Vita vya Gaza: Israeli hupata wapi silaha zake?

Muda wa kusoma: Dakika 7

Na David Gritten ,

BBC News

TH

Chanzo cha picha, AFP

Hali katika eneo zima la Mashariki ya Kati inaendelea kuhofisha wengi kutokana na tishio la Iran kupiliza kisasi dhidi ya Israel kwa mauaji ya kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh. Hatua hiyo inachukuliwa kama inayoweza 'kuzidisha mzozo' katika eneo zima na hata kusababisha vita vitakavyohusisha makundi kadhaa yanayoungwa mkono na Iran.Tayari Marekani imetangaza kutuma ndege na mli za kivita katika eneo hilo ili kuilinda Israel.

Serikali za Magharibi zinakabiliwa na shinikizo kubwa la kusitisha uuzaji wa silaha kwa Israel kuhusu jinsi inavyoendesha vita dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Israel ni muuzaji mkubwa wa silaha nje ya nchi, lakini jeshi lake limekuwa likitegemea zaidi ndege zinazoagizwa kutoka nje, mabomu ya kuongozwa na makombora kufanya kile ambacho wataalam wamekitaja kuwa moja ya kampeni kali na za uharibifu zaidi katika historia ya hivi karibuni.

Vikundi vya kampeni na baadhi ya wanasiasa miongoni mwa washirika wa Magharibi wa Israel wanasema usafirishaji wa silaha unapaswa kusitishwa kwa sababu, wanasema, Israel inashindwa kufanya vya kutosha kulinda maisha ya raia na kuhakikisha misaada ya kutosha ya kibinadamu inawafikia Wapalestina.

Siku ya Ijumaa, Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa liliunga mkono marufuku ya silaha, huku nchi 28 zikipiga kura ya ndio, sita zilipinga na 13 hazikupiga kura. Marekani na Ujerumani - ambazo zinachangia sehemu kubwa ya uagizaji wa silaha za Israel - zote zilipiga kura ya kupinga. Ujerumani ilisema ilifanya hivyo kwa sababu azimio hilo halikulaani kwa uwazi Hamas.

Vita hivyo vilichochewa na shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba, ambalo liliua takriban watu 1,200, hasa raia, kulingana na hesabu za Israel. Zaidi ya watu 33,000 wameuawa huko Gaza, 70% yao wakiwa watoto na wanawake, wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas inasema.

Israel inasisitiza kuwa vikosi vyake vinafanya kazi ili kuepusha maafa ya raia, inaishutumu Hamas kwa kuwaweka raia kwenye mstari wa moto kimakusudi na imesema hakuna kikomo katika utoaji wa misaada.

Unaweza pia kusoma

Marekani

Marekani ndiyo muuzaji mkuu zaidi wa silaha kwa Israel, baada ya kuisaidia kujenga mojawapo ya wanajeshi waliobobea zaidi kiteknolojia duniani.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) , Marekani ilichangia asilimia 69 ya silaha zilizoingizwa nchini Israel kati ya 2019 na 2023.

Marekani inaipa Israel $3.8bn (£3bn) kama msaada wa kijeshi wa kila mwaka chini ya makubaliano ya miaka 10 ambayo yananuiwa kuruhusu mshirika wake kudumisha kile inachokiita "makali ya kijeshi" juu ya nchi jirani.

Nani huisambazia Israel silaha nyingi?

% ya silaha inazopewa Israel na wasambazaji wake

th
Maelezo ya picha, Chanzo:SIPRI makadirio ya silaha zilizosambazwa kwa Israel 2013-2023
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Israel imetumia ruzuku hizo kufadhili maagizo ya F-35 Joint Strike Fighters, ndege ya siri inayochukuliwa kuwa ya juu zaidi kuwahi kutengenezwa. Hadi sasa imeagiza 75 na kupeleka zaidi ya 30 ya ndege hizo. Ilikuwa nchi ya kwanza kando na Marekani kupokea F-35 na ya kwanza kutumia moja katika mapigano.

Sehemu ya misaada hiyo - $500m kila mwaka - imetengwa kufadhili programu za ulinzi wa makombora, ikijumuisha mifumo ya Iron Dome, Arrow na David's Sling iliyoendelezwa kwa pamoja. Israel imeitegemea wakati wa vita hivyo kujilinda dhidi ya mashambulizi ya roketi, makombora na ndege zisizo na rubani kutoka kwa makundi ya Wapalestina yenye silaha huko Gaza, pamoja na makundi mengine yenye silaha yanayoungwa mkono na Iran yaliyoko Lebanon, Syria na Iraq.

Siku chache baada ya shambulio la Hamas la Oktoba 7, Rais Joe Biden alisema Marekani ilikuwa "inaongeza msaada wa kijeshi" kwa Israel.

Tangu kuanza kwa vita, ni mauzo mawili tu ya kijeshi ya Marekani kwa Israel ambayo yametangazwa hadharani baada ya kupata idhini ya dharura - moja kwa risasi 14,000 za mizinga yenye thamani ya $106m na nyingine kwa $147m ya vifaa vya kutengeneza makombora ya 155mm.

Lakini vyombo vya habari vya Marekani vinaripoti kwamba utawala wa Rais Joe Biden pia umefanya kimya kimya zaidi ya mauzo ya kijeshi 100 kwa Israeli, mengi yakiwa chini ya kiwango cha dola ambacho kingehitaji bunge la Congress kujulishwa rasmi. Inasemekana kuwa ni pamoja na maelfu ya risasi zinazoongozwa kwa usahihi, mabomu ya kipenyo kidogo na silaha ndogo ndogo .

TH

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Betri za Iron Dome za Israeli husaidia kulinda miji dhidi ya ya roketi na makombora

Hata hivyo, ripoti ya SIPRI inasema licha ya kufikishwa kwa silaha hizo, jumla ya kiasi cha silaha za Israel zilizoagizwa kutoka Marekani mwaka 2023 kilikuwa karibu sawa na mwaka 2022.

Ofa moja ambayo ni kubwa ya kutosha kuhitaji arifa ya Bunge la Congress ni mauzo ya $18bn ya hadi ndege 50 za kivita za F-15, habari ambazo zimeibuka wiki hii . Congress bado haijaidhinisha mpango huo.

Ingawa ndege hiyo ingehitaji kujengwa kutoka mwanzo na isingewasilishwa mara moja, mauzo hayo yanatarajiwa kujadiliwa vikali na chama cha Bw Biden Democratic Party, ambacho wengi wao wawakilishi katika Bunge la Congress na wafuasi wake wanazidi kuhangaishwa na vitendo vya Israel huko Gaza.

Seneta Elizabeth Warren amesema yuko tayari kuzuia mpango huo na ameishutumu Israel kwa "mashambulizi ya kiholela" huko Gaza.

Ujerumani

Ujerumani ndiyo nchi inayofuatia kwa wingi zaidi kusafirisha silaha kwa Israel, ikichukua asilimia 30 ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje kati ya 2019 na 2023, kulingana na SIPRI.

Kufikia mwanzoni mwa Novemba, mauzo ya silaha za taifa hilo la Ulaya kwa Israeli mwaka jana yalikuwa na thamani ya €300m ($326m; $257m) - ongezeko la mara 10 ikilinganishwa na 2022 - huku leseni nyingi za mauzo ya nje zikitolewa baada ya mashambulizi ya Oktoba 7.

Vipengele vya mifumo ya ulinzi wa anga na vifaa vya mawasiliano vilichangia mauzo mengi, kulingana na wakala wa habari wa DPA.

Kansela Olaf Scholz amekuwa mfuasi mkubwa wa haki ya Israel ya kujilinda wakati wote wa vita na, ingawa sauti yake kuhusu hatua za Israel huko Gaza imebadilika katika wiki za hivi karibuni na kumekuwa na mjadala nchini Ujerumani, uuzaji wa silaha hauonekani utasistishwa .

TH

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Israel inakanusha shutuma kwamba inashindwa kufanya vya kutosha kulinda raia huko Gaza na badala yake inalaumu Hamas.

Italia

Italia ni nchi ya tatu kwa mauzo ya silaha kwa Israel, lakini ilichangia asilimia 0.9 pekee ya bidhaa zilizoagizwa na Israeli kati ya 2019 na 2023. Zinaripotiwa kuwa zimejumuisha helikopta na silaha za kijeshi za majini.

Mauzo yalifikia €13.7m ($14.8m; £11.7m) mwaka jana, kulingana na ofisi ya taifa ya takwimu ISTAT.

Baadhi ya Euro milioni 2.1 za mauzo ya nje ziliidhinishwa kati ya Oktoba na Desemba , licha ya uhakikisho wa serikali kwamba ilikuwa inazizuia chini ya sheria inayopiga marufuku uuzaji wa silaha kwa nchi zinazopigana au zinazochukuliwa kuwa zinakiuka haki za binadamu.

Waziri wa Ulinzi Guido Crosetto aliliambia bunge mwezi uliopita kwamba Italia iliheshimu kandarasi zilizopo baada ya kuzikagua kulingana moja baada ya nyingine na kuhakikisha "hazina uwezo wa kutumika dhidi ya raia".

Nchi nyingine

Uuzaji wa silaha wa Uingereza kwa Israel ni "mdogo", kulingana na serikali ya Uingereza, kiasi cha £42m ($53m) pekee mwaka 2022 .

Kampeni dhidi ya Biashara ya Silaha (CAAT) inasema kuwa tangu mwaka 2008, Uingereza imetoa leseni ya kuuza silaha kwa Israel yenye thamani ya £574m ($727m) kwa jumla.

Mengi ya hayo ni ya vipuri vinavyotumika katika ndege za kivita zilizotengenezwa na Marekani ambazo huishia Israel. Lakini serikali ya Uingereza inakuja chini ya shinikizo kubwa la kusimamisha hata mauzo hayo ya nje.

Waziri Mkuu Rishi Sunak amesema Uingereza ina "usimamizi wa karibu sana wa kutoa leseni za kuuza nje" na akasema Israel lazima "ichukue hatua kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu". Serikali ya Uingereza pia inaandaa tathmini ambayo itashauri juu ya hatari ya Israeli kukiuka sheria za kimataifa katika hatua zake kutoka mapema 2024.

Lakini chanzo kikuu cha serikali kiliiambia BBC kwamba vikwazo vya silaha kwa Israel "havitafanyika".

Serikali ya Kanada, ambayo mauzo ya silaha kwa Israel yalikuwa na thamani ya dola za Canada milioni 21.3 ($15.7m; £12.4m) mnamo 2022, ilisema mnamo Januari kwamba ilisitisha kuidhinisha vibali vipya vya kusafirisha silaha hadi itakapohakikisha kuwa zinatumika kwa mujibu wa sheria ya Canada. Hata hivyo, vibali vilivyokuwepo awali viliendelea kuwa halali.

Sekta ya ulinzi ya Israeli

TH

Chanzo cha picha, AFP

Israel pia imeunda sekta yake ya ulinzi kwa usaidizi wa Marekani na sasa inashika nafasi ya tisa katika kuwa muuzaji silaha mkubwa zaidi duniani, kwa kuzingatia bidhaa za kiteknolojia za hali ya juu badala ya vifaa vikubwa.

Ilishikilia asilimia 2.3 ya mauzo ya kimataifa kati ya 2019 na 2023, kulingana na SIPRI, huku India (37%), Ufilipino (12%) na Marekani (8.7%) zikiwa wapokeaji wakuu watatu. Mauzo hayo yalikuwa na thamani ya $12.5bn (£9.9bn) mwaka 2022 , kulingana na wizara ya ulinzi ya Israel.

Ndege zisizo na rubani (UAVs) ziliunda 25% ya mauzo hayo, ikifuatiwa na makombora, roketi na mifumo ya ulinzi wa anga (19%) na mifumo ya vita vya rada na elektroniki (13%), wizara hiyo ilisema.

Mnamo Septemba, kabla ya vita kuanza, Ujerumani ilikubali mkataba wa $ 3.5bn na Israeli kununua mfumo wa kisasa wa ulinzi wa makombora wa Arrow 3, ambao huzuia makombora ya masafa marefu. Mkataba huo - mkubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Israel - ulilazimika kuidhinishwa na Marekani kwa sababu ilitengeneza mfumo huo kwa ushirikiano na Israel.

Hifadhi ya jeshi la Marekani huko Israeli

TH

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Marekani imeripotiwa kuiruhusu Israel kutumia makombora ya mizinga kutoka kwenye hifadhi yake huko

Israel pia ni nyumbani kwa ghala kubwa la silaha la Marekani lililoanzishwa mwaka 1984 ili kutayarisha vifaa kwa ajili ya wanajeshi wake iwapo kutatokea mzozo wa kieneo, na pia kuipa Israel upatikanaji wa haraka wa silaha katika dharura.

Pentagon ilisafirisha takriban makombora 300,000 ya 155mm kutoka kwa Hifadhi ya Risasi za Vita-Israel hadi Ukraine kufuatia uvamizi wa Urusi.

Mabomu yaliyorundikwa kwenye ghala hilo pia yameripotiwa kutolewa kwa Israeli tangu kuanza kwa vita vya Gaza.

Unaweza pia kusoma

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah