Siri zinazozunguka operesheni ya kijasusi ya kumkamata Maduro

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Gordon Corera
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Wiki moja baada ya operesheni ya Marekani nchini Venezuela ambayo ilifikia kilele cha kukamatwa kwa Nicolás Maduro, maelezo ya kijasusi yanayozunguka misheni hiyo yanaanza kuwa wazi, ingawa bado kuna baadhi ya mafumbo.
Misheni hiyo ilihitaji miezi kadhaa ya kupanga na kukusanya taarifa za kijasusi. Inaaminika mwezi Agosti, shirika la kijasusi la Marekani, CIA lilituma kwa siri timu ya maafisa nchini Venezuela.
Marekani haina ubalozi nchini humo, kwa hivyo timu hiyo haikuweza kutumia ulinzi wa kidiplomasia na ilifanya kazi katika kile kinachojulikana katika ulimwengu wa ujasusi kama "eneo lililofungwa." Lengo lao lilikuwa kutambua maeneo na kuajiri watu ambao wangeweza kutoa msaada.
Maafisa wa Marekani wamesema walikuwa na chanzo maalum kilichotoa taarifa za kina kuhusu mahali alipo Maduro, jambo ambalo lilikuwa muhimu kwa operesheni hiyo.
Utambulisho wa chanzo hicho kwa kawaida unalindwa, lakini ikajulikana kwamba chanzo hiki kinatoka serikalini na lazima kiko karibu sana na Maduro na ni sehemu ya watu wake wa karibu ili kujua yuko wapi na lini.
Taarifa zote za kijasusi zilizokusanywa ardhini zilitumika kupanga operesheni hiyo, pamoja na taarifa za kiufundi kama vile ramani na picha za setilaiti.
Operesheni

Chanzo cha picha, Trump
Ukubwa, kasi, na mafanikio ya operesheni hiyo ni mambo ambayo hayakutegemewa.
"Kila kitu kilifanya kazi kikamilifu," anaelezea David Fitzgerald, mkuu wa zamani wa operesheni za Amerika Kusini za CIA, ambaye pia alishiriki katika kupanga misheni hiyo na jeshi la Marekani.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Sio mbinu za kijeshi zinazoendesha operesheni hiyo, bali ni ujasusi."
Karibu ndege 150 zilishiriki katika misheni hiyo, huku helikopta zikiruka mita thelathini tu juu ya ardhi ili kufika kwenye eneo la Maduro.
Hata hivyo, kuna mafumbo kadhaa yanayosalia. Mojawapo ni jinsi Marekani ilivyoweza kuifumba macho Caracas ili kuruhusu kuwasili kwa vikosi maalum.
"Umeme wa Caracas ulizima na kwa kiasi kikubwa ni kutokana na uzoefu fulani tulio nao; kulikuwa na giza na ilikuwa hatari," alitangaza Rais wa Marekani Donald Trump.
Ukweli ni kwamba Kamandi ya Mtandao ya Marekani ilipokea shukrani za umma kwa jukumu lake katika operesheni hiyo na kuna uvumi kwamba wadukuzi wa kijeshi wa Marekani waliingilia mitambo ya Venezuela mapema ili kuzima gridi ya umeme wakati unaofaa.
Kushindwa kwa ulinzi wa anga wa China na Urusi pia kumezua uvumi kuhusu aina ya teknolojia ambayo Marekani iliitumia angani ili kusaidia operesheni hiyo.
Kamandi ya Anga za Juu ya Marekani, ambayo huendesha satelaiti, pia inaelezwa iliunda "njia" ya vikosi maalum kuingia bila kugunduliwa.
Ndege zisizo na rubani pia zinaaminika zilitumika. Maelezo kamili ya operesheni hiyo bado hayajafichuliwa, lakini wapinzani wa Marekani watafanya kila wawezalo kuelewa kilichotokea.
Mapigano

Chanzo cha picha, Reuters
Wale waliopanga operesheni hizo tata wanasema ni jambo la ajabu kwamba kila kitu kilikwenda kulingana na mpango, jambo ambalo hutokea mara chache. Helikopta moja ilipigwa lakini iliweza kuendelea kuruka, na hakuna mwanajeshi wa Marekani aliyeuawa.
Kuna maelezo machache kuhusu mapigano yaliyotokea katika ngome ya Maduro, Ngome ya Tiuna.
Serikali ya Cuba iliripoti kwamba raia wake 32 waliuawa na vikosi vya Marekani. Walikuwa walinzi waliotolewa na Cuba ili kumlinda Maduro. Taifa hilo la Karibiani halitoi tu walinzi bali pia linaunga mkono usalama wa serikali.
"Kikosi cha karibu cha kumlinda Maduro, pengine hakukuwa na maafisa wa usalama wa Venezuela, na katika eneo la nje labda kulikuwa na mchanganyiko wa maafisa," Fitzgerald anasema.
Na kutofanikiwa kumlinda Maduro, kumeibua mashaka huenda baadhi ya maafisa wa utawala wake waliwezesha misheni hiyo kutokea.
Vikosi vya Marekani pia vilifanikiwa kumfikia Maduro alipojaribu kujifungia kwenye chumba, lakini kabla hajafunga mlango.
Walikuwa na vilipuzi tayari kufungua mlango ikiwa angefanikiwa kujifungia, na kasi ya kukamatwa inaonyesha ujuzi wa kina wa jengo hilo.
Baada ya operesheni

Chanzo cha picha, CBS
CIA ilifanya tathmini ya siri kabla ya operesheni hiyo, ikichambua kile kinachoweza kutokea ikiwa Maduro ataondolewa madarakani.
Wachambuzi walichunguza chaguzi kadhaa na inasemekana walihitimisha kwamba kufanya kazi na utawala uliopo kunatoa nafasi kubwa zaidi ya utulivu kuliko kujaribu kuwaweka madarakani wapinzani walio uhamishoni.
Hilo limesaidia kuimarisha wazo kwamba Marekani itafanya kazi na Delcy Rodríguez, makamu wa rais.
Inaaminika kwamba kulikuwa na mawasiliano ya siri na yasiyo rasmi na watu katika utawala wa Maduro kabla ya operesheni hiyo ili kujadili jinsi pande tofauti zitakavyo fanya kazi.
Maelezo kamili ya mawasiliano haya yanabaki kuwa fumbo, lakini yanawezekana yanaelezea mengi kuhusu kwa nini misheni hiyo ilitekelezwa, kwa nini ilifanikiwa, na hali ilivyo sasa.














