Vikwazo dhidi ya Iran ni vipi,Tehran inatumia mbinu gani kuvikwepa?

Chanzo cha picha, EPA
Iran inashuhudia kushuka kwa mauzo yake ya mafuta kwa sababu ya vikwazo ilivyowekewa katika miezi michache iliyopita na marais wa Marekani, Donald Trump na Joe Biden.
Trump amesema anataka kuyarudisha mauzo ya mafuta hadi "sifuri," ili kuzuia mpango wa Iran wa nyuklia. Ni sera ya kuweka shinikizo dhidi ya Iran kama alivyofanya katika muhula wake wa kwanza.
Wote wawili yeye na Biden wameweka vikwazo dhidi ya "meli za magendo" za mafuta ambazo husafirisha mafuta mengi ya Iran nje ya nchi.
Trump ameulenga "mtandao wa kimataifa wa makampuni" yanayodaiwa kuisaidia Iran kufanya biashara haramu ya mafuta.
Iran ina akiba kubwa zaidi ya mafuta duniani. Mapema 2024, ilikuwa ikisafirisha takribani mapipa milioni 1.8 kwa siku, kulingana na makadirio kutoka S&P Global, shirika la data.
Lakini S&P Global inasema vikwazo vya hivi karibuni vimepunguza kiwango cha usafirishaji hadi wastani wa mapipa milioni 1.2 kwa siku kufikia Januari 2025.
Wachambuzi katika sekta hiyo wanaamini, 90% ya mauzo yote ya mafuta ghafi ya Iran yamekuwa yakienda China. China inanunua licha ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, kwa sababu inasema haitambui vikwazo vya upande mmoja kuwa ni halali.
Hata hivyo, kituo cha kupokea mafuta katika bandari ya Shandong nchini China hivi karibuni kimeacha kuchukua mafuta ya Iran kwa sababu ya vikwazo vya Marekani, na kushusha uagizaji wa mafuta kutoka Iran hadi mapipa 851,000 mwezi Januari 2025 kutoka mapipa milioni 1.48 mwezi Desemba 2024, kulingana na S&P Global.
Kwanini inawekewa vikwazo?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Marekani na nchi nyingine zimeiwekea Iran vikwazo ili kuzuia utengenezaji wa silaha za nyuklia na makombora ya balistiki.
Vikwazo hivyo pia vilikusudiwa kuizuia kutuma pesa kwa vikundi kama vile Hamas, Hezbollah na Houthi, kwani Marekani na mataifa mengine wanasema ni mashirika ya kigaidi.
Baada ya kuwekwa wazi mwaka 2002 kwamba Iran inarutubisha nyenzo za nyuklia, Umoja wa Mataifa, EU, Marekani na nchi nyingine zimeweka vikwazo kujaribu kuzuia utengenezaji wa silaha za nyuklia.
Wanasema Iran inakiuka ahadi yake, ilipotia saini Mkataba wa Kuzuia kurutubisha silaha hizo mwaka 1967, na kamwe lisiwe taifa lenye silaha za nyuklia.
Iran imesema ina haki ya kurutubisha nyenzo za nyuklia. Inasisitiza kuwa malengo yake ni ya amani – ili kuzalisha nishati ya nyuklia. Hata hivyo, shirika la uangalizi wa nyuklia duniani - limeshindwa kuthibitisha hilo.
Mwaka 2006, Umoja wa Mataifa uliweka vikwazo juu ya usambazaji wa silaha na teknolojia ya nyuklia kwa Iran. Mwaka 2011, Marekani iliweka vikwazo vingi kwa sekta yake ya mafuta, na 2012, EU ilipiga marufuku uagizaji wa mafuta kutoka Iran.
Mwaka 2015, wakati Barack Obama akiwa rais wa Marekani, Iran ilitia saini makubaliano na Umoja wa Mataifa, Marekani na mataifa mengine ya kuzuia shughuli zake za nyuklia.
Kama sehemu ya makubaliano - vikwazo dhidi ya mafuta (na bidhaa zingine) vililegezwa.
Hata hivyo, mwaka 2018 Rais Trump alijiondoa katika makubaliano hayo, na kurudisha vikwazo vya awali na kuongeza vingine katika juhudi za "shinikizo" ili kujaribu kupata makubaliano zaidi na serikali ya Iran kuhusu shughuli zake za nyuklia.
Vikwazo hivi vilikuwa vikali sana hadi kufikia 2020, kwani mauzo ya mafuta ya Iran yalipungua hadi mapipa 400,000 kwa siku.
Vikwazo vililegezwa na mrithi wake, Rais Joe Biden, kujaribu kuishawishi Iran irudi kwenye mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Kujibu shambulio la kombora la Iran dhidi ya Israel mnamo Oktoba 2024, Biden alikaza msimamo wake, na kuweka vikwazo mwezi Oktoba na Desemba kwa meli kadhaa za mafuta zinazosafirisha mafuta ya Iran.
Vikwazo vya hivi karibuni zaidi kutoka utawala wa Trump vinalenga kile inachokitaja kama "mtandao wa kimataifa wa makampuni" ambayo inadai yanahusika katika mikataba haramu ya kuuza mafuta ya Iran kwa China na kuelekeza mapato hayo kwa majeshi ya nchi hiyo.
Serikali ya Trump inasema hatua zake zinalenga kuzuia fedha ambazo Iran inatuma kwa makundi ya wapiganaji kama vile Hamas, Hezbollah na Houthis.
Trump amesema anataka kupunguza mauzo ya mafuta ya Iran hadi kufikia sifuri. Kwa lengo la kuweka shinikizo kwa serikali ya Iran. Amesema: "Nataka mapatano na Iran juu ya shughuli za nyuklia."
Iran imesema vikwazo vya Marekani kwa mauzo yake ya mafuta vinahatarisha kuyumbisha soko la kimataifa la mafuta ghafi. Imetoa wito kwa wanachama wenza wa kundi la wazalishaji wa mafuta la OPEC kuchukua hatua za kukabiliana na athari ya vikwazo hivyo.
Aina nyingine za vikwazo

Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani imeiwekea vikwazo serikali ya Iran tangu mwaka 1979, wakati ubalozi wa Marekani mjini Tehran ulipotekwa na maafisa kushikiliwa mateka.
Marekani ilianza kuweka vikwazo kwa mpango wa nyuklia wa Iran mwaka 1992. Sasa imeweka vikwazo vingi zaidi dhidi ya Iran kuliko dhidi ya nchi nyingine yoyote.
Marekani imepiga marufuku makampuni yake kufanya biashara na Iran.
Imeweka vikwazo kwa benki za Iran na benki yake kuu, na kuzuia taasisi za kifedha kote ulimwenguni ambazo zinafanya biashara na Iran pia kufanya biashara na Marekani, au kutumia dola ya Marekani.
Lengo ni kuitenga Iran na mfumo wa fedha wa kimataifa.
Marekani pia imezuia mali za taasisi kuu za Iran, kama vile Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Athari kwa maisha ya Wairan

Chanzo cha picha, Getty Images
Kati ya mwaka 2012 na 2016, wakati vikwazo vya Marekani na Umoja wa Ulaya kwa mauzo ya mafuta ya Iran vilipowekwa, Iran ilipoteza zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 160 katika mapato.
Trump alipoanza kampeni yake ya "shinikizo" mwaka 2018, Iran ilishuhudia uchumi wake ukidorora, na thamani ya rial ya Irani ikaanguka.
Rial imeshuka tena chini kabisa mwanzoni mwa mwezi Februari 2025, kufuatia safu ya vikwazo vya hivi karibuni vya Trump.
Kwa mujibu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kiwango cha mfumuko wa bei huko Iran kiliongezeka katika muhula wa kwanza wa Trump, na kufikia hadi 54% mwaka 2022. Mwishoni mwa 2024, bei ya bidhaa ilikuwa ikiongezeka kwa 30% kwa mwaka.
Taasisi ya Uhusiano wa Kimataifa ya Clingendael yenye makao yake makuu Uholanzi inasema kupanda kwa bei ya bidhaa, pamoja na ukuaji dhaifu wa uchumi, kumewasukuma Wairani wengi zaidi katika umaskini.
Karibu 8% ya wafanyakazi hawana kazi. Ukosefu wa ajira kwa vijana unazidi 20%.
Ripoti ya Clingendael inasema hali hiyo ni kutokana na vikwazo, pamoja na mambo mengine kama vile madai ya rushwa na usimamizi mbovu wa uchumi ndani ya Iran.
Katika ripoti ya 2019, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilisema vikwazo ambavyo Trump aliviweka katika muhula wake wa kwanza vilisababisha Iran kushindwa kuagiza nje aina fulani ya dawa.
HRW ilisema, hilo limesababisha "matatizo makubwa kwa Wairani wa kawaida... na kuhatarisha afya ya watu."
Iran inakwepa vipi vikwazo?

Chanzo cha picha, Reuters
Wanasiasa wa nchi za Magharibi na wanaharakati, kama vile Umoja wa Kupambana na Nyuklia ya Iran, wamesema Iran ina "meli za magendo" za kusafirisha mafuta yake ghafi nje ya nchi kwa njia ya siri.
Hizi ni meli zinazodaiwa kusajiliwa katika nchi ambazo huruhusu wamiliki kuficha maelezo yao. Pia, inasemekana huzima mawimbi ya redio zikiwa baharini ili kufanya safari zao kuwa siri.
Iran haikukubali kwamba inatumia "meli za magendo" lakini haijakanusha kufanya hivyo, na vyombo vya habari vya Iran vinasema meli inazotumia ni "jinamizi la vikwazo. "
Iran pia inadaiwa kufanya biashara ya kimataifa ya mafuta kupitia mitandao ya siri ya benki na makampuni, kuepuka vikwazo vya kifedha vya Marekani dhidi ya Iran ambavyo vimezuia benki nyingi za kimataifa na taasisi za fedha kufanya biashara yoyote na nchi hiyo.
Dk Burcu Ozcelik, kutoka taasisi ya fikra tunduizi yenye makao yake makuu nchini Uingereza, Royal United Services (RUSI) anasema, "Marekani inaweza kuzilenga benki nchini Iraq ambazo zimekuwa zikifanya kazi hii kwa ajili ya Iran."















