaliwa miezi mitano iliyopita na tulianza kwa njaa.
Tuliteseka kwa kukosa nepi na maziwa ya kopo, na leo baridi inatuathiri mimi na mtoto wangu… Hana nguo za kujikinga na tuaingiwa na baridi ndani ya hema letu.”
Rais Trump atia saini agizo la kupunguza vikwazo vya bangi Marekani
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Majimbokadhaa ya Marekani yanaruhusu bangi kutumika kwa madhumuni fulani ya matibabu, na katika majimbo 24 inaruhusiwa kwa matumizi ya burudani.
Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini amri kuu ya kuainisha tena bangi kama dawa isiyo hatari sana.
Rais Trump alisema: “Sijataka kutumia, lakini wengi wanataka na wanahitaji.
”Aliongeza kuwa dawa zilizodhibitiwa zina hatari na utafiti wa majaribio haumvutii.
Agizo hilo linaamuru Wakili Mkuu kuharakisha mchakato wa kuainisha upya bangi.
Ikiwa litatekelezwa, mmea huu wenye athari za akili utaorodheshwa pamoja na dawa za kawaida za maumivu, ketamine na testosterone kama dawa isiyo hatari sana.
Hatua hiyo ni mabadiliko makubwa zaidi katika udhibiti wa bangi katika zaidi ya miaka hamsini nchini Marekani, ila serikali kuu haijahalalisha dawa hiyo kwa matumizi ya burudani.
Agizo linaiainisha upya bangi kutoka kiwango cha kwanza hadi cha tatu ambapo dawa zawa viwango hivyo zinadhibitiwa kwa matumizi halali ya matibabu. Rais Trump alisema hilo litaruhusu utafiti zaidi kuhusu dawa hiyo.
Majimbo mengi ya Marekani tayari yamehalalisha bangi.Kiongozi wa Democratic katika Seneti, Chuck Schumer, alikubaliana na hatua hiyo, huku baadhi ya wanasheria wa chama cha Republican cha Trump wakilaumu uamuzi huo.
Mapendekezo yatahitajika kupitiwa upya na Utawala wa Utekelezaji wa Dawa za Kulevya.
Australia yatangaza mpango wa kununua silaha kufuatia shambulio la Bondi
Chanzo cha picha, Getty Images
Australia imetangaza mpango wa kununua silaha kutoka kwa raia baada ya shambulio la ufukwe wa Bondi, tukio baya zaidi la ufyatuaji risasi wa halaiki nchini humo katika miongo kadhaa.
Mpango huo ni mkubwa zaidi tangu mauaji ya Port Arthur mwaka 1996, ambapo watu 35 waliuawa na baadaye Australia ikaweka sheria kali za kudhibiti silaha.
Watu 15 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa Jumapili, baada ya washambuliaji wawili wanaodaiwa kuhamasishwa na itikadi ya Islamic State kufyatua risasi katika tamasha la Wayahudi lililofanyika katika ufuo maarufu wa Bondi.
Polisi wamesema shambulio hilo, ambalo limetangazwa kuwa la kigaidi, lilitekelezwa na baba na mwanawe.
Naveed Akram, mwenye umri wa miaka 24, ameshtakiwa kwa makosa 59, yakiwemo mashtaka 15 ya mauaji na kosa la kutekeleza kitendo cha kigaidi.
Baba yake, Sajid, aliuawa wakati wa tukio hilo.
Siku moja baada ya shambulio, baraza la mawaziri la kitaifa lilikubaliana kukaza zaidi sheria za umiliki wa silaha.
Waziri Mkuu Anthony Albanese alisema kwa sasa kuna zaidi ya silaha milioni nne nchini Australia, idadi iliyo kubwa kuliko ilivyokuwapo mwaka 1996.
Alisema mmoja wa washambuliaji alikuwa na leseni halali ya silaha na alimiliki bunduki sita, jambo lililoibua maswali kuhusu sababu ya mtu anayeishi katika vitongoji vya jiji kuwa na silaha nyingi kiasi hicho.
Kamishna wa Polisi wa Shirikisho, Krissy Barrett, alisema mpango wa kununua silaha ni hatua muhimu katika kupunguza idadi ya silaha mikononi mwa raia.
Mpango huo utanunua silaha zisizohitajika, zilizopigwa marufuku na silaha haramu, kwa ufadhili wa pamoja kati ya serikali ya shirikisho na majimbo.
Serikali inatarajia kukusanya na kuharibu mamia ya maelfu ya silaha. Pia kumekubaliwa kuweka kikomo cha idadi ya silaha anazoweza kumiliki mtu mmoja, kudhibiti utoaji wa leseni, kuainisha aina za silaha zinazoruhusiwa kisheria, na kufanya uraia wa Australia kuwa sharti la kupata leseni ya silaha.
Hatua za kuanzisha daftari la kitaifa la silaha zitaongezwa kasi, huku wasimamizi wa silaha wakipewa taarifa bora za kijasusi kuhusu uhalifu.
Polisi wa New South Wales wamesema wanaume saba waliokuwa wakishukiwa kwa misimamo mikali wataachiliwa, lakini wataendelea kufuatiliwa.
Polisi hawajathibitisha kuwepo kwa uhusiano wa moja kwa moja kati yao na shambulio la ufukwe wa Bondi, ingawa eneo hilo lilikuwa miongoni mwa maeneo waliyopanga kutembelea.
Kamishna wa Polisi wa NSW, Mal Lanyon, alisema ingawa tishio halikujulikana wazi, uwezekano wa tukio la vurugu ulikuwa mkubwa kiasi kwamba polisi hawakuwa tayari kuhatarisha usalama wa umma.
EU yaamua kukopa fedha kusaidia Ukraine badala ya kutumia mali za Urusi
Chanzo cha picha, EPA
Umoja wa Ulaya umebadilisha mkakati wa kusaidia Ukraine kwa kuamua kukopa fedha kwa pamoja badala ya kutumia mali za Urusi zilizozuiwa kutumika.
Viongozi wa EU walikubaliana Ijumaa kutoa msaada wa euro bilioni 90 kwa Ukraine katika kipindi cha mwaka 2026 hadi 2027 ili kusaidia ulinzi wake dhidi ya Urusi.
Fedha hizo zitapatikana kupitia mikopo kutoka masoko ya mitaji, ikidhaminiwa na bajeti ya Umoja wa Ulaya.
Makubaliano hayo hayatawalazimisha Hungary, Slovakia na Jamhuri ya Czech kushiriki katika ufadhili huo, kwani nchi hizo hazikuwa tayari kuchangia msaada kwa Ukraine.
Hata hivyo, EU itaendelea kujadili mpango wa mkopo utakaotegemea mali za benki kuu ya Urusi zilizozuiwa kutumika.
Mkopo huo utalipwa na Ukraine pale itakapopokea fidia ya vita kutoka Urusi.
Hadi wakati huo, mali za Urusi zitaendelea kuzuiwa, na EU itabaki na haki ya kuzitumia kulipa mkopo endapo italazimika.
Wanadiplomasia wamesema uamuzi huu unahakikisha Ukraine inapata ufadhili wa uhakika kwa kipindi cha miaka miwili ijayo.
Awali, viongozi wa EU walijaribu kutumia mali za Urusi zilizozuiwa kutumika moja kwa moja, lakini mpango huo ulionekana kuwa mgumu kiteknolojia na kisiasa.
Changamoto kubwa ilikuwa ni kuilinda Ubelgiji, ambako mali nyingi za Urusi barani Ulaya zimehifadhiwa, dhidi ya hatari za kifedha na kisheria zinazoweza kutokea iwapo Urusi ingerudisha mashambulizi ya kiuchumi au kisheria.
Kwa hatua hii, EU inalenga kuhakikisha msaada kwa Ukraine unaendelea bila kucheleweshwa, huku ikiepuka migogoro ya kisheria na kisiasa ndani ya umoja huo.
Haya yanajiri baada ya Rais wa Urusi Vladimir Putin kusema Urusi itatwaa maeneo zaidi nchini Ukraine kwa kutumia nguvu iwapo Kyiv na wanasiasa wa Ulaya aliowaita "nguruwe" hawatakubali mapendekezo ya Marekani kuhusu makubaliano ya amani.
Akizungumza katika mkutano wa kila mwaka wa masuala ya ulinzi ya Urusi, Putin alisema nchi yake inapiga hatua katika pande zote za vita na akasisitiza kuwa Urusi itatimiza malengo yake ama kwa njia ya diplomasia au kwa nguvu, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump unaendesha mazungumzo tofauti na Moscow na Kyiv, pamoja na viongozi wa Ulaya, kuhusu mapendekezo ya kumaliza vita nchini Ukraine.
Hata hivyo, hadi sasa hakujapatikana makubaliano.
Kyiv na washirika wake wa Ulaya wana wasiwasi kuhusu madai ya Urusi yanayosisitiza kuyatwaa maeneo ya Ukraine.