Jimmy Carter alipokutana na Kim ili kuzuia vita vya nyuklia na Korea Kaskazini

fv

Chanzo cha picha, AP

Maelezo ya picha, Jimmy Carter na Kim Il-sung wakiwa kwenye boti ya familia tawala ya Korea Kaskazini
Muda wa kusoma: Dakika 5

Miongo mitatu iliyopita, ulimwengu ulikuwa ukingoni mwa mzozo wa nyuklia - hadi Jimmy Carter alipokwenda nchini Korea Kaskazini.

Juni 1994, rais wa zamani wa Marekani aliwasili Pyongyang kwa mazungumzo na kiongozi wa wakati huo Kim Il-sung. Lilikuwa ni jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa; ni mara ya kwanza kwa rais aliye madarakani na aliyestaafu wa Marekani kutembelea nchi hiyo.

Wengi wanaamini ziara hiyo iliepusha vita kati ya Marekani na Korea Kaskazini ambavyo vingeweza kugharimu mamilioni ya maisha.

Pia unaweza kusoma

Mvutano wa nyuklia

RF

Chanzo cha picha, Kydo

Maelezo ya picha, Mvutano uliongezeka baada ya tuhuma za Marekani juu ya kinu cha nyuklia huko Yongbyon. Picha hii ni 2008.

Mapema mwaka 1994, mvutano ulikuwa mkubwa kati ya Washington na Pyongyang, pale maafisa walipokuwa wakijaribu kukomesha mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.

Mashirika ya kijasusi ya Marekani yalishuku kuwa licha ya mazungumzo yanayoendelea, huenda Korea Kaskazini inatengeneza silaha za nyuklia kwa siri.

Katika tangazo la kushangaza, Korea Kaskazini ilisema imeanza kuchomoa maelfu ya silinda kutoka katika kinu chake cha nyuklia cha Yongbyon kwa ajili ya kuchakatwa upya.

Hii ilikiuka makubaliano ya awali na Marekani ambapo hatua hiyo ilihitaji kuwepo kwa wakaguzi kutoka Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA). Faula ya hilo, Korea Kaskazini pia ilitangaza kujiondoa kwenye IAEA.

Mashaka ya Marekani yaliongezeka huku Washington ikiamini kuwa Pyongyang inatayarisha silaha za nyuklia. Washington ilianza kuandaa hatua kadhaa za kulipiza kisasi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha vikwazo kupitia Umoja wa Mataifa na kuimarisha jeshi nchini Korea Kusini.

Maafisa wa Marekani walifichua pia kuwa walifikiria kurusha kombora huko Yongbyon - hatua ambayo walijua ingesababisha vita kwenye rasi ya Korea na uharibifu wa mji mkuu wa Korea Kusini, Seoul.

Sababu hii ndio ilimfanya Carter kufanya ziara. Kwa miaka mingi, alibembelezwa kimya kimya na Kim Il-sung, kwa kutuma maombi binafsi ya kumtaka Carter atembelee Pyongyang.

Juni 1994, baada ya kusikia mipango ya kijeshi ya Washington, na majadiliano kati ya serikali ya Marekani na China - mshirika mkuu wa Korea Kaskazini - Carter aliamua kukubali mwaliko wa Kim.

Nadhani tulikuwa katika ukingo wa vita," aliliambia shirika la utangazaji la umma la Marekani PBS. "Inawezekana ikawa Vita vya pili vya Korea, ambapo watu milioni moja au zaidi wangeuawa."

Ziara ya Carter

f

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Carter na mke wake, Rosalynn, walikaa Korea Kaskazini kwa siku nne mwezi Juni 1994

Kwanza, Carter alipima utayari wa Kim. Alitoa msururu wa maombi, ambayo yote yalikubaliwa, isipokuwa la mwisho: Carter alitaka kusafiri hadi Pyongyang kutokea Seoul kupitia eneo lisilo la kijeshi (DMZ), ukanda wa ardhi ambao ni kizuizi kati ya Korea mbili.

"Jibu lao la haraka lilikuwa, hakuna mtu aliyewahi kufanya hivi kwa miaka 43 iliyopita, hata katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa alilazimika kwenda Pyongyang kupitia Beijing. Na nikasema, 'Sawa, siendi, basi'," alisema.

Wiki moja baadaye, Kim alikubali.

Carter kwanza aliamua kumfahamisha rais wa wakati huo wa Marekani Bill Clinton kwamba anakwenda Korea ya Kaskazini, hata iweje.

"Lakini makamu wa rais Al Gore alinipigia simu na kuniambia ikiwa nitabadilisha maneno kutoka 'nimeamua kwenda' hadi 'nina tamani sana kwenda,' nitajaribu kuomba ruhusa moja kwa moja kutoka kwa Clinton."

Alinipigia simu tena asubuhi iliyofuata na kusema nina ruhusa ya kwenda."

Mvutano na Marekani

RF

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Carter na Clinton mwaka 2000
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tarehe 15 Juni 1994, Carter alivuka hadi Korea Kaskazini, akifuatana na mkewe Rosalyn, kikundi kidogo cha wasaidizi na wafanyakazi wa TV.

Kwa siku kadhaa, Carter na timu yake alikuwa na mikutano na Kim, walichukuliwa kwenye ziara ya kutembelea Pyongyang na wakasafiri kwa boti ya kifahari inayomilikiwa na mtoto wa Kim, Kim Jong-il.

Carter aligundua kuwa mawazo yake yako sahihi: Korea Kaskazini sio tu iliogopa mashambulizi ya kijeshi ya Marekani huko Yongbyon, lakini pia ilikuwa tayari inajitayarisha kwa vita.

"Niliwauliza [washauri wa Kim], ikiwa wanafanya mipango ya kwenda vitani. Na walijibu, 'Ndiyo," alisema.

Carter aliwasilisha orodha ya matakwa kutoka Washington pamoja na mapendekezo yake mwenyewe: Kuanza tena mazungumzo na Marekani, kuanza mazungumzo ya amani ya moja kwa moja na Korea Kusini, kuondoa vikosi vya kijeshi pamoja na kuisaidia Marekani kupata mabaki ya wanajeshi wa Marekani waliozikwa katika ardhi ya Korea Kaskazini.

"Alikubali yote," anasema Carter. "Kama nilivyojua wakati huo na sasa, Kim alikuwa mkweli kabisa na mimi."

La muhimu zaidi, Carter alikuja na makubaliano ambapo Korea Kaskazini ingesimamisha shughuli zake za nyuklia, kuruhusu wakaguzi wa IAEA kurudi kwenye vinu vyake, na hatimaye kubomoa kinu cha Yongbyon.

Kwa upande wake, Marekani na washirika wake wangeunda vinu vya nyuklia nchini Korea Kaskazini, ambavyo vinaweza kuzalisha nishati ya nyuklia lakini si kuzalisha nyenzo za silaha.

Saa kadhaa baadaye, alipanda mashua na Kim, na mbele ya kamera za televisheni, alimwambia Kim kwamba Marekani imeacha kuandaa vikwazo – kauli mbayo inakinzana na msimamo wa Clinton.

Ikulu ya White House ikiwa imekasirika, ilijiweka mbali na Carter. Lakini matumizi ya akili ya Carter mbele ya vyombo vya habari ya kuushinikiza utawala wa Clinton yalifanya kazi.

Kwa kutangaza makubaliano yake mara kwa mara, aliipa serikali ya Marekani muda wa kutafakari. Na mara baada ya safari yake, kulionekana mageuzi katika sera ya Marekani kuelekea Korea Kaskazini.

Tarehe 9 Julai 1994, siku ambayo maafisa wa Marekani na Korea Kaskazini walipoketi Geneva kuzungumza, vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini vilitangaza kuwa: Kim Il-sung amekufa kwa mshtuko wa moyo.

Mkataba wa Carter mara moja ukawa hauna tena uhakika. Lakini wawakilishi wa pande zote mbili walifanikiwa, na wiki kadhaa baadaye walitengeneza mpango rasmi wa pamoja.

Ingawa makubaliano hayo yalivunjika mwaka 2003, yanajulikana kwa kuzuia mpango wa nyuklia wa Pyongyang kwa karibu muongo mmoja.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah