Kwa nini Qatar imeruhusu uwepo wa ofisi ya Hamas nchini mwake?

Chanzo cha picha, Getty images
Huku kukiwa na mazungumzo magumu yanayolenga kufikia mwafaka kati ya Hamas na Israel, uvumi umetanda katika vyombo vya habari vya Magharibi na Kiarabu kuhusu iwapo Hamas itahamisha ofisi yake ya kisiasa kutoka Qatar hadi nchi nyingine, au Qatar inakusudia kuwafukuza viongozi wa Hamas na kufunga ofisi hiyo.
Pamoja na kwamba Qatar na Hamas zimekanusha uvumi huo, lakini la uhakika ni kwamba Qatar iko chini ya shinikizo, jambo lililoifanya itangaze kuwa iko mbioni kutathmini upatanishi wake kati ya Hamas na Israel.
Doha ilianza kuwa mwenyeji wa ofisi ya kisiasa ya Hamas mwaka 2012. Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya vuguvugu hilo wakati huo, Khaled Meshaal, aliondoka Syria kuelekea Doha, kufuatia kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe huko.
Ismail Haniyeh, alichaguliwa kuwa mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas kumrithi Meshaal mwaka 2017, kwa sasa anaishi Qatar.
Kwa mujibu wa taarifa za maafisa kadhaa wa Marekani na Qatar. Nchi hiyo ilikubali kuwa na ofisi ya Hamas kutokana na ombi la Marekani, ambayo ilitaka kufungua njia isiyo ya moja kwa moja ya mawasiliano na harakati hiyo ili kutuliza makali ya migogoro inayozuka kati ya Wapalestina na Israel.
Qatar kama mpatanishi

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Tangu shambulio la kushtukiza lililofanywa na Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba, na baadae vita vikali vilivyoanzishwa na Israel katika Ukanda wa Gaza, Qatar imekuwa na jukumu muhimu katika mazungumzo kati ya pande hizo mbili.
Ilifanikiwa kupatanisha mapatano ya wiki moja mwishoni wa mwa mwezi Novemba, ambapo Hamas iliwaachilia mateka 81 wa Israel, na wafungwa 280 wa Kipalestina waliokuwa wakishikiliwa katika jela za Israel waliachiliwa.
Lakini mazungumzo yote yaliyofuata yalishindwa kufikia mapatano, na upatanishi wa Qatar ulikosolewa na Israel na Marekani.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Qatar imekuwa ikikosolewa mara kwa mara na Israel, haswa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, ambaye husema kuwa inafadhili Hamas, na mwishoni mwa Januari aliiomba Qatar kuishinikiza harakati hiyo kuwaachilia mateka wa Israel.
Wiki iliyopita, ubalozi wa Qatar mjini Washington ulieleza kutoridhishwa kwake na matamshi yaliyotolewa na Mbunge wa Democratic, Steny Hoyer, ambapo aliitaka Marekani kutathmini upya uhusiano wake na Qatar ikiwa haitoi shinikizo kwa Hamas.
Ripoti za vyombo vya habari hapo awali ziliripoti, zikimnukuu afisa wa Marekani, kwamba Rais wa Marekani Joe Biden aliwataka viongozi wa Qatar na Misri kuishinikiza Hamas kufikia makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka wa Israel.
Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumanne, Aprili 23, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Majid Al-Ansari, alirudia mazungumzo kuhusu kutathmini upya upatanishi wa nchi yake, akisisitiza kuwa jukumu la mpatanishi ni kufanya kazi na pande zote ili kufikia suluhu inayokubalika na sio kushinikiza suluhu.
Qatar itafunga ofisi ya Hamas?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Gazeti la Marekani, Wall Street Journal liliripoti Jumamosi iliyopita, likiwanukuu maafisa kutoka nchi za Kiarabu, kwamba uongozi wa kisiasa wa vuguvugu la Hamas unazingatia uwezekano wa kuhamisha makao yake nje ya Qatar, umewasiliana na nchi mbili katika eneo hilo, moja kati yao ni Oman, kuona kama iko tayari kuwakaribisha viongozi wake wa kisiasa.
Kabla ya afisa wa Hamas kukanusha uhalali wa ripoti hiyo, Al-Ansari alisema katika mkutano na waandishi wa habari uliotajwa hapo juu kwamba "kwa vile uwepo wa viongozi wa Hamas hapa Doha ni wa manufaa na chanya kwa juhudi za upatanishi, wataendelea kuwa hapa."
Uturuki iliibuka miongoni mwa nchi hizo, haswa kutokana na kuwasili kwa Ismail Haniyeh, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, mjini Istanbul mwishoni mwa juma lililopita na kuwa na mkutano na Rais Recep Tayyip Erdogan.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa nafasi ya Uturuki katika juhudi za upatanishi, Al-Ansari alisema Uturuki ni moja ya nchi muhimu zinazounga mkono juhudi zinazoongozwa na Qatar kusitisha vita huko Gaza, na ushirikiano unaendelea katika suala hili.
Baadhi ya ripoti pia zimeitaja Algeria, kama vile gazeti la Ufaransa la Le Monde liliporipoti kuhusu hati ya Saudi Arabia iliyowasilishwa kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa inayopendekeza mpango wa kumaliza mgogoro wa Gaza, ikiwa ni pamoja na kuhamishwa kwa viongozi wa Hamas kwenda Algeria na kutumwa vikosi vya kulinda amani katika Ukanda huo.
Miongoni mwa nchi zinazotajwa kuwa mwenyeji wa ofisi ya kisiasa ya Hamas ni Iran na wanachama wengine wa kile kinachoitwa "mhimili wa upinzani, Lebanon, Syria na Yemen.
Hamas itaondoka?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Jost Hiltermann, kutoka International Crisis Group anasema, "ikiwa Hamas italazimishwa kuondoka Qatar, itakuwa vigumu kupata nchi mwenyeji, kwa sababu baadhi ya nchi hizo zinaweza kuangukia kwenye vikwazo.”
Mtafiti Hassan Abu Haniyeh, anasema, ‘iwapo ofisi ya kisiasa ya Hamas itaondoka Qatar, uwezo wa nchi za Ulaya na Marekani kuwa na mazungumzo na harakati hiyo utapungua.’’
Abu Haniyeh anaongeza kuwa Doha inaweza kuwafukuza viongozi wa Hamas ikiwa Marekani itaiomba, lakini anaamini Washington haitochukua hatua hii “kwa sababu itapoteza njia zozote za mazungumzo na mawasiliano na mambo yatakuwa magumu zaidi.’’
‘Kundi hilo linaweza kutanua uwepo wake, na tayari lipo huko Iran, Yemen na Lebanon, lakini ofisi ya kisiasa itasalia Qatar kwa madhumuni ya mazungumzo’’.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












