Vita vya Gaza vyaendelea kudidimiza uungwaji mkono wa Hamas

A man sits inside a ruined building following an Israeli military operation that rescued four hostages held by Hamas in Nuseirat refugee camp, in central Gaza (15 June 2024)

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mwanamume mmoja akiwa ameketi ndani ya jengo lililoharibiwa kwenye mashambulizi ya Israel wakati wa operesheni ya kuwaokoa mateka wanne waliokuwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Nuseirat mwezi uliopita.
    • Author, Lucy Williamson & Rushdi Aboualouf
    • Nafasi, BBC Mashariki ya Kati & Gaza

Mwanamume katika anaonekana kwenye video akiwa amejawa na hamaki kupitia uso wake uliyojaa damu.

“Mimi ni msomi,” anasema, “Nilikuwa na maisha mazuri, lakini tuna uongozi mbaya [Hamas]. Wamezoea kuona tukiangamizwa, Mungu awalaani! Ni wafedhuli!”

Video hiyo- ambayo haingewahi kunaswa kabla ya vita vya Gaza- ilirekodiwa nje ya hospitali japo haijulikani ni ya lini, inaonyesha mamia ya majeruhi wa Kipalestina baada ya operesheni ya Israel ya kuwakomboa mateka katikati mwa Gaza mwezi uliopita.

Tahadhari: Picha za kutisha

Sekunde chache kabla ya video kumalizika, anageukia kundi la watu.

“Mimi ni mmoja wenu,” anasema, “lakini nyinyi ni watu waoga. Tungelizuia mashambulizi haya!”

Video hiyo ilisambaa kwa kasi mitandaoni. Na sio video ya kwanza.

Katika video ya mtandaoni, mtu aliyejeruhiwa huko Gaza alirekodiwa akishambulia uongozi wa Hamas

Chanzo cha picha, UGC

Maelezo ya picha, Mtu aliyejeruhiwa huko Gaza alikashifu hatua za uongozi wa Hamas katika video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii mwezi uliopita

Ukosoaji wa wazi dhidi ya Hamas umekuwa ukiongezeka Gaza, mitaani na mtandaoni.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baadhi wameikosoa Hamas hadharani kwa kuwaficha mateka katika vyumba karibu na soko lenye shughuli nyingi, au kwa kurusha makombora kutoka maeneo yanayokaliwa na raia.

Wakazi wameiambia BBC kwamba matusi na laana dhidi ya uongozi wa Hamas sasa ni jambo la kawaida sokoni, na kwamba hata baadhi ya waendesha mikokoteni ya punda wamewapa wanyama wao majina ya utani wakimuashiria kiongozi wa Hamas huko Gaza - Yahya Sinwar - kuelekeza punda wakisema " Yallah, Sinwar!"

“Watu husema mambo kama vile, ‘Hamas imetuangamiza’ au hata kumwomba Mungu achukue uhai wao,” mtu mmoja alisema.

"Wanahoji mashambulizi ya Oktoba 7 yalikuwa ya nini - wengine wanasema yalikuwa zawadi kwa Israel."

Wengine hata wanawahimiza viongozi wao kukubaliana kusitisha mapigano na Israel.

Hata hivyo bado kuna Wagaza watiifu kwa Hamas na baada ya miaka kadhaa ya udhibiti wa ukandamizaji, ni vigumu kujua ni kwa kiasi gani kundi hilo linapoteza uungwaji mkono, au ni kwa umbali gani wapinzani waliopo wanahisi kuwa kuwa na uwezo zaidi wa kusema mawazo yao.

Lakini hata wale walio kwenye orodha ya malipo ya kikundi wanayumba.

Mfanyakazi mmoja mkuu wa serikali ya Hamas aliambia BBC kwamba mashambulizi ya Hamas yalikuwa "mkurupuko wa kichaa, usio na tija".

Aliomba tufiche utambulisho wake.

"Ninajua kutokana na kazi yangu na serikali ya Hamas kwamba ilijiandaa vyema kwa mashambulizi ya kijeshi, lakini ilipuuza eneo la nyumbani," alisema.

“Hawakujenga makazi salama ya watu, hawakuhifadhi chakula cha kutosha, mafuta na vifaa tiba. Iwapo mimi na familia yangu tutanusurika katika vita hivi, nitaondoka Gaza, nafasi ya kwanza nitakayopata.”

Picha ya faili inayoonyesha kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar akipeana mikono na mwanamume katika mkutano wa hadhara huko Gaza tarehe 14 Aprili 2023

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar, (anayepunga mkono) amekuwa mafichoni tangu kuanza kwa vita.

Kulikuwa na upinzani dhidi ya Hamas muda mrefu kabla ya vita, ingawa haikufanywa hadharani kwa kuhofia kulipizwa kisasi.

Mara ya mwisho uchaguzi wa Wapalestina ulifanyika, mwaka 2006, katika orodha ya kura ya chama Wagaza waliipigia kura Hamas katika viti 15 kati ya 24 katika eneo hilo - katika wilaya nyingine tisa, wapiga kura walichagua chama tofauti.

Mwaka mmoja baadaye, Hamas iliviondoa kwa nguvu vikosi vya Mamlaka ya Palestina kutoka Gaza na kusababisha mpasuko mkali na vuguvugu pinzani la Fatah, na kuchukua uongozi wa Ukanda wote wa Gaza.

Ameen Abed, mwanaharakati wa kisiasa, alisema alikamatwa mara kadhaa kwa ukosoaji wake dhidi ya Hamas kabla ya vita, lakini akasema - miezi tisa baadaye - upinzani unazidi kuwa wa kawaida.

"Katika eneo la Gaza, watu wengi wanakosoa kile Hamas imefanya," alisema.

“Kila wanapofikiria dhidi wanazopotia kuishi na watoto kwenye mahema, wanawalaani viongozi wao. Lakini Hamas ni msaada mkubwa miongoni mwa wale walio nje ya mpaka wa Gaza, ambao wameketi chini ya viyoyozi katika nyumba zao za starehe, ambao hawajapoteza mtoto, nyumba, maisha ya baadaye, mguu.

Kukata tamaa na vita vinamomonyoa miundo ya kijamii huko Gaza, na udhibiti wa Hamas sivyo ulivyokuwa.

Wagaza wanne kati ya watano wamefurushwa, mara nyingi huhamia kati ya makazi ya muda.

Na sheria na utaratibu umevunjwa katika sehemu fulani, kwa kiasi fulani kutokana na sera ya Israel ya kulenga vikosi vya usalama vya Gaza - sio tu huduma rasmi ya usalama ya ndani ya Hamas, lakini pia polisi wa jamii wanaohusika na uhalifu wa mitaani.

Udhibiti umepungua, magenge ya wahalifu yamestawi, uporaji wa vitongojini na misafara ya misaada; na kampuni za ulinzi za kibinafsi - zingine zinazoendeshwa na familia zenye nguvu - zimeibuka.

Watoto wa Gaza waliofurushwa makwao

Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images

Maelezo ya picha, Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya Wapalestina milioni 1.9 wamekimbia makazi yao kote Gaza

Mfanyikazi mmoja kutoka shirika la misaada linalofanya kazi huko Gaza alielezea "machafuko mitaani" na "hali ya machafuko" hayo, akisema kwamba utaratibu wa kiraia ulikuwa umevunjwa kabisa kutokana na sera ya Israel.

Waziri Mkuu wa Israel ameapa mara kwa mara kuendeleza vita hadi uwezo wa kijeshi na uongozi wa Hamas utakaposambaratishwa.

Lakini baadhi ya mashirika ya misaada - katika maeneo ya kaskazini na kusini mwa Gaza - pia yameripoti ukaguzi wa mara kwa mara wa shughuli zao na maafisa wa eneo la Hamas, na video zinasambazwa mara kwa mara za vikosi vya usalama vya Hamas visivyo rasmi kuwapiga risasi na kuwaua wale waliokamatwa wakipora.

Chanzo kimoja cha habari kiliiambia BBC kwamba makumi ya watu waliuawa na Hamas katika ghasia za umwagaji damu kutokana na mvutano kati ya makundi ya ndani, baada ya wanajeshi wa Israeli kuondoka kutoka eneo moja.

Hofu ya kuwakosoa viongozi wa Gaza inaweza kuwa imepungua, lakini haijapita kiasi, hivyo bado ni vigumu kupima kwa usahihi, zaidi ya ushuhuda wa mtu binafsi, jinsi uungwaji mkono wa kundi hilo unavyobadilika.

Baadhi yao, kama vile Jihad Talab mwenye umri wa miaka 26, bado anaunga mkono Hamas kwa dhati.

Japo amefurushwa kutoka eneo la Zeitoun katika Mji wa Gaza akiwa na mkewe, binti yake na mama yake, na sasa wanaishi Deir al Balah, alisema kundi hilo halihusiki na mateso yao.

"Lazima tuiunge mkono [Hamas] kwa sababu ndiyo inayofanya kazi mashinani, ndiyo inayoelewa vita - sio wewe au mimi," alisema. "Mashtaka tupu yanatumikia tu Kazi [Israeli]. Tutaiunga mkono hadi pumzi yetu ya mwisho."

Mwanaume wa Kipalestina akielekea kwenye bwawa la maji huko Gaza

Chanzo cha picha, Anadolou via Getty Images

Maelezo ya picha, Baada ya karibu miezi tisa ya vita, mfanyakazi wa misaada alisema Gaza ilikuwa katika "hali ya machafuko"

Kura ya maoni ya mara kwa mara iliyofanywa na taasisi yenye makao yake makuu katika Ukingo wa Magharibi, Kituo cha Palestina cha Utafiti wa Sera na Utafiti, unapendekeza kwamba watu wengi wa Gaza bado wanailaumu Israel na washirika wake kwa vita, badala ya Hamas.

Utafiti wa hivi punde mwezi Juni uligundua kuwa karibu theluthi mbili ya wahojiwa wa Gaza waliridhika na Hamas - ongezeko la pointi 12 kutoka Desemba - na kwamba karibu nusu bado wanapendelea Hamas kuendesha Gaza baada ya vita kumalizika, juu ya chaguo jingine lolote.

Matokeo haya yanatofautiana na akaunti kadhaa zilizotolewa kwa BBC, ikiwa ni pamoja na kutoka kwa afisa mkuu wa Hamas ambaye alikiri kwa faragha kwamba walikuwa wakipoteza uungwaji mkono kutokana na vita.

Mtazamo huu kupitia vizuizi vya vyombo vya habari karibu na Gaza hauwezi kamwe kutoa tathmini kamili ya hali ilivyo. Waandishi wa habari wa kimataifa wamezuiwa na Israel na Misri kuripoti moja kwa moja hali ilivyo huko.

Kilicho wazi ni kwamba Hamas inasalia kuwa nyeti sana kwa maoni ya umma.

Barua pepe zinazofanana sana huonekana mara kwa mara kwenye majukwaa fulani ya mitandao ya kijamii ili kuhalalisha vitendo vyake, mara nyingi kwa kujibu ukosoaji wa nyumbani.

Chanzo kinachoifahamu Hamas iliiambia BBC kuwa kuna mtandao wa kimataifa uliopangwa kuratibu ujumbe wa mitandao ya kijamii kwa kundi hilo.

Baada ya familia za Israel kutoa video inayoonyesha wakati wanajeshi wa kike walitekwa nyara na vitengo vya Hamas tarehe 7 Oktoba, baadhi ya watu huko Gaza walihoji kama kuwalenga wanawake wakati wa vita ni sawa na mafundisho ya Kiislamu.

Katika kujibu, akaunti kadhaa za mitandao ya kijamii zinazounga mkono Hamas zilitoa ujumbe sawa na huo zikisisitiza kwamba wanajeshi - wanaume au wanawake - walihalalishwa kulengwa na jeshi, na kusema kitengo hicho kilihusika katika kuwapiga risasi waandamanaji wa Gaza wakati wa maandamano miaka sita iliyopita.

Ukosoaji wa Hamas unazidi kuongezeka, na mgawanyiko uliozikwa kwa muda mrefu juu ya utawala wa Hamas huko Gaza unazidi kuwa wazi.

Kati ya uharibifu ulioachwa na vita vya Israeli na Hamas, vita vipya vinaibuka: vita vya kudhibiti maoni ya umma ndani ya Gaza yenyewe.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Yusuf Jumah