Jinsi njaa inavyotumika kama silaha ya vita duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
Mbali ya risasi na silaha, rasilimali muhimu kama vile chakula, maji, na dawa zimetumika kama silaha za vita katika historia ya binadamu, na kulingana na wataalam na mashirika ya kimataifa, njaa kwa sasa pia inatumika kama silaha ya vita huko Gaza.
Huku jeshi la Israel likizingira na kulipua kwa mabomu, vifo vinavyotokana na utapiamlo vinaripotiwa kila siku, hasa miongoni mwa watoto. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaelezea maeneo ya usambazaji wa misaada kama maeneo ya "mitego ya mauaji ya kusikitisha."
Katika siku mbili zilizopita, takriban watu 33, wengi wao wakiwa watoto, wamekufa kwa njaa katika Ukanda wa Gaza, kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza.
Ripoti za hivi punde za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa uhaba wa chakula katika Ukanda wa Gaza umefikia Kiwango cha 5 (janga), kiwango cha juu zaidi katika viwango vinavyoonyesha hatari ya njaa, kulingana na Mgawanyo wa Viwango vya Usalama wa Chakula (IPC).
Kulingana na tathmini ya Mei 2025, watu 470,000 - sawa na robo ya wakazi wa Gaza, wanakabiliwa na njaa kali, huku wengine waliobaki wanaishi bila chakula cha kutosha.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limekanusha siku ya Jumanne kwamba kuna njaa baa huko Gaza, lakini limeonya kuwa njaa inaweza kutokea hivi karibuni.
Jeshi hilo linasema Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa ya misaada yana hifadhi ya malori 950 ya misaada kwenye mpaka wa Gaza ambayo hayasafirishwi kwenda katika eneo hilo.
Kulingana na IDF, kukataa kwa mashirika hayo kuleta msaada katika Ukanda huo kunatokana na kutokukubaliana kwao na vigezo vinavyotumiwa na Israel kuamua ni bidhaa gani zinaweza kuingia Gaza na zipi haziwezi, limeripoti gazeti la Jerusalem Post.
Hali ya Gaza

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mujibu wa ripoti kutoka mashirika ya kimataifa kama vile OCHA, UNRWA, Oxfam, na Save the Children, zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa Gaza wanakabiliwa na hali ngumu ya kuishi, na ripoti hizo hizo zinaonya maelfu ya watoto wako katika hatari ya kufa kutokana na ukosefu wa chakula na dawa.
Katika kitabu chake Mass Famine: Its History and Future, mtafiti Alex de Waal anaelezea, baa la njaa katika mazingira ya sasa mara nyingi hutokana na maamuzi ya kimakusudi ya kisiasa na kijeshi, badala ya uhaba wa chakula asilia.
Israel inadai lengo lake si kuwadhibu raia, bali ni kuizuia Hamas kutumia rasilimali (kama vile chakula na dawa) kwa madhumuni ya kijeshi au kama kificho kwa "shughuli za kigaidi."
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amekanusha kuwepo kwa sera ya makusudi ya kuwaweka na njaa wakaazi wa Gaza, akiita shutuma hizo ni "uongo na kashfa," akisisitiza kuwa lengo ni kuzuia rasilimali kuwafikia Hamas, sio kuwaadhibu wakazi.
Kwa upande wa jeshi la Israel, pamoja na kukiri kuwepo kwa vikwazo vikali vya kuingia kwa misaada hiyo, lilikanusha kuwepo kwa amri za kuwapiga risasi raia wanaotafuta chakula.
Njaa, haswa inayopangwa, ni uhalifu chini ya sheria ya kimataifa na njaa inaainishwa kama njia ya mauaji ya kimbari katika mikataba ya kimataifa.
Maana ya Njaa na sheria za kimataifa

Chanzo cha picha, Getty Images
"Njaa" katika vita ni kuwanyima raia chakula na maji makusudi, kwa lengo la kuwashinikiza wale wanaohusika - iwe mashirika au serikali - kujisalimisha kisiasa au kijeshi.
Njaa ni pamoja na uharibifu wa mazao na mifugo, kama ilivyotokea katika vita vya Sudan na Ukraine ya Usovieti (Holodomor), kuzuia au kuchelewesha kuingia kwa misaada ya kibinadamu, kama ilivyoandikwa na Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa katika ripoti zake kuhusu Gaza na Tigray (2023-2024).
Pia kushambulia miundombinu ya kilimo na vyanzo vya maji, na kuweka vikwazo vya kiuchumi, kuwafurusha wakulima au au kuwanyang'anya ardhi wakulima.
Uchunguzi wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) unaonyesha kuwa njaa inakuwa silaha ya vita pale inapotumiwa kusababisha madhara ya moja kwa moja kwa raia kwa kuvuruga mfumo wa upatikanaji wa chakula.
Chini ya sheria za kimataifa, kuna mikataba kadhaa ambayo inakataza matumizi ya njaa kama silaha ya vita na sheria hizo zinaonya dhidi ya kuitumia njaa katika vita vyovyote:
- Mikataba ya Geneva ya 1949 na Itifaki ya Ziada 1 ya 1977: inakataza matumizi ya njaa kama silaha ya vita, haswa dhidi ya raia.
- Mkataba wa Roma wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, 1998: "Njaa ya makusudi kwa raia ni uhalifu wa kivita ikiwa inatekelezwa kwa kuwanyima mahitaji muhimu kwa maisha yao."
- Azimio la Baraza la Usalama la 2417, 2018: Linalaani matumizi ya njaa kama silaha na linaunganisha migogoro ya kivita, ukosefu wa chakula na hatari ya njaa.
Ugumu wa mashtaka

Chanzo cha picha, Getty Images
Sheria ya kimataifa inaharamisha utumiaji wa njaa kama silaha ya vita na inachukulia kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, haswa pale raia wanaponyimwa chakula na dawa, kama inavyotokea leo huko Gaza, anasema wakili Hassan Al-Hattab.
Licha ya uwazi wa sheria, uwajibikaji unabaki kuwa nadra. Hadi sasa, hakuna mtu katika historia ya hivi karibuni ambaye amewajibishwa kwa kutumia njaa kama silaha ya vita, licha ya kesi za awali nchini Sudan, Syria, na Tigray.
Ingawa sheria za kimataifa zinaharamisha matumizi ya njaa kama silaha ya vita na ni kosa la jinai, mashitaka ya aina hii dhidi ya wahalifu bado ni nadra kwa sababu kadhaa:
Ugumu wa kuthibitisha. Moja ya changamoto kuu katika aina hizi za kesi ni kuonyesha nia ya makusudi ya kusababisha njaa, hasa katika mazingira magumu ambapo mambo ya kijeshi, kiuchumi, na mazingira yanaingiliana.
Kama mtafiti Alex de Waal anavyosema, njaa mara nyingi ni "uhalifu bila wahalifu wanaoonekana," na hivyo kuifanya kuwa vigumu kwa wahalifu kuwajibishwa.
Jambo jingine ni matatizo ya kisiasa na ukosefu wa uangalizi wa kimataifa. Mara nyingi, wale wanaohusika ni washirika wa mataifa makubwam na kuifanya iwe vigumu kuwawajibisha.
Mifano ya njaa

Chanzo cha picha, MINISTRY
"Katika historia, njaa imekuwa ikitumika kama silaha ya 'kuwatiisha watu,' kama ilivyokuwa katika Mlima Lebanoni wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, katika mauaji ya Waarmenia na Waashuri, na baadaye huko Bosnia na Herzegovina.
“Katika hali zote, lengo lilikuwa kuvunja muundo wa kijamii na kuwalazimisha watu kuhama au kujisalimisha," anasema mwanahistoria Essam Khalifam.
Njaa ya "Holodomor" huko Ukraine (1932-1933), ilitumika kama silaha ya kisiasa ya kutawala watu na kubadilisha idadi ya watu, kulingana na mwanahistoria wa Marekani, Timothy Snyder katika kitabu chake Bloodlands of Europe. Mamilioni ya watu walikufa kwa sababu ya sera hiyo, na sio majanga ya asili.
Kuzingirwa kwa Leningrad, Urusi (1941-1944). Wanazi waliuzingira mji huo kwa siku 870, na karibu raia milioni moja walikufa kwa njaa katika jaribio la kuwaangamiza watu bila mapigano.
Sarajevo, Bosnia (1992–1996). Vikosi vya Serbia viliuzingira mji huo na kuzuia chakula na umeme, na kusababisha njaa na vifo vya maelfu ya watu licha ya misaada ya kimataifa.
Ghouta na Madaya, Syria (2013-2016). Vikosi vya utawala huo wa zamani viliweka mzingiro uliosababisha vifo vya raia kutokana na njaa na picha za kutisha za watoto waliodhoofika.
Yemen (2015 hadi sasa). Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilifunga bandari na kuzuia chakula, na kusababisha mzozo unaoelezewa kuwa "mbaya zaidi ulimwenguni," huku zaidi ya watu milioni 17 wakikabiliwa na njaa.
Tigray, Ethiopia (2020-2022). Ripoti zinathibitisha kuwa serikali ya Ethiopia ilitumia njaa kama silaha ya vita kwa kuwanyima chakula na dawa katika eneo hilo lililozingirwa.















