Putin asema Urusi itachukua eneo lote la Ukraine la Donbas kwa nguvu
Putin alituma makumi ya maelfu ya wanajeshi nchini Ukraine mnamo Februari 2022 baada ya miaka minane ya mapigano kati ya watu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi na wanajeshi wa Ukraine katika eneo la Donbas.
Muhtasari
- Kasisi wa Kikatoliki alitekwa nyara katika Jimbo la Kaduna nchini Nigeria, Dayosisi inasema
- Iraq kurekebisha orodha ya makundi yatakayositishiwa ufadhili ikisema ya awali ilikuwa na makosa
- Tume ya Vatican yapiga kura dhidi ya kuwaruhusu wanawake kuwa mashemasi wa Kikatoliki
- Putin asema Urusi itachukua eneo lote la Ukraine la Donbas kwa nguvu
- Meta yaanza kuwaondoa watoto wa Australia kwenye mtandao wa Instagram na Facebook
- Marekani yatishia kupiga marufuku viza kwa raia wa Nigeria wanaowatesa wenzao kwa misingi ya imani za kidini
- Watano wauawa katika shambulio la anga la Israel kwenye mahema yaliyo karibu na Khan Younis, madaktari wasema
- Wajumbe wa Ukraine na Marekani kukutana Florida baada ya mazungumzo ya Moscow - Whitehouse
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid & Asha Juma
Kasisi wa Kikatoliki alitekwa nyara katika Jimbo la Kaduna nchini Nigeria, Dayosisi inasema

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Kasisi wa Kikatoliki alitekwa nyara kutoka kwa makazi yake katika Jimbo la Kaduna, kaskazini mwa Nigeria, Jimbo Katoliki la Zaria lilisema Jumatano.
Mch. Emmanuel Ezema alichukuliwa Jumanne saa 11:30 jioni (0030 GMT Jumatano) kutoka Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro huko Rumi, dayosisi hiyo ilisema katika taarifa iliyoonekana na Reuters siku ya Alhamisi. Haikusema ikiwa watekaji nyara walikuwa wamewasiliana au walidai fidia.
Utekaji nyara kwa ajili ya fidia umekuwa jambo la kawaida nchini Nigeria, hasa kaskazini magharibi, ambako magenge yenye silaha yamelenga makasisi, wasafiri na wanakijiji.
Soma zaidi:
Iraq kurekebisha orodha ya makundi yatakayositishiwa ufadhili ikisema ya awali ilikuwa na makosa

Chanzo cha picha, Reuters
Iraq itasahihisha orodha ya makundi ambayo ufadhili wao umesitishwa, shirika la habari la serikali liliripoti Alhamisi, baada ya Hezbollah inayoungwa mkono na Iran na Houthis kujumuishwa katika chapisho la awali la serikali.
Gazeti rasmi la Wizara ya Sheria mwezi uliopita lilichapisha orodha ya makundi na mashirika ambayo fedha zao zingezuiwa, na kuzitaja kundi la Hezbollah la Lebanon na Wahouthi wa Yemen, hatua ambayo ingefurahiwa na Marekani na kuongeza shinikizo kwa Tehran.
Kamati ilisema kuwa makundi kadhaa ambayo hayahusiani yalijumuishwa kimakosa kwa sababu orodha hiyo ilitolewa kabla ya kukamilika kwa marekebisho ya mwisho.
Majina hayo yataondolewa katika toleo lililosahihishwa na kutolewa tena kwenye gazeti rasmi la serikali, iliongeza.
Hezbollah na Houthis hawakujibu mara moja maombi ya kutoa maoni.
Soma zaidi:
Tume ya Vatican yapiga kura dhidi ya kuwaruhusu wanawake kuwa mashemasi wa Kikatoliki

Chanzo cha picha, Reuters
Tume ya ngazi ya juu ya Vatican ilipiga kura dhidi ya kuruhusu wanawake wa Kikatoliki kuhudumu kama mashemasi, kudumisha desturi ya Kanisa la kimataifa ya makasisi wanaume wote, kulingana na ripoti iliyotolewa kwa Papa Leo siku ya Alhamisi.
Tume, katika kura 7-1, ilisema utafiti wa kihistoria na uchunguzi wa kitheolojia "haujumuishi uwezekano" wa kuruhusu wanawake kuhudumu kama mashemasi kwa wakati huu lakini ilipendekeza utafiti zaidi wa suala hilo.
Ripoti hiyo ilisema tathmini ya kundi hilo kuhusu suala hilo ilikuwa na nguvu, lakini "hadi leo hairuhusu uamuzi mahususi kufanywa".
Marehemu Papa Francis alianzisha tume mbili za kuchunguza uwezekano wa wanawake kutumikia kama mashemasi wa Kikatoliki, ambao, kama mapadre, wametawazwa, lakini hawawezi kuadhimisha Misa.
Tume hizo zilikutana kwa siri. Ripoti ya Alhamisi ni mara ya kwanza kwa matokeo ya majadiliano hayo kuwekwa hadharani.
Papa John Paul II alipiga marufuku wanawake kuhudumu kama makasisi mwaka wa 1994, lakini hakuzungumzia hasa suala la mashemasi wanawake.
Wanaotetea suala hilo wanaonyesha ushahidi kwamba wanawake walitumika kama mashemasi katika karne za mwanzo za Kanisa. Mwanamke mmoja, Phoebe, anatajwa kuwa shemasi katika mojawapo ya barua za mtume Mtakatifu Paulo.
Soma zaidi:
Putin asema Urusi itachukua eneo lote la Ukraine la Donbas kwa nguvu

Chanzo cha picha, Reuters
Rais Vladimir Putin amesema katika mahojiano yaliyochapishwa Alhamisi kwamba Urusi itachukua udhibiti kamili wa eneo la Donbas la Ukraine kwa nguvu labda vikosi vya Ukraine vijiondoe, jambo ambalo Kyiv imekataa kabisa.
Putin alituma makumi ya maelfu ya wanajeshi nchini Ukraine mnamo Februari 2022 baada ya miaka minane ya mapigano kati ya watu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi na wanajeshi wa Ukraine katika eneo la Donbas, ambayo inajumuisha mikoa ya Donetsk na Luhansk.
"Ama tukomboe maeneo haya kwa nguvu ya silaha, au wanajeshi wa Ukraine waondoke," Putin aliambia India Today kabla ya kuzuru New Delhi, kulingana na video iliyoonyeshwa kwenye televisheni ya taifa ya Urusi.
Ukraine inasema haitaki kuizawadia Urusi eneo lake ambalo Moscow imeshindwa kushinda katika uwanja wa vita, na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema Moscow haipaswi kutuzwa kwa vita ilivyoanzisha.
Kwa sasa Urusi inadhibiti 19.2% ya Ukraine, ikiwa ni pamoja na Crimea, ambayo ilitwaa mwaka 2014, Luhansk yote, zaidi ya 80% ya Donetsk, karibu 75% ya Kherson na Zaporizhzhia, na slivers ya mikoa ya Kharkiv, Sumy, Mykolaiv na Dnipropetrovsk.
Soma zaidi:
Kesi dhidi ya Mange yaahirishwa Tanzania

Chanzo cha picha, Mange IG
Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mwanamitindo na mwanaharakati wa Tanzania anayeishi Marekani Mange Kimambi imeahirishwa hadi Januri 28 2026.
Wakili wa Jamuhuri Clemence Kato ameileza mahakama upelelezi wa shauri hili haujakamilika, shauri hilo limetajwa leo mahakama ya hakimu mkazi Kisutu mbele ya hakimu Mwandamizi Hassan Makube.
Serikali ya Tanzania imemfungulia mashataka ya kiuchumi mwanaharakati Mange Kimambi ambaye anayeishi nchini Marekani.
Hatua hii inakuja mwezi mmoja baada ya mwanasheria mkuu wa serikali nchini humo Hamza Johari kumlaumu mwanaharakati huyo kwa kuchochea maandamano ya ghasia yaliyotokea katika Oktoba 29 2025 siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Unaweza kusoma;
Israel yatambua mabaki ya mateka waliokabidhiwa na Hamas kuwa raia wa Thailand

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Jihad ya Kiislamu ya Palestina imesema kuwa imepata mwili wa mateka kaskazini mwa Gaza Israel imetambua kuwa mwili uliopelekwa kupitia shirika la Msalaba Mwekundu Jumatano ni wa Suthisak Rintalak, mfanyakazi wa kilimo mwenye umri wa miaka 43 kutoka Thailand, kwa mujibu wa ofisi ya waziri mkuu.
Rintalak alikuwa mmoja wa mateka wawili waliokufa waliokuwa bado Gaza.
Mwili wa mateka wa mwisho aliye baki, Ran Gvili, afisa wa polisi wa Israel mwenye umri wa miaka 24, bado upo Gaza.
Israel ilipokea jeneza lililo na mwili wa Rintalak baada ya tawi la kijeshi la Jihadi ya Kiislamu ya Palestina (PIJ) kusema kuwa limepata mwili wa mateka kaskazini mwa Gaza.
Ukabidhi huo ulifanyika masaa machache baada ya ofisi ya waziri mkuu wa Israel kusema kuwa vipimo vilionyesha kuwa mabaki mengine yaliyopewa Israel na Hamas siku ya Jumanne havikuhusiana na mateka waliokufa.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema limewajulisha familia ya Rintalak na kutoa “rambi rambi za dhati.”
IDF iliongeza kuwa itaendelea kusukuma jitihada za kurejeshwa kwa mwili wa Gvili, ikiihimiza Hamas “kufanya juhudi zote zinazohitajika” kumrejeshea familia yake.
Maafisa wa Israel wanashirikiana na ubalozi wa Thailand nchini Israel kuhakikisha mabaki ya Rintalak yarejeshwe Thailand, ofisi ya waziri mkuu ilisema katika taarifa.
Maafisa wa Israel na Thailand wanasema mateka hao wote waliuawa wakati wa shambulio la Hamas lililofanyika kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, na kwamba miili yao ilipelekwa Gaza baada ya hapo.
Kwenye awamu ya kwanza ya makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyoongozwa na Marekani, ambayo yalianza kutekelezwa tarehe 10 Oktoba, Hamas ilikubali kurejesha mateka 20 wa Israeli waliokuwa hai na miili ya mateka 28 waliokufa wa Israeli na wageni waliobaki Gaza ndani ya masaa 72.
Mateka wote waliokuwa hai walitachiwa huru tarehe 13 Oktoba kwa kubadilishana na wafungwa 250 wa Kipalestina na watu 1,718 waliokuwa wanashikiliwa Gaza.
Hadi sasa, mabaki ya mateka 23 wa Israeli waliokufa yamekabidhiwa, pamoja na mabaki ya mateka wanne wa kigeni wawili wao wakiwa Thailand, mmoja Nepal na mmoja Tanzania.
Kwa kubadilishana, Israel imekabidhi miili ya Wapalestina 345 waliouawa wakati wa vita.
Israel imekashifu Hamas kwa kuchelewesha kwa makusudi urejeshaji wa miili ya mateka, huku Hamas ikisisitiza kuwa inakumbana na changamoto za kuyapata chini ya mabaki ya majengo yaliyoromoka.
Kasi ndogo ya mchakato huo imesababisha kuwa hakuna maendeleo kwenye awamu ya pili ya mpango wa amani wa Gaza wa Rais Donald Trump.
Hii inajumuisha mipango ya utawala wa Gaza, kujiondoa kwa wanajeshi wa Israel, kumalisha silaha za Hamas na ujenzi upya.
Mateka aliyekufa bado amezuiwa Gaza alikuwa miongoni mwa watu 251 waliotekwa na Hamas na washirika wake tarehe 7 Oktoba 2023, wakati takriban watu 1,200 wakiuwawa.
Israel ilijibu shambulio hilo kwa kuzindua kampeni ya kijeshi Gaza, ambapo zaidi ya watu 70,100 wameripotiwa kuuliwa, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas.
Soma zaidi:
Bunge la Kenya lakemea wanajeshi wa Uingereza wa BATUK kwa madai ya unyanyasaji wa kingono

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Uingereza wamekuwa wakifanya mazoezi katikati mwa Kenya kwa miongo kadhaa chini ya makubaliano ya kijeshi Bunge la Kenya limewashutumu wanajeshi wa Uingereza kwa miongo kadhaa ya unyanyasaji wa kingono, mauaji, ukiukaji wa haki za binadamu na uharibifu wa mazingira walipokuwa wakifanya mafunzo nchini humo.
Ripoti hiyo ilieleza kwa kina ushuhuda wa kutisha kutoka kwa jamii za kaunti za Laikipia na Samburu, karibu na vituo vya mafunzo ya kijeshi.
Wanajeshi hao wa Uingereza wanatuhumiwa kukwepa uwajibikaji kwa kukataa kushirikiana na uchunguzi wa bunge.
Tume Kuu ya Uingereza nchini Kenya ilisema inasikitika kwamba uwasilishaji wake haukuonyeshwa katika hitimisho la ripoti hiyo na ikathibitisha utayari wake wa kuchunguza madai hayo "chini ya mamlaka yetu kikamilifu, mara ushahidi utakapotolewa".
Kwa miongo kadhaa, wanajeshi kutoka Kituo cha Mafunzo ya Jeshi la Uingereza nchini Kenya (Batuk) wamekuwa wakifanya mafunzo katikati ya Kenya.
Hata hivyo, uwepo wao umekuwa ukiibua utata, huku wakikashifiwa kwa tabia zisizo za kimaadili na ukiukaji wa haki za binadamu.
Zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Kenya hupata mafunzo ya kijeshi kutoka Uingereza kila mwaka, huku maelfu ya wanajeshi wa Uingereza wakitumwa Kenya kwa mazoezi ya kijeshi.
Soma pia:
Rais Macron akutana na Xi huku EU ikitayarisha sheria kali zaidi za biashara

Chanzo cha picha, EPA
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anakutana na mwenzake wa China Xi Jinping mjini Beijing kwa mazungumzo yanayotarajiwa kutuama juu ya vita vya Ukraine.
China ambayo imekuwa ikisisitiza haiegemei upande wowote katika mzozo wa Ukraine,lakini imekuwa ikishutumiwa kwa kuiunga mkono Urusi kwa kununua kwa wingi mali ghafi za Urusi na kuiuzia Urusi teknolojia ya kutengeza silaha za kisasa.
Umoja wa Ulaya inataka China ichangie zaidi katika juhudi za kuvimaliza vita vya Ukraine.
Soma pia:
Meta yaanza kuwaondoa watoto wa Australia kwenye mtandao wa Instagram na Facebook

Chanzo cha picha, Getty Images
Kampuni ya Meta imesema imeanza kuondoa akaunti za vijana walio chini ya umri wa miaka 16 kutoka kwa mitandao yao ya kijamii nchini Australia kuelekea marufuku iliyotangazwa na serikali ya nchi hiyo kuwa watoto walio chini ya umri wa miaka 16 hawataruhusiwa kuwa na akaunti katika mitandao ya kijamii kama Tiktok,Facebook,Youtube na Instagram.Sheria hiyo inaanza kutekelezwa rasmi Jumatano ijayo.
Kampuni hiyo kubwa ya teknolojia ilitangaza mwezi uliopita kuwa imeanza kuwafahamisha watumiaji wenye umri wa kati ya miaka 13 hadi 15 kwamba akaunti zao zitaanza kufungwa kuanzia tarehe 4 Desemba.
Takriban watumiaji 150,000 wa Facebook na akaunti 350,000 za Instagram wanatarajiwa kuathirika.
Mitandao ya Threads, sawa na X, zinaweza kupatikana tu kupitia akaunti ya Instagram.
Marufuku ya kwanza duniani ya mitandao ya kijamii nchini Australia itaanza tarehe 10 Disemba, huku kampuni zikikabiliwa na faini ya hadi A$49.5m (US$33m, £25m) iwapo zitashindwa kuchukua "hatua zinazofaa" kuwazuia watoto chini ya miaka 16 kuwa na akaunti.
Vijana wanaoamini kuwa wameainishwa kimakosa kama walio na umri wa chini ya miaka 16 wanaweza kuomba ukaguzi na kuwasilisha "selfie ya video au video wakijieleza" ili kuthibitisha umri wao. Wanaweza pia kutoa leseni ya udereva au kitambulisho kilichotolewa na serikali.
Unaweza kusoma;
Marekani yatishia kupiga marufuku viza kwa raia wa Nigeria wanaowatesa wenzao kwa misingi ya imani za kidini

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Kigeni Marekani, Marco Rubio Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Marco Rubio amesema nchi yake inachukua hatua madhubuti kukabiliana na madhila yanayofanywa dhidi ya Wakristo nchini Nigeria na kwigineko.
Rubio amesema wanawawekea vikwazo vya usafiri wanaofadhili, kuunga mkono au kutekeleza vitendo vya kukiuka uhuru wa kuabudu.
Tangazo hili linakuja wakati ambapo mvutano kati ya Washington na Abuja unaendelea kupanda.
Mwezi uliopita, Rais Donald Trump aliwashutumu viongozi wa Nigeria kwa kushindwa kuwalinda Wakristo dhidi ya kile alichokitaja mateso na mauaji makubwa yanayofanywa na makundi ya kijihadi,madai ambayo serikali ya Rais Bola Tinubu imeyakanusha.
Rais Bola Tinubu ametafuta kupunguza shinikizo la Marekani kwa kutangaza hatua kadhaa katika wiki za hivi karibuni. Hatua hizo zinajumuisha kuimarisha operesheni za kijeshi katika maeneo hatarishi, kupeleka vikosi vya ziada kulinda jamii za vijijini, pamoja na kufanya marekebisho katika uratibu wa shughuli za ujasusi.
Serikali ya Nigeria pia imeahidi kuharakisha mageuzi yanayolenga kuimarisha taasisi za usalama ambazo zimekuwa zikikabiliwa na mzigo mkubwa.
Soma zaidi:
Watano wauawa katika shambulio la anga la Israel kwenye mahema yaliyo karibu na Khan Younis, madaktari wasema

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Hema karibu na Khan Younis wiki iliyopita (picha za awali) Maafisa wa afya kusini mwa Gaza wamesema watu watano wameuawa katika shambulizi la angani la Jeshi la Israel ambalo Israel imesema ilikuwa ikilenga maeneo makhususi baada ya wanajeshi wake kushambuliwa.
"Shirika la kigaidi la Hamas lilifanya ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano, ambapo magaidi waliwashambulia wanajeshi wa IDF waliowekwa katika eneo la Rafah," Jeshi la Ulinzi la Israeli lilisema katika taarifa.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikuwa ameapa "kujibu shambulizi hilo ipasavyo".
Walioshuhudia shambulizi lililotokea katika eneo linalowahifadhi watu walioachwa bila ya makazi la al Mawasi wamesema shambulizi la kwanza lililenga hema moja kisha likafuatia jingine karibu na hospitali ya Kuwait.
Timu za madaktari zilisema waliofariki ni wanawake wawili wenye umri wa miaka 46 na 30, mwanamume mwenye umri wa miaka 36, na wavulana wawili, wenye umri wa miaka minane na 10 mtawalia.
Takriban watu 32 waliojeruhiwa walitibiwa hospitalini, madaktari walisema.
Wafanyakazi wa uokoaji waliiambia BBC kwamba waliona miili kutoka kambi ya al-Najaat, nguzo ya mahema ambayo yamehifadhi mamia ya watu waliokimbia makazi katika miezi ya hivi karibuni.
Hamas imeyataja mashambulizi hayo kuwa unyama na ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani wiki saba zilizopita.
Soma pia:
Wajumbe wa Ukraine na Marekani kukutana Florida baada ya mazungumzo ya Moscow - Whitehouse

Chanzo cha picha, Getty Images
Ikulu ya Rais wa Marekani ya White House imethibitisha kuwa mjumbe maalum wa Rais Donald Trump Steve Witkoff atakutana na mjumbe mkuu wa Ukraine leo Alhamisi kujadili namna Urusi ilivyopokea mpango wa amani unaopendekezwa na Marekani.
Bwana Witkoff alikutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin siku ya Jumanne kwa mkutano ambao pande zote mbili ziliutaja wenye tija lakini ulishindwa kufikia makubaliano ya kuvimaliza vita vya Ukraine.
Rais Trump amesema itabidi wasubiri waone Urusi ina mipango gani.
Rais wa Marekani, Donald Trump, alisema mazungumzo hayo ambayo pia yalihusisha mkwe wake, Jared Kushner yalikuwa “ya kuridhisha,” lakini akaongeza kuwa bado ni mapema kujua kitakachofuata kwa sababu “mazungumzo huhitaji ushirikiano wa pande zote.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrii Sybhia, alisema Urusi inapaswa “kukomesha umwagaji damu,” na akamshutumu Putin kwa “kupoteza muda wa dunia.”
Alipoulizwa kama Witkoff na Kushner wanaamini Putin anataka kumaliza vita kwa dhati, Trump alijibu: “(Putin) angependa kumaliza vita. Huo ndiyo mtazamo waliokuwa nao.”
Mapema Jumatano, Rais Volodymyr Zelensky alisema mkutano wa wajumbe wa Marekani na Ukraine unatarajiwa kufanyika “karibuni.” Katika taarifa aliyotoa kupitia mtandao wa X, Zelensky alisema: “Kwa sasa, dunia inaona wazi kuwa kuna nafasi halisi ya kumaliza vita.”
Hata hivyo, alisisitiza kuwa mazungumzo lazima “yaambatane na shinikizo kwa Urusi.” Mazungumzo ya Marekani na Urusi Kremlin yalifanyika kufuatia siku kadhaa za mikutano kati ya Marekani, Ukraine na viongozi wa Ulaya, baada ya wasiwasi kuibuka kuwa rasimu ya makubaliano ya amani ilikuwa inaegemea mno matakwa ya Urusi.
Ushauri wa Kremlin, Ushakov, alisema: “Baadhi ya mapendekezo ya Marekani yanaweza kujadiliwa zaidi,” huku akiongeza kuwa mengine yalipingwa moja kwa moja na Putin.
Ingawa hakutoa maelezo zaidi, masuala mawili makuu bado yanasababisha mvutano kati ya Moscow na Kyiv: hatima ya maeneo ya Ukraine yaliyotekwaliwa na Urusi, na suala la dhamana za kiusalama kwa Ukraine.
Soma pia:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ya 04/12/2025.Tutakuarifu kuhusu mkutano wa kusitisha mapigano wa Rwanda na DRC Congo unaofanyika Marekani na taarifa za kimataifa kadri zinavyochipuka.
