Vita vya Gaza: Ni mambo gani yanayokwamisha mapatano ya Israel na Hamas?

Chanzo cha picha, Reuters
Baada ya miezi kadhaa ya mkwamo, utafutaji wa amani huko Gaza umefikia hatua muhimu. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema kuwa huu ni "wakati wa maamuzi kwa watu wa Palestina na Israel na kwa hatima ya eneo zima."
Inaonekana hoja kuu kwa pande zote ni; usitishaji vita na kuachiliwa kwa mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina. Matoleo kadhaa ya makubaliano yametayarishwa, kiashiria cha ugumu wa jinsi mchakato huu utakavyofanya kazi.
Kuna kutokukubaliana juu ya nini kifanyike kwa nani, lini, na kwa mpangilio gani. Mamlaka za Israel kwa mfano, zinasema, wanajeshi wa kike wanapaswa kuachiliwa mapema.
Pia wanasema makubaliano hayo yanapaswa kuwa wazi, wakisema mateka 33 wa kwanza kuachiliwa lazima wawe hai - na wana wasiwasi juu ya kutokuwa na kura ya turufu kuhusu ni wafungwa gani wa Kipalestina wanapaswa kuachiliwa.
Masuala haya yanaweza kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo.
Lakini kuna hoja ya msingi katika mzozo huu ambayo inaweza kuwa ngumu kuifafanua; ni wakati gani vita vinapaswa kumalizika?
Maandishi ya ufunguzi wa rasimu ya makubaliano hayo - yanayoungwa mkono na Hamas - yanasema kunapaswa kuwepo "kusitishwa kwa muda kwa operesheni za kijeshi kati ya pande hizo mbili."
Hii kwa ujumla sio shida. Ndani ya wiki sita, watu wataachiliwa, vikosi vya Israel vitaondoka katika baadhi ya maeneo, waliohamishwa wanaweza kurejea – ikiwa wanapo pa kurejea.
Hatua ya Pili
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hatua ya pili itakapo anza. Rasimu ya makubaliano inazungumzia "kurejea kwa utulivu endelevu," inafafanua kama "usitishwaji wa kudumu wa operesheni za kijeshi."
Hili ndilo linaloonekana kutokukubalika na serikali ya Israel. Katika taarifa yake, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Benjamin Netanyahu, alisema:
"Israel haitaruhusu Hamas kurudisha utawala wake mbaya katika Ukanda wa Gaza, Israel haitaruhusu (Hamas) kurejesha uwezo wake wa kijeshi ili kuendelea kupanga kutuangamiza. Israel haiwezi kukubali pendekezo ambalo linaweka usalama wa raia wetu katika hatari na mustabkali wa taifa letu la Israel."
Kwa maneno mengine, serikali ya Israel inataka kuendelea kupambana na Hamas kwa muda mrefu. Kwa upande wake, Hamas inataka usitishaji wa kudumu wa vita.
Jambo ambalo haliko wazi ni iwapo kuna njia ya wapatanishi kutoka Qatar, Misri na Marekani kutafuta mwafaka katika jambo hili.
Tangazo la Hamas kwamba inaafiki makubaliano linaweza kuwa jaribio la kuilazimisha Israel kukubali pia – ama kuifanya itengwe na washirika wake.

Chanzo cha picha, Reuters
Milipiko mikali ya makombora imeripotiwa katika mji wa Rafa, licha ya Rais Joe Biden kusema Marekani haitasambaza silaha kwa ajili ya mashambulizi makubwa.
Hatua ya Israel kuanzisha operesheni ya huko Rafah inaweza kuwa jaribio la kupata masharti bora kutoka Hamas.
Lakini suala la usitishaji mapigano wa kudumu, linaonekana kuwa gumu kulipatanisha na lugha ya kidiplomasia.
Israel ilikubali kutuma ujumbe Cairo, lakini sio kufikia makubaliano, bali "kuweka njia ya kufikia makubaliano chini ya masharti yanayokubalika na Israel."
Hadi sasa, wasemaji wa serikali ya Marekani wamechukua hatua ya kuepuka kutoa maoni yao kuhusu makubaliano yaliyokubaliwa na Hamas. Walijiwekea mipaka kwa kusema makubaliano bado yanaweza kufikiwa, na kuonya vikali dhidi ya operesheni ya kijeshi huko Rafah.
Hii ni kwa sababu, ikiwa Marekani itaunga mkono makubaliano ya sasa, Netanyahu anaweza kulazimishwa kuchagua kati ya mshirika wake mkuu au watu wenye msimamo mkali wa serikali yake na wanaopinga makubaliano yoyote.
Netanyahu amenusurika misukosuko mingi katika maisha yake ya kisiasa kwa kuahirisha maamuzi magumu.
Lakini Rais wa Marekani Joe Biden ana uwezo wa kumlazimisha kiongozi wa Israel kufanya maamuzi ambayo hayapendi.
Imetafsiriwa na Rashid Abdala na kuhaririwa na Ambia Hirsi












