Je, eneo la Mashariki ya Kati linakaribia kugubikwa na vita vikubwa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Eneo la Mashariki ya Kati limeingia katika kipindi hatari, likisubiri jibu la Iran kwa mauaji ya Ismail Haniyeh, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu mjini Tehran, na jibu la Hizbullah nchini Lebanon kwa mauaji ya kiongozi wa pili wa Hizbullah, Fouad Shukr, katika viunga vya kusini mwa mji mkuu, Beirut.
Khamenei aamuru mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya Israel

Chanzo cha picha, AFP
Nchini Iran, wito wa jibu kali la kijeshi dhidi ya Israel umetolewa na viongozi wakuu wa utawala wa Iran.
Ripoti za vyombo vya habari zinaonyesha kuwa, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, Ayatollah Ali Khamenei, ameamuru shambulio la moja kwa moja dhidi ya Israel na kutayarishwa mipango ya mashambulizi na ya kujihami katika tukio ambalo vita na Israel vitaenea.
Khamenei alisema kwamba "kulipiza kisasi cha damu ya shahidi Haniyeh ni jukumu la Iran kwa sababu aliuawa katika ardhi yake."
Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi wa Iran, Meja Jenerali Mohammad Bagheri, aliapa kuijibu Israel na kusema: "Taasisi ya Kizayuni itajuta." Kwa mujibu wa ripoti katika vyombo vya habari vya Marekani, Iran inafikiria kufanya mashambulizi yaliyoratibiwa kwa makombora na ndege zisizo na rubani katika Haifa na Tel Aviv, kwa uratibu wa makundi ya Syria, Yemen na Iraq.
Nasrallah: “Majibu yetu yanakuja’’

Chanzo cha picha, AFP
Mjini Beirut, Katibu Mkuu wa Hezbollah Hassan Nasrallah aliapa kuilipiza kisasi Israel kwa mauaji ya kamanda wa kijeshi wa chama hicho, Fouad Shukr.
Alisema makabiliano hayo na Israel yameingia katika awamu kubwa ya vita, na kuongeza kuwa "jibu kwa Israel haliepukiki, na litakuwa kubwa, la kweli na la haki.
Nasrallah alisisitiza katika hotuba yake wakati wa mazishi ya Fouad Shukr kwamba "adui na wale walio nyuma yake lazima wangoje majibu yetu yasioepukika, na hakutakuwa na mjadala au mijadala.
Kuna siku na uwanja kati yetu ... Tunatafuta jibu la kweli, lisilo rasmi...
Eneo hili linakabiliwa na vita vikubwa ambavyo vitakuwa na athari ambazo wengine hawatambui kuhusu mustakabali wa adui... Kujisalimisha kwa Hamas au Lebanon ni suala lisilowezekana.
Nasrallah aliwahutubia Waisraeli kwa vitisho akisema, "Cheka kidogo kwa sababu utalia sana na hujui umeingia kwenye mtego gani."
Mjini Sanaa, Abdul-Malik al-Houthi, kiongozi wa kundi la Ansar Allah nchini Yemen, aliapa kujibu mauaji ya Ismail Haniyeh, akisema: "Lazima kuwe na jibu la kijeshi kwa uhalifu uliotekelezwa na Israel.’’
Israel inajiandaa kwa hatua kali za kiusalama

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Nchini Israel, Mamlaka ya Utangazaji ya Israel inasema kuwa mamlaka imechukua hatua za kipekee za usalama na kuimarisha hali ya tahadhari kwa kutarajia jibu kutoka kwa Iran, Hamas na Hezbollah.
Jeshi lilighairi likizo ya wanajeshi katika vitengo vya mapigano na kuweka mfumo wa ulinzi wa anga katika hali ya tahadhari ili kuzuia tishio lolote kutoka kaskazini, kusini, mashariki au magharibi.
Channel 12 ilisema kuwa huduma ya usalama ya Shin Bet imeimarisha kiwango cha usalama kwa waziri mkuu na mawaziri wa serikali.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Israel, Israel inaweza kukabiliwa na vita vya pande nyingi ambavyo vinaweza kusukuma Mashariki ya Kati katika vita vya kikanda, na lazima ijiandae kukabiliana na mashambulizi ya makombora na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kutoka Lebanon na Yemen, na hata kutoka Iran, ambayo itajaribu kuhamasisha makundi yenye silaha kutoka Iraq na Syria hadi upande wa kaskazini kuunga mkono Hezbollah.
Mchambuzi wa kijeshi wa Israel Amos Harel, akiiandikia Haaretz, alisema kuwa Israel inakabiliwa na dharura ya kuongezeka kwa vita hivyo vinavyotishia kuzua mzozo mkubwa zaidi wa kikanda.
Alisema, "Tel Aviv inatumai kuudhibiti mzozo huo na kuuzuia kuzidi kuwa vita kamili kwenye eneo la kaskazini, kwa sababu Netanyahu havutiwi na makabiliano kamili na Hezbollah na eneo la Gaza tayari linawaka moto."
Mchambuzi huyo wa masuala ya kijeshi alihitimisha kuwa serikali na jeshi la Israel hawana suluhu za kutuliza hali na kujiondoa katika mgogoro wa kimkakati wa kaskazini na miji ya mpakani ambayo imehamisha wakazi wake tangu Oktoba mwaka jana, na kwamba hatari ya kugeuka kuwa vita vikubwa dhidi ya mauaji ya Haniyeh huko Tehran imetimia.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












