Matokeo ya uchaguzi Uganda 2026: Kura zinahesabiwa, upinzani wadai uchaguzi ulikumbwa na udanganyifu

.

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Sammy Awami
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Kampala
    • Author, Wycliffe Muia
    • Nafasi, BBC Africa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Shughuli za kuhesabu kura zimeanza katika baadhi ya maeneo ya Uganda licha ya mtandao wa intaneti kuzimwa na upinzani kudai uchaguzi wa rais na wabunge ulikumbwa na visa vya udanganyifu.

"Matukio ya masanduku kujazwa kura yameripotiwa kila mahali," alidai mgombea wa urais wa chama cha upinzani cha NUP Ssentamu Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa kijamii, bila kutoa uthibitisho madai hayo.

Mamlaka inayosimamia uchaguzi huo haijatoa kauli yoyote kuhusu madai ya udanganyifu katika uchaguzi, wala madai ya Wine kwamba mawakala "wengi" wa wapiga kura na wasimamizi wa chama chake cha NUP "walitekwa nyara, na wengine kufukuzwa katika vituo vya kupigia kura".

Changamoto za kiufundi zilichelewesha shughuli ya upigaji kura hadi saa baada ya mashine zinazotumiwa kuwatambua wapiga kura kwa njia ya kielektroniki kukumbwa na hilafu.

Baadhi ya watu wamehusisha changamoto hiyo na kuzimwa kwa intaneti - pamoja na ukosefu wa vifaa vya kupigia kura, au vifaa kutowasilishwa katika baadhi ya vituo kwa wakati uliopangwa.

Vituo vya kupigia kura sasa vitafungwa baadaye na sio muda uliokuwa umepangwa.

Tume ya uchaguzi ilisema mtu yeyote aliyekuwa kwenye foleni ya kupiga kura kufikia saa kumi na moja jioni saa za ndani (14:00GMT) ataruhusiwa kupiga kura yake.

Hapo awali, Tume ya uchaguzi iliomba msamaha kufuatia "changamoto kiufundi" zilizoshuhudiwa katika vituo vya kupigia kura kote nchini na kuongeza kuwa maafisa wake walikuwa wanafanya kila wawezalo kutatua hitilafu hiyo.

Katika kinyang'anyiro cha urais, Yoweri Museveni, 81, ambaye amekuwa madarakani tangu 1986, anagombea muhula wa saba mtawalia huku akikabiliwa na ushindani kutoka kwa Bobi Wine, nyota wa muziki wa pop mwenye umri wa miaka 43.

Matokeo ya uchaguzi wa urais yanatarajiwa kutangazwa siku ya Jumamosi saa kumi jioni saa za ndani (13:00 GMT), tume ya uchaguzi imesema.

Alhamisi asubuhi, BBC ilishuhudia hali ya mfadhaiko ikiongezeka miongoni mwa wapiga kura waliokuwa wakipanga foleni katika baadhi ya vituo vya kupigia kura katika mji mkuu, Kampala.

Japo data ya waliojitokeza kushiriki mchakato huo bado haijapatikana, waandishi walishuhudia kile kilichoonekana kuwa idadi ndogo ya watu kuliko kawaida, na hali ya kutojali miongoni mwa wapiga kura.

Wapiga kura wanakusanyika karibu na dawati wakizungumza na maafisa wa uchaguzi mjini Kampala

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Wapiga kura katika baadhi ya maeneo ya Kampala, walipata vituo vya kupigia kura bado havijafunguliwa saa chache baada ya upigaji kura kuanza
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baadhi ya watu waliripotiwa kuondoka katika vituo vya kupigia kura bila kupiga kura, wakisema hawawezi kusubiri changamoto za kiufundi kutatuliwa.

Mkuu wa uchaguzi Simon Byabakama aliamuru matumizi ya sajili ya kitaifa ya wapiga kura katika vituo ambavyo mashine za kibayometriki zilishindwa kufanya kazi.

Changamoto hiyo ilionekana kuathiri maeneo yote yanayoonekana kuwa na uungwaji mkono mkubwa wa serikali pamoja na yale yanayosadikiwa kuwa ngome za upinzani.

"Nina hasira kwa sababu sijapiga kura mpaka sasa. Upigaji kura ulitarajiwa kuanza kuanza saa moja, lakini hadi sasa saa mbili hatujaanza. Karatasi za kupigia kura hata hazipo, sina hata la kusema," Kaweesi Ismail, mpiga kura mjini Kampala, aliiambia BBC.

Akipiga kura yake katika Kijiji alichozaliwa cha Rwakitura katika mkoa wa Mbarara magharibi, Rais Museveni alisema pia alipata matatizo.

"Niliweka alama ya kidole gumba kwenye mashine lakini haikukubali. Hata hivyo uso wangu ulikubaliwa papo hapo na mashine. Mashine inafanya kazi," alisema.

Alipoulizwa kama atakubali matokeo ya uchaguzi, rais alisema: "Hii ni moja wapo wa njia za udanganyifu - inabidi tujue ni kwa nini, tatizo lilikuwa nini?"

"Sasa tunathibitisha ikiwa hii ilikuwa ya njama," aliongeza.

,

Chanzo cha picha, Reuters

Kura ya maoni ya urais inaashiri kuwa uchaguzi huu na mbio za farasi wawili kati ya Museveni na Wine, lakini ikizingatiwa kuwa rais ameshinda chaguzi sita zilizopita, wachambuzi wanasema huenda akaongeza muda wake madarakani.

Wine ameahidi kukabiliana na ufisadi na kuleta mageuzi makubwa, huku Museveni akihoji kuwa yeye ndiye mdhamini pekee wa utulivu na maendeleo nchini.

Kipindi cha kampeni kilikumbwa na purukushani huku shughuli za upinzani zikivurugwa mara kwa mara - vikosi vya usalama vimeshutumiwa kwa kuwashambulia na kuwaweka kizuizini wafuasi wa Bobi Wine.

Msemaji wa polisi Kituuma Rusoke alipuuzilia mbali malalamishi hayo, akiwashutumu wafuasi wa upinzani, hasa wale wa chama cha Wine cha National Unity Platform (NUP) kuwa wasumbufu.

Mtandao wa intaneti ulizimwa siku ya Jumanne, huku Tume ya Mawasiliano ya Uganda ikisema hatua hiyo ilichukuliwa ili kudhibiti uenezaji wa taarifa ghushi, ulaghai na uchochezi wa ghasia - Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Iimelaani hatua hiyo na kuelezea kuwa "inatia wasiwasi sana".

.