Man United ilikataa kumsajili Osimhen 'kwasababu ya Afcon'

Chanzo cha picha, Getty Images
Ratiba ya Kombe la mataifa Afrika (Afcon) ni moja ya sababu kuu zilizoifanya Manchester United kutofanya jaribio la kumsajili mshambuliaji Victor Osimhen, kwa mujibu wa aliyekuwa kocha wa timu ya kwanza wa klabu hiyo, Benni McCarthy.
Osimhen, mshambuliaji wa Nigeria, alivutia vilabu vikubwa barani Ulaya baada ya kufunga mabao 26 ya ligi msimu wa 2022-23 na kuisaidia Napoli kutwaa ubingwa wa Italia kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 33.
McCarthy, aliyekuwa sehemu ya benchi la ufundi la Old Trafford chini ya aliyekuwa meneja Erik ten Hag, amesema alihusika katika mchakato wa kusaka washambuliaji na aliamini Osimhen “angefaa kikamilifu” ndani ya kikosi cha United.
Hata hivyo, kufanyika kwa Afcon kila baada ya miaka miwili na mara nyingi katikati ya msimu wa soka Ulaya kuliifanya United kuelekeza macho kwa wachezaji wengine licha ya Osimhen kuwa “juu kabisa ya orodha” mwanzoni.
“Ukitumia pauni milioni 100 kumsajili mchezaji, hutaki kumpoteza kwa mwezi mzima kutokana na Afcon,” McCarthy aliiambia BBC World Service.
“Nadhani angefanikiwa sana pale. Lakini Afcon ilikuwa kikwazo kikubwa.
“Kukosekana katika mechi nyingi muhimu, timu huathirika inapokosa mshambuliaji wake mkuu.
“Hivyo uamuzi ukafanyika. Kwa kiasi kikubwa sana ilikuwa kwa sababu ya Afcon, na jina la Victor Osimhen likaondolewa kwenye orodha ya wachezaji waliokuwa wakivutia.”
Badala yake, United ilimsajili Rasmus Højlund kutoka Atalanta kwa pauni milioni 72 Agosti 2023. Mshambuliaji huyo wa Denmark alifunga mabao 26 katika mechi 95 kabla ya kujiunga na Napoli kwa mkopo Septemba mwaka uliofuata.
Osimhen, ambaye alitajwa kuwa Mwanasoka Bora wa Afrika mwaka 2023, aliondoka Napoli na kujiunga na Galatasaray kwa mkopo Septemba 2024, kabla ya kukamilisha uhamisho wa kudumu Julai mwaka uliofuata.
McCarthy, ambaye sasa ni kocha mkuu wa timu ya soka ya Kenya, wenyeji wa Afcon 2027, anaamini mashindano hayo yanapaswa kuendelea kufanyika kila baada ya miaka miwili ili kuipa Afrika jukwaa la kuonesha vipaji vyake, lakini akasisitiza haja ya kupanga ratiba isiyogongana na mashindano ya vilabu.
“Nafikiri Caf inapaswa kushirikiana vyema na Fifa na Uefa kupanga muda wa mashindano haya ili yasihatarishe taaluma za wachezaji,” alisema McCarthy mwenye umri wa miaka 48.
“Yangeweza kufanyika wakati wa mapumziko rasmi ya ligi au dirisha la Juni–Julai baada ya msimu kumalizika.
“Lakini pia hapo wachezaji hawapati mapumziko.
“Kwa maoni yangu, hilo ndilo suluhisho bora, kwa sababu baadhi ya vilabu vinaepuka wachezaji wa Afrika kwa kuhofia kuwapoteza kwa mwezi mmoja wakati wa Afcon.
“Naamini mashindano yabaki ya kila baada ya miaka miwili, lakini yafanyike wakati usiogongana na ratiba za vilabu.”
Soma zaidi:







