Tume ya Uchaguzi Uganda yaomba radhi kwa changamoto zilizokumba upigaji kura

Uchaguzi huu unafanyika katika mazingira ambayo sio tofauti sana na chaguzi zilizopita hali ya wasiwasi ikiwa imetanda na ulinzi mkali ukiimarishwa.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Ambia Hirsi

  1. Wanajeshi wa Ulaya wawasili Greenland, Trump asema Marekani inakihitaji kisiwa hicho

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Image

    Kikosi cha wanajeshi 15 wa Ufaransa kimewasili katika mji mkuu wa Greenland Nuuk, huku mataifa kadhaa ya Ulaya yakituma wanajeshi huko kama sehemu ya kile kinachoitwa ujumbe wa upelelezi.

    Hatua hiyo, ambayo pia itajumuisha kupelekwa Greenland kwa wanajeshi kutoka mataifa ya Ujerumani, Uswidi, Norway, Uholanzi na Uingereza, inakuja wakati Rais wa Marekani, Donald Trump kuendelea na mpango wake wa kutaka kukimiliki kisiwa hicho cha Arctic, ambacho ni sehemu inayojitegemea ya Denmark.

    Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kikosi cha kwanza kitaimarishwa hivi karibuni na "mali ya ardhini, angani na baharini".

    Mwanadiplomasia mkuu Olivier Poivre d'Arvor anatafsiri kuwasili kwa ujumbe huo kama ishara kali ya kisiasa: "Hili ni zoezi la kwanza... tutaonyesha Marekani kuwa Nato iko."

    Harakati za wanajeshi hao zinakuja baada ya mawaziri wa mambo ya nje wa Denmark na Greenland kuzuru Washington kukutana na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance siku ya Jumatano.

    Kufuatia mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark, Lars Lokke Rasmussen alisema wakati mazungumzo hayo yakiwa ya kujenga, kumesalia "kutokubaliana kwa msingi" kati ya pande hizo mbili na baadaye kukosoa azma ya Trump ya kutaka kuinunua Greenland.

    Pia unaweza kusoma:

  2. CAF yamfungia Eto’o mechi nne, yatoza faini ya dola 20,000

    .

    Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limemfungia Rais wa Shirikisho la Soka Cameroon (Fecafoot), Samuel Eto’o, kucheza au kushiriki shughuli za soka kwa mechi nne.

    CAF pia imemtoza Eto’o faini ya dola 20,000, kufuatia tuhuma za utovu wa nidhamu wakati wa mashindano yanayoendelea ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

    Katika taarifa yake, CAF ilisema Eto’o alipatikana na hatia ya kukiuka misingi ya uungwana na maadili ya michezo, tukio lililotokea wakati wa mchezo wa robo fainali kati ya Cameroon na Morocco.

    Wakati wa mchezo huo wa Januari 9, Rais huyo wa Fecafoot alionekana akionesha hasira kali kufuatia baadhi ya maamuzi ya mwamuzi.

    Cameroon hatimaye ilipoteza mtanange huo kwa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji wa mashindano. Rais wa CAF, Patrice Motsepe, aliyekuwepo uwanjani, inaelezwa alishuhudia moja kwa moja hali ya kutoridhika ya Eto’o.

    Mnamo Januari 12, CAF ilitangaza kuanzisha uchunguzi kuhusu matukio ya vurugu na tabia zisizokubalika miongoni mwa wachezaji na maofisa wakati wa mechi.

    Hata hivyo, Fecafoot ilikataa vikali uamuzi wa CAF, ikiuelezea mchakato huo kuwa unaacha maswali makubwa kuhusu misingi ya haki na usikilizwaji wa kesi kwa haki.

    Katika taarifa yake ya Jumatano, shirikisho hilo lilithibitisha kumuunga mkono Rais wake, huku likidokeza kuwa Eto’o atakata rufaa dhidi ya adhabu hiyo.

    Tangu achukue uongozi wa Shirikisho la Soka Cameroon mwaka 2021, taswira ya Eto’o kama gwiji wa soka barani Afrika imekuwa ikikumbwa na misukosuko ya mara kwa mara.

    Amekuwa akikabiliwa na tuhuma za utendaji usioridhisha, uongozi dhaifu, pamoja na madai ya ukiukwaji mkubwa wa taratibu ndani ya Fecafoot.

    Mshambuliaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 44 amekuwa akikanusha mara kwa mara madai hayo, akisisitiza mafanikio aliyoyapata tangu alipokabidhiwa jukumu la kuongoza soka la Cameroon.

  3. Uchaguzi Uganda 2026: Wagombea wawili wakuu wa urais wapiga kura

    Museveni na Bobi Wine

    Chanzo cha picha, Getty/Reuters

    Mgombea urais wa upinzani nchini Uganda Ssentamu Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine amepiga kura.

    Bobi alifika katika kituo cha Freedom Square Magere akiandamana na mkewe Barbie.

    Bobi Wine wa chama cha NUP anakabiliana na rais wa sasa Yoweri Kaguta Museveni ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 40.

    Hapo awali mgombea urais wa chama cha NRM Yoweri Kaguta Museveni alipiga katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya Upili ya Karo.

    Mara baada ya kupiga kura Museveni alisema mitambo ya kupigia kura iko sawa.

    "Mashine hizi za kibayometriki zinafanya kazi, lakini baadhi ya watu waliziogopa na hawakutaka zifanye kazi." aliliambia shirika la habari la Uganda UBC.

    Museveni alidai kuwa amearifiwa kwamba baadhi ya maafisa wa EC walikuwa hawajatuma maelezo ya waendeshaji wa shughuli hiyo kwenye mashine BVVK kufikia leo asubuhi, data ya kibaolojia ilikuwa bado haijatumwa kwa baadhi ya mashine.''

    Amesema serikali inafanya kila juhudi kuthibitisha kama hitilafu hiyo ilikuwa ya makusudi au la."

    Pia unaweza kusoma:

  4. Tume ya Uchaguzi Uganda yaomba radhi kwa changamoto zilizokumba upigaji kura

    Mpiga Kura

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Tume ya Uchaguzi ya Uganda inasema inajutia usumbufu uliosababishwa na changamoto za kiufundi zilizosababisha kuchelewa kuanza kwa shughuli ya upigaji kura kote nchini.

    Katika taarifa iliyotumwa kwenye mtandao wake wa ‘X’, Mamlaka ya uchaguzi iliwaagiza wasimamizi wa uchaguzi kutumia Sajili ya Kitaifa ya Wapigakura badala ya Vifaa vya Kielektroniki vya Kuthibitisha Wapiga Kura vya Biometric (BVVKs).

    "Wakati huo huo, maafisa wa kiufundi za Tume ya Uchaguzi wanajitahidi kushughulikia changamoto za kiufundi zilizoripotiwa," ilisema taarifa hiyo.

    Shughuli ya upigaji kura kwa sasa unaendelea kote nchini baada ya kucheleweshwa kwa takribani saa nne.

    Hata hivyo, baadhi ya wapiga kura wameripotiwa kuondoka katika vituo vya kupigia kura bila kupiga kura, wakisema hawawezi kusubiri changamoto za kiufundi zitatatuliwa au agizo jipya la kutumia Daftari la Taifa la Wapigakura kutekelezwa.

    Tume ya Uchaguzi haikueleza katika taarifa yake ikiwa saa za upigaji kura zitaongezwa ili kufidia kuchelewa kuanza kwa mchakato huo uliosababishwa na changamoto za kiufundi.

    Soma zaidi:

  5. Uchaguzi Uganda 2026: Upigaji kura waanza baada ya hitilafu za kiufundi

    Wapiga kura Uganda

    Sammy Awami

    BBC News Kampala

    Shughuli ya upigaji kura unaendelea katika vituo mbali mbali vya upigaji kura baada ya mchakato huo kuanza kuchelewa kutokana na hitilafu za kiufundi.

    Katika vituo vingi vya kupigia kura, upigaji kura ulianza hadi saa nne baadaye kuliko ilivyopangwa.

    "Shughuli ya upigaji kura ulicheleweshwa. Ilitakiwa kuanza saa moja asubuhi, lakini tulianza karibu saa 10. Kuna watu wengi hapa sasa, lakini wengine walikwenda kazini, kwa hivyo hatujui ni lini watarudi kupiga kura. Pia hatujui kama muda wa kupiga kura utaongezwa," alisema Sydney Ibrahim, wakala wa NRM aliyezungumza na BBC.

    "Upigaji kura unaendelea vizuri hapa katika Shule ya Greenhill. Hakuna matatizo na mchakato unaendelea vizuri. Ingawa masanduku ya kura yalichelewa kufika, kila kitu sasa kinaendelea vizuri," Toteela Florence, mpiga kura alisema.

    Bado haijulikani ni nini kilisababisha hitilafu hiyo ya kiufundi, japo baadhi ya wapiga kura wanashuku kuwa huenda umesababishwa na kuzimwa kwa mtandao wa intaneti nchini.

    Wakati Tume ya Mawasiliano ya Uganda ilipotangaza kuzima kwa mtandao siku ya Jumanne, iliwahakikishia Waganda kwamba huduma muhimu na baadhi ya kazi muhimu za serikali hazitaathirika kutokan na hatua hiyo.

    Kufikia sasa, haijulikani ikiwa saa za kupiga kura zitaongezwa.

    Hata hivyo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Byabakama Simon hapo awali alisema sheria inaruhusu tume kuongeza muda wa kupiga kura katika mazingira kama haya.

    .
    .
  6. Uchaguzi wa Uganda 2026: Tume ya uchaguzi yatoa mwongozo wa upigaji kura

    Mkuu wa tume ya Uchaguzi Uganda Jaji Simon Byabakama.

    Chanzo cha picha, Uganda Electoral Commission

    Maelezo ya picha, Mkuu wa tume ya Uchaguzi Uganda Jaji Simon Byabakama.

    Tume ya Uchaguzi nchini Uganda imetoa mwongozo kuhusu mchakato wa upigaji kura katika vituo vya kupigia kura.

    Hii ni baada hitilafu za kiufundi kuripotiwa kote nchini leo asubuhi na kusababisha shughuli ya upigaji kura kukwama.

    Tume hiyo sasa imewaelekeza maafisa wanaosimamia uchaguzi kuwaruhusu wapiga kura kutumia daftari ;a kitaifa la wapiga kura.

    "Pale ambapo mashine ya BVVK itashindwa kufanya kazi, mchakato wa kupiga kura unapaswa kuanza mara moja kwa kutumia daftari la kitaifa la wapiga kura," alisema mkuu wa Tume hiyo Jaji Simon Byabakama.

    Jaji Byabakama aidha amesema: "Vituo vya kupigia kura vitaendelea kuwa wazi hadi wapiga kura wote waliojiandikisha na waliopo kwenye folenii ifikapo saa kumi jioni wawe wamepiga kura zao."

    Soma zaidi:

  7. Trump asema 'mauaji yamekoma' nchini Iran baada ya msako mkali wa maandamano

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais Donald Trump amesema ameambiwa "mauaji nchini Iran yamekoma", lakini rais wa Marekani haijaondoa uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya nchi hiyo kutokana na matukio ya ukandamizaji dhidi ya waandamanaji wanaopinga serikali.

    Kulingana na makundi ya haki za binadamu, zaidi ya watu 2,400 wameuawa katika ukandamizaji wa hivi karibuni uliofanywa na mamlaka ya Iran kujibu maandamano ya kitaifa.

    Matamshi ya Trump Jumatano yanatolewa baada ya Marekani na Uingereza kupunguza idadi ya wafanyakazi katika kambi ya anga ya Al-Udeid huko Qatar.

    Maafisa waliiambia CBS, mshirika wa BBC wa Marekani, kwamba kujiondoa kwa sehemu kwa Marekani ni "hatua ya tahadhari".

    Anga ya Iran ilifungwa kwa karibu safari zote za ndege kwa saa tano usiku kucha, huku mashirika kadhaa ya ndege yakitangaza kwamba yatabadilisha njia za ndege kuzunguka Iran.

    Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza pia imefunga kwa muda ubalozi wa Uingereza mjini Tehran, ambao sasa utafanya kazi ukiwa mbali, msemaji wa serikali alisema.

    Hapo awali Trump alitishia "kuchukua hatua kali sana" dhidi ya Iran ikiwa serikali ingewaua waandamanaji, baada ya ripoti kuibuka.

    Soma zaidi:

  8. Marekani yazindua awamu ya pili ya mpango wa kukomesha vita Gaza

    ,

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mjumbe wa Marekani Steve Witkoff ametangaza kuanza kwa awamu ya pili ya mpango wa Rais Donald Trump wa kukomesha vita huko Gaza, huku serikali ya Palestina yenye kuendeshwa na wataalam ikianzishwa katika eneo hilo.

    Chini ya awamu ya kwanza, Hamas na Israel zilikubaliana kusitisha mapigano mnamo mwezi Oktoba, pamoja na kubadilishana mateka na wafungwa, kujiondoa kwa kiasi fulani kwa Israel, na ongezeko la misaada.

    Witkoff alisema awamu ya pili pia itajumuisha ujenzi mpya na kuondolewa kabisa kwa wanajeshi wa Gaza, ikiwa ni pamoja na kupokonywa silaha kwa kundi la Hamas na makundi mengine ya Wapalestina.

    "Marekani inatarajia Hamas kutekeleza kikamilifu majukumu yake," ilionya, ikibainisha kuwa haya ni pamoja na kurejeshwa kwa mwili wa mateka wa mwisho wa Israeli aliyekufa. "Kushindwa kufanya hivyo kutasababisha athari mbaya."

    Hata hivyo, mambo mawili muhimu ya awamu ya pili yanaweza kuwa changamoto.

    Hamas hapo awali ilikataa kuachana na silaha zake kabla ya kuundwa kwa taifa huru la Palestina, na Israeli haijajitolea kujiondoa kikamilifu Gaza.

    Soma zaidi:

  9. Ukraine yatangaza hali ya dharura katika sekta ya nishati wakati huu wa baridi kali

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ukraine imetangaza hali ya dharura katika sekta ya nishati nchini humo, ikilenga zaidi Kyiv, huku Urusi ikiendelea kufanya mashambulizi na kuwaacha maelfu ya wakazi bila umeme.

    Rais Volodymyr Zelensky aliishutumu Moscow kwa kutumia kimakusudi hali ngumu ya majira ya baridi kali kama sehemu ya mkakati wake wa vita, huku halijoto ya usiku kucha huko Kyiv ikishuka hivi karibuni hadi karibu -20C.

    Tamko hilo linakuja Rais Donald Trump, akisema anasitisha juhudi za kupata makubaliano ya amani ili kukomesha karibu miaka minne ya vita na Urusi.

    Aliambia shirika la habari la Reuters Jumatano kwamba Ukraine "haiko tayari kabisa kufikia makubaliano" ikilinganishwa na rais wa Urusi Vladimir Putin.

    Soma zaidi:

  10. Kwa Picha: Shughuli ya upigaji kura ilivyotatizika Uganda

    .
    .
    .
    .
  11. Uchaguzi Uganda 2026: Upigaji kura wachelewa kuanza

    .

    Shughuli ya kupiga kura imechelewa kuanza katika maeneo mengi nchini Uganda.

    Awali ilitarajiwa kuwa vituo vingefunguliwa saa moja asubuhi, lakini kufikia saa mbili na nusu asubuhi, wapiga kura walikuwa bado hawajaanza kupiga kura.

    Zaidi ya raia milioni 21 wanatazamiwa kushiriki uchaguzi wa leo kuwachagua rais na wabunge.

    Mwanahabari wetu RoncliffeOdit amezuru vituo kadhaa na anaripoti kwamba mashine za kuwatambua wapiga kura ndio changamoto kubwa.

    Soma zaidi:

  12. Denmark yaonya juu ya 'kutokubaliana' na Marekani kuhusu eneo la Greenland

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Waziri wa mambo ya nje wa Denmark amesema kuna "kutokubaliana" na Marekani kuhusu eneo la Greenland baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu ya White House.

    Lars Lokke Rasmussen alisema mkutano na Makamu wa Rais JD Vance na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio siku ya Jumatano ulikuwa "wa kuambiana ukweli na wenye tija". Lakini aliongeza kuwa Rais wa Marekani Trump alikuwa akisisitiza "kuchukua" eneo la Greenland jambo ambalo "halikubaliki kabisa".

    "Tuliweka wazi kabisa kwamba hili sio miongoni mwa maslahi ya [Denmark]," alisema.

    Baadaye Trump alisisitiza nia yake ya kuchukua kisiwa hicho chenye utajiri wa rasilimali, msimamo ambao umewasumbua vichwa hata washirika wake kote Ulaya na kuchochea mvutano na Nato.

    Soma zaidi:

  13. Uchaguzi Uganda 2026: Usalama waimarishwa huku mawakala wa vyama mbalimbali wakiwa tayari vituoni

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maafisa wa usalama wamesambazwa katika maeneo mbalimbali wakati raia wanaamkia siku ya kupiga kura.

    Tayari wapiga kura wameanza kuwasili katika vituo vya kupiga kura ingawa asubuhi hii bado ni taratibu.

    Maafisa wa usalama pia wanajishughulisha na kuondoa picha za wagombea mbalimbali ambazo zilikuwa zimesambazwa wakati wa kampeni.

    Waandishi wa habari waliokita kambi katika eneo hilo wameshuhudia maafisa wa usalama katika karibu kila pembe ya jiji la Kampala wakiwa kwenye magari huku wengine wakiwa wanatembea kwa miguu.

    Lakini pia ifahamike kuwa mjini Kampala watu wanaendelea na shughuli zao kama kawaida ingawa idadi ya maafisa wa polisi waliosambazwa inaonekana kama kwa kiasi fulani kuwatia hofu raia.

    Eneo la Soroti watu wanazuiliwa kutoka nje ikifika maeneo ya jioni.

    Pia mawakala wa vyama tofauti tofauti wameshafika kwenye vituo vya kupiga kura.

    Shughuli ya upigaji kura nchini Uganda inaanza saa moja asubuhi na kuendelea hadi saa kumi jioni na watakaokuwa kwenye milolongo wakati huo wataruhusiwa kuendelea kupiga kura.

    Soma zaidi:

  14. Uchaguzi Uganda 2026: Matayarisho siku ya upigaji kura yako tayari

    .

    Maandalizi ya leo ambayo ni siku ya upigaji kura nchini Uganda yamekamilika.

    Vifaa vya kupigia kura na vifaa vingine vilifikishwa katika vituo mbalimbali vya usambazaji hapo jana huku matarajio yakiwa ni kuvipeleka katika vituo vya kupigia kura mapema asubuhi leo.

    Mawakala wa vyama na wagombea walikuwepo kwenye vituo vya usambazaji ili kuhakikisha vifaa ni vya kweli na viko katika hali nzuri, kama inavyotakiwa kisheria.

    Katika vituo ambavyo BBC ilitembelea, mawakala walisema wameridhishwa na vifaa hivyo lakini wakaonya kwamba wasiwasi wao mkuu unasalia kuwa siku ya leo ambayo raia wanakwenda debeni kufanya maamuzi.

    Pia walilalamikia kuzimwa kwa mtandao, jambo ambalo wanasema limetatiza mawasiliano na uratibu miongoni mwao.

    Hapo jana, maafisa wa upigaji kura walikuwa na fursa ya kujiandaa kwa kupokea vifaa vilivyokuwa vinasambazwa na hata kufanya mazoezi ya kuiga ili kuhakikisha wanajifahamisha na mchakato wa upigaji kura ipasanyo.

    Soma zaidi:

  15. Uchaguzi Uganda 2026: Raia wanapiga kura kumchagua rais

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Raia wa Uganda wanapiga kura leo katika uchaguzi wa rais, ambapo Rais Yoweri Museveni - ambaye amekuwa madarakani kwa miongo minne - anawania muhula mwingine.

    Shughuli ya upigaji kura inafanyika wakati intaneti imeminywa.

    Uchaguzi huu unafanyika katika mazingira ambayo sio tofauti sana na chaguzi zilizopita hali ya wasiwasi ikiwa imetanda na ulinzi mkali ukiimarishwa.

    Rais aliye madarakani, Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka themanini na moja, anawania muhula wa saba baada ya kuwa madarakani kwa zaidi ya miaka arobaini, akiwa kinyang’anyironi na wagombea wengine saba.

    Mpinzani wake mkuu, ambaye ana karibu nusu ya umri wake, ni Robert Kyagulanyi, almaarufu Bobi Wine, ambaye anagombea urais kwa mara ya pili na kuungwa mkono sana na wapiga kura vijana.

    Waangalizi wa uchaguzi hawaruhusiwi kisheria kutoa maoni yao kuhusu mchakato huo kupitia njia za mawasiliano zilizozoeleka au mitandao ya kijamii, na hivyo kuzuia uchunguzi huru wa umma wa shughuli ya upigaji kura inavyoendeshwa.

    Vituo vya kupigia kura vinafunguliwa saa moja asubuhi na vitafungwa saa kumi alasiri kwa saa za eneo, huku mshindi akitarajiwa kutangazwa ifikapo Jumamosi mchana.

    Soma zaidi:

  16. Hujambo msomaji wetu na karibu katika matangazo yetu mubashara. Leo ni siku ambayo raia wa Uganda wanapiga kura na miongoni mwa tuliokuandalia ni kukujuza jinsi shughu hiyo inavyoendelea. Karibu uungane nasi hadi tamati.