Kwanini uchaguzi wa Uganda unafuatiliwa kwa ukaribu na Jumuiya ya Afrika Mashariki

g

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Mariam Mjahid
    • Nafasi, Mwandishi BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Kwa mtazamo wa kikatiba, uchaguzi wa Uganda unaofanyika Alhamisi ya leo, Januari 15, 2026, ni tukio la kitaifa.

Hata hivyo, katika uhalisia wa kisiasa na kiuchumi wa Afrika Mashariki, hakuna uchaguzi unaobaki ndani ya mipaka.

Sanduku la kura lipo Uganda, lakini uzito wa matokeo yake utahisiwa kwa kina zaidi Nairobi, Dar es Salaam na katika ukanda mzima wa Maziwa Makuu.

Rais Yoweri Museveni, aliyeingia madarakani mwaka 1986, anatafuta muhula mwingine ambao utausukuma utawala wake kuvuka miongo minne. Hili si shindano jipya katika siasa za Uganda; kilicho tofauti ni mazingira ya kikanda yanayofanya matokeo ya uchaguzi huu kuwa nyeti kuliko wakati mwingine wowote.

Lakini je, ni kwanini Ulimwengu unafuatilia kwa ukaribu uchaguzi wa Uganda hasa ikiwa ina idadi kubwa ya wapiga kura vijana?.... je, ni kutaka kujua ukomavu wa demokrasia, mtazamo wa vijana hasa kizazi cha Gen Z au hata ni hasa kwa kimaslahi zaidi ya kiuchumi?

G

Chanzo cha picha, AFP

Uchaguzi Uganda unawahusu majirani

''Kenya na Tanzania inafuatilia kwa ukaribu Uchaguzi wa Uganda wakitaka kuona kama demokrasia ambayo Rais wa sasa Yoweri Musevei amekuwa akijigamba kuwa ipo Uganda ni ya aina gani.'' anasema mchanganuzi wa kisiasa wa kimataifa Augustine Omondi.

Uchaguzi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki inaingia kwa taifa la pili, Kenya ikitarajiwa kufanya uchaguzi mkuu 2027, ambao siasa zake tayari zimeanza kutokota.

''Raia wa Afrika Mashariki wanataka kujua kama kuna nchi ambayo inaweza kuwa na ukomavu wa kideomkrasia kiasi ya kumuondoa rais aliyehudumu kwa miongo mitatu madarakani,'' Augustine aliongezea,

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Awali uganda imekuwa ikijiweka kama nchi ambayo inafanya uchaguzi wa haki na uwazi, hata hivyo Augustine anasema hili linaanza kutafsiriwa tofauti kutokana na yaliyojiri siku chache kabla ya uchaguzi wa leo Alhamisi.

''Juzi Jumatatu, Tume ya mawasiliano ya Uganda UCC iliminya intaneti nchi nzima japokuwa imejitetea kuwa ni kwa misingi ya usalama na kuzuia habari potofu.Lakini kwamisingi ya kisiasa kuminywa kwa intaneti ni jazanda tosha kuwa uchaguzi sio wa haki wala wazi kwani wagombea watajuaje mtiririko wa matokeo, Augustine anaiambia BBC Swahili.

Kwa Kenya, pia uchaguzi wa Uganda hauhusiani sana na maigizo ya ushindani wa kidemokrasia bali unagusa moja kwa moja maslahi ya msingi ya kiuchumi. Nchi hizi mbili zimefungamana kwa uhusiano wa kibiashara uliojengeka kwa miongo kadhaa.

Uganda ni soko kubwa zaidi la bidhaa za Kenya, likipokea bidhaa za viwandani, mafuta ya petroli, dawa, vyakula na huduma mbalimbali.

Msukosuko wowote wa kisiasa magharibi mwa mpaka wa Kenya husafiri haraka kupitia Ukanda wa Kaskazini, mhimili muhimu zaidi wa biashara katika Afrika Mashariki.

Istoshe, maelfu ya malori husafirisha mizigo kutoka badari ya Mombasa hadi Kampala. Na iwapo uchukuzi utatatizika hata kwa lisaa limoja, athari zake huenda zikaonekana mara moja kuanzia kupanda kwa gharama za usafirishaji, bima kuongezeka, na wafanyabiashara kukadiria hasara ambayo itasikika katika uchumi na mapato ya kitaifa.

Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Augustine Omondi, Uganda inapoyumba, mizani ya biashara ya Kenya huathirika.

''Uganda ni lango kuu la Kenya kuelekea Sudan Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, pamoja na masoko ya Rwanda na Burundi. Uchaguzi wenye utata au kipindi kirefu cha sintofahamu unaweza kudhoofisha azma ya Kenya kujijenga kama kitovu cha usafirishaji na uzalishaji wa kikanda''Augustine anaendelea kuiambia BBC.

Ikiwa ni nchi ambayo ina nguvu na Rais Ruto ana nguvu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki haijatoa tamko rasmi wala misimamo ya wazi.

Diplomasia na usalama wa kikanda

Zaidi ya biashara, kuna masuala nyeti ya usalama.

Kenya na Uganda hushirikiana kwa karibu katika kukabiliana na ugaidi na kubadilishana taarifa za kijasusi.

Uchaguzi unaozua mgogoro unaweza kuilazimisha Uganda kuelekeza nguvu zake ndani ya mipaka yake, hali inayoweza kupunguza uwezo wake wa kushiriki majukumu ya kikanda na kuongeza hatari za kiusalama, hasa katika magharibi mwa Kenya.

Kwa mtazamo wa Nairobi, Uganda iliyo tulivu si anasa ya kisiasa bali ni ngao ya kimkakati.

Hesabu hii ya kimkakati imewahi kusababisha maamuzi yenye utata.

Hivi karibuni, Kenya ilishirikiana na mamlaka za Uganda kumkamata na kumkabidhi kiongozi wa muda mrefu wa upinzani, Kizza Besigye, aliyekamatwa akiwa Nairobi. Tukio hilo lilidhihirisha ushirika wa kikanda uliyojengeka kwa muda mrefu: kutoingilia siasa za ndani kwa sauti, lakini kulinda maslahi ya taifa kwa vitendo.

''Kenya inalinda ushirikiano wa kibiashara na Uganda kwa kusalia kimya au kujibu kiupole hata pale Rais Museveni alipotangaza kuwa Kisiwa cha Migingo kinafaa kumilikiwa na Uganda, serikali ya Kenya haikujibu wazi, na hii ndio sababu kwanini inafuatilia kwa ukaribu uchaguzi bila kuingilia kinachoendelea'' anasema Augustine Omondi.

Ni hali ya kinaya: serikali hunyamaza kidiplomasia, lakini raia wake huzungumza kwa sauti kubwa mtandaoni.

Serikali ya Kenya, hata hivyo, imeendelea kushikilia ukimya wa kimkakati. Hakuna kauli rasmi kuhusu mwenendo wa uchaguzi wala maelekezo ya kidemokrasia. Kwa watunga sera, wafanyabiashara na wasafirishaji, kilicho hatarini kinajulikana bila kusemwa.

Wanatazama matokeo kwa jicho la tahadhari, si kwa misingi ya itikadi, bali kwa dalili za utulivu.

Tanzania pia inafuatilia, kwanini?

Athari za uchaguzi wa Uganda hazimalizii Kenya pekee.

Tanzania, nayo, ina maslahi makubwa katika matokeo ya kura hii. Ikiwa ni nchi ambayo ilifanya uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka jana uliokumbwa na utata na hadi kusababisha vifo vya vijana wengi waliokuwa wakitaka mabadiliko.Ilianza kufuatilia mchakato wa uchaguzi Uganda tangu mwaka jana.

Uganda ni mshirika muhimu wa Tanzania katika biashara ya dhahabu, mafuta yaliyosafishwa na mpunga.

Wakati huohuo, Tanzania ni lango kuu la bahari kwa Uganda isiyo na pwani, kupitia Bandari ya Dar es Salaam na miradi mikubwa ya kimkakati kama Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki (EACOP).

Kupitia Ukanda wa Kati, biashara kati ya nchi hizi mbili inatarajiwa kuongezeka kwa kasi, huku Uganda ikipata fursa ya kusafirisha mafuta ghafi kupitia Bandari ya Tanga.

Tanzania hunufaika kwa ada za usafirishaji na ukuaji wa miundombinu, huku Uganda ikipanua masoko na mapato yake ya kitaifa.

Kwa sasa, Tanzania imeipiku Kenya na kuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Uganda, hali inayoakisi mienendo inayobadilika ya biashara na ujumuishaji wa kiuchumi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Na kwa muktadha wa mitandaoni, Gen z wa Tanzania pia wanafuatilia kwa ukaribu kutaka kuona iwapo vijana wa Uganda watathubutu kuondoa kiongozi aliyehudumu kwa miongo mitatu kama rais.

Lakini Mchanganuzi anaeleza kuwa hilo huenda lisitokee.

''Ilikuwa rahisi kwa Gen z wa Tanzania na Kenya kupinga viongozi wao kwakuwa ilikuwa ni mara ya kwanza kwa viongozi hao kuingia debeni.

Lakini kwa Uganda hali ni tofauti kwani kiongozi wa sasa amehudumu tangu miaka ya themanini na haitakuwa rahisi kwao kuthubutu kupinga matokeo au hata kumuondoa madarakani kupitia sanduku ya kura'' anasema Augustine.

Sababu za Ulimwengu kufuatilia kura ya Uganda

Iwe wamevaa rangi ya manjano ya chama tawala au wamevaa rangi nyekundu ya chama kikuu cha upinzani, vijana ndio wanaongoza miongoni mwa wafuasi katika kampeni za uchaguzi nchini Uganda wakiwa ni zaidi ya asilimia 78 wako chini ya umri wa miaka 30 .

Na hili ndilo linavutia macho ya dunia kufuatilia ima kwa mitandao na hata kupitia asasi za kupigania haki za kibinadamu.

Ulimwengu una hamu kuona iwapo uanaharakati wa vijana mitandaoni kuhusu demokrasia Uganda utakuwa na athari yoyote katika matokeo ya uchaguzi kwani ni ni nchi ambayo imekuwa ikitawaliwa na viongozi walioingia madarakani miongo kadhaa iliyopita na hawajawahi kuondoka.

Na si hayo tu, ulimwengu pia unataka kujua ukomavu wa demokrasia.

Tunavyojua mchakato wa kabla ya uchaguzi huwa una nguvu na huwa na athari moja kwa moja ya matokeo ya uchaguzi. Na ili ujue uchaguzi ulikuwa wa haki, usawa na wazi kilichokuwa kikijiri kabla ya uchaguzi lazima kifuatiliwe.

Kabla ya Uchaguzi, mateso ya mgombea urais Bobi Wine, ambaye amekuwa mwiba mkubwa kwa Rais Yoweri Museveni, yamevutia hisia za dunia.

Mnamo, mwaka 2018 wanamuziki maarufu akiwemo Chris Martin wa Coldplay na Damon Albarn wa Gorillaz, walisaini ombi la kumtaka aachiliwe kutoka kizuizini.

Bobi Wine alikamatwa kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume cha sheria, lakini kesi hiyo ilionekana na wengi kuwa na msukumo wa kisiasa. Baadaye pia alikamatwa kwa tuhuma za uhaini, lakini hatimaye kesi zote hizo zilifutwa.

Katika kipindi cha kuelekea siku ya kupiga kura, Bobi Wine amekuwa akifanya kampeni kote nchini, mara nyingi akiwa amevaa koti la kujikinga na risasi pamoja na kofia ya chuma.

Picha na video zinaonyesha wafuasi wake wakiandamana na msafara wake, wakikabiliana na gesi ya kutoa machozi na mipigo ya maji iliyotumiwa na vikosi vya usalama.Hali ambayo haikuonekana kwa wagombea wengine 7 wanaotaka urais.

Licha ya hatari ya vurugu, wafuasi wake wanaendelea kuwa imara na wenye kujitolea, wakijaza mikutano ya kampeni bila kuyumbishwa.

Naye Bobi Wine hakati tamaa.

"Uchaguzi huu ni kuhusu ukombozi," anasema. "Ni kuhusu uhuru, ni kuhusu wananchi kudai na kutumia sauti zao. Tunawaomba watu wajitokeze na kuandamana kupitia sanduku la kura."

Dunia sasa, inataka kujua hatima yake ni ipi na iwapo ataingia madarakani atabadilisha nini?

Ubadilishanaji wa mamlaka

Uganda haijawahi kushuhudia uhamisho wa madaraka kwa amani tangu ipate uhuru.

Ukweli huu ni kivuli kinachotanda juu ya kila uchaguzi. Kupitia tawala tisa, mwisho wake umekuwa vurugu. Museveni mwenyewe aliingia madarakani kupitia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka mitano na kusababisha vifo vya zaidi ya nusu milioni ya watu.

Hata hivyo, serikali yake ya awali ilionekana kama nguzo ya uthabiti. Ilifungua milango ya mazungumzo ya kitaifa, ikaweka katiba yenye haki za msingi za kiraia, kisiasa, kijamii na kiuchumi, ikarejesha mali za jamii ya Wahindi, na ikatumia misaada na mikopo ya kimataifa kuanzisha huduma za ustawi kama elimu na afya kwa kiwango fulani.

Historia hii tata ndiyo inayofanya kila uchaguzi Uganda kuwa zaidi ya mchakato wa kidemokrasia; ni mtihani wa uthabiti wa taifa uanaofuatiliwa na raia kutoka nchi tofauti.

Kwa Kenya, Tanzania na majirani wengine, swali kuu si nani atashinda, bali kama Uganda itabaki tulivu. Katika uchumi wa kisiasa wa Afrika Mashariki, utulivu ni sarafu muhimu zaidi.

''Afrika Mashariki, siasa za ndani haziishii ndani ya mipaka ya taifa. Kura hupigwa kitaifa, lakini matokeo yake husambaa kikanda.'' Augustine anasema.