Hezbollah inapata wapi pesa zake?

- Author, Shereen Sherif na Abdirahim Saeed
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 8
Ufadhili wa kundi la wanamgambo wa Lebanon la Hezbollah umeanza kuchunguzwa upya kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel mwishoni mwa mwaka jana.
Hezbollah ni jeshi lenye nguvu zaidi nchini Lebanon, na pia ni chama chenye ushawishi cha Waislamu wa madhehebu ya Shia. Wapo katika bunge la Lebanon na serikali.
Hezbollah inatajwa kama shirika la kigaidi na Israel na nchi nyingi za Magharibi. Kundi hilo lilijipatia umaarufu katika miaka ya 1980, baada ya kuingia vitani na Israel baada ya nchi hiyo kuyakalia kwa mabavu maeneo ya kusini mwa Lebanon wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1975-1990 nchini humo.
Mwezi Oktoba, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilishambulia matawi kadhaa ya taasisi ya kifedha ya Al-Qard Al-Hassan (AQAH), kwa madai kuwa inafadhili shughuli za kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.
AQAH inakanusha na kusisitiza kuwa shirika lake la kifedha ni shirika la kiraia linalotoa mikopo midogo kwa watu wanaohitaji.
Baada ya miezi miwili ya makabiliano kati ya Hezbollah na Israel nchini Lebanon mwaka 2024, ambayo yamesababisha uharibifu mkubwa katika maeneo ambayo kundi hilo lina uwepo wake mkubwa.
Mapigano hayo yalimalizika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, ambayo yalianza kutekelezwa tarehe 27 Novemba.
Hayo yote na kusambaratika kwa utawala wa Assad katika nchi jirani ya Syria. Yana athari kubwa kwa ufadhili wa Hezbollah na uwezo wake wa kupata zana za kijeshi.
Ufadhili wa Iran

Chanzo cha picha, EPA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwaka 2022, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitoa makadirio kuwa Iran iliipatia Hezbollah kiasi cha dola milioni 700 kila mwaka.
Kiongozi marehemu wa Hezbollah Hassan Nasrallah - ambaye aliuawa katika shambulizi la anga la Israel Septemba 2024 - alijigamba katika hotuba yake mwaka 2016 kwamba ufadhili wa kundi hilo ulitoka zaidi Iran. Lakini hakufichua takwimu zozote za kifedha.
"Bajeti yetu, mishahara, matumizi, chakula, maji, silaha na makombora ni kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran," alisema.
Iran inaifadhili Hezbollah kupitia Jeshi lake lenye nguvu la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), ambalo lilisaidia kuanzishwa kwa kundi hilo katika miaka ya 1980.
IRGC pia ndio wasambazaji wakuu wa silaha kwa Hezbollah, ikijumuisha makombora na ndege zisizo na rubani.
Ingawa ufadhili wa Iran unaweza kuwa ndio uliochangia sehemu kubwa ya bajeti ya Hezbollah hapo awali, kundi hilo lina vyanzo vingine, kwa mujibu wa Hanin Ghaddar, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati, katika Taasisi ya Washington.
"Kwa sababu ya vikwazo dhidi ya Iran, ilifika mahali Iran haikuweza kutuma kiasi kikubwa cha fedha kwa Hezbollah," anaeleza Ghaddar.
Kundi hilo linapata mapato kupitia shughuli mbalimbali haramu za kifedha, ikiwa ni pamoja na utakatishaji fedha, kulingana na Matthew Levitt, mwandishi wa kitabu cha Hezbollah: The Global Footprint of Lebanon's Party of God.
Al-Qard Al-Hassan

Chanzo cha picha, EPA
AQAH ni taasisi linayoshutumiwa kwa utakatishaji fedha kwa niaba ya Hezbollah. Ni sehemu muhimu ya mtandao wa huduma za kijamii wa Hezbollah. Kabla ya mashambulizi ya anga ya Israel kwenye ofisi zake tarehe 20 Oktoba, ilikuwa na matawi zaidi ya 30, ambayo mara nyingi yako kwenye ghorofa za chini za majengo ya makazi.
Huruhusu watu kuchukua mikopo midogo, isiyo na riba kwa dola za Marekani, kwa kuweka rehani dhahabu au mdhamini, na kufungua akaunti za akiba.
Nasrallah, alisema katika hotuba yake mwaka 2021 kwamba AQAH ilitoa mikopo ya dola bilioni 3.7 (£2.8bn) kwa watu milioni 1.8 nchini Lebanon tangu ilipoanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1980, na karibu watu 300,000 walikuwa na mikopo wakati huo.
"Benki hi haisudii kuzalisha faida. Inatoa usaidizi wa kifedha hasa kwa maeneo ambayo ni ngome ya Hezbolla," anasema Joseph Daher.
Muda mfupi baada ya mashambulizi dhidi ya AQAH, Israel iliishutumu Hezbollah kwa kutumia taasisi hiyo ya kifedha "kufadhili shughuli zake za kigaidi".
Marekani pia iliiwekea vikwazo taasisi hiyo mwaka 2007, na maafisa wa Marekani walisema inatumiwa na Hezbollah kama kificho cha kusimamia shughuli zake za kifedha na kupata kutumia mfumo wa fedha wa kimataifa.
AQAH imejibu maswali ya BBC kuhusu madai ya uhusiano wake na Hezbollah, na imesisitiza kuwa sio tawi la kifedha la kundi hilo la wapiganaji na kukanusha madai utakatishaji wa fedha.
Taasisi hiyo inasema kuwa ni sehemu ya mfumo mpana wa kitaasisi wa Hezbollah, unaolenga kutoa masuala ya kibiadamu na huduma, badala ya miamala ya kifedha au uwekezaji.
AQAH imesisitiza hakuna uhusiano wa moja kwa moja na mashirika au serikali za kigeni, ikiwa ni pamoja na Iran.
"Sisi ni sehemu ya taasisi ya Hezbollah, lakini lengo letu ni katika nyanja za kibinadamu na huduma, sio shughuli za kifedha. Hakuna uhusiano na mataifa au mashirika yoyote ya kigeni, Iran au vinginevyo."
Wadukuzi wa SpiderZ
Taarifa zinaeleza kwamba mwezi Desemba 2020, kikundi kiitwacho SpiderZ kilidukua akaunti za chama hicho, na kufichua taarifa nyeti, kama vile orodha zinazodaiwa kuwa za wakopaji na walioweka amana, pamoja na kanda zinazodaiwa kuwa za kiusalama kutoka katika matawi yake.
Taasisi yenye makao yake mjini Washington ya Kutetea Demokrasia (FDD) inasema nyaraka zilizodukuliwa zinaonyesha kuwa AQAH inasimamia zaidi ya akaunti 400,000, huku nyingi, ikidai, zinahusishwa na washirika wa Hezbollah na Iran.
FDD inasema haichukui michango kutoka serikali yoyote na inajieleza kama isiyoegemea upande wowote. Hata hivyo, inaihesabu Iran na Hezbollah kuwa tishio kwa Marekani na washirika wake.
Akaunti moja, iliyoandikwa "Vali al-Faqih," inadaiwa kuwa ni ya ofisi ya Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei.
Taasisi zinazohusishwa na Khamenei, kama vile Wakfu wa Martyrs wa Lebanon, pia ina akaunti ya AQAH, iliripoti FDD.
AQAH ilithibitisha 2020 kutokea kwa udukuzi, lakini ilipinga kufichuliwa kwa shughuli zake na madai ya utambulisho wa baadhi ya wateja wake.
AQAH haikuthibitisha au kukanusha kwa BBC kama inasimamia akaunti zinazohusiana na Ali Khamenei. Hata hivyo, imesema mtu yeyote ndani ya eneo la Lebanon anaweza kuwa na akaunti, ikiwa ni pamoja na akaunti za michango.
Pia imesema ina uhusiano mzuri na Wakfu wa Martyrs wa Lebanon kwa sababu ni sehemu ya taasisi za huduma za kijamii za Hezbollah.
AQAH imesema haishirikiani na taasisi za kifedha za nje na haipokei fedha zinazotumwa na kutoka nje ya nchi.
Inasema mkazi yeyote nchini Lebanon anaweza kufaidika na mikopo inayotoa, vile vile, mkazi yeyote anaweza kufungua akaunti ya mchango na kuweka pesa "kwa madhumuni ya hisani na kidini."
Afrika na Amerika

Chanzo cha picha, Idara ya Haki ya Marekani
Kulingana na shirika na FDD, hati zilizodukuliwa 2020 zinaonyesha AQAH ilikuwa na akaunti za watu wanaoishi nje ya Lebanon, ikiwa ni pamoja na Afrika na Amerika Kusini.
"Hezbollah ina washirika wengi wa kibiashara katika nchi nyingi za Afrika," anaelezea Ghaddar.
"Wanajihusisha na kila aina ya sekta ikiwa ni pamoja na biashara ya madin na biashara," anaongeza.
Mwaka 2019, Hazina ya Marekani, ilimuwekea vikwazo mfanyabiashara wa kazi za sanaa Nazem Said Ahmad, ikimtuhumu kuwa "mmoja wa wafadhili wakuu wa Hezbollah."
Maafisa wa Marekani pia walisema Ahmad "ana uhusiano wa muda mrefu na biashara ya 'almasi."
Mahali alipo hapajulikani.
Hezbollah pia inashutumiwa kujipatia pesa kutokana na ulanguzi wa dawa za kulevya huko Amerika Kusini.
Uchunguzi nchini Venezuela mwaka 2011 unadaiwa kufichua mpango tata wa mamilioni ya dola za ulanguzi wa dawa za kulevya na utakatishaji fedha, kulingana na ripoti ya hivi majuzi ya shirika la fikra huria la United Nations.
Hezbollah ilikuwa na shughuli huko Colombia, na kundi la wanamgambo wa Farc, na kundi la madawa ya kulevya la Venezuela, kulingana na Taasisi ya Utafiti wa Uhalifu na Haki ya Umoja wa Mataifa (Unicri).

Chanzo cha picha, Reuters
Kundi hilo la wapiganaji liliongeza uwepo wake katika eneo la mpakani la Argentina, Brazili na Paraguay, imeeleza Unicri.
Miongo kadhaa iliyopita, Hazina ya Marekani pia iliweka vikwazo kwa watu na biashara kadhaa zilizoko katika nchi hizo, zikituhumiwa kuunga mkono mitandao ya kifedha ya Hezbollah duniani kote.
Hassan Moukalled, mfanyabiashara wa Lebanon aliwekewa vikwazo na Marekani mwaka 2023, anasema vikwazo hivyo na Marekani vilichochewa kisiasa.
"Lengo hasa ni kuyumbisha misingi ya kiuchumi ya Hezbollah na kuzuia mifumo yoyote mbadala ya kiuchumi mbali na ile inayoungwa mkono na Marekani katika kanda," Moukalled aliiambia BBC News Arabic.
Mikataba, magendo, na fedha za mtandaoni

Chanzo cha picha, Getty Images
Hezbollah inaripotiwa kuzalisha fedha kupitia njia nyingine kadhaa.
"Kundi limeweza kutengeneza kiasi kikubwa cha pesa kupitia sekta ya afya, elimu, na huduma nyingine za Lebanon," anasema Leveitt.
Hezbollah inanufaika kutokana na sheria za fedha na mikataba ya umma nchini Lebanon, kulingana na utafiti wa Chatham House lenye makao yake London ya mwaka 2021.
Hezbollah hutumia makampuni binafsi, yanayohusiana nayo, kutoa zabuni na kushinda kandarasi za umma, unasema utafiti huo.
Utafiti huo huo unaeleza kuwa Hezbollah ilizalisha karibu dola milioni 300 kwa mwezi kwa usafirishaji wa mafuta ya dizeli kwenda Syria kabla ya Rais wa zamani wa Syria Bashar al-Assad kung'olewa madarakani Desemba 2024.
Wakati huo huo, uchunguzi wa BBC wa 2023 ulihusisha kundi hilo na biashara haramu ya dawa za kulevya ya Captagon ya mabilioni ya dola.
Miaka miwili kabla ya hapo, Hezbollah ilitupilia mbali madai kwamba ilihusika katika utengenezaji wa dawa hiyo na kusema ni "habari ya uongo."
Juni 2023, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Galant alitangaza kuzishikilia sarafu za mtandaoni zinazodaiwa kuhusishwa na Hezbollah.
Ofisi ya Kukabiliana na Ugaidi ya Israel ilikamata karibu dola milioni 1.7 za sarafu ya mtandaoni ya Tron, na Galant alisema ni za Hezbollah na Kikosi cha Quds cha Iran.
Novemba 2023, Reuters ilimnukuu Hayward Wong, msemaji wa Visiwa vya Virgin vya Uingereza ambako Tron ndio imesajiliwa, akiliambia shirika hilo kwamba teknolojia zote zinaweza "kutumika kwa shughuli zinazotiliwa shaka."
Wong alitoa mfano wa dola za Marekani kutumika kwa utakatishaji fedha. Alisema Tron haina udhibiti kwa wanaotumia teknolojia yake na haihusiani na makundi hayo yanayotajwa na Israel.
Mwaka mmoja baadaye, Hazina ya Marekani ilimuwekea vikwazo mbadilisha fedha wa Lebanon, ikimtuhumu kwa kuipatia Hezbollah pochi za kidijitali ili kupokea fedha kutoka mauzo ya mafuta ya Iran.
Hezbollah haikujibu ombi la BBC la kutoa maoni kuhusu makala haya.











