Lebanon yasema watu 18 wameuawa katika shambulizi la Israel kusini mwa Beirut

Takribani watu 18, wakiwemo watoto wanne, wameuawa katika shambulizi la anga la Israel karibu na hospitali kubwa ya umma ya Lebanon kusini mwa Beirut, kulingana na wizara ya afya ya Lebanon.
Watu wengine 60 walijeruhiwa wakati takribani majengo matatu yapatayo umbali wa 50m (160ft) kutoka hospitali ya Chuo Kikuu cha Rafik Hariri yalipoharibiwa katika kitongoji cha Jnah Jumatatu usiku.
Wizara ya afya ilisema shambulio hilo, moja kati ya 13 lililoripotiwa katika mji mkuu, lilisababisha "uharibifu mkubwa" kwa hospitali.
Jeshi la Israel lilisema lilipiga "lengo la kigaidi la Hezbollah" karibu na hospitali hiyo, bila kutoa maelezo, na kusisitiza kuwa hospitali hiyo haikulengwa.
Siku ya Jumanne asubuhi, waokoaji walipekua marundo ya saruji iliyovunjika na chuma kilichosokotwa, wengine wakiwa wamebeba majembe, wengine kwa mikono yao tu, kwenye eneo lilipotokea shambulizi.
Mahali pazuri palikuwa kitongoji masikini na chenye watu wengi.
Takribani majengo matatu ya ghorofa nyingi yaliporomoka na mengine kadhaa kuharibiwa vibaya.
Mmoja wa waokoaji alisema hawakujua ni watu wangapi wanaweza kuwa chini ya vifusi.
Timu ya BBC iliona mwili mmoja ukitolewa, huku mwingine ukipatikana walipokuwa wakiondoka.
Mkazi mmoja alisema shambulio hilo lilitokea baada ya gari kuwasili katika eneo hilo, lakini akaongeza kuwa hawawezi kusema ni nani aliyekuwa ndani ya chombo hicho.













