Taka za nyuklia: Mwanadamu hatakwenda katika eneo hili kwa miaka laki moja

[p'

Chanzo cha picha, Erika Benke

Maelezo ya picha, Bomba za mafuta zilizotumika kutoka katika vinu vya nishati ya nyuklia kwa sasa zimehifadhiwa katika vituo vya kuhifadhi vya muda
    • Author, Erika Benke
    • Nafasi, BBC

Natarajia kutembelea eneo la kwanza la kudumu la kuhifadhi mafuta ya nyuklia yaliyotumika. Kutembelea eneo hili huko Onkalo, lililoko mita 450 chini ya ardhi, ambako kuna mahandaki yamechimbwa ndani ya miamba ili kuhifadhi taka zenye mionzi kwa miaka laki moja, kunanifanya niwe na wasiwasi.

Ninapoendesha gari kwenye barabara isiyo na shghuli nyingi kusini-magharibi mwa Finland, ninapunguza mwendo nikijaribu kufikiria jinsi eneo hili la mashambani linavyopendeza na miti yake mirefu, litakavyokuwa miaka elfu moja au elfu kumi kutoka sasa.

Je! bado kutakuwa na watu katika eneo hili? Watazungumza lugha gani? Na zaidi ya yote, watakuwa wanafahamu hatari iliyopo chini ya miguu yao?

Bomba za mafuta zilizotumika kutoka katika vinu vya nishati ya nyuklia kwa sasa zimehifadhiwa katika vituo vya kuhifadhi vya muda. Finland ni nchi ya kwanza kutekeleza kile inachotarajia kuwa suluhu la kudumu. Ndani ya miaka miwili au mitatu, taka za mionzi zitazikwa chini ya ardhi huko Onkalo, zitafunikwa kwa chuma, katika mitungi ya shaba na kufunikwa na udongo.

Safari ya Chini ya Ardhi

dscx

Chanzo cha picha, Erika Benke

Maelezo ya picha, Mwandishi Erika Benke

Kwanza tunaangalia video inayotoa maelekezo ya kiusalama. Usijitenge na wenzako. Katika hali ya dharura, fuata maagizo ya anayekuongoza. Kazi zinaendelea huko, kwa hivyo jihadhari na magari na mashine zetu. Moto unapotokea, fuata mwongozo kwenda kwenye eneo la kujihifadhi la karibu.

Kisha tunatakiwa kuvaa mavazi ya usalama: koti la njano lenye kung’aa, buti zisizo pitisha maji, kofia ngumu yenye kioo na mkanda wenye tochi. Kila mmoja wetu amepewa begi dogo lenye barakoa ya kuzuia gesi za sumu. Nimefarijika kusikia kwamba helmeti zina kifaa cha kufuatilia, kwa hivyo watu walio katika chumba cha kufuatilia watajua sehemu nilipo.

Majira ya mchana tunapita kwenye kizingiti cha lango la usalama na kuingia kwenye gari. Gari inapita kwenye handaki bila kusita. Mara moja, kila kitu kinakuwa gizani sasa. Inachukua dakika kumi na tano hadi kituo cha mafuta cha Onkalo, ambacho kiko mita 437 chini ya ardhi.

Safari ndani ya handaki la kilomita 4.5 inapoanza, tunaona ishara ya alama za barabarani, bango la kikomo cha spidi 20. Pia, kuna ishara za kijani kwenye handaki. Ishara za kijani kwenye ukuta wa handaki zinaonyesha umbali tuliopo na uso wa dunia.

Inatisha kidogo kuliko vile nilivyofikiria. Nadhani kinachonipa ahueni ni kuona kwamba siko peke yangu. Handaki ni nyembamba - imekusudiwa kwa gari moja tu - lakini tunapofika mbele tunaona malori na magari. Ni kama kuendesha katika barabara yenye ujenzi, lakini hapa ni chini ya ardhi.

Miaka laki Moja

oijkl.

Chanzo cha picha, Erika Benke

Maelezo ya picha, Ni eneo ambalo mafuta ya nyuklia yaliyotumiwa yatahifadhiwa kwa milenia
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tunafika kwenye kituo cha kujaza gesi, kuna chumba chenye mwanga wa kutosha na sakafu nyororo ya jiwe. Kuna mashine nyingi kubwa hapa na safu ya makontena makubwa yaliyojaa vifaa vya ujenzi.

Mazingira ni ya kawaida, watu hufanya kazi zao kana kwamba wako kwenye kiwanda kilicho juu ya ardhi. Na joto ni 14 ° C na hewa ni safi, mfumo wa uingizaji hewa umewekwa na hakuna harufu ya vumbi au unyevu.

Waongozaji wetu wanatufafanulia jinsi vyombo vya taka za nyuklia vitafika kwenye eneo hili, kupitia lifti ambayo inashuka moja kwa moja kutoka katika mtambo ulio juu ya ardhi. Hatuwezi kuona shimoni la lifti, kwani ujenzi wake bado unaendelea. Kwa sasa, limefunikwa na mlango mkubwa uliowekwa alama ya X nyekundu.

Mafuta yaliyotumiwa yanapoanza kuhifadhiwa hapa, makontena yatashushwa kupitia lifti hii hadi hapa kisha yatachukuliwa na magari ya roboti na yatawapeleka kwenye mashimo marefu, mahali pa pamwisho.

Ni eneo ambalo mafuta ya nyuklia yaliyotumiwa yatahifadhiwa kwa milenia. Ni mahali ambapo, kutoka 2025, hakuna mwanadamu anayepaswa kukanyaga kwa miaka laki moja.