Uchaguzi Uganda 2026: UCC yatoa maelezo kuhusu kuminya intaneti
UCC ilieleza kuwa hatua ya kusitisha kwa muda huduma za intaneti ilichukuliwa ili kuzuia usambazaji wa habari potofu, wizi wa kura, pamoja na shinikizo la mtandaoni linaloweza kuchochea ghasia au vurugu.
Muhtasari
- Marekani yasimamisha kwa muda uchakatishaji wa Viza kwa raia wa nchi 75
- Trump asisitiza kuwa Marekani inahitaji Greenland kwa usalama wakati mazungumzo White House yakiendelea
- Amnesty International yakosoa vikali kuminywa intaneti kabla ya uchaguzi wa Uganda
- Marekani yapunguza idadi ya wafanyakazi katika kambi ya kijeshi ya Qatar, afisa aiambia CBS
- UCC yatoa maelezo kuhusu kuminya huduma za intaneti nchini Uganda
- Uchaguzi Uganda 2026: Usalama waimarishwa uchaguzi ukikaribia
- EU yagawanya msaada wa kifedha kwa Ukraine
- Trump awahimiza waandamanaji wa Iran kudhibiti taasisi za nchi
- Waendesha mashtaka wataka rais wa zamani wa Korea Kusini ahukumiwe kifo
- Meli ya mafuta iliyokamatwa na Marekani yaonekana Scotland
- Marekani kusitisha ulinzi wa kufukuzwa kwa Wasomali
- Kreni ya ujenzi yaanguka juu ya treni Thailand
- Trump aahidi 'kuchukua hatua kali' ikiwa Iran itawaua waandamanaji
- Mamia wa maafisa wa polisi wajitangaza kuwa wanachama wa Freemason Uingereza
- Mwaka jana ulikuwa mbaya zaidi kwa raia wa Ukraine tangu 2022, UN inasema
- Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Uganda adai kutishiwa maisha
- Zaidi ya watu 2,000 waripotiwa kuuawa katika maandamano ya Iran
Moja kwa moja
Asha Juma na Mariam Mjahid
Marekani yasimamisha kwa muda uchakatishaji wa Viza kwa raia wa nchi 75

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Ofisi ya Upelelezi wa Jinai katika jijini Nairobi inachunguza mamia ya malalamiko kuhusu mashirika yanayodai kuwatafutia watu ajira Ikulu ya Marekani imetangaza kuwa serikali ya nchi hiyo itasitisha kwa muda uchakataji wote wa viza za uhamiaji kwa raia wa mataifa sabini na tano.
Miongoni mwa nchi zilizoathiriwa na uamuzi huo ni Urusi, Iran, Afghanistan, pamoja na mataifa kadhaa ya Afrika.
Hatua hiyo pia inahusisha nchi zisizo za Afrika kama Thailand na Brazil.
Kwa mujibu wa waraka wa ndani wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, balozi zote za Marekani zimepewa maelekezo ya kusitisha utoaji wa viza huku taratibu za uchunguzi na uhakiki wa waombaji zikifanyiwa tathmini na mapitio mapya.
Hatua hii itaanza kutekelezwa wiki moja kuanzia leo, ingawa serikali ya Marekani haijaeleza ni kwa muda gani zuio hilo litaendelea.
Uamuzi huo unatekelezwa katika mazingira ambayo utawala wa Rais Donald Trump unaendelea kuimarisha sera kali za kudhibiti uhamiaji.
Mwishoni mwa mwaka jana, Trump aliwahi kueleza nia ya kusimamisha kabisa uhamiaji kutoka kile alichokiita “nchi za Dunia ya Tatu,” kauli iliyokuja kufuatia tukio la kupigwa risasi kwa mwanachama wa Kikosi cha Walinzi wa Taifa (National Guard) na raia wa Afghanistan.
Soma Zaidi:
Trump asisitiza kuwa Marekani inahitaji Greenland kwa usalama wakati mazungumzo White House yakiendelea

Chanzo cha picha, EPA/Bloomberg via Getty Images
Maelezo ya picha, Mkutano huo unafanyika katika Jengo la Ofisi ya Mtendaji wa Eisenhower, linaloonekana hapa karibu na upande wa Magharibi wa Ikulu ya White House Rais wa Marekani, Donald Trump, amesisitiza kuwa Marekani inaihitaji Greenland kwa ajili ya “usalama wa taifa,” akiongeza kuwa chochote kisichohusisha udhibiti wa Marekani juu ya eneo hilo ni “kisichokubalika.”
Kauli hiyo imetolewa wakati Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio, wakikutana na mawaziri wa mambo ya nje wa Denmark na Greenland katika Ikulu ya White House.
Madai ya Trump ya kuchukua udhibiti wa kisiwa hicho yamekataliwa na viongozi wa Greenland pamoja na Denmark, mwanachama wa NATO ambako Greenland ni eneo lenye mamlaka ya kujitawala kwa kiwango fulani.
Mataifa ya Ulaya yameeleza kuunga mkono kikamilifu mamlaka ya Denmark juu ya Greenland.
Wakati huo huo, jeshi la Denmark limesema linaongeza uwepo wake wa kijeshi nchini Greenland kwa “ushirikiano wa karibu na washirika wa NATO.”
Soma pia;
Amnesty International yakosoa vikali kuminywa intaneti kabla ya uchaguzi wa Uganda

Chanzo cha picha, Amnesty
Kufuatia uamuzi wa Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC) wa kusitisha kwa muda usiojulikana huduma za intaneti pamoja na baadhi ya huduma za simu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa kesho, Amnesty International imeeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu athari za hatua hiyo kwa haki za binadamu.
Akizungumza kwa niaba ya shirika hilo, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini wa Amnesty International, Tigere Chagutah, alisema kuwa ''kuzimwa kwa intaneti kwa muda usiojulikana ni shambulio la moja kwa moja dhidi ya haki ya uhuru wa kujieleza, haki inayojumuisha pia upatikanaji wa taarifa''.
Alibainisha kuwa hatua hiyo inatia hofu zaidi kwa kuwa inatekelezwa katika kipindi nyeti cha uchaguzi ambao tayari umezingirwa na ukandamizaji mkubwa, pamoja na msako usio na kikomo dhidi ya vyama vya upinzani na sauti za wakosoaji.
Chagutah alisisitiza kuwa ''kuzimwa kwa intaneti kwa jumla kunavuruga kwa kiasi kikubwa maisha ya wananchi, likiwemo uwezo wao wa kusafiri, kujipatia riziki na kupata taarifa muhimu kwa wakati. Aliongeza kuwa hatua kama hizo, kwa asili yake, hazilingani na viwango vya sheria za kimataifa za haki za binadamu na hazipaswi kamwe kutekelezwa katika jamii inayoheshimu haki na utawala wa sheria''.
Kwa mujibu wa Amnesty International, kukatwa kwa huduma za intaneti kwa kisingizio cha kuzuia habari potofu au kulinda usalama wa taifa ni ukiukaji wa haki za msingi, hasa katika wakati nyeti kama wa uchaguzi.
Hatua hiyo, ilielezwa, huzalisha ombwe la taarifa na “giza la kidijitali” linaloweza kutoa mwanya wa kufanyika kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu bila uangalizi wa umma.
Shirika hilo pia lilieleza wasiwasi kuhusu kukosekana kwa muda mahsusi wa kumalizika kwa zuio hilo, likisema hali hiyo ni ishara ya kutia wasiwasi zaidi.
Kutokana na hali hiyo, Amnesty International imetoa wito kwa mamlaka za Uganda kuondoa mara moja vikwazo vyote vinavyokwamisha upatikanaji wa intaneti na kurejesha huduma zote za simu zilizoathiriwa.
Siku ya Jumanne, Tume ya Mawasiliano ya Uganda ilitangaza kusitishwa kwa huduma za intaneti kuanzia saa kumi na mbili jioni kwa saa za nchini humo, ikieleza kuwa hatua hiyo itaendelea hadi itakapotolewa taarifa nyingine.
Siku iliyofuata, shirika la kimataifa la ufuatiliaji wa huduma za intaneti, NetBlocks, liliripoti kuzimwa kwa huduma hizo kwa kiwango kikubwa kote nchini.
Soma zaidi:
Marekani yapunguza idadi ya wafanyakazi katika kambi ya kijeshi ya Qatar, afisa aiambia CBS

Chanzo cha picha, TSGT Scott Reed, USAF
Marekani inapunguza idadi ya wafanyakazi wake katika kambi yake ya kijeshi ya Al-Udeid nchini Qatar, kwa mujibu wa mshirika wa BBC nchini Marekani, CBS News.
Maafisa wameeleza hatua hiyo kuwa ni “tahadhari ya kiusalama.” Katika taarifa yake, serikali ya Qatar imesema hatua hiyo inachukuliwa “kufuatia mvutano wa sasa katika eneo hilo.”
Hatua hiyo inakuja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kusema kuwa Marekani itachukua “hatua kali sana” dhidi ya Iran iwapo mamlaka zake zitatekeleza adhabu ya kifo kwa waandamanaji wanaopinga serikali.
Iran, kwa upande wake, imesema italipiza kisasi endapo itashambuliwa na Marekani.
Kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu, zaidi ya waandamanaji 2,400 wanaopinga serikali wameuawa katika msako mkali wa hivi karibuni uliofanywa na mamlaka za Iran.
Soma Pia:
UCC yatoa maelezo kuhusu kuminya huduma za intaneti nchini Uganda

Maelezo ya picha, Intaneti imeminywa nchini Uganda tangu jana Jumanne jioni Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC) imetoa ufafanuzi kuhusu uamuzi wa serikali wa kuminya huduma za intaneti nchini wakati wa uchaguzi mkuu, ikisema hatua hiyo imelenga kulinda amani, usalama na uadilifu wa mchakato wa uchaguzi.
Kupitia taarifa iliyotolewa kwenye mtandao wa kijamii wa X, UCC ilieleza kuwa hatua ya kusitisha kwa muda huduma za intaneti ilichukuliwa ili kuzuia usambazaji wa habari potofu, wizi wa kura, pamoja na shinikizo la mtandaoni linaloweza kuchochea ghasia au vurugu.
UCC ilisisitiza kuwa si taasisi zote zilizoathiriwa na hatua hiyo, ikibainisha kuwa taasisi za msingi ziliendelea kupata huduma za intaneti ili kuhakikisha majukumu muhimu ya kitaifa yanaendelea bila kuvurugika.
“Taasisi zinazotegemea intaneti lakini zisizo za msingi zitaendelea kukosa huduma ya intaneti katika kipindi hiki cha uchaguzi,” UCC iliandika katika taarifa yake.
Hata hivyo, tume hiyo imewahimiza wahudumu na wafanyabiashara wanaoamini kuwa huduma zao ni za kimsingi lakini wameathiriwa na kizuizi hicho, kuwasilisha maombi rasmi kwa maandishi kwa UCC ili yafanyiwe tathmini upya.
Kwa mujibu wa UCC, maombi hayo yatafanyiwa mapitio na kamati ya usalama ili kubaini kama huduma husika zinastahili kuruhusiwa kuendelea kutumia intaneti wakati wa kipindi cha uchaguzi.
Hata hivyo, hatua za kuminya upatikanaji wa intaneti wakati wa chaguzi si jambo geni nchini Uganda.
Katika uchaguzi wa mwaka 2021, kuzimwa kwa intaneti kwa takribani wiki moja kuliripotiwa kuambatana na vifo vya watu kadhaa, huku wapiga kura wakinyimwa taarifa muhimu za uchaguzi.
Kuzima kwa intaneti safari hii pia kumekuja muda mfupi baada ya Ofisi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Uganda kusimamisha vibali vya angalau mashirika sita na kufunga kwa muda akaunti zao za benki, hatua iliyodhoofisha uhuru wa kushirikiana unaolindwa na Katiba ya Uganda pamoja na sheria za kimataifa za haki za binadamu.
Aidha, mapema mwezi huu, Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ilieleza wasiwasi wake kuhusu vikwazo vya taarifa kabla ya uchaguzi nchini Uganda, pamoja na vitendo vilivyoenea vya unyanyasaji, vitisho, kukamatwa kiholela na manyanyaso dhidi ya waandishi wa habari.
Soma pia:
Uchaguzi Uganda 2026: Usalama waimarishwa uchaguzi ukikaribia

Maelezo ya picha, Maandalizi yaendelea Uganda uchaguzi mkuu ukitarajiwa kufanyika Alhamisi Baada ya kufungwa kwa kampeni za uchaguzi jana, leo kumekuwa na maandalizi ya mwisho kuelekea siku ya kupiga kura itakayofanyika kesho.
Vifaa vya kupigia kura na nyenzo nyingine za uchaguzi vimeshawasilishwa katika vituo mbalimbali na vinatarajiwa kusambazwa kwa vituo vya kupigia kura mapema kesho asubuhi.
Mawakala wa vyama vya siasa na wa wagombea wamekuwepo katika vituo vya usambazaji ili kuhakikisha vifaa hivyo ni halali na viko katika hali nzuri, kama inavyotakiwa kisheria.
Katika mji wa mbale, kasha lililokuwa limebeba vifaa vya kupigia kura viliwasili katika ofisi ya uchaguzi ya mkoa jumatatu usiku na wajumbe ikiwemo vikosi vya usalama, waangalizi wa uchaguzi wanahabari na wagombea wa nyadhifa mbalimbali walishuhudia upokezi huo kutoka vituo vya kupigia kura 377.”
“Vifaa vya kupigia kura vitawasilishwa kwa vituo vya kupigia kura 6:30 asubuhi “ anasema Michael Aribaitwe, afisa mkuu msimamizi wa kituo cha kupigia kura cha Mbale.
Katika vituo BBC Swahili ilivyovitembelea, mawakala walisema wameridhishwa na vifaa hivyo, lakini walionya kuwa hofu yao kubwa bado ni kuhusu siku yenyewe ya kupiga kura. Pia walilalamikia kuzimwa kwa huduma ya intaneti, wakisema hali hiyo imeathiri mawasiliano na uratibu miongoni mwao.
Katika eneo jingine, BBC Swahili ilikuta maafisa wa uchaguzi, wengi wao wakiwa vijana wakipewa maelekezo kuhusu mchakato wa kupiga kura na matumizi ya vifaa mbalimbali, ikiwemo karatasi za mfano za kura.
Wakati huo huo, hali ya usalama yaimarishwa Uganda ikijiandaa kufanya uchaguzi mkuu kesho Alhamisi ya tarehe 15 Januari 2026.
Wakaazi mitaani wako kati hali ya atiati wakisubiri kuchagua rais na wabunge.
Pia Unaweza Kusoma:
EU yagawanya msaada wa kifedha kwa Ukraine

Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Rais wa Tume ya Ulaya aliliambia Bunge mjini Strasbourg kwamba Ulaya itaendelea kusimama na Ukraine Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, alisema Jumatano kwamba Umoja wa Ulaya (EU) unapanga kugawanya msaada wa kifedha wa euro bilioni 90 uliokubaliwa kuisaidia Ukraine.
Kulingana na mpango huo, theluthi moja ya fedha hizo sawa na euro bilioni 30 itatumika kusaidia bajeti ya kawaida ya serikali ya Ukraine, huku theluthi mbili zilizobaki euro bilioni 60 zitaelekezwa katika ununuzi wa vifaa vya kijeshi.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Brussels, von der Leyen alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha msaada wa EU ili kujenga Ukraine iliyo imara na yenye uthabiti zaidi.
Aliongeza kuwa fedha za euro bilioni 60 zitakazotumika kwa ajili ya vifaa vya kijeshi zitatumika hasa kununua silaha na vifaa vingine kutoka nchi wanachama wa EU na zile za EFTA (Jumuiya ya Biashara Huria ya Ulaya).
Soma pia:
Trump awahimiza waandamanaji wa Iran kudhibiti taasisi za nchi

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Maelezo ya picha, Trump hakufichua maelezo zaidi baada ya kuwasilisha ujumbe huo mzito kwa waandamanaji wa Iran. Rais wa Marekani, Donald Trump, ametoa ujumbe usiotarajiwa kwa wananchi wa Iran wanaoendelea kuandamana dhidi ya serikali katika miji kadhaa kwa zaidi ya wiki mbili sasa.
Kupitia mtandao wake wa Truth Social siku ya Jumanne, Trump aliwahimiza waandamanaji hao kuendeleza shinikizo lao dhidi ya mamlaka.
“Wazalendo wa Iran, endeleeni kuandamana. Dhibitini taasisi zenu. Andikeni majina ya wauaji na wahusika wa ukiukwaji wa haki za binadamu. Watalipa gharama kubwa,” aliandika.
Trump pia alitangaza kusitisha mawasiliano ya kidiplomasia na Tehran, akisema: “Nimefuta mikutano yote na maafisa wa Iran hadi mauaji yasiyo na maana dhidi ya waandamanaji yakomeshwe. Msaada uko njiani.”
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Wanaharakati wa Haki za Binadamu (HRANA) lenye makao yake Marekani, zaidi ya watu 2,500 wamepoteza maisha tangu maandamano hayo yalipoanza tarehe 28 Desemba.
Takwimu hizo zinafanana na kauli ya afisa mmoja wa Iran aliyekiri kuwa takribani watu 2,000 wameuawa ikiwa ni mara ya kwanza kwa utawala wa Aayatola kukubali hadharani ukubwa wa vifo vinavyohusishwa na maandamano hayo, ingawa uliwalaumu wahusika wa nje kwa machafuko hayo.
Alipoulizwa kuhusu taarifa kwamba baadhi ya waandamanaji walikuwa wanakabiliwa na adhabu ya kifo Jumatano, Trump alisema Marekani ingechukua “hatua kali sana” iwapo mauaji hayo yangetekelezwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alijibu kwa kuonya kuwa taifa lake litajilinda dhidi ya “uovu wa kigeni na kuingiliwa kwa masuala yake ya ndani.”
Kauli hiyo ilionekana kuashiria kuongezeka kwa mvutano kati ya mataifa hayo mawili.
Chapisho la Trump lililosisitiza maneno “MSAADA UKO NJIANI” lilitafsiriwa na wachambuzi kama ishara wazi ya nia ya Marekani kuingilia kati kwa njia ya moja kwa moja.
Wakati huo huo, maafisa wakuu wa serikali ya Marekani wanatarajiwa kukutana Ikulu ya White House Jumanne hii kujadili hatua mbadala zinazoweza kuchukuliwa.
Ingawa mwishoni mwa wiki Trump alikuwa ameashiria uwezekano wa kufungua njia za kidiplomasia kufuatia madai ya pendekezo la mazungumzo kutoka Iran, inaonekana juhudi hizo zimesitishwa kwa sasa.
Kwa mtindo wake unaotambulika wa kutumia lugha kali mtandaoni, Trump mara nyingi hutumia herufi kubwa kusisitiza vitisho au maonyo, ingawa si mara zote hutekeleza aliyoyasema.
Hata hivyo, kwa kuzingatia ukubwa wa vifo vilivyoripotiwa na ahadi yake ya wazi ya kuwaunga mkono waandamanaji wa Iran, inaonekana Rais wa Marekani tayari amechukua mwelekeo thabiti.
''Kwa hali ilivyo sasa, ni vigumu kuona akirudi nyuma'',mchambuzi wa masuala ya kisiasa Iran anaeleza.
Soma Zaidi:
Waendesha mashtaka wataka rais wa zamani wa Korea Kusini ahukumiwe kifo

Chanzo cha picha, Getty Images
Waendesha mashtaka wameomba rais wa zamani wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol ahukumiwe kifo ikiwa atapatikana na hatia kutokana na jaribio lake la kutaka kulazimisha sheria za kijeshi.
Mahakama mjini Seoul ilisikiliza hoja za mwisho katika kesi ya Yoon, ambapo alishtakiwa kwa kuwa "kiongozi wa uasi".
Shtaka hilo linatokana na jaribio la Yoon mnamo Desemba 2024 la kulazimisha utawala wa kijeshi nchini Korea Kusini - kitendo kilichodumu kwa saa chache lakini kiliiingiza nchi hiyo katika machafuko ya kisiasa.
Baadaye aliondolewa madarakani na bunge na kukamatwa ili kukabiliwa na kesi.
Yoon amekanusha mashtaka dhidi yake, akisema kwamba sheria ya kijeshi ilikuwa ishara ya kuvutia nadhari kwa umma kwa makosa ya chama cha upinzani.
Soma zaidi:
Meli ya mafuta iliyokamatwa na Marekani yaonekana Scotland

Chanzo cha picha, Peter Jolly/Northpix
Meli ya mafuta iliyokamatwa na Marekani katika Atlantiki Kaskazini wiki iliyopita imepelekwa Scotland kuchukua bidhaa mpya, serikali ya Uingereza imesema.
Marekani imeishutumu meli hiyo kwa kuvunja vikwazo kwa kubeba mafuta kwa ajili ya Venezuela, Urusi na Iran.
Meli hiyo, ambayo hapo awali ilijulikana kama Bella 1, ilipatikana ikiwa kusini mwa Iceland katika operesheni iliyoungwa mkono na vikosi vya Uingereza.
Meli ya Marinera iko katika eneo lililohifadhiwa la bahari kati ya pwani ya mashariki ya Nyanda za Juu na pwani za Moray na Aberdeenshire - pamoja na meli zinazotumika kuvuta zingine na za Walinzi wa Pwani ya Marekani.
Msemaji wa serikali ya Uingereza alisema: "Meli ya Bella 1 iliingia majini Uingereza ili kujazwa vifaa muhimu - ikiwa ni pamoja na chakula na maji kwa wafanyakazi - mapema leo kabla ya kuendelea na safari yake."
Wizara ya Ulinzi ya Uingereza (MoD) ilisema "kuzuia, kuvuruga na kudhalilisha" meli za Urusi ilikuwa kipaumbele.
Msemaji alisema: "Pamoja na washirika wetu, tunaongeza mwitikio wetu kwa ukamataji wa meli zilizokiuka vikwazo - na tutaendelea kufanya hivyo."
Pia unaweza kusoma zaidi:
Marekani kusitisha ulinzi wa kufukuzwa kwa Wasomali

Chanzo cha picha, Getty Images
Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump unakomesha ulinzi wa muda wa kufukuzwa nchini na vibali vya kufanya kazi kwa baadhi ya raia wa Somalia nchini Marekani huku ikiwapa mamia ya raia hao muda wa miezi miwili kuondoka nchini humo au kukabiliwa na mkono wa sheria.
Waziri wa Usalama wa Ndani Kristi Noem alisema siku ya Jumanne kwamba utawala wa Trump unasitisha Hadhi ya Muda ya Kulindwa, ambayo huwalinda wahamiaji wasifukuzwe ili kupelekwa nchi ambazo zinaonekana si salama.
"Hali nchini Somalia imeimarika hadi kufikia kiwango ambachohakikidhi tena kigezo cha sheria ya kupewa Ulinzi wa Muda," Noem alisema katika taarifa.
"Ulinzi wa muda inamaanisha ni wa kipindi kifupi," na kuongeza kuwa kuwaruhusu raia wa Somalia kubaki nchini Marekani ni "kinyume na maslahi yetu ya kitaifa." "Kipaumbele chetu ni kwa Wamarekani."
Uamuzi huo unatarajiwa ukakabiliwa na changamoto za kisheria.
Utawala wa Trump ulikuwa umetangaza kwa mara ya kwanza nia yake ya kusitisha ulinzi kwa raia wa Somalia mnamo mwezi Novemba, huku Trump akiandika kwenye jukwaa lake la Truth Social kuhusu Minnesota, ambayo ni nyumbani kwa jamii kubwa ya Wasomali: "Magenge ya Wasomali yanawatisha watu wa Jimbo hilo kubwa, na MABILIONI ya Dola yanapotea. Warudishe walikotoka. IMEISHA Sasa!"
Soma zaidi:
Kreni ya ujenzi yaanguka juu ya treni Thailand

Chanzo cha picha, Facebook / State Railway of Thailand
Kreni kubwa ya ujenzi imeanguka kwenye treni iliyokuwa safarini na abiria katika jimbo la Nakhon Ratchasima nchini Thailand, vyombo vya habari vya ndani vinaripoti.
Zaidi ya watu 20 wameripotiwa kujeruhiwa huku vikosi vya uokoaji vikiendelea na shughuli ya kuwanasua waliokwama kwenye mabehewa.
Ajali hiyo ilitokea takriban saa 3:00 AM (2:00 AM GMT) siku ya Jumatano katika wilaya ya Sikhio ya mkoa wa Nakhon Ratchasima, kilomita 230 (maili 143) kaskazini mashariki mwa Bangkok, kulingana na polisi wa eneo hilo.
Kreni ilikuwa ikifanya kazi katika mradi wa reli ya mwendo wa kati kabla ya kuanguka na kusababisha treni kuacha njia na kushika moto kwa muda mfupi.
Trump aahidi 'kuchukua hatua kali' ikiwa Iran itawaua waandamanaji

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock/Hengaw Organization for Human Rights/X
Rais Donald Trump amesema Marekani itachukua "hatua kali" dhidi ya Iran ikiwa itawaua waandamanaji, huku makundi ya haki za binadamu yakisema zaidi ya waandamanaji 2,400 wanaopinga serikali wameuawa katika msako mkali uliofanywa na mamlaka ya Iran.
Jamaa wa Erfan Soltani mwenye umri wa miaka 26, ambaye alikamatwa wiki iliyopita, wameiambia BBC Persian kwamba anatarajiwa kunyongwa Jumatano.
Mwakilishi kutoka Shirika la Haki za Binadamu la Hengaw pia aliambia BBC kwamba "hawajawahi kushuhudia kesi ikisikilizwa kwa haraka namna hiyo".
Akizungumza na mshirika wa BBC wa Marekani, CBS News, Trump alisema: "Wakiwanyonga, mtaona mambo kadhaa... Tutachukua hatua kali sana wakitenda jambo kama hilo."
Jamaa wa Soltani aliambia BBC Persian kwamba mahakama ya Iran imetoa hukumu ya kifo "katika mchakato ulioendeshwa kwa haraka sana, ndani ya siku mbili tu".
Awyar Shekhi, mwakilishi wa Hengaw, alisema kwamba kesi hiyo ilionyesha kwamba serikali ya Iran "inatumia kila mbinu wanayoijua kuwakandamiza watu na kueneza hofu".
Afisa mmoja wa Iran aliambia Reuters kwamba watu 2,000 wameuawa, lakini "magaidi" ndio wa kulaumiwa kwa hilo.
Soma zaidi:
Mamia wa maafisa wa polisi wajitangaza kuwa wanachama wa Freemason Uingereza

Chanzo cha picha, PA Media
Maafisa zaidi ya 300 wa Jeshi la Polisi wa Jiji la wametangaza kuwa wanachama wa Freemason au "miungano mingine ya aina hiyo" baada ya kikosi hicho kuwataka kufanya hivyo mwezi uliopita, jaji wa Mahakama Kuu amesema.
Polisi ilitangaza mnamo mwezi Desemba kwamba uanachama wa Freemason au mashirika kama hayo yataongezwa kwenye sera yake ya vyama vinavyoweza kutangazwa.
Maafisa na wafanyakazi walitakiwa kutangaza uanachama "wa zamani au wa sasa" wa shirika au muungano wowote wa kijamii "wenye uanachama wa siri na unahitaji wanachama kusaidiana na kulindana".
Hatua hiyo ilisababisha mashirika yenye kuwawakilisha Freemason kuanza hatua za kisheria kuhusu uamuzi wa kikosi hicho katika Mahakama Kuu yakitaka sera hiyo kusitishwa hadi uamuzi wa kesi iliyowakilishwa mahakamani utakapotolewa.
Kikosi hicho kiliongeza kwamba hakukuwa na pendekezo kwamba kimepanga kuwachukulia hatua za kinidhamu maafisa au wafanyakazi kwa kujitangaza hadharani kuwa wanachama wa Freemason.
Jeshi hilo lilithibitisha kwamba maafisa na wafanyakazi 316 walikuwa wametangaza uanachama wa Freemason au miungano mingine sawia na huo.
Soma zaidi:
Mwaka jana ulikuwa mbaya zaidi kwa raia wa Ukraine tangu 2022, UN inasema

Chanzo cha picha, Getty Images
Shirika la Umoja wa Mataifa limetoa ripoti inayoonyesha kuwa Mwaka 2025 ulikuwa mbaya zaidi kwa raia nchini Ukraine tangu 2022.
Vurugu zinazohusiana na migogoro ziliua takriban raia 2,514 mwaka jana, Ujumbe wa Ufuatiliaji wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine ulisema, ikilinganishwa na 2,088 mwaka wa 2024 na 1,974 mwaka wa 2023. Idadi ya raia waliojeruhiwa pia iliongezeka kwa kasi kila mwaka.
Shambulio baya zaidi la mwaka huo liliua raia wasiopungua 38 katika mji wa magharibi wa Ternopil mnamo mwezi Novemba ikiwa ni pamoja na watoto wanane.
Siku ya Jumanne Rais Volodymyr Zelensky alisema mashambulizi ya Urusi usiku kucha yaliwaua watu wanne huko Kharkiv na kuacha "kaya laki kadhaa" bila umeme ndani na karibu na Kyiv huku hali ya hewa ikiwa baridi kali.
Zelensky pia alisema karibu ndege zisizo na rubani 300, makombora 18 ya masafa marefu na makombora saba ya kusafiri kwa meli yalilenga miji kote nchini humo.
Jumla ya idadi ya raia waliouawa na kujeruhiwa mwaka wa 2025 iliongezeka kwa 31% ikilinganishwa na mwaka wa 2024, na 70% mwaka wa 2023, kulingana na ujumbe wa Umoja wa Mataifa .
Mnamo 2022, watu 8,423 waliuawa na 12,670 walijeruhiwa baada ya Urusi kuanza uvamizi wake mwezi Februari.
Mnamo mwezi Novemba mwaka jana, iliripoti zaidi ya raia 14,534 wameuawa tangu vita kuanza.
Mkuu wa ujumbe huo Danielle Bell alisema takwimu za mwaka jana zinawakilisha "kuzorota kwa kiwango kikubwa kwa ulinzi wa raia".
"Ufuatiliaji wetu unaonyesha kwamba ongezeko hili halikuchochewa tu na uhasama ulioongezeka vitani, lakini pia na matumizi makubwa ya silaha za masafa marefu, ambayo yaliweka raia kote nchini katika hatari kubwa."
Pia unaweza kusoma:
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Uganda adai kutishiwa maisha

Chanzo cha picha, Getty Images
Mkuu wa Tume ya Uchaguzi nchini Uganda anasema ametishiwa maisha juu ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.
Bw Simon Byabakama alikuwa akijibu swali la BBC kuhusu klipu ya video mtandaoni ambapo msaidizi mkuu wa rais anadai kuwa Tume ya Uchaguzi haitawahi kumtangaza mgombea wa upinzani Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, kuwa rais.
Katika video hiyo, Msaidizi Maalum wa Rais wa Utoaji Huduma na Ufuatiliaji, Bw Yiga Kisakyamukama, anasikika akisema: "Usitarajie, hata usifikirie, kwamba Simon Byabakama anaweza kumtangaza Bobi Wine. Rais Museveni, ambaye yuko madarakani, atasalia uongozini. Usifikirie kwamba Museveni ataondoka madarakani kwa kupiga kura. Hapana, usipoteze wakati wetu."
Bw.Byabakama alisisitiza kuwa Tume hiyo iko huru kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kusisitiza kuwa itamtangaza mshindi kwa misingi ya hesabu ya kura.
"Sheria ya Uchaguzi wa Rais inaagiza Tume ya Uchaguzi kuhakikisha, kutangaza na kuchapisha matokeo ya uchaguzi wa urais. Hivyo ndivyo ilivyo. Huwezi kukwepa kifungu hicho cha sheria," Bw Byabakama alisema.
Aliendelea kufichua kuwa watu fulani walikuwa wamemwonya kwamba ikiwa atashindwa kutangaza wagombeaji mahususi kama washindi, kuna athari fulani zitakazomkabili.
"Mnajua niliwaambia nini? "Mheshimiwa, sifanyi kazi ya kuchangia kura, sichangii kura. Ni mpiga kura ndiye anayeamua mgombea apate kura ngapi, na kile ambacho wapiga kura wamesema ndicho nitatangaza kwa taifa," alisema.
Alipoulizwa na BBC aliyehusika na vitisho hivyo, Bw Byabakama alijibu: "Watu wasio na kazi akiongeza kwamba ni wale ambao hawana la kufanya. Lakini unaweza kuona kutokana na tabia yangu kwamba hofu ni neno lisilokuwepo katika msamiati wangu."
Alisisitiza kuwa hana wasiwasi na kusema anaendelea kuzingatia kutekeleza majukumu yake kwa watu wa Uganda.
Bw Byabakama alisisitiza kuwa Uganda itasalia kuwa nchi salama hata baada ya uchaguzi.
Raia wa Uganda wanatarajiwa kupiga kura tarehe 15 Januari kumchagua rais na wabunge.
Soma zaidi:
Zaidi ya watu 2,000 waripotiwa kuuawa katika maandamano ya Iran

Chanzo cha picha, Reuters
Watu zaidi ya 2,000 wameuawa wakati wa msako mkali wa vikosi vya usalama dhidi ya maandamano nchini Iran, kundi la haki za binadamu limesema, huku Rais Trump akiwaahidi Wairani kwamba msaada "unakaribia".
Shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake Marekani (HRANA), liliripoti kwamba hadi sasa limethibitisha mauaji ya waandamanaji 1,850, watu 135 walioshirikiana na serikali, raia wengine tisa pamoja na watoto tisa katika kipindi cha siku 17 zilizopita licha ya kukatika kwa mtandao.
Afisa mmoja wa Iran pia aliambia Reuters kwamba watu 2,000 wameuawa lakini "magaidi" ndio wa kulaumiwa.
Trump atahudhuria mkutano kuhusu Iran Jumanne jioni, na ameahidi kupata takwimu "sahihi" za vifo.
"Idadi ya waliouawa inaonekana kuwa kubwa lakini bado hatuna taarifa za uhakika," Trump aliwaambia waandishi wa habari wakati akirejea Ikulu ya White House.
Mara tu atakapopata idadi kamili, alisema, "tutachukua hatua ipasavyo."
Mapema Jumanne, Trump aliandika kwenye jukwaa lake la Truth Social kwamba mamlaka ya Iran "italipa gharama kubwa" kwa mauaji hayo, na akawasihi watu "waendelee kuandamana".
Soma zaidi:
Karibu tena katika matangazo yetu mubashara. Tarehe ni 14/01/2026.
