Moja kwa moja, Waganda waonywa dhidi ya kutumia VPN kufikia mitandao ya kijamii iliyodhibitiwa
Muunganisho wa intaneti umerejeshwa kote nchini Uganda baada ya kuzimwa kwa zaidi ya siku tatu.
Muhtasari
- Waganda waonywa dhidi ya kutumia VPN kufikia mitandao ya kijamii iliyodhibitiwa
- Trump kuhudhuria mkutano na viongozi wa Ulaya wiki hii
- Jeshi la Syria ladhibiti eneo kubwa zaidi la mafuta nchini humo
- Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Khamenei, amtuhumu Trump kwa machafuko
- Waangalizi wa EAC wapongeza amani aatika kchaguzi wa Uganda 2026, waibua changamoto
- 36 wauawa katika shambulio la droni Amhara, Ethiopia
- Tishio la ushuru wa Trump juu ya Greenland 'halikubaliki' - viongozi wa Ulaya
- Mtandao wa intaneti warejeshwa Uganda
Moja kwa moja
Na Ambia Hirsi
Wanamgambo 40 wauawa kasakazi mashariki mwa Nigeria

Chanzo cha picha, AFP
Mamlaka nchini Nigeria zimesema kuwa zaidi ya wanamgambo 40 wa Kiislamu wanauawa katika shambulizi la angani lililofanywa katika jimbo la Borno, ili kutibua mashambulio yaliyokuwa yamepangwa katika maeneo ya jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Jeshi la Wanahewa la Nigeria (NAF) limesema operesheni hizo zilifanyika tarehe 15 na 16 Januari katika maeneo ya Azir na Musarram chini ya Operesheni Hadin Kai, baada ya taarifa za kijasusi kuonyesha wapiganaji wanaohusishwa na Boko Haram na wanamgambo wa ISWAP) wakijiandaa kwa mashambulizi.
"Masaa ya mapema ya tarehe 16 Januari 2026, ndege za NAF zilijibu haraka vitendo vya uhasama vya kigaidi huko Azir," jeshi la anga lilisema.
Siku moja kabla, shambulio la Musarram katika ardhioevu ya Tumbuns, ambapo takriban mitumbwi 10 iliyokuwa imebeba zaidi ya watu 40 wanaoshukiwa kuwa wapiganaji ilionekana ikijiandaa kushambulia mhimili ya Baga na Fish Dam.
Mkuu wa Wanajeshi wa anga, Sunday Kelvin Aneke alinukuliwa katika taarifa akisema kwamba shambulio hilo lilionyesha utayari wa jeshi la anga kuchukua hatua wakati wanajeshi wakikabiliwa na tishio.
"Tutaendelea kuwanyima magaidi uwezo wa kujipanga upya, kufanya ujanja au kufanya mashambulizi," alisema.
Waganda waonywa dhidi ya kutumia VPN kufikia mitandao ya kijamii iliyodhibitiwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Mkuu wa Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC) amewaonya watumiaji wa mtandao dhidi ya kutumia mitandao ya kibinafsi ya kibinafsi, au VPN, kufikia majukwaa ya mitandao ya kijamii yaliyodhibitiwa.
Muunganisho wa intaneti umerejeshwa kote nchini Uganda usiku wa kuamkia leo baada ya kuzimwa kwa zaidi ya siku tatu kote nchini.
UCC inasema kukatizwa kwa mtandao wa inataneti kulikuwa muhimu ili kudumisha usalama wa taifa wakati wa uchaguzi.
Hata hivyo, ufikiaji wa majukwaa ya mitandao ya kijamii bado umedhibitiwa lakini inaweza kufikiwa kupitia VPN.
Baadhi ya waendeshaji wa mtandao wa simu wamewaambia wateja kwamba ingawa wameidhinishwa kurejesha huduma za mawasiliano, ufikiaji wa mitandao ya kijamii bado imedhibitiwa.
"Ndugu mteja wa Airtel, tumeagizwa na UCC kurejesha huduma za mtandao, bila kujumuisha mitandao ya kijamii na programu za ujumbe," Airtel ilisema katika ujumbe mfupi uliotumwa kwa wateja wake.
Mkurugenzi mtendaji wa UCC Nyombi Thembo sasa amewaonya watumiaji wanaojaribu kukwepa vikwazo hivyo kwamba watachukuliwa hatua, hasa ikiwa majukwaa hayo yatatumiwa kuvunja sheria.
"Kuna watu wanaofikiri wanaweza kukwepa maagizo haya kwa kutumia VPN," alisema.
"Nataka kukuambia kwamba sasa tuna uwezo wa kubaini - hasa ikiwa njia hiyo ya mkato inatumiwa kuvunja sheria - kwa kulenga kifaa chako moja kwa moja" alionya Thembo.
Hatua hizi za kuminya mitandao ya kijamii pia zilitumika wakati wa uchaguzi wa 2021.
Kiongozi wa upinzani Bobi Wine anasema kuzimwa kwa intaneti kulifanya iwe vigumu kuthibitisha matokeo ya uchaguzi yaliyomuidhinisha Rais Yoweri Museveni kuwa mshindi.
Maelezo zaidi:
Trump kuhudhuria mkutano na viongozi wa Ulaya wiki hii

Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Donald Trump atahutubia Kongamano la Kimataifa la Kiuchumi mjini Davos, Uswizi Trump atahudhuria Kongamano la Kimataifa la Kiuchumi la Duniani mjini Davos, Uswizi, baadaye wiki hii - pamoja na viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi na Finland.
Wataunganishwa na wanachama wa Nato kama vile Canada, Uhispania na Ubelgiji.
Kongamano hilo linakuja baada ya Trump kutishia kuziongezea ushuru baadhi ya nchi za Ulaya kufuatia mvutano uliozuka juu ya umiliki wa Greenland.
Kongamano la Davos ni tukio la kila mwaka ambapo wanasiasa mashuhuri hushirikiana na wakuu wa tasnia kujadili "maswala ya kimataifa".
Trump atahutubia kongamano hilo Jumatano wiki hii ambapo mada ya mwaka huu ni "tunawezaje kushirikiana katika ulimwengu unaozidi unaoshindaniwa?".
Bila shaka viongozi kama Emmanuel Macron, Friedrich Merz na Ursula von der Leyen watafuatilia kwa karibu atakachosema Trump kuhusu mada hiyo.
Jeshi la Syria ladhibiti eneo kubwa zaidi la mafuta nchini humo

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Jeshi la Syria lililiingia katika vitongoji vya ndani vya mji wa Deir Hafeer baada ya Vikosi vya Syria Democratic kuondoka kufuatia operesheni ya kijeshi iliyoanza magharibi mwa Mto Euphrates, mashariki mwa Aleppo, Syria, Januari 17, 2026. Vikosi vya jeshi la Syria vimeudhibiti kikamilifu mji wa Tabqa ulioko kaskazini mwa nchi hiyo, kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Syria Noureddine al-Baba.
Baba aliieleza BBC kuwa msako unaendelea katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha kuwa hakuna vitisho vyovyote vya usalama.
Vyanzo vitatu vya usalama vilisema mapema leo kwamba vikosi vya Syria vinavyopambana na vikosi vinavyoongozwa na Wakurdi vimechukua udhibiti wa eneo la mafuta la al-Omar, ambalo ni kubwa zaidi nchini Syria, pamoja na eneo la gesi la Conoco mashariki mwa nchi hiyo.
Vikosi vya Syrian Dempcratic vilijiondoa Jumapili kutoka kwa kisima cha mafuta cha al-Omar, eneo kubwa zaidi la mafuta nchini Syria, lililoko mashariki mwa mkoa wa Deir ez-Zor, kulingana na Shirika la uangalizi wa haki la Syrian Observatory.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Rami Abdel Rahman, aliiambia shirika la habari la AFP, "Vikosi vya Syria democratic viliondoka alfajiri ya Jumapili kutoka maeneo yote yaliyokuwa chini ya udhibiti wao mashariki mwa mashambani ya Deir Ezzor, ikiwa ni pamoja na maeneo ya mafuta ya Al-Omar na Al-Tanek," huku jimbo la Deir Ezzor likitoa wito kwa "raia kutunza mali za umma, huduma za umma kama vile hospitali."
Soma zaidi:
Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Khamenei, amtuhumu Trump kwa machafuko

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Ayatollah Ali Khamenei Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, siku ya Jumamosi alimlaumu Rais wa Marekani Donald Trump kwa wiki kadhaa za maandamano ambayo makundi ya kutetea haki za binadamu yanasema yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 3,000.
“Tunamchukulia rais wa Marekani kuwa mhalifu kwa vifo, uharibifu na kashfa alizolisababishia taifa la Iran,” Khamenei alinukuliwa akisema na vyombo vya habari vya serikali ya Iran.
Trump amekuwa akitishia mara kwa mara kuingilia kati, ikiwemo kutishia kuchukua “hatua kali sana” endapo Iran ingewanyonga waandamanaji.
Hata hivyo, siku ya Ijumaa, kupitia ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, Trump aliwashukuru viongozi wa Tehran akisema walikuwa wamefuta mpango wa kunyonga watu. Iran ilikanusha madai hayo, ikisema “hakuna mpango wa kuwanyonga watu”.
Katika kauli zilizotafsiriwa kuwa jibu kwa Trump, Khamenei alisema: “Hatutaivuta nchi kwenye vita, lakini hatutawaacha wahalifu wa ndani au wa kimataifa waende bila kuadhibiwa,” kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.
Katika mahojiano na jarida la Politico siku ya Jumamosi, Trump alisema “ni wakati wa kutafuta uongozi mpya nchini Iran” na kutoa wito wa kumalizika kwa utawala wa miaka 37 wa Khamenei.
Vyombo vya habari vya serikali vimeripoti kukamatwa kwa maelfu ya watu waliodaiwa kuwa “wachochezi wa ghasia na magaidi” kote nchini, wakiwemo watu wanaohusishwa na makundi ya upinzani yaliyo nje ya nchi yanayotetea kuangushwa kwa Jamhuri ya Kiislamu.
Miongoni mwa waliokamatwa ni watu kadhaa waliotajwa na vyombo vya habari vya serikali ya Iran kama “vinara wa ghasia”, akiwemo mwanamke aliyetajwa kwa jina la Nazanin Baradaran, aliyekamatwa kufuatia kile kilichoelezwa kuwa “operesheni tata za kijasusi”.
Ripoti zilisema Baradaran alikuwa akitumia jina bandia Raha Parham kwa niaba ya Reza Pahlavi — mwana wa shah wa mwisho wa Iran aliye uhamishoni — na alidaiwa kuwa na jukumu la kuongoza maandalizi ya machafuko hayo.
Shirika la habari la Reuters limesema halikuweza kuthibitisha madai hayo wala utambulisho wake.
Pahlavi, ambaye amekuwa sura ya upinzani kwa muda mrefu, amejipambanua kama mgombea anayeweza kuongoza endapo utawala wa sasa utaanguka, na amesema atatafuta kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Iran na Israel iwapo atachukua nafasi ya uongozi nchini humo.
Soma pia:
Waangalizi wa EAC Wapongeza Amani Katika Uchaguzi wa Uganda 2026, Waibua Changamoto

Chanzo cha picha, reu
Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umepongeza Uganda kwa kuendesha Uchaguzi Mkuu wa Januari 2026 kwa amani, huku ukiibua changamoto kadhaa za kiufundi na kisheria zinazohitaji kushughulikiwa.
Katika taarifa ya awali, ujumbe huo ulisema uchaguzi uliendeshwa chini ya mfumo thabiti wa kikatiba na kisheria unaozingatia viwango vya kikanda na kimataifa vya kidemokrasia.
Waangalizi 58 wa EAC, wakiongozwa na Balozi Edda Mukabagwiza wa Rwanda, walipelekwa katika maeneo yote ya nchi na kushuhudia zoezi la kampeni, upigaji kura, kuhesabu na kujumlisha matokeo katika vituo 184 vya kupigia kura.
Kwa mujibu wa waangalizi, mazingira ya uchaguzi yalikuwa ya amani kwa ujumla, ingawa vituo vingi vilifunguliwa kwa kuchelewa hadi saa tatu kutokana na kuchelewa kwa vifaa vya uchaguzi na hitilafu za mitambo ya uthibitishaji wa wapiga kura.
Licha ya hali hiyo, upigaji kura uliendelea kwa utulivu na uwazi, huku maafisa wa uchaguzi na vyombo vya usalama wakionesha weledi. EAC ilisifu Tume ya Uchaguzi kwa maandalizi ya mapema, ikibainisha ongezeko la asilimia 17 ya wapiga kura waliosajiliwa ikilinganishwa na uchaguzi wa 2021, ambapo wanawake walichangia asilimia 53 ya wapiga kura.
Hata hivyo, ujumbe huo ulionyesha wasiwasi kuhusu idadi kubwa ya kura zilizoharibika na ukosefu wa takwimu zilizogawanywa kwa jinsia na umri wa wagombea.
Waangalizi pia walikosoa kusitishwa kwa huduma za intaneti siku ya uchaguzi, wakisema kulikwamisha upatikanaji wa taarifa na ufuatiliaji wa uchaguzi.
Ujumbe huo wa EAC umetoa wito wa marekebisho ya sheria za ufadhili wa kampeni, kuimarishwa kwa elimu ya mpiga kura na mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ndani ya vyama, pamoja na kuboreshwa kwa maandalizi ya kiufundi katika chaguzi zijazo.
Maelezo zaidi:
36 wauawa katika shambulio la droni Amhara, Ethiopia

Chanzo cha picha, Sehala Woreda Communication
Takriban watu 36 waliuawa na wengine 16 kujeruhiwa katika shambulio la ndege isiyo na rubani iliyolenga wanamgambo wa serikali katika eneo la Amhara nchini Ethiopia, mamlaka za mitaa na wakaazi waliiambia BBC.
Shambulio hilo lilitokea Alhamisi, Januari 15, 2025, katika kambi ya wanamgambo katika wilaya ya Sehala Seyemt katika eneo la Waghimira.
Maafisa wa wilaya walisema shabulio hilo lilitekelezwa wakati wanamgambo hao walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya mkutano na kiamsha kinywa mbele ya kambi hiyo.
Walioshuhudia waliripoti kuwa silaha zilizokuwa zimehifadhiwa mahali hapo ziliharibiwa pia, na kambi hiyo “ilichomwa moto.”
Kulingana na wakaazi, wanamgambo hao walikuwa wamewekwa kambini kuzuia wapiganaji wa Fano-ambao wamekuwa wakipigana na jeshi la serikali kwa zaidi ya miaka miwili tangu Aprili 2023-kuingia katika wilaya hiyo.
Siku ya shambulio, wapiganaji wa Fano waliripotiwa kujiandaa kushambulia wanamgambo wa eneo hilo, na kusababisha maafisa wa wilaya kuomba msaada kutoka kwa vikosi vya ulinzi vya kitaifa.
Pia unaweza kutazama:
Tishio la ushuru wa Trump juu ya Greenland 'halikubaliki' - viongozi wa Ulaya

Chanzo cha picha, reu
Maelezo ya picha, Waandamanaji huko Greenland waliandamana Jumamosi dhidi ya hatua yoyote ya Marekani kuchukua eneo hilo Tishio la Rais wa Marekani Donald Trump la kutoza ushuru mpya kwa washirika wanane wanaopinga pendekezo lake la kutwaa eneo la Greenland limekosolewa vikali na viongozi wa Ulaya.
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema hatua hiyo "ni haifai kabisa", huku Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiitaja kuwa "haikubaliki".
Maoni hayo yanakuja baada ya Trump kutangaza ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa kutoka Denmark, Norway, Sweden, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Uholanzi na Finland akisema itaanza kutekelezwa tarehe 1 Februari, lakini baadaye inaweza kupanda hadi 25% - na utadumu hadi makubaliano yafikiwe.
Trump anasisitiza kuwa eneo linalojitawala la Denmark ni muhimu kwa usalama wa Marekani na hajafutilia mbali uwezekano wa kuliteka kwa nguvu.
Umoja wa Ulaya umeitisha mkutano wa dharura mjini Brussels (16:00 GMT) leo Jumapili kufuatia vitisho vya Trump.
Mkutano huo utahusisha mabalozi kutoka nchi 27 za Umoja wa Ulaya, kulingana na shirika la habari la Reuters.
Siku ya Jumamosi maelfu ya watu waliandamana huko Greenland na Denmark wakipinga mapendekezo ya Marekani kuchukua mamlaka.
Soma sio:
Mtandao wa intaneti warejeshwa Uganda

Chanzo cha picha, Getty Images
Muunganisho wa intaneti umerejeshwa nchini Uganda saa chache baada ya Rais Yoweri Museveni kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu uliomalizika hivi punde.
Siku ya Jumanne (Januari 13), Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC) ilitangaza kuwa inasitisha huduma za mtandao kufuatia "pendekezo" kutoka kwa kamati ya kitaifa ya usalama.
UCC ilichukuwa hatua hiyo ili kuzuia usambazaji wa taarifa ghushi, wizi wa kura, pamoja na shinikizo la mtandaoni linaloweza kuchochea ghasia au vurugu.
Shirika la kutete haki za binadamu la Umoja wa Mataifa lilielezea hatua hiyo kama "kusumbua sana"
Hata hivyo, hatua za kuminya upatikanaji wa intaneti wakati wa chaguzi si jambo geni nchini Uganda.
Katika uchaguzi wa mwaka 2021, huduma za intaneti zilikatizwa kwa takribani wiki moja, hatua ambayo iliwaathiri zaidi ya watumiaji milioni 10 wa huduma hiyo.
Kurejeshwa kwa huduma za mtandao kunaweza kutafsiriwa kama ishara ya imani ndani ya vikosi vya usalama kwamba nchi imeepuka hali ya wasiwasi iliyoenea wakati wa uchaguzi, sawa na ilivyoshuhudiwa katika chaguzi zilizopita.
Hata hivyo,ghasia zinazohusiana na uchaguzi zimeripotiwa katika maeneo tofauti ya nchi, kama vile Mukono na Bwaise viungani mwa jiji la Kampala.
Ripoti zinadai makabiliano yalizuka kati ya vikosi vya usalama na wafuasi wa upinzani.
Muda mfupi baada ya Tume ya Uchaguzi kumtangaza Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi wa Alhamisi kwa asilimia 72, mpinzani wake mkuu Bobi Wine, ambaye alipata asilimia 25, alitoa taarifa kwa njia ya video kupinga matokeo hayo akiyataja kuwa ''feki''.
Ametoa wito kwa wafuasi wake kupinga matokeo hayo kwa kujitokeza na kuandamana kwa amani dhidi ya kile alichosema ni juhudi za kuhujumu mchakato wa kidemokrasia.
Maelezo zaidi:
Natumai hujambo
