Vita vimembadilisha Zelensky - lakini sasa ni wakati wa kubadilika tena

- Author, James Waterhouse
- Nafasi, BBC Kyiv
- Muda wa kusoma: Dakika 5
"Mfanyabiashara bora katika historia." Donald Trump aliwahi kumwita Volodymyr Zelensky kwa sababu ya kiasi cha misaada ambayo Marekani imetoa kwa Ukraine.
Iwe jina hilo ni la haki au la, jukumu la Zelensky katika kuiweka nchi yake katika jicho la kimataifa na kuwashawishi washirika kutoa misaada ya kijeshi kwa hakika ni mambo muhimu katika vita vya Ukraine.
Alitoka kuwa mchekeshaji hadi rais wa wakati wa vita. Mwaka 2022 aliamua kubaki Kyiv pale wanajeshi wa Urusi walipokaribia mji mkuu. Uamuzi huo ulimaanisha Ukraine itaendelea kupambana.
Kutokana na kutotabirika kwa muhula wa pili wa Trump - kufuatia kutupiana maneno kati ya wawili hao mwezi Februari katika Ikulu ya Marekani - Zelensky sasa anaweza kubadilika tena.
Kuna changamoto kubwa mbili; kupata amani na kulinda maslahi ya nchi yake.
Mahesabu ya Zelensky

Chanzo cha picha, Getty Images
Muungano wa mataifa yaliyoahidi kusimama na Ukraine, watakutana leo katika makao makuu ya Nato - bila uwepo wa Marekani.
Kabla ya Trump kuingia tena madarakani, kiongozi wa Ukraine aliyashawishi mataifa ya magharibi kutoa ulinzi wa anga, vifaru, roketi na ndege za kivita, huku mataifa kama Ujerumani yakisitasita kutokana na hofu ya vita kuongezeka, kabla ya kuitikia ombi lake.
"Zelensky alitumia akili na alipiga mahesabu katika siku za mwanzo za vita," anasema Ed Arnold kutoka taasisi ya ulinzi na usalama, ya Royal United (Rusi).
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Uamuzi wake kwenda katika mkutano wa usalama wa Munich wiki mbili kabla ya uvamizi wa Urusi, licha ya kushauriwa ni hatari kwa usalama, ulikuwa muhimu, anasema Bw Arnold.
Serhiy Leshchenko, mshauri wa ofisi ya Zelensky, anaeleza: "Lazima tuonekane na ulimwengu. Ikiwa maoni ya umma yatakuwa upande wa Ukraine, kuna fursa nzuri zaidi ya kupata usaidizi kutoka jumuiya ya kimataifa."
Leshchenko anagusia video za kila siku za Zelensky, tangu kuanza kwa uvamizi.
Ushindi wa Ukraine katika vita vya Kyiv ulimtia nguvu Zelensky, na kuongeza kasi ya kuomba msaada wa kijeshi kutoka kwa washirika wa nchi za magharibi.
Mwaka 2022, Zelensky aliweza kuonyesha faida ya usaidizi huo baada ya maeneo mengi ya Ukraine, ikiwa ni pamoja na jiji la Kherson, kukombolewa.
"Amepitia mawaziri wakuu wanne wa Uingereza tangu kuanza kwa vita ... na wote wametia saini maazimio mapya na Ukraine, tena kupitia Zelensky.
"Ameweza kukabiliana na mabadiliko katika siasa za kitaifa ndani ya Ulaya katika kipindi chake chote," anasema Arnonal.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hata mafanikio makubwa yaliposhindikana, ujumbe wa Zelensky haukubadilika - na kadiri muda ulivyosonga, hilo lilianza kuleta madhara.
Kwa mfano, baada ya Ukraine kushindwa kukabiliana na mashambulizi katika majira ya kiangazi ya 2023, manufaa ya kuiunga mkono Kyiv yalizidi kutiliwa shaka na Wana-Republican wa Marekani.
Maria Zolkina, mtaalamu wa masuala ya usalama na migogoro katika Wakfu wa Democratic Initiatives, taasisi yenye makao yake mjini Kyiv, anaamini Zelensky anahusika kwa kiasi fulani.
"Yeye na watu wake wa karibu waliegemea kwenye utamaduni wa kwamba kila mara wawe wanadai silaha tu wanapozungumza na washirika wao. Ingawa hilo lilifanya kazi vizuri mwaka 2022, lakini kwa Marekani na wengine aina hii ya ujumbe uliacha kufanya kazi mwaka 2023," anasema.
Zelensky na Trump

Chanzo cha picha, Getty Images
Tarehe 27 Septemba 2024, katika ukumbi wa New York, mambo yalibadilika kwa Ukraine kutoka kwa mshirika wake wa kijeshi na kisiasa, Marekani.
Siku hiyo, zaidi ya mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wa Rais wa Marekani, Zelensky alikuwa na mkutano wa dakika za mwisho na Trump katika jengo la Trump Tower.
Mvutano kati ya wawili hao uliibuka kabla ya mkutano huu: Zelensky alidai siku chache mapema kwamba Trump "hajui jinsi ya kumaliza vita," baada ya Trump kudai atamaliza vita kwa "siku moja."
Baada ya mkutano wa Trump Tower, watu hao wawili waliibuka. Licha ya kutangaza "mtazamo wa kawaida" wa kutaka kumaliza vita, mwonekano wa wawili hao ulipendekeza ukosefu wa maelewano.
Wawili hao hawakukutana tena hadi miezi mitano baadaye katika Ofisi ya Ikulu, ambapo mkutano wao ukawa janga la kidiplomasia kwa Kyiv.
Aliyekuwa balozi wa Ukraine nchini Uingereza, Vadym Prystaiko kabla ya kufutwa kazi mwaka wa 2023. Kyiv hakutoa sababu rasmi ya kufutwa kazi, lakini ilikuja baada ya Bw Prystaiko kukosoa jibu la Zelensky kuhusu shukrani kwa msaada wa kijeshi wa Uingereza. Anasema:
"Zelensky hajawahi kuwa mwanadiplomasia. Hajawahi kuwa kiongozi wa kawaida wa kisiasa ambaye huwabusu watoto na kupeana mikono."
Trump amemlaumu Zelensky kwa kuanzisha vita hivyo, na kumwita "dikteta," huku kiongozi wa Ukraine akimshutumu mwenzake wa Marekani kwa "kuishi katika upotovu wa Urusi."
"Kuna pembetatu kati ya utawala wa Marekani, Kremlin na Kyiv. Ukraine inachukuliwa kuwa sehemu ndogo ya pembetatu hii. Kwa Trump, Zelensky hayuko kwenye ligi moja, na hilo ndilo tatizo," anasema mtaalamu wa siasa Volodymyr Fesenko kutoka kituo cha Pento for Political Studies.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Vita hubadilisha kila mtu, vimetubadilisha sote kwa namna fulani. Lakini sidhani Zelensky amebadilika - kwa uzuri au ubaya katika baadhi ya matukio," anasema Olga Onuch, profesa wa Siasa za Ukraine katika Chuo Kikuu cha Manchester.
"Ni wazi kabisa kwamba baadhi ya washirika wanasema ni vigumu kufanya mazungumzo na Zelensky. Kwa nini? Kwa sababu ameweka mistari mekundu ambayo anaishikilia."















