Unapaswa kufanya nini unapokutana na simba?

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, unafahamu cha kufanya ikiwa utakutana na simba au wanyamapori wengine hatari?
Hakuna kinachochanganya hisia kama kukutana na simba wa porini.
Ni tukio la kushangaza, la kutisha na la kipekee lakini pia linaweza kuwa hatari ikiwa hutachukua tahadhari zinazofaa.
Simba mara chache huwawinda wanadamu ili kupata chakula.
Watajaribu kuzuia makabiliano wakati mwingi.
Hata hivyo, kumekuwa na visa hapo awali wakati simba waliwawinda wanadamu kama wale wafanyikazi waliokuwa wakijenga reli eneo la Tsavo na kuhangaishwa na simba waliokuwa katika mazingira yao.
Hii ni kwa sababu ya uhaba wa chakula au majeraha ambayo huwazuia simba hao kuwinda na kugeukia binadamu ambao ni rahisi kuvamia.
Kisa cha hivi punde, nchini Kenya ni siku ya Jumamosi tarehe 19 mwezi Aprili ambapo simba alivamia familia moja iliyoko eneo la Emakoko linalopakana na mbuga ya wanyama ya Nairobi.
Msichana wa miaka 14 aliuawa na simba viungani mwa jiji la NairobiShirika la Huduma ya Wanyamapori nchini (KWS) lilisema.
Mtoto huyo alinyakuliwa kutoka kwa makazi ya watu kwenye shamba karibu na Hifadhi ya Kitaifa ya Nairobi, kulingana na shirika la uhifadhi.
Kijana mwingine alitoa taarifa hiyo na walinzi wa KWS walifuata nyayo hadi Mto Mbagathi ulio karibu, ambapo walipata mabaki ya msichana huyo wa shule ya msingi.
Simba huyo hajapatikana lakini KWS ilisema kuwa imeweka mtego na kupeleka timu za msako kumtafuta mnyama huyo.
Shirika hilo limeongeza kuwa hatua za ziada za usalama zimechukuliwa ili kuzuia shambulio lingine kama hilo.
Kuongezeka kwa mashambulizi ya simba
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Utafiti uliochapishwa mwaka wa 2023 katika jarida la PLOS Biology uligundua kuwa mashambulizi ya wanyama wanaokula nyama yameongezeka tangu miaka ya 1950, huku Afrika na Asia zikiwa na visa vilivyoongezeka zaidi.
Sehemu ya sababu hiyo ni kupunguzwa kwa makazi asilia kutokana na ongezeko la joto duniani .
Wakati huo huo, wanadamu wanazidi kuingia katika maeneo ambayo hapo awali yalikuwa yanamilikiwa na wanyamapori kadiri idadi ya watu inavyoongezeka.
Hifadhi ya Kitaifa ya Nairobi iko kilomita 10 tu kutoka katikati mwa jiji na ni nyumbani kwa wanyama kama vile simba, nyati, twiga, chui na duma.
Imezungushiwa uzio kwa pande tatu ili kuzuia wanyama kuzurura mjini lakini iko wazi kuelekea kusini ili kuwezesha wanyama kutoka na kuingia eneo hilo.
Wakati simba mara nyingi huingia kwenye migogoro na binadamu nchini Kenya, hasa kuhusu mifugo, si jambo la kawaida kwa watu kuuawa.
Mwaka jana, picha za CCTV zilinasa wakati simba alipomshika mbwa aina ya Rottweiler kutoka kwa nyumba nyingine karibu na Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi.
KWS pia iliripoti kuwa mzee wa miaka 54 aliuawa na tembo siku ya Jumamosi. Kisa hicho kilitokea katikati mwa eneo la Nyeri, takriban kilomita 130 (maili 80) kaskazini mwa Nairobi.
Tembo huyo alikuwa kwenye msitu wa Mere alipomvamia mwanaume huyo ambaye alipata majeraha mabaya kifuani, kuvunjika mbavu na majeraha ya ndani.
Alipelekwa hospitali ambapo alifariki kutokana na majeraha yake.
Na wakaazi wa Rongai mji ulio karibu na mbuga ya wanyama pia wamekuwa wakirusha video kwa mitandao zikionyesha simba wakizurura majumbani mwa watu usiku.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanadamu wanapaswa kufanya nini ikiwa watakutana na simba?
Hakuna mbinu maalum iliyowekwa kukabiliana na tishio la kuvamiwa wanyama pori.
Lakini Dk. Rae Wynn-Grant, Mtaalamu wa Ikolojia ya Wanyamapori na mwenyeji Mwenza wa Mutual of Omaha's Wild Kingdom Protecting the Wild, anasema unaweza kuja ukiwa tayari.
"Ninapendekeza kujijulisha na tabia na makazi ya simba wa milimani ikiwa unaishi au unapanga kutembelea maeneo ambayo wapo na kuwa makini sana," anasema.
Pia anashauri kubeba vijiti au vitoa kelele "ili usimshtue mnyama na kuwapa muda wa kutosha wa kuondoka kutoka kwako".
Fahamu mambo matano unapaswa kufanya ili ujisalimishe kutoka kwa simba anayekuvamia au unapotangamana nao.
1. Usikimbie – Hii si mbio za mita 100
Kwa kawaida, simba wa mlimani atakimbia mara moja anaposikia au kuona binadamu, Bensen anasema. Ikiwa hatokimbia chaguo lako bora ni kuwa kuonekana kama tishio iwezekanavyo.
Simba ni wakimbiaji hodari, wanaweza kufikia kasi ya hadi 60 km/h kwa muda mfupi.
Ukianza kukimbia, unageuka moja kwa moja kuwa mawindo.
Kwao, hiyo ni ishara tosha kwamba "chakula" kimejitokeza.
Badala yake, simama wima na jaribu kutuliza moyo wako.
Hii ni vita ya kisaikolojia, na mshindi ni yule anayebaki mtulivu.
Keith Bensen, mwanabiolojia wa wanyamapori katika Huduma ya Hifadhi ya Kitaifa, asema kwamba kuepuka kupanda milima peke yako ni shauri zuri la kufuata ukiwa nje, pia.
2. Usimgeuzie Mgongo Simba
Hii ni kanuni ya dhahabu ya porini.
Kuachana na kutazamana na simba ni kama kusema: "Sina ulinzi, nichukue." Badala yake, songa nyuma taratibu ukiendelea kumwangalia moja kwa moja machoni hadi upate umbali salama.
Ukisonga nyuma endelea kupiga kelele na kupunga mikono au mavazi yako wakati wote." Anasema Bensen mnyama kukushambulia itakuwa "nadra sana" lakini ikiwa hilo litafanyika basi "kupigana kwa bidii iwezekanavyo" kwani ndilo chaguo lako bora.
Pendekezo hilo ni muhimu kukumbuka, haswa kwa sababu ni ushauri sawa kabisa unapaswa kufuata unapokutana na dubu mweusi(Black bear), Bensen anasema.
Dubu wa kahawia (Brown Bear) hawaogopi kirahisi kama dubu weusi, kwa hivyo usijaribu kuwatisha, na hupaswi kukimbia, kulingana na Kamati ya Interagency Grizzly Bear , shirika la Montana linalojitolea kurejesha na kuhifadhi dubu hao.
Badala yake, jitahidi utulie na urudi nyuma polepole. Dubu akikushambulia, usipigane naye - jifanye tu kama uliyekufa.
3. Panua mwonekano wako
Kwa mujibu wa shirika la Geographical Kenya inapendekea unapokutana na simba jifanye kuwa mrefu uonekane wazi.
Simba anapokutathmini, anajaribu kuamua kama wewe ni tishio au chakula. Jionyeshe kuwa mkubwa.
inua mikono juu, pepea jaketi au vazi lolote.
Unapojiongeza kwa sura, unaweza kumfanya aone huwezi kushughulikiwa kirahisi.
4.Tumia sauti na vitu vilivyo karibu
Kama unacho kitu cha kurusha kama jiwe au fimbo kitumie kumtupia simba ukiwalenga kichwani au kwenye macho.
Piga kelele kwa nguvu au vuma kwa sauti nzito.
Lengo ni kumtisha na kumfanya ajue wewe si mwepesi kushambuliwa.
5.Usikaribie simba wanaojamiiana au walio na watoto wao
Simba dume huwa wakali sana wakati wa kujamiiana na wenza wao.
Naye malkia wa mbuga hulinda watoto wao kwa ujasiri mkubwa.
Usijaribu kuwakaribia, hata kama inaonekana kama fursa nzuri ya kupiga picha.
Kama huna uzoefu, kamwe usiingie porini peke yako.
Ukiwa pekee unaonekana kuwa mnyonge na ni rahisi kushambuliwa.
Kuwa na mwongozo au mtu mwenye uzoefu ni njia bora ya kuongeza usalama wako.
Usikate tamaa kuna watu waliopona mashambulizi ya simba kwa kupigana kwa ujasiri.
Mashambulizi ya wanyama hutokea, lakini wataalam wana wasiwasi kuhusu kuenea kwa habari zisizo sahihi.
McClelland anasema kwamba tunapoona mashambulizi ya wanyama katika habari, inaweza kuwa rahisi kudhani kwamba wanyama wanaokula nyama, ikiwa ni pamoja na simba wa milimani, ni viumbe wabaya, wenye ukatili kwa asili na wakali wakati sivyo.
Kwa kweli, wanataka tu maeneo yao yaheshimiwe, na inawapasa wanadamu kuzingatia hilo.















