Kipi kitamzuia Putin asiendelee na vita Ukraine?

- Author, James Landale
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Seneta wa Marekani marehemu John McCain alitania kwamba alipomtazama machoni rais wa Urusi, Vladimir Putin, aliona vitu vitatu, "K na G na B", akimaanisha maisha yake ya zamani kama afisa wa ujasusi wa Soviet.
Nami nililiona hilo nilipotazama video akiwa ameketi na wajumbe wa Marekani huko Kremlin. Hakuweza kuficha hisia zake; alionyesha hali ya kujiamini kupita kiasi.
Rais Putin anaamini diplomasia iko upande wake, huku uhusiano na Marekani ukiimarika na mafanikio katika uwanja wa vita yamepatikana.
Baadhi ya wachambuzi wanasema Putin hana sababu ya kuachana na madai yake: kwamba Ukraine itoe asilimia 20 iliyobaki ya Donetsk ambayo bado inaidhibiti; anataka eneo lote hilo litambuliwe kimataifa kama sehemu ya Urusi, huku akiamini jeshi la Ukraine limepigwa hadi kiwango cha kutokuwa na nguvu; na uanachama wa Nato umekataliwa kabisa.
Kwa hivyo, kuna chochote - kinachoweza kubadilisha mawazo ya Putin? Na ni nini kingine ambacho Ukraine, Marekani, Ulaya au hata China, zinaweza kufanya?
Ulaya inaweza kufanya nini?

Chanzo cha picha, WPA Pool/Getty Images
Kwa sasa, bara hilo linajiandaa kwa ajili ya kusitisha mapigano. Chini ya bendera ya "muungano wa walio tayari", linaandaa kikosi cha kijeshi cha kimataifa kusaidia Ukraine kuzuia uvamizi wa Urusi katika siku zijazo, pamoja na juhudi za kifedha kusaidia kujenga upya nchi hiyo iliyoharibiwa na vita.
Lakini baadhi ya maafisa wanapendekeza Ulaya inapaswa badala yake kujiandaa na vita kuendelea.
Wanataka kuisaidia Ukraine siyo tu "kwa ndege zisizo na rubani na pesa; lakini pia kutoa usaidizi wa muda mrefu na kujiandaa kwa vita vya miaka 15 hadi 20 na Urusi.
Ulaya pia inaweza kufanya zaidi kusaidia kulinda anga za Ukraine dhidi ya ndege zisizo na rubani na makombora. Tayari kuna mpango - unaoitwa Mpango wa Ngao ya Anga ya Ulaya - ambao unaweza kupanuliwa ili kuruhusu ulinzi wa anga wa Ulaya kulinda magharibi mwa Ukraine.
Wengine wanasema wanajeshi wa Ulaya wanaweza kutumwa magharibi mwa Ukraine kusaidia doria mipakani, na kuwafanya wanajeshi wa Ukraine kuwa huru kupigana kwenye mstari wa mbele. Mapendekezo mengi kama haya yamekataliwa kwa hofu ya kuchochea vita na Urusi au kuzidisha mzozo.
Mkakati huu bila shaka utakuwa na ugumu mkubwa kisiasa - huku baadhi ya wapiga kura Ulaya magharibi wakiwa hawataki kuhatarisha kuingia katika mzozo na Urusi.
Vikwazo na uchumi kwa Urusi

Chanzo cha picha, Sputnik/Alexander Kazakov/Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kisha kuna vikwazo. Hakika, uchumi wa Urusi unateseka. Mfumuko wa bei uko 8%, viwango vya riba 16%, ukuaji wa uchumi unapungua, nakisi ya bajeti inaongezeka, mapato halisi yanashuka, kodi zinaongezeka.
Ripoti ya Jukwaa la Amani na Utatuzi wa Migogoro inasema, "uchumi wa Urusi hauna uwezo mkubwa wa kufadhili vita kuliko ilivyokuwa mwanzoni mwa mwaka 2022.”
Lakini hadi sasa hakuna hata moja kati ya haya, linaloonekana kubadilisha mawazo ya Kremlin, hasa kwa sababu biashara zake zimepata njia za kuepuka vikwazo, kama vile kusafirisha mafuta kwenye meli ambazo hazijasajiliwa.
Tom Keatinge, mkurugenzi wa Kituo cha Fedha na Usalama cha Rusi, anasema ikiwa nchi za Magharibi zinataka kweli kuathiri uchumi wa Urusi, zipige marufuku mafuta yote ya Urusi na kutekeleza kikamilifu vikwazo vya kwa nchi ambazo bado zinanunua mafuta hayo.”
Jingine, Umoja wa Ulaya inabidi ukubali kutumia takriban €200bn (£176bn) mali ya Urusi iliyozuiliwa ili kuzalisha kile kinachoitwa "mkopo wa fidia" kwa Ukraine.
Huko Kyiv, maafisa tayari wanazitaka pesa hizo. Lakini bado EU inasita.
Ubelgiji, ambapo sehemu kubwa ya mali za Urusi zinashikiliwa, kwa muda mrefu imekuwa ikiogopa kushtakiwa na Urusi - na siku ya Ijumaa, Benki Kuu ya Urusi ilitangaza hatua za kisheria dhidi ya benki ya Ubelgiji ya Euroclear katika mahakama ya Moscow.
Ubelgiji inasema haitakubali mpango huo isipokuwa hatari za kisheria na kifedha zielezwe waziwazi kwa wanachama wengine wa EU. Ufaransa ina wasiwasi, kutumia mali zilizozuiliwa kunaweza kudhoofisha utulivu wa ukanda wa euro.
Viongozi wa EU watafanya jaribio lingine la kukubaliana juu ya jambo hilo watakapokutana Brussels tarehe 18 Desemba kwa ajili ya mkutano wao wa mwisho kabla ya Krismasi. Lakini wanadiplomasia wanasema hakuna uhakika wa mafanikio.
Pia kuna kutokubaliana kuhusu pesa hizo zitumike kwa nini: kuweka akiba kwa serikali ya Ukraine au kulipia ujenzi wake baada ya vita.
Ukraine inaweza kufanya nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuhusu Ukraine, inaweza kuongeza vikosi vyake kuwa vingi zaidi. Linasalia kuwa jeshi la pili kwa ukubwa barani Ulaya (nyuma ya Urusi), na limeendelea.
Baada ya karibu miaka minne ya vita, wanajeshi wengi wamechoka na viwango vya kutoroka vinaongezeka.
Waajiri wa jeshi wanapata shida kujaza mapengo huku baadhi ya vijana wakijificha au wakikimbia nchi.
Kwa sasa ni wanaume wenye umri wa miaka 25 hadi 60 pekee ndio wanaopaswa kupigana. Huu ni mkakati wa makusudi wa Kyiv wa kudhibiti changamoto ya idadi ndogo ya watu nchini Ukraine; nchi yenye kiwango cha chini cha kuzaliana na mamilioni na watu wanaishi nje ya nchi.
Hili linawashangaza watu. "Naona ni jambo la kushangaza kwamba Ukraine haijawahamasisha vijana kwenda vitani," mwanajeshi mmoja mwandamizi wa Uingereza aliniambia.
"Ukraine ni moja ya nchi pekee katika historia kuingia vitani na haijawataka vijana wake wa miaka 20 kuingia vitani."
Jambo jingine, kama Ukraine ingeweza kuingiza na kutengeneza makombora zaidi ya masafa marefu, ingeweza kuipiga Urusi kwa nguvu zaidi.
Mwaka huu iliongeza mashambulizi yake ya angani dhidi ya maeneo yaliyokaliwa na Shirikisho la Urusi.
Mapema mwezi huu makamanda wa kijeshi wa Ukraine waliiambia Radio Liberty kwamba walishambulia zaidi ya vituo 50 vya mafuta na miundombinu ya kijeshi na viwanda nchini Urusi wakati wa majira ya vuli.
Alexander Gabuev, mkurugenzi wa Kituo cha Carnegie Russia Eurasia, anasema baadhi ya Warusi walipata uhaba wa mafuta mapema mwaka huu.
"Kufikia mwishoni mwa Oktoba, ndege zisizo na rubani za Ukraine zilipiga zaidi ya nusu ya viwanda vikubwa thelathini na nane vya kusafisha mafuta vya Urusi angalau mara moja."
Je, mashambulizi makali zaidi dhidi ya Urusi yataweza kumbadilisha Putin?
Dkt. Sidharth Kaushal, mtafiti wa masuala ya kijeshi katika taasisi ya ushauri ya Royal United Services Institute (Rusi), anasema mashambulizi zaidi yataharibu miundombinu ya nishati na kijeshi ya Urusi, pamoja na makombora yake ya ulinzi wa anga. Lakini anaonya mbinu hiyo inaweza kuwa na matokeo mabaya.
"Inaweza kuimarisha hoja ambayo uongozi wa Urusi inaitoa kwamba Ukraine inaleta tishio kubwa la kijeshi.”
Diplomasia ya Marekani

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Baadhi ya wachambuzi wanasema ikiwa Putin atapewa njia ya kutoka vitani, anaweza kuichagua.
Nadharia hii inasema: ni kupitia makubaliano ambayo yanaruhusu pande zote mbili kudai ushindi.
Makubaliano ya aina hii yanahitaji Marekani na Urusi, kuanzisha timu za mazungumzo, na Marekani kwa kutumia uwezo wake kuendesha makubaliano.
Thomas Graham anasema. "Mtu hawezi kudharau jukumu la Marekani - na Trump – kusaka amani na Urusi kama taifa kubwa na Putin kama kiongozi wa kimataifa."
Ushawishi wa China

Chanzo cha picha, Shutterstock
Rais Xi Jinping ni mmoja wa viongozi wachache wa dunia ambaye Putin anamsikiliza. Wakati Xi alipoonya mapema katika mzozo dhidi ya vitisho vya Urusi vya matumizi ya silaha za nyuklia, Kremlin haraka ilitii sheria za kimataifa.
Vita vya Urusi pia vinategemea usambazaji wa China wa bidhaa - kama vile vifaa vya elektroniki au mashine ambazo zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiraia na kijeshi.
Kwa hivyo ikiwa Beijing itaamua kuwa vita hivyo havina tena maslahi kwa China ikiwa vitaendelea, basi hilo litaletha athari kubwa juu ya mawazo ya Kremlin.
Kwa sasa, Marekani haionyeshi dalili zozote za kujaribu kuihimiza - au kuilazimisha - China kuiwekea shinikizo Moscow. Kwa hivyo swali ni ikiwa Rais Xi yuko tayari kutumia nguvu yoyote yeye mwenyewe.
Kwa sasa China inaonekana kufurahi kwamba Marekani inashughulikia suala hilo, washirika wa nchi za ng'ambo ya Atlantiki kugawanyika, na ulimwengu wote kuiona China kama chanzo cha utulivu.
Lakini ikiwa uvamizi wa Urusi utaongezeka, ikiwa masoko ya kimataifa yatavurugwa, ikiwa Marekani itaweka vikwazo kwa China kama adhabu kwa matumizi yake ya nishati ya bei nafuu ya Urusi, basi mawazo huko Beijing yanaweza kubadilika.
Kwa sasa, Putin anaamini amekaa pazuri, huku muda ukiwa upande wake. Kadiri mzozo huu unavyoendelea, wachambuzi wanasema, ndivyo ari ya Ukraine inavyopungua, ndivyo washirika wake watakavyogawanyika zaidi, na ndivyo Urusi itakavyopata eneo kubwa zaidi huko Donetsk.















