Vita vya Israel na Gaza: Kwanini inaonekana kuwa vigumu zaidi kufikia amani kuliko wakati mwingine wowote

Miezi sita baada ya mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel, vita, magonjwa, njaa na vifo vinawaangamiza Wapalestina huko Gaza. Israel imegawanyika pakubwa, huku waziri mkuu wake akihangaika kutimiza ahadi yake ya ushindi kamili. Marekani, mshirika muhimu zaidi wa Israel, imegeuka kinyume na Israel na jinsi inavyopigana vita hii.

Huku Iran ikiapa kulipiza kisasi kwa mauaji ya Israel ya jenerali mkuu wa Iran nchini Syria, na miezi kadhaa ya mgogoro wa kuvuka mpaka na mshirika wa Iran Hezbollah nchini Lebanon, hatari za vita vya Mashariki ya Kati zinaongezeka.

Takwimu zinarekodi matukio ya kutisha ya miezi sita iliyopita. Zaidi ya watu 33,000 wa Gaza, wengi wao wakiwa raia, wameuawa, kulingana na wizara ya afya. Kwa mujibu wa Save the Children, watoto 13,800 wa Kipalestina huko Gaza wameuawa na zaidi ya 12,009 kujeruhiwa. Unicef inaripoti kuwa angalau watoto 1,000 wamekatwa mguu mmoja au wote wawili.

Zaidi ya Waisraeli 1,200, wengi wao wakiwa raia, waliuawa na Hamas tarehe 7 Oktoba, na watu 253 walipelekwa Gaza kama mateka. Israel inasema kuwa kati ya mateka 130 bado wapo, angalau 34 wamefariki. Timu ya Umoja wa Mataifa iliripoti mwezi Machi kwamba ilikuwa na "taarifa za wazi na zenye kushawishi" kwamba mateka wamefanyiwa ukatili wa kijinsia "ikiwa ni pamoja na kubakwa, kunyanyaswa kingono, ukatili na udhalilishaji". Ilisema kuna "sababu nzuri" za kuamini kuwa ghasia dhidi ya mateka zinaendelea.

.

Chanzo cha picha, Oren Rosenfeld

Kibbutz Nir Oz iko kwenye mpaka wa Israeli na Gaza.

Ron Bahat alinionyesha eneo la karibu. Yuko katika miaka ya 50 na alikulia Nir Oz. Ron alinusurika na familia yake kwa bahati aliposhikia mlango wa chumba chake kwa nguvu wakati Hamas walipoingia nyumbani kwake.

Tulitembea kwenye nyumba ndogo nzuri nzuri ambazo ambazo sasa zimejaa matundu ya risasi au zilichomwa moto na hazijakuwa na mtu tangu miili ya waliofariki ilipopatikana.

Ron alionyesha nyumba za marafiki na majirani ambao waliuawa au kuchukuliwa mateka hadi Gaza. Katika nyumba moja iliyoharibiwa vibaya, rundo la nguo za watoto zilizopigwa pasi nadhifu zilinusurika moto lakini familia iliyoishi hapo haikufanikiwa.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Jambo moja la kutisha ni kwamba Nir Oz ni sehemu ya vuguvugu la mrengo wa kushoto ambalo kijadi wanachama wake wanaunga mkono wazo la amani na Wapalestina. Miezi sita baada ya Hamas kuvuka hadi Nir Oz, Ron hayuko tayari kufanya makubaliano yoyote na Gaza.

"Angalia, natamani kuwe na kiongozi wa kuleta mafanikio huko, kwa sababu mwisho lazima tuwe na amani. Lakini mtu yeyote anayeunga mkono Hamas ni adui. Wakiacha silaha zao, vita itakoma. Israeli inaacha silaha zake, sisi hatutakuwepo. Hiyo ndiyo tofauti."

Mjini Nir Oz, vioo vilivyovunjwa bado vinaanguka chini na nyumba zilizochomwa zinanuka harufu ya kuni zilizochomwa na plastiki. Hakuna mtu wa kusafisha. Wakazi wachache walionusurika wamerudi kwa ziara fupi, lakini wengi hawaendi, wakiishi katika hoteli katikati mwa Israeli.

Ushahidi unazidi kuongezeka kuwa Hamas na Israel wanaweza kuwa wamefanya uhalifu wa kivita. Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) mjini The Hague inaichunguza Israel kwa tuhuma "zinasemekana" kuwa za mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini. ICJ haiwezi kusikiliza kesi dhidi ya Hamas, ambayo imeainishwa kama shirika la kigaidi na Marekani na Uingereza, na wengine wengi, kwa vile si taifa.

Israel inakataa shtaka kwamba ina hatia ya mauaji ya halaiki. Kwa raia na wafuasi wake wengi ni jambo la kuchukiza kudai kwamba serikali iliyoundwa baada ya Ujerumani ya Nazi kuwaua Wayahudi milioni sita kwenye Holocaust yenyewe inafanya mauaji ya kimbari. Mmoja wa mawakili wa Israel, Tal Becker, aliwaambia majaji katika mahakama ya The Hague kwamba "mateso ya kutisha ya raia, Waisraeli na Wapalestina, kwanza kabisa ni matokeo ya mkakati wa Hamas".

Wapalestina wanaona mashtaka kupitia mtazamo tofauti, kutokana na miaka ya uvamizi wa kijeshi na Israel. Wapalestina wengi wanaamini kuwa Israel tayari imeunda taifa la ubaguzi wa rangi ambalo linawanyima haki zao za kimsingi. Huko Jerusalem wakati wa Pasaka, mwanaharakati mashuhuri wa kisiasa wa Kikristo wa Palestina, Dimitri Diliani, alisema kwamba "kuua watoto ni kuua watoto. Haijalishi ni mtoto gani anayeuawa. Haijalishi ni nani anayefanya mauaji".

"Ninatambua mauaji ya Holocaust, lakini hiyo haimaanishi ni ruhusa kwa Israeli kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wangu au watu wengine wowote."

Majadiliano ya ICJ yatachukua miaka mingi na washtaki wa Israeli watalazimika kuthibitisha nia ya kushinda kesi yao. Vita na vifo vya raia havijumuishwi kwenye mauaji ya kimbari peke yake.

Timu ya wanasheria wa Afrika Kusini inahoji kuwa matamshi kama yale yaliyotolewa na waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant tarehe 9 Oktoba yanaonyesha nia ya mauaji ya halaiki. "Nimeamuru kuzingirwa kabisa kwa Ukanda wa Gaza. Hakutakuwa na umeme, hakuna chakula, hakuna mafuta, kila kitu kimefungwa," alisema baada ya kutembelea Kamandi ya Kusini ya IDF huko Beersheba. "Tunapambana na wanyama binadamu na tunafanya ipasavyo."

Maafa ya kibinadamu ya Gaza pia yamerekodiwa kwa kina na waandishi wa habari wa Kipalestina, raia wanaoweka matukio kwenye mitandao ya kijamii, na mashirika ya kimataifa yanayoendesha operesheni hiyo ya misaada, ambayo wafanyakazi wake wanaruhusiwa kuingia katika eneo hilo. Saba kutoka World Central Kitchen (WCK), ambalo lilikuwa likitoa mamilioni ya chakula, waliuawa na jeshi la Israel tarehe 1 Aprili.

Vifo vyao vilimkasirisha Rais Biden na viongozi wengine wa Magharibi ambao ni washirika wakubwa wa Israel. Kulaani kwao mauaji hayo kuliifanya Israeli kutengwa zaidi. Israeli haitarajii huruma kutoka kwa sehemu kubwa ya ulimwengu. Lakini inatarajia msaada na uelewa kutoka kwa washirika wenye nguvu wa Magharibi. Badala yake, wamekataa madai ya Israeli kwamba haizuii usafirishaji wa misaada.

Kuuawa kwa timu ya WCK kunaonekana kuwa kidokezo kwa Rais Biden, ambaye uungaji mkono wake kwa Israel umekuwa wa kudumu katika maisha yake ya muda mrefu katika siasa. Kuiunga mkono Israel bado ni kanuni yake thabiti, lakini Marekani haiko tayari tena kugeuza hilo kuwa njia ya usalama kwa Benjamin Netanyahu na washirika wake wa muungano wenye itikadi kali.

Wapalestina wanauliza, kwa hasira na kufadhaika, kwa nini ilichukuwa vifo vya wafanyakazi saba wa shirika la kutoa misaada, wakiwemo Wamagharibi sita, kuleta mabadiliko, baada ya maelfu ya watu wa Gaza kuuawa. Mashirika ya misaada yanayofanya kazi huko Gaza yanasema shambulio dhidi ya wafanyakazi wa misaada halikuwa tukio la pekee, bali ni matokeo ya kutojali maisha ya raia wa Palestina.

Benjamin Netanyahu ametoa "kisasi kikubwa" alichowaahidi Waisraeli tarehe 7 Oktoba. Ahadi zake nyingine, za ushindi kamili, kuangamizwa kwa Hamas, na kurejea kwa mateka hazijafikiwa. Ndani ya Israel, anakabiliwa na shinikizo kali la kisiasa. Ukadiriaji wa idhini yake katika kura za maoni umeshuka.

Wiki iliyopita mjini Jerusalem maelfu ya waandamanaji waliokuwa wakipeperusha bendera za Israel walifunga mitaa kuzunguka bunge wakitaka waziri mkuu ajiuzulu na uchaguzi mpya ufanyike.

"Netanyahu ana nia ya kurefusha vita kadiri awezavyo, kwa sababu maadamu vita bado vinaendelea, anaweza kusema kuwa sasa si wakati wa uchaguzi mpya," alisema Nava Rosalio, mmoja wa viongozi wanaompinga Netanyahu.

"Anasema sasa si wakati wa kutafuta nani anahusika, ambaye ni yeye. Hivyo anapendelea kuwaweka mateka huko Gaza, na anapendelea kurefusha vita."

Miezi sita baadaye, haichukuliwi tena kuwa sio uzalendo kuandamana dhidi ya kushindwa kumaliza vita na kuwaachilia mateka. Migawanyiko ya Israeli iko wazi kwa mara nyingine tena.

.

Chanzo cha picha, Oren Rosenfeld

Bw Netanyahu anakabiliwa na shutuma kali kwamba kipaumbele chake ni kujinusuru kisiasa. Ili kusalia madarakani, ni lazima ahifadhi muungano wake, ambao umejengwa kwa kuungwa mkono na vyama vya Kiyahudi vyenye msimamo mkali.

Hawapingi tu kuachiliwa kwa wingi kwa wafungwa wa usalama wa Kipalestina kununua uhuru wa mateka wa Israeli, bila hivyo, usitishaji wa mapigano hautafanyika.

Washirika wakuu wawili wa Bw Netanyahu wasiopenda ukabila, Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich na Waziri wa Usalama wa Kitaifa Itamar Ben-Gvir, wanataka mengi zaidi. Wapalestina waondoke Gaza ili Wayahudi waweze kukaa huko badala yake.

Waziri mkuu, anayesifika kwa ustadi wake katika siasa, anafanya kitendo cha kusawazisha kuwafurahisha huku akikana kwamba maoni ya Bw Smotrich na Bw Ben-Gvir yanaakisi sera ya serikali.

Kabla ya Oktoba, mgawanyiko wa Israel lazima uwe umeifanya ionekane kuwa Hamas ni hatari. Miezi sita baadaye, mifarakano sawa ndani ya Israeli kuhusu sasa na siku zijazo inafanya kuwa vigumu kushinda vita.