Ni nchi gani ambazo zimechukua hatua dhidi ya Israel kwa vita vya Gaza?

fg

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Maandamano ya kupinga vita huko Gaza yameenea katika nchi kadhaa
    • Author, Paula Rosas
    • Nafasi, BBC

Jeshi la Israel siku ya Jumatatu liliamuru raia wa Palestina wapatao 100,000 kuondoka katika eneo la mashariki mwa mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, kabla ya kutekeleza operesheni ya kijeshi .

Nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Marekani, zimeionya Israel kuepuka kuishambulia Rafah, kimbilio la mwisho kwa Wapalestina zaidi ya milioni moja. Wakati huo huo, idadi ya sauti kutoka jumuiya ya kimataifa zinazotaka Israel kukomesha mashambulizi yake katika eneo hilo zinaongezeka.

Baadhi ya nchi zimeamua kuchukua hatua za kuishinikiza serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu; kwa kukata uhusiano wa kidiplomasia, kusimamisha uuzaji wa silaha au kutumia sheria za kimataifa.

Colombia, wiki iliyopita ilitangaza kukata uhusiano wa kidiplomasia na Israel, Uturuki ilisitisha biashara na nchi hiyo. Si mara ya kwanza kwa Israel kulaaniwa na nchi nyingine kwa vita vyake huko Gaza au Ukingo wa Magharibi .

Hata hivyo, shinikizo la kimataifa halijawahi kuwa kubwa kama ilivyo sasa, hasa kutokana na ukubwa wa uharibifu usio na kifani unaosababishwa na Israel katika kujibu shambulio la Hamas la Oktoba 7.

Jibu la Israel halikuwa na huruma; zaidi ya watu 34,000 wamefariki Gaza, 85% ya watu wamehamishwa kutoka makazi yao na takribani watu milioni 1.1, wako kwenye ukingo wa njaa, kulingana na Umoja wa Mataifa (UN).

Mahusiano ya kidiplomasia

 BV

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Rais wa Colombia Gustavo Petro alitangaza mnamo Mei 1 kukata uhusiano wa kidiplomasia na Israel

Baada ya kuzuka vita, na uharibifu wa Gaza ulipoongezeka, nchi chache ziliamua kuwaondoa mabalozi wao au kusitisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel.

Jordan, Bahrain na Uturuki, ziliwarudisha mabalozi wao nyumbani, huku Chad na serikali kadhaa za Amerika ya Kusini, kama vile Chile, Honduras na Colombia, ziliamua pia kufanya hivyo.

Colombia sasa imeamua kupiga hatua mbele na kusitisha uhusiano wa kidiplomasia, hivyo kujiunga na Bolivia na Belize.

Lakini hakuna hata nchi moja kati ya hizi tatu yenye ushawishi mkubwa wa kisiasa katika Mashariki ya Kati, na uhusiano wao wa kibiashara na kidiplomasia na Israel kabla ya mgogoro huu ulikuwa mdogo.

Colombia, hata hivyo, ni mshirika wa pili wa kibiashara wa Israel katika Amerika ya Kusini, baada ya Brazil. Colombia na Israel zilitia saini makubaliano ya biashara huria 2020.

Jeshi la Colombia linatumia ndege na silaha za Israel kupambana na wauzaji wa dawa za kulevya na vikundi vya waasi. Lakini mkataba huu kwa sasa hauonekani kuathiriwa.

Mahusiano ya kibiashara

F

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wiki iliyopita, Uturuki ilitangaza kuwa itasitisha biashara zote na Israel hadi serikali inayoongozwa na Benjamin Netanyahu ikubali mtiririko wa kutosha wa misaada ya kibinadamu huko Gaza.

Kulingana na Waziri wa Biashara wa Uturuki, "shughuli za kuuza na kuagiza kutoka Israel, za bidhaa zote, zimesimamishwa."

Biashara kati ya nchi hizo mbili ilifikia jumla ya dola za kimarekani bilioni 7 mwaka jana. Uturuki ni nchi yenye Waislamu wengi kuitambua Israel, mwaka 1949. Lakini uhusiano baina ya nchi hizo mbili umekuwa mbaya katika miongo ya hivi karibuni.

Kipindi cha mvutano zaidi kilitokea mwaka 2010, wakati Uturuki ilipovunja uhusiano wa kidiplomasia na Israel baada ya nchi hiyo kushambulia kundi la meli sita za Uturuki katika maji ya kimataifa zikijaribu kwenda Gaza, ili kuvunja kizuizi cha baharini ambacho Israel inaweka katika eneo hilo.

Shambulio hilo la jeshi la Israel lilisababisha vifo vya wanaharakati 10 wa Uturuki wanaoiunga mkono Palestina.

Uhusiano ulianzishwa tena mwaka 2016, lakini nchi zote mbili ziliwafukuza mabalozi wao miaka miwili baadaye kutokana na mzozo kuhusu mauaji ya Wapalestina kwenye mpaka wa Gaza. Na hali imekuwa mbaya zaidi tangu Oktoba 7.

Kusimamishwa uuzaji wa silaha

V

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Idadi kubwa ya silaha ambazo Israel inaagiza zinatoka Marekani na Ujerumani

Nchi kadhaa - kama vile Canada, Italia, Japan, Ubelgiji na Uhispania - zilitangaza katika miezi ya hivi karibuni zitaacha kuuza silaha kwa Israel.

Hata hivyo, ukweli uliopo ni tofauti kidogo: Nchini Ubelgiji, ni mkoa wa Wallonia tu ulioamua kusitisha uuzaji wa silaha kwa Israel.

Italia pia ilitangaza kusitisha uuzaji wa silaha nje ya nchi tangu Oktoba 7, ingawa waziri wake wa ulinzi alikiri kwamba wameendelea kuitaka Israel kutotumia silaha hizo kwa Gaza. Kama sehemu ya makubaliano ya kabla ya Oktoba 7.

Uhispani ilitangaza itasimamisha usafirishaji wa silaha - na baadaye, iligunduliwa kuwa ilikuwa ikiendelea kutuma silaha. Na ilisema zilikusudiwa kwa mazoezi ya kijeshi.

Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau, alitangaza kuwa mikataba mipya ya uuzaji wa silaha kwa Israel itasitishwa, lakini si ile ambayo tayari ilikubaliwa.

Huko Japan, kampuni ya Itochu Corporation, ilisitisha ushirikiano na kampuni ya utengenezaji silaha ya Israel.

Na huko Uholanzi, mahakama iliilazimisha nchi hiyo kusitisha uuzaji wa ndege za kijeshi kwa Israel.

Zaidi ya asilimia 95 ya uagizaji wa silaha za Israel unatoka Marekani na Ujerumani, ambazo hazijatoa ishara kwamba zitazisimamisha.

‘Athari za vizuizi hivi kwa uuzaji wa silaha ni mdogo, kwani ni Marekani na Ujerumani ndizo hutoa silaha nyingi, kwa hivyo hakuna kitakachobadilika,” anasema Yossi Mekelberg kutoka Chatham House.

Kesi dhidi ya Israel

FG

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Waziri wa Sheria wa Afrika Kusini Ronald Lamola akielezea kuhusu kesi ambayo nchi yake ilifungua dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki

Disemba mwaka jana Afrika Kusini iliigeukia Mahakama ya kimataifa. Mawakili wake waliwasilisha kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) mjini The Hague, kuishutumu Israel kwa kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Palestina wa Gaza, jambo ambalo taifa la Israel linakanusha.

Januari, mahakama hiyo iliiamuru Israel kuchukua hatua za kuzuia vitendo vya mauaji ya halaiki huko Gaza, lakini haikuiamuru kusitisha.

"Israel haukudhurika kutokana na mchakato huu, lakini mchakato ulimaanisha Israel imeshindwa vita," anasema Michael Oren, aliyekuwa balozi wa Israel nchini Marekani kati ya 2009 na 2013.

Na kwa sasa kuna uwezekano wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), kutoa hati za kukamatwa kwa viongozi wakuu wa kisiasa na kijeshi wa Israel, akiwemo Netanyahu mwenyewe.

Mahakama ya ICC, ambayo ina uwezo wa kuwafungulia mashtaka watu binafsi kwa uhalifu wa kivita au uhalifu dhidi ya ubinadamu, imekuwa ikichunguza matendo ya Israel katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kwa muda wa miaka mitatu – na wanaichunguza pia Hamas.

Mekelberg anasema: "sijui hili litatupeleka wapi, sijui, lakini linatuma ujumbe kwa Israel kwamba kila tendo lina athari zake."

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah