Kwa nini Putin yuko kimya wakati Trump anazidisha ubabe?

cx

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Brian Windsor, Daria Mosolova
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Zamani ikiwa Marekani ingefanya vitendo vya uchokozi katika ardhi ya kigeni, kungekuwa na jibu la haraka na kali kutoka Urusi. Lakini, hali inaonekana tofauti kidogo tangu mwaka 2026.

Marekani ilifanikisha kukamatwa kwa kiongozi wa Venezuela Nicolas Maduro na kukamatwa kwa meli ya mafuta yenye bendera ya Urusi. Pia inatishia kuivamia Greenland.

Licha ya haya yote kutokea, Kremlin bado iko kimya. Urusi imewekeza sana katika maeneo kama Venezuela na Aktiki ili kupambana na ushawishi wa wa Marekani. Hata hivyo, Rais wa Urusi Vladimir Putin bado hajatoa kauli yoyote kuhusu yaliyotokea.

Tangu kuanza kwa mwaka mpya, Putin ameonekana hadharani Januari 6, aliposhiriki sherehe za Krismasi.

Msemaji wake, Dmitry Peskov, na chaneli za televisheni za serikali ya Urusi pia hazijatoa maoni yoyote kuhusu suala hilo. Ukimya huu pengine unaonyesha kwamba Putin hataki kuvuruga mazungumzo nyeti ambayo Urusi inayafanya na Marekani kuhusu Ukraine.

“Kuna maslahi kwa Urusi”

oo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maafisa wa Marekani wakimsafirisha Nicolas Maduro na mke wake

Donald Trump ameanza mwaka 2026 kwa kuonyesha nguvu zake kwa njia ya ajabu. Kiongozi wa Venezuela Nicolas Maduro amekamatwa na kupelekwa New York kwa mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya. Zaidi ya hayo, amesema nchi hii ya Amerika Kusini kwa sasa iko chini ya udhibiti wa Marekani kwa muda.

Wachambuzi katika vyombo vya habari duniani wanasema kuondolewa Maduro kutoka serikalini kuna maslahi kwa Urusi, kwani Marekani imeipa Kremlin uhuru wa kufanya vivyo hivyo.

Fyodor Lukyanov, mtaalamu wa sera za kigeni aliye karibu na Kremlin, anasema kukamatwa kwa Maduro ni ushahidi wa mkakati mpya wa usalama wa Marekani.

Urusi imewekeza Venezuela

l

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Urusi imewekeza nchini Venezuela kwa miongo kadhaa
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Urusi imewekeza sana nchini Venezuela kwa miongo kadhaa, lakini ushawishi wake katika eneo hilo umepungua kwani imeelekeza rasilimali kwenye vita vya Ukraine.

Hanna Note, mkurugenzi wa Eurasia Nonproliferation Program katika Kituo cha James Martin cha Mafunzo ya Nonproliferation, ameiambia BBC, sababu ya Urusi kujizuia kukosoa kilichotokea Venezuela ni kwamba rais anaepuka kumkasirisha Trump kwa wakati huu, kwa sababu Putin ana masuala makubwa ya kushughulikia.

Hana anaamini kipaumbele cha Urusi ni kumfanya Trump kuwa upande wa Urusi katika suala la Ukraine au kumzuia Trump asiipinge Urusi.

"Kremlin imefanikiwa katika suala hili kwa mwaka uliopita. Urusi inataka kuendelea na mafanikio haya. Kwa sababu Ukraine ndiyo kipaumbele chake kikubwa," anasema.

"Putin ana jambo zito zaidi la kujadili na Trump. Ni Ukraine," anasema.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imekaribisha uteuzi wa Delcy Rodriguez kama rais wa mpito wa Venezuela. Imesema ni hatua ya kuelekea utulivu katika kukabiliana na shinikizo la nje.

Wizara hiyo imesema Venezuela ina haki ya kuamua mustakabali wake bila shinikizo la nje, bila kuitaja moja kwa moja Marekani.

Meli ya Urusi yakamatwa

p

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Marekani imeikamata meli ya mafuta ya Marinera yenye bendera ya Urusi.

Urusi pia ilijibu kwa tahadhari baada ya Marekani kuikamata meli ya mafuta ya Marinera iliyokuwa na bendera ya Urusi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ilitaka tu kuachiliwa huru kwa wafanyakazi wa Urusi waliokuwa ndani ya meli ya Marinera, na imesema Trump amekubaliana na hilo.

Licha ya haya yote kutokea, na licha ya ripoti za uwepo wa meli za kijeshi za Urusi katika eneo hilo, Urusi haijasema kuwa itairudisha meli hiyo ya mafuta au kupambana ili kuipata meli hiyo.

Urusi pia haijatoa dalili yoyote kwamba itachukua hatua za kulipiza kisasi dhidi ya Marekani au meli zingine zenye bendera za kigeni.

Kujizuia huku kwa Urusi kumekosolewa vikali.

Mbunge Alexei Zhuravlev, ambaye anataka Urusi ijibu kijeshi amesema, "kama sehemu ya hatua za kulipiza kisasi, meli mbili za Walinzi wa Pwani wa Marekani zinapaswa kuzamishwa kwa kutumia torpedo (kombora la majini).

Blogu ya Telegram inayounga mkono Kremlin, Visioner, iliwaambia wasomaji wake kukamatwa kwa meli ya mafuta katika maji ya kimataifa ni shambulio dhidi ya Urusi.

Januari 2025, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema Urusi inafuatilia kwa karibu hatua yoyote kuhusu Greenland.

Alielezea madai ya Marekani katika kisiwa hicho cha Aktiki, ambacho ni mali ya Denmark, kama suala la pande mbili kati ya Marekani na Denmark.

Ingawa Trump alisema Januari 7 kwamba Marekani inakusudia kuchukua udhibiti wa eneo hilo, hakuna taarifa rasmi Kremlin hadi sasa.

Waungaji mkono wa serikali ya Urusi wanaonekana kufurahishwa na madai ya kwamba Trump atachukua udhibiti wa Greenland.

Kwa sababu wanaona ni ishara ya udhaifu wa Ulaya. Wanaiona kama hoja yenye nguvu ya kuhalalisha vitendo vya Urusi nchini Ukraine.