Nini chimbuko la uhasama kati ya Israel na Iran?

kl

Chanzo cha picha, MANU BRABO/GETTY

Maelezo ya picha, Uadui kati ya Iran na Israel ni moja ya chanzo cha ukosefu wa utulivu katika Mashariki ya Kati.

Hofu ya kupanuka kwa vita Mashariki ya Kati kati ya Israel na Iran inazidi kukua hivi sasa.

Iran ameahidi kujibu mauji ya Jumatatu ya makamanda wake wakuu wa kijeshi - katika shambulio la Israel dhidi ya ubalozi wake mdogo mjini Damascus.

Hofu imetanda kwenye mitaa ya Israel. Baadhi ya wananchi wakikimbilia kuchukua maji na vitu vingine vya muhimu.

Kadhalika, jeshi limeitisha wanajeshi wa ziada na huduma za GPS zimezuiwa ili kutatiza ungiaji wa ndege zisizo na rubani na makombora.

Israel na Iran zimekuwa katika mizozo kwa miaka. Mivutano yao yamekuwa mojawapo ya vyanzo vya ukosefu wa utulivu katika Mashariki ya Kati.

Kwa Tehran, Israel haina haki ya kuwepo. Watawala wake huiona ni ‘shetani mdogo’ mshirika wa Marekani katika Mashariki ya Kati, ambayo wanaiita “Shetani mkuu,” na wanataka wote wawili watoweke katika eneo hilo.

Israel inaishutumu Iran kwa kufadhili vikundi vya kigaidi na kufanya mashambulizi dhidi ya maslahi yake.

Uhasama huo umesababisha vifo, mara nyingi ni matokeo ya operesheni za siri ambapo hakuna serikali inayokubali umehsika. Na Vita vya Gaza vimefanya mambo kuharibika zaidi.

Pia unaweza kusoma

Uhasama wa Israel na Iran ulianzaje?

cv

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979 nchini Iran ndio ulikuwa mwanzo wa Wairani kuikataa Israel.

Uhusiano kati ya Israel na Iran ulikuwa wa kuridhisha hadi mwaka 1979 baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Ayatollahs huko Tehran.

Igawa ilipinga mpango wa kugawanywa kwa Palestina uliosababisha kuundwa kwa Taifa la Israel mwaka 1948, Iran ilikuwa nchi ya pili ya Kiislamu kuitambua Israel, baada ya Misri.

Wakati huo, Iran ilikuwa na utawala wa kifalme wa Shah wa nasaba ya Pahlavi na mmoja wa washirika wakuu wa Marekani katika Mashariki ya Kati.

Kwa sababu hiyo, mwanzilishi wa Israel na mkuu wake wa kwanza wa serikali, David Ben-Gurion, alijenga urafiki na Iran kama njia ya kukabiliana na kukataliwa kwa dola mpya ya Kiyahudi na majirani zake wa Kiarabu.

Lakini mwaka 1979, Mapinduzi ya Ruhollah Khomeini yalimpindua Shah na kuweka jamhuri ya Kiislamu ambayo ilijidhihirisha kuwa mtetezi wa wanyonge na moja ya alama zake kuu za utambulisho ni kuukataa ubeberu wa Marekani na mshirika wake Israel.

FD

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Khomeini na viongozi wengine wa Mapinduzi ya Kiislamu wanaunga mkono mapambano ya Palestina dhidi ya Israel.

Utawala mpya wa Ayatollah ulivunja uhusiano na Israel, ukaacha kutambua uhalali wa hati za kusafiria za raia wa Israel na ukauteka ubalozi wa Israel mjini Tehran ili kuukabidhi kwa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO), ambayo wakati huo ilikuwa ikiongoza mapambano ya kulipigania taifa la Palestina dhidi ya serikali ya Israel.

Alí Vaez, kutoka International Crisis Group, anasema "chuki dhidi ya Israel ilikuwa nguzo ya utawala mpya wa Iran kwa sababu viongozi wake wengi walipata mafunzo na kushiriki vita vya msituni na Wapalestina katika maeneo kama Lebanoni na waliwahurumia sana.”

"Iran mpya pia ilitaka kujionyesha kama nguvu ya Kiislamu na kuibua hoja ya Palestina dhidi ya Israel ambayo nchi za Kiislamu za Kiarabu zilikuwa zimeiacha."

Kwa hivyo, Khomeini aliichukua kadhia ya Palestina kama yake mwenyewe na maandamano makubwa ya kuunga mkono Wapalestina yakawa yanafanyika mara kwa mara mjini Tehran.

EW

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Maandamano dhidi ya Israel yakawa ya mara kwa mara mjini Tehran.

Vaez anasema “huko Israel, uadui dhidi ya Iran ulianza katika ya miaka ya 1990, kwa sababu Iraq ya Saddam Hussein hapo awali ilichukuliwa kuwa tishio kubwa zaidi katika eneo hilo.”

Kiasi kwamba serikali ya Israel ilikuwa ni miongoni mwa wapatanishi waliofanikisha kile kinachoitwa Iran-Contra, mpango wa siri ambao Marekani ilipeleka silaha Iran ili zitumike katika vita dhidi ya Iraq kati ya 1980 na 1988.

Lakini baada ya muda, Israel ilianza kuiona Iran kuwa hatari zaidi kwa kuwepo wake. Hatimaye uhasama kati ya nchi hizo ulitoka kuwa wa maneno hadi wa vitendo.

DC

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran ni moja ya malengo ya Israel
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Vaez anabainisha kwamba, pia Iran ilikabiliana na Saudi Arabia, nchi nyingine kubwa ya kikanda. Hapa ni muhimu kujua kuwa Iran ni taifa la Kiajemi na ki-Shia katika ulimwengu wa Kiislamu wenye Wasunni wengi na Waarabu.

Kwa hivyo, mtandao wa mashirika yaliyofungamana na Tehran uliongezeka na kufanya vitendo kwa maslahi yake. Kile kinachoitwa "mhimili wa upinzani" wa Iran umeenea Lebanon, Syria, Iraqi na Yemen.

Israel haikukaa kimya na imefanya mashambulizi na operesheni nyingine dhidi ya Iran na washirika wake, mara nyingi katika nchi ambako Iran inafadhili na kuunga mkono makundi yenye silaha.

Mwaka 1992, kikundi cha Islamic Jihad, kinachohusishwa na Iran, kililipua ubalozi wa Israel huko Buenos Aires, na kusababisha vifo vya watu 29. Baada ya kiongozi wa Hezbollah Abbas al-Musawi kuuwawa, katika shambulio ambalo lilihusishwa na idara za ujasusi za Israel.

Israel pia inapambana kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran na kuzuia Iran kuwa na silaha za nyukilia. Israel haiamini maneno ya Iran kwamba mpango wake wa nyukilia ni kwa ajili ya matumizi ya kiraia.

Kwa kushirikiana na Marekani, Israel ilitengeneza virusi vya kompyuta vya Stuxnet, ambavyo vilisababisha uharibifu mkubwa kwa vituo vya nyuklia vya Iran katika muongo wa kwanza ya miaka ya 2000.

Tehran pia imeshutumu idara za kijasusi za Israel kuhusika na mashambulizi dhidi ya wanasayansi wakuu wanaosimamia mpango wake wa nyuklia.

VC

Chanzo cha picha, MENAHEM KAHANA/GETTY

Maelezo ya picha, Mashambulizi ya Israel huko Gaza yamezidisha uhasama kati ya Israel na Iran.

Mfano ni mauaji ya 2020 ya Mohsen Fakhrizadeh, anaeaminika kuwa msimamizi wa ngazi ya juu wa programu hiyo. Serikali ya Israel haijawahi kukubali kuhusika na vifo vya wanasayansi wa Iran.

Israel, pamoja na washirika wake wa Magharibi, wanaishutumu Iran kufadhili mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na roketi dhidi ya Israel, pamoja na kufanya mashambulizi kadhaa ya mtandaoni.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka nchini Syria tangu mwaka 2011 vilikuwa sababu nyingine ya mvutano.

Ujasusi wa nchi za Magharibi unaonyesha kuwa Iran ilituma fedha, silaha na wakufunzi kuunga mkono vikosi vya Rais Bashar al-Assad.

Israel inaamini kuwa jirani ya Syria ni mojawapo ya njia kuu ambayo Iran hutumia kutuma silaha na vifaa kwa Hezbollah nchini Lebanon.

Mwaka 2021 Israel iliilaumu Iran kwa mashambulizi dhidi ya meli za Israel katika Ghuba ya Oman. Iran kwa upande wake iliishutumu Israel kwa kushambulia meli zake katika bahari ya Shamu.

Mambo yalivyo sasa Israel na Iran

Tangu Oktoba 7, 2023 baada ya mashambulizi ya wanamgambo wa Hamas dhidi ya Israel na mashambulizi makubwa ya kijeshi yaliyoanzishwa na jeshi la Israel huko Gaza.

Wachambuzi na baadhi ya serikali duniani wameelezea wasiwasi kwamba mzozo huo unaweza kuenea katika eneo hilo. Na kuzusha makabiliano ya wazi na ya moja kwa moja kati ya Iran na Israel.

Mapigano kati ya wanajeshi wa Israel na wanamgambo wa Hezbollah kwenye mpaka na Lebanon yameongezeka katika miezi ya hivi karibuni.

DX

Chanzo cha picha, AMMAR GHALI/GETTY

Maelezo ya picha, Shambulio dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran jijini Damascus, majenerali kadhaa waliuawa, limeikasirisha Iran.

Kulingana na Vaez, "hakuna nchi inataka mzozo uenee. Israel iko katika vita kwa miezi sita sasa dhidi ya Hamas huko Gaza, ambavyo vimeathiri vibaya sana sifa yake katika jukwaa la kimataifa na kupelekea kutengwa zaidi kuliko hapo awali.”

"Iran kwa upande wake, ina matatizo mengi ya kiuchumi na serikali yake inakabiliwa na upinzani wa ndani baada ya miezi kadhaa ya maandamano. Hivyo haiko katika hali nzuri.”

Lakini shambulio dhidi ya makao yake makuu ya kidiplomasia mjini Damascus, ambalo lilisababisha vifo vya watu 13, wakiwemo maafisa wakuu mashuhuri wa Iran, kama vile Jenerali wa Walinzi wa Mapinduzi, Mohammad Reza Zahedi na naibu wake, Hadi Hajriahimi, limeiumiza zaidi Tehran.

Wizara yake ya Mambo ya Nje imeahidi "adhabu kwa mshambuliaji" na balozi wake nchini Syria, Hossein Akbari, alitangaza kuwa jibu litakuwa kali.

Wachambuzi wa masuala ya kijasusi, waandishi wa habari na wanadiplomasia wamekuwa wakikisia wakisema majibu ya Iran yanaweza kuwa - shambulio la ndege zisizo na rubani, shambulio baharini au mtandaoni au yote hayo.

Vyovyote itakavyokuwa, na wakati wowote itakapokuwa, unaweza kucheza kamari kuwa haitakuwa mara ya mwisho kwa mvutano huu wa muda mrefu.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah