Kwa nini Israel haijatia saini mkataba wa kuzuia kuenea silaha za nyuklia?

GV

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Israel haidhibitishi wala kukanusha kuwa inamiliki silaha za nyuklia.
    • Author, Alessandra Corrêa
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Mzozo kati ya Israel na Iran kwa mara nyingine tena umeibua swali la nyuklia ya Israel. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametetea mashambulizi dhidi ya Iran kwa lengo la kuizuia Tehran kutengeneza silaha za nyuklia.

"Tusipoizuia, Iran inaweza kuzalisha silaha za nyuklia kwa muda mfupi sana," alisema Netanyahu.

Iran inakanusha kutaka kutengeneza silaha za nyuklia. Mpango wa kurutubisha uranium—ambao unazua shaka na wasiwasi kwa Israel, Marekani, na nchi nyingine—unakusudiwa kwa madhumuni ya amani, kama vile nishati, dawa, au kilimo, kulingana na maafisa wa Iran.

Serikali ya Israel imepitisha sera ya kutothibitisha wala kukanusha kuwa inamiliki silaha za nyuklia.

John Erath, mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti kuhusu Udhibiti wa Silaha hatari, ameiambia BBC. "Israel haijawahi kutangaza kuwa inamiliki silaha za nyuklia. Haijawahi kutangaza kuwa haina silaha hizo."

Pia unaweza kusoma

Nyuklia ya Israel

GHB

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mashirika yanatabiri ongezeko la silaha za nyuklia katika muongo ujao.

Israel inachukuliwa kuwa miongoni mwa nchi tisa duniani ambazo kwa sasa zinamiliki silaha za nyuklia, zikiwemo; Marekani, Russia, China, Ufaransa, Uingereza, Pakistan, India na Korea Kaskazini.

"Israel inakadiriwa kuwa na takriban mabomu 90 ya nyuklia," linasema shirika la Kimataifa ya Kukomesha Silaha za Nyuklia (ICAN), lenye makao makuu Uswizi, ambalo limetunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel 2017.

Makadirio haya yanakaribiana na yale ya mashirika mengine, ikiwa ni pamoja na Shirikisho la Wanasayansi wa Marekani (FAS), lililoanzishwa mwaka 1945 kwa lengo la "kupunguza hatari ya silaha za nyuklia, silaha za kibayolojia na kemikali, na mabadiliko ya hali ya hewa."

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Zaidi ya hayo, Israel inakadiriwa kuwa na akiba ya nyenzo za nyuklia, zinazotosha kutengeneza takriban mabomu 200. Hata hivyo, usiri hufanya iwe vigumu kuelewa picha sahihi juu ya nyuklia ya Israel.

"Wataalamu wanaamini Israel inaweza kurusha mabomu ya nyuklia kwa kutumia makombora, nyambizi na ndege," inasema ICAN.

Kwa mabomu 90 ya nyuklia, Israel inakuwa ya pili kutoka chini kati ya nchi tisa zilizotajwa, baada ya Korea Kaskazini.

Kulingana na makadirio ya FAS, nchi hizi tisa zina jumla ya takriban vichwa 12,300 vya nyuklia, karibu asilimia 90 ni vya Marekani au Urusi.

Idadi kamili ya silaha za nyuklia kwa kila nchi ni siri ya taifa husika, hivyo makadirio haya, yanaweza yasiwe sahihi.

Inaaminika kuwa mpango wa Israel ulianza miaka ya 1950, na silaha ya kwanza ya nyuklia iliundwa katika miaka ya 1960. Ujasiri, ujanja, na ufichaji, yalikuwa mambo muhimu katika uundaji wa nyuklia ya Israel.

Kupitia nyaraka mpya za kihistoria zilizofichuliwa, inaelezwa hata Marekani mwanzoni ilikuwa haifahamu ukubwa wa mradi huo.

Katika miaka ya hivi karibuni, kauli za baadhi ya maafisa wa Israel pia zimetafsiriwa kuwa ni dalili kuwa nchi hiyo inamiliki silaha za nyuklia.

Mwaka 2023, katikati ya mzozo huko Gaza, Waziri wa Urithi Amichai Eliyahu alipendekeza katika mahojiano na vyombo vya habari vya ndani kwamba bomu la atomiki lirushwe kwenye ardhi ya Palestina.

Nyuklia Duniani

GFVC

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kulingana na mashirika ya wataalamu, Marekani imepitisha sera ya kutoishinikiza Israel kujiunga na Mkataba wa Kuzuia Uenezaji Silaha za Nyuklia (NPT).

Uundaji wa silaha za nyuklia duniani kote unaonekana kupungua kwa kiasi kikubwa tangu kipindi cha Vita Baridi (1947-1991), wakati huo ghala za silaha za nyuklia zilifikia karibu vichwa 70,000, kulingana na ICAN.

Wakati baadhi ya nchi zinapunguza silaha zao, zingine zinaongeza.

Serikali ya Israel ni miongoni mwa nchi chache ambazo hazijatia saini Mkataba wa Kuzuia Silaha za Nyuklia (NPT), mkataba wa kimataifa ambao ulianza kutekelezwa mwaka 1970 na nchi 190 zimetia saini.

Watia saini wamejitolea kuzuia kuenea kwa silaha hizi na kukuza matumizi ya nishati ya nyuklia kwa madhumuni ya amani.

"NPT ni makubaliano ya udhibiti wa silaha za nykulia, huku Sudan Kusini, India, Israel, na Pakistan pekee zikisalia nje ya mkataba huo," linasema shirika la Kudhibiti Silaha, lenye makao yake nchini Marekani.

Mbali na nchi hizi nne ambazo hazikuwahi kusaini makubaliano hayo, Korea Kaskazini ilitia saini na ilijitoa rasmi mwaka 2003.

NPT inazigawanya nchi katika makundi mawili: zile zinazomiliki silaha za nyuklia, yaani Marekani, Urusi, China, Ufaransa na Uingereza, na zile ambazo hazina.

Wakati mkataba huo ulipojadiliwa, mataifa yote matano tayari yalikuwa na nguvu za nyuklia, na lengo lilikuwa kuzuia orodha ya nchi hizo kukua.

NPT inazichukulia nchi zenye silaha za nyuklia kuwa ni zile tu ambazo "zimetengeneza na kulipua silaha za nyuklia au kifaa kingine cha nyuklia kabla ya tarehe 1 Januari 1967."

Kwa hivyo, ikiwa Israel, India au Pakistan wataamua kujiunga, watalazimika kujiunga kama "nchi zisizo na silaha za nyuklia."

Kisha watapaswa kuharibu silaha zao za nyuklia na kuziweka nyenzo zao za nyuklia chini ya ulinzi wa kimataifa, kama Afrika Kusini ilivyofanya ilipojiunga na NPT mwaka1991.

Nyaraka za miaka ya 1960 zilizokusanywa na Hifadhi ya Kitaifa ya Usalama katika Chuo Kikuu cha George Washington zinaonyesha kwamba Marekani hapo awali ilitarajia Israel kujiunga na NPT. Hata hivyo, serikali ya Israel iliamua kutotia saini mkataba huo.

"Israel iliuona mpango wake wa nyuklia kama sera ya kulinda uhai wa taifa hilo," anasema Nicholas Miller, mtaalam wa nyuklia na profesa katika Chuo cha Dartmouth, New Hampshire, Marekani

Wataalamu wanasema, Israel imezungukwa na nchi ambazo zinaichukia. Hii ndiyo sababu inaamini silaha za nyuklia ni muhimu ili kuhakikisha uwepo kwake.

Kutoaminiana

GB

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Shambulio la Israel kwenye mji mkuu wa Iran, Tehran, Juni 15.

"Marekani haijatoa mashinikizo makubwa kwa Israel, kwa sababu ya uhusiano wa karibu kati ya Israel na Washington, na kwa sehemu kwa sababu Israel haijaweka wazi juu ya uwezo wake wa nyuklia," anasema Miller.

Hata hivyo anadokeza kuwa, wapinzani wa Israel kwa muda mrefu wamekuwa wakitetea kutokuwepo silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati ili kutoa shinikizo la kidiplomasia kwa serikali ya Israel kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Msimamo wa Israel na Marekani umekosolewa kuwa unaweza kudhoofisha juhudi za kuzuia kuenea kwa silaha hizo na kuyumbisha eneo hilo.

Ukosefu wa uwazi na kile ambacho wengine wanaona kuwa ni unafiki pia hukosolewa, kwani Israel imekuwa ikitumia juhudi za kidiplomasia na kijeshi kuzuia nchi zingine katika eneo hilo kupata silaha za nyuklia.

"Israel kumiliki silaha za nyuklia na kukubalika kimyakimya kwao na Marekani na serikali nyingi za Magharibi, kunaleta hatari ya wazi ya kuenea na kunaweza kuzihimiza serikali nyingine katika eneo hilo kuzingatia silaha za nyuklia..." ripoti ya ICAN inasema.

Bwana Miller anasema "hakuna shaka kwamba mpango wa nyuklia wa Israel umezihimiza nchi nyingine katika eneo hilo kuzindua mipango yao ya silaha za nyuklia, na kusababisha mvutano."

"Kwa nyakati tofauti, Iraq, Iran, Libya, na Syria zilijaribu kupata silaha za nyuklia, na kila moja imechochewa, kwa kiasi fulani, na uwezo wa nyuklia wa Israel," anaeleza.