Kifo cha Sinwar ni pigo kubwa kwa Hamas, lakini sio mwisho wa vita

Kifo chake ni pigo kubwa kwa Hamas

Chanzo cha picha, EPA

Muda wa kusoma: Dakika 5

Kuuawa kwa Yahya Sinwar ni ushindi mkubwa zaidi wa Israel katika vita vyake dhidi ya Hamas huko Gaza.

Kifo chake ni pigo kubwa kwa Hamas, shirika aliloligeuza kuwa jeshi la mapigano ambalo liliisababishia taifa la Israel kushindwa zaidi katika historia yake.

Sinwar hakuuawa katika operesheni iliyopangwa na vikosi maalum, lakini kwa bahati mbaya, wakati alipokutana na vikosi vya Israeli huko Rafah, kusini mwa Gaza.

Picha iliyopigwa katika eneo la tukio inamwonesha Sinwar, akiwa amevalia mavazi ya kivita, akiwa amekufa kwenye vifusi vya jengo lililoshambuliwa.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliwasifu wanajeshi hao na kuweka wazi kuwa hata ushindi ukiwa mkubwa kiasi gani haumaanishi mwisho wa vita.

"Leo tumeweka wazi kwa mara nyingine tena kile kinachotokea kwa wale wanaotudhuru. Leo tumeionesha dunia kwa mara nyingine tena ushindi wa wema dhidi ya uovu, lakini vita bado havijaisha, ni vigumu, na tunalipa gharama kubwa. "Netanyahu aliongeza.

Netanyahu alisema, "Bado kuna changamoto kubwa mbele yetu. Tunahitaji uvumilivu, umoja, ujasiri na uthabiti. Tutapigana pamoja, na kwa msaada wa Mungu tutashinda pamoja."

Netanyahu na idadi kubwa ya Waisraeli wanaounga mkono vita huko Gaza walihitaji ushindi.

Muandamanaji mjini Tel Aviv akiwa ameshikilia bango

Chanzo cha picha, Reuters

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Waziri Mkuu alirudia mara kwa mara malengo yake ya vita: "kuangamiza Hamas kama jeshi na jeshi la kisiasa na kuwarudisha mateka nyumbani." Hakuna lengo lolote lililofikiwa, licha ya mwaka mmoja wa vita ambavyo vimesababisha vifo vya Wapalestina wasiopungua 42,000 na kuacha maeneo makubwa ya Ukanda wa Gaza kuwa magofu.

Mateka waliosalia sio huru, na Hamas wanapigana na wakati mwingine wanaua vikosi vya Israeli.

Kumuua Sinwar ndio ushindi ambao Israeli walitaka. Lakini hadi Netanyahu aweze kudai kuwa malengo mengine ya vita yamefikiwa, vita, anasema, vitaendelea.

Yahya Sinwar alizaliwa mwaka 1962 katika kambi ya wakimbizi huko Khan Younis, katika Ukanda wa Gaza. Alikuwa na umri wa miaka mitano Israeli ilipoteka eneo hilo kutoka Misri katika Vita vya Mashariki ya Kati vya 1967.

Familia yake ilikuwa miongoni mwa Wapalestina zaidi ya 700,000 waliokimbia au kufukuzwa makwao na majeshi ya Israel katika vita vya mwaka 1948 ambapo Israel ilishinda na kujitangazia uhuru.

Familia yake inatoka katika jiji ambalo sasa linajulikana kama Ashkeloni, ambalo liko karibu na mpaka wa kaskazini wa Ukanda wa Gaza.

Katika miaka yake ya 20, alitiwa hatiani na Israel kwa kuwaua watoa habari wanne wa Kipalestina. Katika miaka yake 22 gerezani, alijifunza Kiebrania, alisoma adui yake na kuamini kwamba alikuwa amejua jinsi ya kupigana nao. Ambayo pia inamaanisha kuwa Israel ina rekodi zake za meno na sampuli ya DNA, inayoiwezesha kutambua mwili kuwa wake.

Sinwar aliachiliwa huru kati ya zaidi ya wafungwa 1,000 wa Kipalestina katika mpango wa kubadilishana mwaka 2011 na mwanajeshi mmoja wa Israel, Gilad Shalit.

Mnamo Oktoba 7, 2023, katika mfululizo wa mashambulizi yaliyopangwa kwa uangalifu, Sinwar na watu wake walisababisha kushindwa vibaya zaidi kwa Israeli.

Kuuawa kwa Waisraeli wapatao 1,200, kutekwa nyara na kusherehekea maadui zao kulirudisha akilini mwa Waisraeli wengi Mauaji ya Nazi.

Uzoefu wa Sinwar wa kubadilishana wafungwa lazima uwe ulimshawishi juu ya thamani na uwezo wa kuchukua mateka.

Huko Tel Aviv, familia za mateka 101 waliosalia huko Gaza, ambao nusu yao Israeli inasema kuwa tayari wamekufa, walikusanyika katika uwanja ambao walikuwa wamekusanyika mwaka mmoja uliopita, wakiitaka serikali ya Israeli kuanzisha mazungumzo mapya ya kuwarudisha watoto wao nyumbani.

Einav Zangawker, mama wa mateka Matan Zangawker, alimwomba waziri mkuu, akisema: "Netanyahu, usiwazike mateka. Nenda sasa kwa wapatanishi na umma na uwasilishe mpango mpya wa Israeli. Kwa Matan na wengine wa mateka kwenye vichuguu, muda umekwisha Una picha za ushindi.

Aliongeza: "Ikiwa Netanyahu hatanyakua wakati huu na hatasimama sasa kuwasilisha mpango mpya wa Israeli, hata kwa gharama ya kumaliza vita, hii ina maana kwamba ameamua kuwaacha mateka katika jaribio la kurefusha vita. na kuimarisha utawala wake.Hatutajisalimisha mpaka kila mtu atakaporejea.''

Waisraeli mjini Netanya walishangilia na kupeperusha bendera za taifa la Israel kushangilia kifo cha Sinwar.

Chanzo cha picha, Getty Images

Waisraeli wengi wanaamini kuwa Netanyahu anataka kurefusha vita huko Gaza ili kuahirisha siku ya hesabu ya jukumu lake katika kushindwa kwa usalama kulikomruhusu Sinwar na watu wake kuivamia Israel, na kuahirisha labda kwa muda usiojulikana kuanzishwa tena kwa kesi yake kwa mashtaka makubwa ya ufisadi.

Netanyahu anakanusha shutuma hizo akisisitiza kuwa ni kile tu anachokiita "ushindi kamili" huko Gaza dhidi ya Hamas ndio utakaorejesha usalama wa Israel.

Kama mashirika mengine ya habari, Israeli inaruhusu BBC kuingia Gaza tu kwa safari adimu zinazosimamiwa na jeshi.

Katika eneo lililoharibiwa la Khan Younis, mji alikozaliwa Sinwar, Wapalestina waliohojiwa na BBC na wanahabari wa kujitegemea wanaoaminika walisema vita vitaendelea.

Dk. Ramadan Fares alisema: “Vita hivi havitegemei Sinwar, Haniyh, au Mashaal, wala kiongozi au afisa yeyote. Ni vita vya maangamizi dhidi ya watu wa Palestina, kama sisi sote tunajua na kuelewa. Suala ni kubwa zaidi kuliko Sinwar au mtu mwingine yeyote.”

Adnan Ashour alisema baadhi ya watu walikuwa na huzuni, na wengine hawakujali kuhusu Sinwar.

"Sio tu baada yetu. Wanataka Mashariki ya Kati nzima. Wanapigana Lebanon, Syria, Yemen... Hivi ni vita kati yetu na Wayahudi tangu 1919, zaidi ya miaka 100 iliyopita," Ashour aliongeza.

Aliulizwa kama kifo cha Sinwar kitaathiri Hamas.

“Situmaini, Mungu akipenda. Hebu nifafanue: Hamas sio Sinwar tu… ni suala la watu.”

Vita vinaendelea huko Gaza. Wapalestina 25 waliuawa katika shambulizi kaskazini mwa Gaza, ambalo Israel ilisema lilipiga kituo cha kamandi cha Hamas, huku madaktari katika hospitali ya eneo hilo wakithibitisha kwamba makumi ya majeruhi waliowatibu walikuwa raia.

Kupungua kwa misaada kulianza tena baada ya Wamarekani kusema kuwa Israeli lazima iruhusu chakula zaidi na vifaa vya msaada.

Kila kiongozi wa Hamas tangu miaka ya 1990 ameuawa na Israel, lakini daima kumekuwa na mrithi. Wakati Israel inaadhimisha kifo cha Sinwar, Hamas bado ina mateka wake na bado inapigana.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Seif Abdalla