Je, Israel itafanikiwa kuiondoa Hamas?

Chanzo cha picha, Getty
- Author, Dalia Hadar and Natalie Merzoughui
- Nafasi, BBC Arabic
Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema lengo la Israel huko Gaza ni "kuharibu uwezo wa kiutawala na kijeshi wa Hamas" na kuwaondoa Hamas.
Baada ya takribani miezi mitano ya mapigano, na karibu Wapalestina 30,000 wakiuawa kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas, Israel inasema imepata maendeleo makubwa na lazima isonge mbele hadi "ushindi kamili."
Hamas ni shirika lenye uwezo wa kijeshi - pia ni vuguvugu la kisiasa, kiitikadi na kijamii. Je, lengo la Israeli la kuliondoa kabisa linawezekana?
Nini kinatokea ardhini?
Israel inasema imeharibu vikosi 18 kati ya 24 vya Hamas huko Gaza, na "kukamilisha kuvunja mfumo wa kijeshi wa Hamas kaskazini mwa Ukanda wa Gaza."
Vikosi vya Ulinzi vya Israel (IDF) vinasema Hamas ilikuwa na wapiganaji wapatao 30,000 wakati kundi hilo lilipoanzisha mashambulizi yake dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba, na kuuwa takribani watu 1,200 na kuwachukua mateka karibu 250.
IDF inadai imewauwa wapiganaji 13,000 na Netanyahu alisema mapema Februari, vikosi vya Israel "vimeua, kujeruhi au kukamata zaidi ya magaidi 20,000 - zaidi ya nusu ya kikosi cha mapigano cha Hamas."
BBC haiwezi kuthibitisha takwimu hizi, na IDF haijajibu maombi ya kufafanua mbinu zake. Idadi hiyo ya Israel ina mkanganyiko, kwani takwimu za wizara ya afya zinaonyesha vifo 9,000 tu huko Gaza ndio vya wanaume watu wazima wakiwemo raia.
Ofisi ya kisiasa ya Hamas iliiambia BBC inakataa madai ya Israel, na tawi lake la kijeshi linaendelea kufanya kazi kwa katika maeneo yote ya Gaza. Wakati huo huo, ripoti katika gazeti la Israel la Haaretz inasema Hamas imeanza kurejesha tena baadhi vikosi vyake.
Hamas inaweza "kuajiri wapiganaji wapya kwa urahisi sana," anasema Jeremy Binnie, mhariri wa Mashariki ya Kati wa jarida la Jane's Defense Weekly.
Kanali Mstaafu wa Israel, Miri Eisin kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Kukabiliana na Ugaidi katika Chuo Kikuu cha Reichman nchini Israel anasema, majeshi ya Israel "yamewaua makamanda na wamepata "mabaki ya silaha" na "wanalipua mahandaki ya chini ya ardhi ya Hamas.”
Binnie anasema mfumo wa mahandaki ni "mkubwa zaidi kuliko ilivyokadiriwa hapo awali" na Waisraeli "wana safari ndefu ya kuyaharibu, huku wakitatizwa na hatari dhidi ya mateka wanaoshikiliwa huko.
Je, unaweza kuitokomeza itikadi?
Kundi la Hamas linaonekana kuwa kundi la kigaidi na nchi za Magharibi, lakini wanaonekana kuwa harakati ya upinzani na ulimwengu wa Kiarabu.
Hmas imetawala Ukanda wa Gaza tangu 2007 baada ya kushinda uchaguzi mwaka 2006 na kuwaondoa Fatah kwa nguvu.
Ukanda wa Gaza umezingirwa na Israel na kwa kiasi kidogo Misri tangu wakati huo - nchi zote mbili zinasema ni kwa ajili ya usalama.

Chanzo cha picha, Getty
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Makundi ya Wapalestina yamerusha maelfu ya maroketi kutoka Gaza dhidi ya Israel katika kipindi cha miongo miwili iliyopita - wakati mwingine kujibu ghasia na mzozo unaohusisha wanajeshi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu au Jerusalem Mashariki.
"Si vuguvugu la kijeshi tu, wala si vuguvugu la kisiasa - ni itikadi pia," anasema Hugh Lovatt, mtaalamu wa Mashariki ya Kati katika Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Kigeni.
"Itikadi hiyo haitatokomezwa, kwa nguvu ya silaha za Israel," anasema "hasa katika mazingira ya sasa, ambapo Wapalestina wanahisi hakuna tena njia ya kisiasa ya kutimiza haki yao ya kujitawala."
Dkt. Amjad Abu El Ezz, mhadhiri wa uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Marekani katika Ukingo wa Magharibi, anasema Wapalestina wengi wanaunga mkono Hamas kwa sababu "hawaoni mustakabali wao."
Waziri Mkuu Netanyahu amepinga kuundwa taifa la Palestina katika muda wake wote wa kisiasa. Anataja wasiwasi wa usalama, na kushindwa kwa Hamas kuitambua Israel.
Lakini wengi katika chama chake cha Likud na washirika wake wa siasa kali za mrengo wa kulia serikalini wanaona Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza kuwa ni mali ya Israel.
Mwaka jana kulikuwa na idadi kubwa zaidi ya nyumba zilizoidhinishwa na serikali ya Israel kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya walowezi huko Ukingo wa Magharibi, kulingana na kundi la wanaharakati wa Israel Peace Now.
Mwaka 2023, Wapalestina wasiopungua 507 waliuawa katika Ukingo wa Magharibi na wanajeshi wa Israel na walowezi wa Israel, wakiwemo watoto wasiopungua 81, na kuwa mwaka mbaya zaidi kwa Wapalestina, tangu Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) kuanza kurekodi takwimu mwaka 2005.
Umoja wa Mataifa pia umerekodi vifo 36 vya wa-Israel katika mashambulizi ya Wapalestina kutoka Ukingo wa Magharibi.
"Kama kuna uvamizi, kuna ukatili, kuna mauaji, bila shaka watu wengi watafuata kile Hamas wanachosema - kwa sababu wanatafuta matumaini," anasema Dkt. Abu El Ezz.

Chanzo cha picha, Getty
Uungwaji mkono wa Hamas waongezeka
Licha ya hasara kubwa ambayo Wapalestina huko Gaza wanapata baada ya matukio ya Oktoba 7, kura ya maoni mwishoni mwa 2023 inaonyesha uungaji mkono kwa Hamas umeongezeka miongoni mwa Wapalestina.
Katika Ukingo wa Magharibi, uungwaji mkono kwa Hamas uliongezeka kutoka 12% mwezi Septemba hadi 42% mwezi Desemba, uchunguzi kwa Wapalestina 750 katika Ukingo wa Magharibi na 481 huko Gaza.
Dkt. Khalil Shikaki wa Kituo cha Utafiti wa Sera cha Palestina huko Ukingo wa Magharibi, ambacho kilifanya uchaguzi huo, anasema uungaji mkono wa Hamas kwa kawaida huongezeka wakati wa mapigano, lakini ongezeko hili limekuwa kubwa.
Wakati wa mapatano kati ya Hamas na Israel mwezi Novemba, wanawake na watoto wa Kipalestina walikuwa wakiachiliwa kutoka jela za Israel.
Anasema hii ilisababisha baadhi ya watu kuona harakati za Hamas ni zenye ufanisi mkubwa katika kufikia malengo ya Palestina.
Mashambulizi ya walowezi na kutoeleweka kwa majibu ya Mamlaka ya Palestina, kulisababisha kuungwa mkono Hamas kuongezeka, Dkt. Shikaki.
Ingawa Gaza ilishuhudia kuongezeka kudogo kwa uungaji mkono kwa Hamas, kutoka 38% hadi 42% .
Watu wachache huko Gaza waliona Hamas ilikuwa sahihi kufanya mashambulizi ya Oktoba 7, 57% waliunga mkono, ikilinganishwa na 82% katika Ukingo wa Magharibi.
Kizazi kipya cha wapiganaji?
Dkt. Abu El Ezz anaamini vijana wengi huko Gaza sasa "wamejaa chuki dhidi ya Israel na dhidi ya uvamizi."
"Nadhani vizazi vijavyo vitajiunga na vikundi hivi vya kijeshi ili kulipiza kisasi, kwa sababu walipoteza familia, watoto, mama zao na wana wao, ndugu zao," anasema.
Hata hivyo, Dkt. Shikaki anasema, "vita vkubwa si lazima vipelekee vijana kuchukua silaha, ikiwa vitafuatiwa na amani."
Netanyahu ameelezea mpango wa baada ya vita ambapo Israel itadhibiti usalama wa Gaza isiyo na jeshi kwa muda usiojulikana, na Wapalestina wasiokuwa na uhusiano na makundi yanayoichukia Israel wataendesha eneo hilo.
Kanali Eisin anaamini Israel itaweza kuondoa "wingi wa Hamas na tishio lao."
"Ikiwa mtu anataka kweli kuwatenga na kuidhoofisha Hamas, basi njia pekee ambayo inawezekana ni kuunda suluhu la kisiasa," anasema Lovatt.
Netanyahu hivi karibuni alisema kwenye X kwamba "ni lazima udhibiti kamili wa usalama wa eneo lote la magharibi mwa Jordan uwe chini ya Israel na hili ni kinyume na matakwa ya taifa la Palestina.”
Pia ni kinyume cha wazi na msimamo wa mshirika mkuu wa Israel, Marekani, ambayo inasema suluhu la kudumu la mzozo wa Israel na Palestina "linaweza tu kuja kwa kupatikana taifa la Palestina".
"Sioni siku ya ushindi kwa Waisraeli," anasema Binnie. "Wanaweza kuimaliza Hamas kwa kiasi kikubwa, lakini jambo la msingi ni jinsi gani unaweza kuzuia Hamas kuibuka tena?"

Chanzo cha picha, Getty
"Ni wazi kwamba wale ambao walikuwa wakiteseka na matokeo ya maamuzi ya Hamas kuhusu vita hivi walikuwa wanaikosoa Hamas," Dk Shikaki anasema.
Waandishi wa habari wa BBC waliokuwa wakiripoti kutoka Gaza hadi mapema Februari wamebainisha dalili za kuongezeka kuichukia Hamas miongoni mwa raia katika miezi ya hivi karibuni.
Baadhi ya wakazi wa Gaza waliozungumza nao walitaja vifo vya wapendwa wao, uharibifu wa nyumba na njaa kuwa sababu ya hasira dhidi ya kundi hilo.
Pia wanaripoti kwamba mara nyingi Wagaza wana wasiwasi kuhusu kuikosoa hadharani Hamas.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












