Je, shambulio dogo la Israel ni onyo kali kwa Iran?

Chanzo cha picha, EPA
- Author, Lys Doucet
- Nafasi, BBC
Israel bado haijathibitisha rasmi kwamba ilifanya shambulio nchini Iran mapema Ijumaa asubuhi. Wakati huo huo, viongozi wa kijeshi na kisiasa wa Iran wameamua kupuuza shambulio hilo.
Ni silaha za aina gani zilitumika katika shambulio? Ni uharibifu kiasi gani ulifanyika? Bado kuna maswali mengi yasiyo na majibu.
Maafisa wa Marekani wanasema shambulio la kombora lilifanyika. Maafisa wa Iran wanasema ndege zisizo na rubani zilisababisha milipuko katika mkoa wa kati wa Isfahan na kaskazini magharibi mwa Tabriz.
"Hakukuwa na uharibifu wowote uliosababishwa na ndege hizo zisizo na rubani. Hakuna aliyeuawa," Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian alinukuliwa akisema na shirika la habari la Tasnim nchini humo.
Shabaha ya mashambulizi haya ni jiji la Isfahan. Ni mkoa wenye majengo mazuri ya urithi wa kale wa ustaarabu wa Kiislamu nchini humo.
Mkoa huo ni nyumbani kwa kituo cha teknolojia ya nyuklia cha Isfahan, kituo cha nyuklia cha Natanz, na kambi ya anga.
Pia kuna viwanda vinavyotengeneza makombora ya balestiki na mamia ya ndege zisizo na rubani zilizotumika katika shambulio la Israel Jumapili iliyopita.
Ni onyo?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Wachambuzi wanaamini tukio hilo ni operesheni ndogo ya Israel kutuma onyo kali kwamba ina ujasusi na nguvu ya kushambulia eneo muhimu la Iran.
Maafisa wa Marekani walisema Israel ililenga mfumo wa rada ya ulinzi wa anga katika eneo la Natanz.
Wakati huu ikiwa ni miaka 85 ya kuzaliwa kwa Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei - ukimya wa Israel umewapa viongozi wakuu wa Iran muda wa kufikiria.
Hatua za kimkakati za Iran

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Rais wa Iran Ibrahim Raisi hakutaja shambulio la Isfahan katika hotuba yake siku ya Ijumaa.
Lakini alitaja shambulio la Jumapili usiku dhidi ya Israel lililoitwa 'Operesheni ya Ahadi ya Kweli.' Ibrahim alisifu uimara wa Iran.
Kwa miaka mingi, Iran imejivunia uvumilivu wake wa kimkakati, sera ya muda mrefu ya kutojibu mara moja na moja kwa moja uchochezi wowote.
Iran inaelekea kwenye suluhisho jipya la kimkakati. Ilizindua sera mpya baada ya shambulio dhidi ya ubalozi wake huko Damascus mnamo Aprili 1.
Ubalozi mdogo wa Iran uliharibiwa katika shambulio hilo. Walinzi saba wa Mapinduzi ya Kiislamu, akiwemo kamanda mkuu, waliuawa.
Israel sio tu imeshambulia mali za Iran, zikiwemo silaha, majengo, kambi na njia za usambazaji silaha nchini Syria na Lebanon, pia imewaua maafisa wake wakuu.
Uadui wa Iran na Israel

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Ushindani wa miongo kadhaa kati ya Israel na Iran umejidhihirisha katika vita vya chinichini na operesheni za siri. Lakini sasa umekuwa mgogoro wa wazi.
Ikiwa mashambulizi hayo yatatokea tena, matokeo yatakuwa mabaya. Lakini inaonyesha kuwa Israel imepunguza hatua zake za kulipiza kisasi - kuitikia wito kutoka kwa washirika wake.
Kila mtu anataka mvutano wa Iran na Israel upngue. Lakini kila mtu anajua kwamba amani kati ya nchi hizi haitodumu kwa muda mrefu.
Vikosi vya Iran viko tayari

Chanzo cha picha, REUTERS
Israeli bado iko katika vita. Kuna vita huko Gaza. Idadi kubwa ya Wapalestina wamepoteza maisha.
Chini ya shinikizo kutoka kwa washirika wake, Israel inaruhusu usambazaji wa misaada kwa wale wanaohitaji, lakini eneo la Gaza bado liko kwenye ukingo wa njaa.
Mateka wa Israel bado hawajarejea nyumbani, mazungumzo ya kusitisha vita bado yamekwama. Wakati huu Israel ikitaka kushambulia ngome ya mwisho ya Hamas huko Rafah.
Makundi yanayoungwa mkono na Iran katika maeneo hayo yanayojulikana kama ‘Mhimili wa Upinzani.’ Ambayo ni Hezbollah nchini Lebanon na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran nchini Iraq na Syria, na Houthis nchini Yemen. Wote wako tayari!
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












