Umoja wa Mataifa: Njaa huko Gaza inaweza kuwa uhalifu wa kivita

Noora Mohammed hawezi kupata matibabu anayohitaji katika hospitali ya Gaza
Maelezo ya picha, Noora Mohammed hawezi kupata matibabu anayohitaji katika hospitali ya Gaza

Baada ya miezi kadhaa ya maonyo, ripoti ya hivi karibuni iliyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ilitoa ushahidi wa takwimu kwamba maafa ya kibinadamu huko Gaza yanageuka kuwa njaa inayosababishwa na mwanadamu.

Imeongeza shinikizo kwa Israel kutekeleza majukumu yake ya kisheria ya kuwalinda raia wa Palestina, na kuruhusu usambazaji wa kutosha wa misaada ya kibinadamu kuwafikia watu wanaohitaji.

Afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu, Volker Türk, alisema katika mahojiano na BBC kwamba Israel inalaumiwa sana, na kwamba kuna kesi "inayowezekana" kwamba Israeli ilikuwa ikitumia njaa kama silaha ya vita huko Gaza.

Bw Türk, ambaye ni kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu, alisema ikiwa nia itathibitishwa, hiyo itakuwa sawa na uhalifu wa kivita.

Waziri wa uchumi wa Israel, Nir Barkat, mwanasiasa mkuu katika chama cha Likud cha Benjamin Netanyahu, alipuuzilia mbali maonyo ya Bw Türk na kusema "upuuzi mtupu - jambo lisilo na maana kabisa kusema".

Sawa na mawaziri wenzake, Bw Barkat alisisitiza kuwa Israel ilikuwa inaruhusu misaada yote inayotolewa na Marekani na dunia nzima. Israel inasema Umoja wa Mataifa unashindwa kusambaza chochote kilichosalia mara baada ya Hamas kujisaidia.

Lakini msururu mrefu wa malori yaliyosheheni vifaa vya msaada vinavyohitajika sana katika Ukanda wa Gaza yako upande wa Misri wa mpaka na Rafah. Yanaweza tu kuingia Gaza kupitia Israeli, baada ya ukaguzi tata na wa ukiritimba.

Kutokuwepo kwa vifaa vya kutosha kumeilazimisha Jordan, na sasa nchi nyingine ikiwa ni pamoja na Marekani na Uingereza, kurusha misaada kutoka angani - njia ya chini kabisa ya kusambaza misaada ya kibinadamu.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wapalestina waliokuwa ardhini wakipigania kupata sehemu wamekufa maji walipokuwa wakijaribu kuogelea hadi kwenye godoro ambazo zimetua baharini, au wamepondwa baada ya miamvuli kufeli.

Jeshi la Wanamaji la Marekani pia linatuma flotilla ya uhandisi katika Bahari ya Atlantiki ili kujenga badari ya muda ya kutua misaada kwa njia ya bahari.

Hakuna lolote kati ya hayo lingekuwa la lazima kama Israel ingetoa ufikiaji kamili wa barabara hadi Gaza na kuharakisha uwasilishaji wa vifaa vya msaada kupitia bandari ya kisasa ya kontena huko Ashdod, umbali wa nusu saa tu kwa gari kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

Katika mahojiano kutoka Geneva, Bw Türk alisema ushahidi umeibuka kuwa Israel inapunguza kasi au inazuia kuwasilisha misaada.

Bw Türk alilaani mashambulizi ya Hamas dhidi ya raia na wanajeshi wa Israel tarehe 7 Oktoba, ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji na utekaji nyara. Lakini pia alisema kwamba hakuna upande wowote katika vita unapaswa kukwepa uwajibikaji kwa matendo yake, ikiwa ni pamoja na jaribio lolote la kuzuia misaada kutoka kwa watu wanaohitaji huko Gaza.

Wasiwasi kuhusu maafa ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza uliongezeka wiki iliyopita kwa kutolewa kwa maoni yaliyoandikwa kwa kiasi pamoja na mfululizo wa ramani, chati na takwimu. Ilisababisha maonyo zaidi kutoka kwa washirika wa Israeli kwamba inapaswa kubadilisha jinsi inavyopigana vita dhidi ya Hamas ili kuwaepusha raia na kifo kutokana na milipuko mikali au njaa.

Utafiti huo ni ripoti ya hivi punde zaidi kutoka kwa mtandao unaoheshimika wa kimataifa, the Integrated Food Security Phase Classification, au IPC.. Inazipa serikali, Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada data ya kisiasa ili kupima ukubwa wa njaa. Kichwa cha habari kwenye ripoti hiyo kilikuwa cha kusikitisha - "Ukanda wa Gaza: Njaa inakaribia kwani watu milioni 1.1, nusu ya Gaza, wanakumbwa na janga la uhaba wa chakula."

Data yake ilieleza jinsi njaa inaweza kuja wakati wowote katika muda wa wiki nane au zaidi kama hakutakuwa na usitishaji mapigano na misaada haitamiminika katika Ukanda wa Gaza.

Wazazi wa Kipalestina ambao walifanikiwa kuwaleta watoto wagonjwa na wenye njaa katika mojawapo ya hospitali chache ambazo bado zinaendelea kufanya kazi huko Gaza baada ya mashambulizi ya Israel hawakulazimika kusubiri takwimu. Kwa majuma na miezi, walipokuwa wakihangaika kuwalisha, wameona watoto wao wakipungua.

Gaza si mahali pa kuwa mgonjwa. Msichana mmoja mdogo katika hospitali hiyo, aliyefikiwa na mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Kipalestina anayefanya kazi na BBC, alikuwa amelala juu ya kitanda akiwa na fahamu.

Msichana huyo, Noora Mohammed, ana uvimbe wa mapafu na ini, hali ambayo inaweza kuwa mbaya hata wakati wa amani. Katika miezi ya njaa tangu vita kuanza, na bila huduma ya matibabu sahihi, afya yake inazorota kwa kasi.

"Binti yangu hawezi kusonga," mama yake alisema. "Ana upungufu wa damu, analala kila wakati, na hakuna chakula."

Angalau Noora alifika hospitalini. Wengi wa zaidi ya wakazi milioni moja wa Gaza wanaofikiriwa kuwa na uhitaji mkubwa hawatakuwa na uwezo huo.

Baadhi ya watoto wana ishara ya kukabiliwa na utapiamlo mkali
Maelezo ya picha, Baadhi ya watoto wana ishara ya kukabiliwa na utapiamlo mkali

Israel imepuuza azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa mara moja kwa mapigano. Nir Barkat, Waziri wa Uchumi wa Israel, alisema kuwa hakuna kitakachoruhusiwa kuzuwia lengo la vita vya Israel la kuisambaratisha Hamas KABISA na kuwaokoa mateka waliochukuliwa tarehe 7 Oktoba.

Washirika duniani kote waliunga mkono lengo la Israel. Nilipowaeleza marafiki wengi wa Israel, kuanzia na Rais wa Marekani Joe Biden, hawakupenda jinsi Israeli walivyokuwa wakipigana vita, Bw Barkat alisema.

"Hiyo ni ngumu. Tutamaliza vita. Tutafanya kila tuwezalo kuwaua magaidi wa Hamas na kupunguza uharibifu mwingine kadri tuwezavyo," alisema.

"Kwa heshima zote, tunapambana na uovu, na tunatarajia ulimwengu utusaidie kupambana na uovu hadi tutakapomaliza Hamas kwenye ramani."

Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu alijibu kwa ufupi ukosoaji mkali kutoka kwa Israeli.

"Kitu pekee ninachoweza kuwaambia ni kwamba kuna maafikiano ya kimataifa yanayoibuka, na huenda hayakuwepo hapo awali, lakini ni wazi yapo sasa, ikiwa ni pamoja na azimio la Baraza la Usalama la wiki hii, kuhusu hali ya kibinadamu," Bw Türk alisema.

"Hali ya haki za binadamu ni ya kusikitisha sana kwamba usitishaji mapigano wa mara moja unahitajika. Hilo ndilo jibu langu."