'Tunahitaji muujiza' - Uchumi wa Israeli na Palestina ulivyoathiriwa na vita

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Jiji la Kale la Yerusalemu linapaswa kujaa wageni wakati huu wa mwaka

Na Wyre Davies,

BBC News Jerusalem

Vita vya Gaza ambavyo vimedumu kwa zaidi ya miezi sita vimekuwa na athari kubwa kwa uchumi wa Israeli na Palestina.

Takriban shughuli zote za kiuchumi huko Gaza zimesitishwa na Benki ya Dunia inasema vita hivyo pia vimeathiri biashara za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Waisraeli wanapoadhimisha sikukuu ya Kiyahudi ya Pasaka, "kuanzishwa kwa taifa" ambalo linathaminiwa sana pia wanajaribu kubaki kuendelea kuwa kivutio cha wawekezaji.

Mitaa ya mawe za Jiji la Kale la Jerusalemu ni tulivu sana. Hakuna foleni ndefu ya kutembelea maeneo takatifu - angalau yale ambayo yamebaki wazi.

Kwa kawaida mara tu baada ya Pasaka na Ramadhani na katikati ya kipindi cha Pasaka, maeno yote manne ya Jiji la Kale huwa yanajaa wageni.

Ni watalii 68,000 pekee waliowasili Israel mwezi Februari, kulingana na ofisi kuu ya takwimu ya nchi hiyo. Idadi ya wageni imepungua sana kutoka kwa wageni 319,100 katika mwezi huo huo walioitembelea israel mwaka jana.

Ingawa linaweza kuwa jambo la kushangaza kwamba wageni wote hupitia Jerusalemu wakati wa hali ya wasi wasi , wengi wa wale wanaofanya hivyo ni wahujaji wa kidini kutoka kote ulimwenguni ambao walikuwa wamelipia ajili ya safari zao mapema.

Zak's Jerusalem Gifts ni mojawapo ya maduka machache tu yaliyopo kwenye Mtaa wa Christian Quarter uliopo katika Jiji la Kale, ambalo liko Jerusalem Mashariki inayokaliwa na watu, ambayo lilifunguliwa siku nilipopita.

g
Maelezo ya picha, ''Baada ya mashambulizi ya Iran-Israel, biashara ilishuka tena. Kwa hiyo tunatarajia kwamba baada ya likizo muujiza mkubwa mkubwa utatokea'' Zak MishrikyMmiliki wa duka la zawadi za Zak
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Kwa kweli tunafanya mauzo ya mtandaoni pekee," anasema Zak, ambaye biashara yake inajishughulisha na mambo ya kale na sarafu za kibiblia.

"Hakuna watu halisi. Wiki iliyopita, baada ya mashambulizi ya Iran na Israel, biashara ilishuka tena. Kwa hiyo tunatumai kwamba baada ya likizo muujiza mkubwa utatokea."

Sio tu katika Jiji la Kale la Yerusalemu ambapo wanahitaji muujiza.

Takriban kilomita 250 (maili 150) kaskazini zaidi, kwenye mpaka wenye hali tete wa Israel na Lebanon, makabiliano ya kila siku ya risasi na Hezbollah yaliyoibuka tangu vita vya Gaza kuanza yamelilazimisha jeshi la Israel kufunga sehemu kubwa ya eneo hilo na wakaazi 80,000 wamehamishiwa kusini zaidi.

Idadi sawa ya Walebanon wamelazimika kuondoka makwao upande wa pili wa mpaka.

Kilimo katika eneo hili la Israel ni sekta nyingine ya kiuchumi ambayo imeathirika pakubwa.

Ofer "Poshko" Moskovitz haruhusiwi kabisa kuingia kwenye bustani yake ya parachichi iliyopo katika eneo la kibbutz ya Misgav Am kwa sababu ya ukaribu wake na mpaka.

Lakini hatahivyo mara kwa mara ahujitosa ndani ya shamba lake akitembea tu katikati ya miti ya shamba lake la parachichi, kutazama "fedha zake zote zikianguka ardhini".

"Lazima niende kuchuma shambani kwasababu ni muhimu sana kwa msimu ujao," Poshko anasema. "Nisipochuma tunda hili, msimu ujao utakuwa mbaya sana."

Anasema anapoteza pesa nyingi kwa sababu hawezi kuchuma parachichi - karibu shekeli 2m ($530,000; £430,000) msimu huu, anasema.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kilimo cha Israeli ni sehemu nyingine ya uchumi iliyoathiriwa sana na vita

Ingawa zinatoa riziki kwa maelfu ya watu, sekta za kilimo na utalii huchangia sehemu ndogo ya uchumi wa Israeli au Palestina.

Kwa hivyo picha pana inaonyesha nini?

Wiki iliyopita shirika la viwango, S&P Global lilishusha makadirio ya muda mrefu ya Israeli (utoka AA- hadi A- ), hii ikionyesha kupoteza imani ya soko baada ya kuongezeka kwa mvutano kati ya Israeli na Iran na wasiwasi kwamba vita huko Gaza vinaweza kuenea katika Mashariki ya Kati.

Kukosekana huko kwa imani pia kulionekana katika kushuka kwa Pato la Taifa la Israeli - jumla ya thamani ya bidhaa na huduma zinazozalishwa katika uchumi - ambazo zilipungua kwa kiwango cha 5.7% katika robo ya mwisho ya 2023.

Wengi wa Waisraeli hatahivyo wanasema umaarufu wa nchi yao wa teknolojia ya juu na kuongezeka kwa sekta zinazochipuka ni uthibitisho kuwa ina "stahimili vita " zaidi kuliko ilivyotarajiwa.

Mji wa pwani wa Tel Aviv uko kilomita 54 tu kutoka Jerusalemu. Na uko chini ya 70km kutoka Gaza.

Wakati fulani, ungesamehewa kwa kusahau - hata hivyo kwa muda mfupi - kwamba Israeli imejiingiza katika vita vya muda mrefu zaidi tangu ipate uhuru wake mnamo mwaka 1948.

g

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Watu wa Tel Aviv wakivinjari kwenye ufuo

Familia hutumia vyema jua la mapema wakati wa kiangazikwa kucheza kwenye mawimbi, wanandoa hula chakula cha mchana katika mikahawa mingi ya ufuo wazi na vijana hupiga gitaa kwenye maeneo ya kijani kibichi kati ya barabara ya pwani na Mediterania.

Mandhari inaonyesha ni jiji ambalo linafanya kazi kiuchumi na linakua haraka.

"Wanatania kwamba ndege wa kitaifa wa Israeli anapaswa kuwa korongo - aina ya mitambo!" anasema Jon Medved, mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa jukwaa la uwekezaji wa ubia wa kimataifa la Umati Wetu.

Medved , mwanaume mchangamfu na mzungumzaji mwenye mtazamo mzuri wa ulimwengu wake, ananiambia kuwa, "katika robo ya kwanza ya mwaka huu, karibu $2bn ziliwekezwa katika uanzishaji wa Israeli ... watu wenye uhusiano na Israeli hawavunji uhusiano."

Medved anasisitiza kuwa, licha ya kila kitu, Israel bado ni "taifa la kuanzia" na chaguo zuri kwa wanaotaka kuwa wawekezaji.

"Kuna mashirika 400 ya kimataifa ambayo yanafanya kazi hapa.

Hakuna hata shirika moja la kimataifa, lililofunga operesheni yake nchini Israel tangu vita vianze."

Kwa kiasi fulani, Elise Brezis anakubaliana na tathmini ya Bw Medved.

Profesa wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Bar-Ilan karibu na Tel Aviv anakiri kwamba licha ya takwimu za robo ya mwisho za Pato la Taifa, uchumi wa Israeli unasalia "kustahimili kwa kiwango cha kushangaza".

"Linapokuja suala la utalii, ndiyo, tuna kupungua kwa mauzo ya nje. Lakini pia tulikuwa na kupungua kwa uagizaji," anasema Brezis. "Kwa hivyo kwa kweli, salio la malipo bado ni sawa. Hilo ndilo tatizo ni kwamba kutokana na data, hauhisi kabisa kuwa kuna hali mbaya kama hiyo nchini Israeli."

Lakini Prof Brezis anagundua udhaifu mkubwa katika jamii ya Israeli ambao hauonekani katika data ya kiuchumi.

"Uchumi wa Israeli unaweza kuwa imara, lakini jamii ya Israel si imara hivi sasa. Ni kama kumtazama mtu na kusema, 'Wow, mshahara wake ni mkubwa,' [...] lakini kwa kweli ana huzuni. Na anafikiri, ' Nitafanya nini juu ya maisha yangu?' - Hiyo ndiyo Israeli hasa leo."

Ikiwa mtazamo katika Israeli umechanganyika, basi kuvuka kizuizi cha utengano kinachogawanya Jerusalemu na Bethlehemu mtazamo kutoka upande wa Palestina ni mbaya sana.

g

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Utalii katika Kanisa la Bethlehemu "ulisimama mara moja" baada ya Hamas kushambulia Israeli Oktoba iliyopita.

Utalii ni muhimu hasa kwa uchumi wa miji kama Bethlehem katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.

Wakati baadhi ya watu bado wanaelekea maeneo ya Yerusalemu, mahali ambapo Wakristo wanaamini kwamba Yesu alizaliwa utalii "ulisimama mara moja" baada ya tarehe 7 Oktoba mwaka jana, anasema Dk Samir Hazboun, mwenyekiti wa Chama cha Biashara na Viwanda cha Bethlehem.

Ni wakati Hamas ilipoishambulia jamii za Waisraeli karibu na Gaza na kuwauwa watu takriban 1,200 hasa raia na kuwachukua mateka wengine wapatao 250 na kuzua vita vya sasa.

Israel inategemea eneo hili pakubwa kiuchumi - lakini hivi karibuni ilifunga Ukingo wa Magharibi usio na bandari baada ya Oktoba 7 na hii imekuwa na athari mbaya kwa maisha na kazi kwa Wapalestina wengi, Dk Hazboun anasema.

"Bethlehemu hivi sasa imefungwa," anasema. "Kuna karibu malango 43 [katika kizuizi cha usalama cha Israel] lakini ni matatu tu yaliyo wazi. Hivyo kutokana na hilo wafanyakazi wa Kipalestina 16,000 na 20,000 kutoka eneo letu wanaofanya kazi nchini Israel, walipoteza mapato yao mara moja."

Baraza la biashara linasema kuwa mapato kutoka kwa Wapalestina wenyeji wanaofanya kazi nchini Israel yalifikia thamani ya shekeli 22bn ($5.8bn) kila mwaka.

"Unaweza kufikiria athari kwa uchumi," anasema Dk Hazboun, ambaye anahojia sana hali ya baadaye ya Wapalestina wachanga kadri vita vinavyoendelea na zaidi kusababisha kutorora kwa uchumi wa Israeli na Ukingo wa Magharibi.

"Kizazi cha vijana sasa hawana kazi, hawafanyi kazi. Wengi wao ni watu wenye vipaji," analaumu. "Mnamo Juni natarajia wahitimu wapya 30,000 kutoka vyuo vikuu vya Palestina. Watafanya nini?

Huko Gaza kwenyewe uchumi umeharibiwa kabisa kutokana na vita vya miezi sita.

Mashambulizi ya angani ya Israel yamesababisha vifo vya watu 34,183, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas.

Tofauti na baadhi ya maeneo ya Israel, ambako kuna matumaini ya kuweza kuondokana na dhoruba na kuendelea kuwavutia wawekezaji, katika Ukingo wa Magharibi na Gaza kuna matumaini kidogo kwamba mambo yatarejea katika hali ya kawaida.

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi