Kwa nini Iran imeishambulia Israel?

TG

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Iran imewekeza fedha nyingi katika makombora na ndege zisizo na rubani

Iran ilirusha ndege zisizo na rubani na makombora kuelekea Israel baada ya kuapa kulipiza kisasi kwa shambulio baya katika ubalozi wake mdogo katika mji mkuu wa Syria, Damascus.

Watu 13 waliuawa, akiwemo Brig Jenerali Mohammad Reza Zahedi - kamanda mkuu katika kikosi cha Quds, tawi la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC). Alikuwa mhusika mkuu katika operesheni ya Iran ya kulipatia silaha kundi la waasi la Lebanon la Hezbollah.

Israel haijasema ikiwa ilitekeleza shambulio hilo katika ubalozi mdogo, lakini inaaminika ndiyo iliyohusika.

Ni mara ya kwanza kwa Iran kuishambulia Israel moja kwa moja. Hapo awali Israel na Iran zilihusika katika vita vya chini chini kwa miaka mingi - kushambulia mali za kila mmoja bila kukiri kuhusika.

Sasa mvutano umeongezeka wakati wa vita vya Gaza - vilivyosababishwa na shambulio la kikundi cha Palestina Hamas dhidi ya Israel Oktoba mwaka jana.

Uadui wa Israel na Iran

jhn

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Shambulio kwenye ubalozi mdogo wa Iran uliua makamanda wakuu

Nchi hizo mbili zilikuwa washirika hadi mapinduzi ya Kiislamu ya 1979 nchini Iran, ambayo yalileta utawala ambao upinzani kwa Israel ni sehemu ya itikadi yake.

Iran halilitambui taifa la Israel na inataka kulitokomeza. Kiongozi mkuu wa nchi hiyo, Ayatollah Ali Khamenei, aliita Israel uvimbe wa saratani ambao utaondolewa na kuangamizwa.

Israel inaamini Iran ni tishio kama inavyothibitishwa na matamshi ya Tehran, vilevile kujenga vikosi vyake vilivyoapa kuiangamiza Israel na ufadhili kwa makundi yenye silaha yakiwemo Hamas na kundi la Lebanon Hezbollah.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

IRGC husafirisha silaha na vifaa, ikiwa ni pamoja na makombora kupitia Syria hadi Hezbollah. Israel inajaribu kuzuia usafirishaji huu, pamoja na kuizuia Iran isiimarishe uwepo wake wa kijeshi nchini Syria.

Iran imeunda mtandao wa washirika Mashariki ya Kati ambayo inasema ni sehemu ya "mhimili wa upinzani" unaopinga maslahi ya Marekani na Israel katika eneo hilo.

Syria ni mshirika muhimu zaidi wa Iran. Iran, pamoja na Urusi, ziliisaidia serikali ya Syria ya Bashar al-Assad kunusurika kupinduliwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa muongo mmoja nchini humo.

Hezbollah nchini Lebanon ndiyo yenye nguvu zaidi kati ya makundi yenye silaha yanayoungwa mkono na Iran.

Iran inaunga mkono makundi ya wanamgambo wa Kishia nchini Iraq ambayo yameshambulia kambi za Marekani huko Iraq, Syria na Jordan kwa kurusha roketi. Marekani ililipiza kisasi baada ya wanajeshi wake watatu kuuawa katika kituo cha kijeshi huko Jordan.

Nchini Yemen, Iran inatoa msaada kwa kundi la Houthi. Ili kuonyesha uungaji mkono kwa Hamas huko Gaza, Wahouthi wamerusha makombora na ndege zisizo na rubani kwenda Israel na pia wamekuwa wakishambulia meli za kibiashara karibu na pwani ya Yemen, na kuzamisha meli moja.

Iran pia inatoa silaha na mafunzo kwa makundi yenye silaha ya Palestina ikiwa ni pamoja na Hamas, ambayo iliishambulia Israel tarehe 7 Oktoba mwaka jana, na kusababisha vita vya sasa huko Gaza.

Uwezo wa kijeshi wa Iran na Israel

TGH

Iran ni kubwa zaidi kuliko Israel kijiografia na ina idadi ya watu karibu milioni 90, karibu mara kumi ya Israeli - lakini hii haitafsiriwi kuwa nguvu ya kijeshi.

Iran imewekeza fedha nyingi kwenye makombora na ndege zisizo na rubani. Ina silaha nyingi ya aina hizo.

Lakini haina mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga na ndege za kivita. Urusi inaaminika inashirikiana na Iran ili kuwa na silaha hizo.

Kwa upande wake Iran inatoa msaada wa kijeshi kwa Moscow katika vita vyake na Ukraine - Iran imetoa ndege zisizo na rubani za Shahed.

Lakini Israel ina moja ya vikosi vya anga vyenye uwezo mkubwa ulimwenguni. Ina angalau ndege 14 - ikiwa ni pamoja na F-15, F-16s na ndege mpya ya F-35.

Israel inadhaniwa kuwa na silaha za nyuklia lakini imegoma kukiri hilo.

Iran haina silaha za nyuklia na pia inakanusha kuwa inajaribu kutumia mpango wake wa nyuklia wa kiraia kuwa taifa lenye silaha za nyuklia.

Mwaka jana shirika la uangalizi wa nyuklia duniani lilipata chembechembe za urani zilizorutubishwa hadi asilimia 83.7% - karibu kuunda silaha - katika kituo cha chini ya ardhi cha Fordo.

Iran imekuwa ikirutubisha urani kwa asilimia 60 kwa zaidi ya miaka miwili kwa kukiuka makubaliano ya nyuklia ya 2015 na mataifa yenye nguvu duniani.

Hata hivyo makubaliano hayo yamekaribia kuporomoka tangu Rais wa Marekani Donald Trump alipojiondoa kwa upande mmoja na kurejesha vikwazo mwaka 2018.

Israel ilikuwa imepinga makubaliano hayo ya nyuklia hapo awali.

Ujumbe wa Iran kupitia mashambulizi

IK,

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Mabaki ya roketi ambayo mamlaka ya Israel inasema ilimjeruhi msichana wa miaka 10 kusini mwa Israel.

"Tulizuia mashambulizi. Kwa pamoja tutashinda," ndivyo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alivyotathmini mashambulizi hayo.

Tom Fletcher, mshauri wa sera za kigeni wa mawaziri wakuu kadhaa wa Uingereza na balozi wa zamani wa Uingereza nchini Lebanon, alisema shambulio hilo ni ishara ya kutisha ya uwezo wa Iran.

Aliiambia BBC shambulio la Iran ambalo halijawahi kutokea lilionekana kufanywa kwa uangalifu.

"Iran iliweka wazi juu ya mashambulio haya mapema jambo ambalo lilifanya yawe rahisi kuzuiwa. Nia ni kuonyesha uwezo lakini si kukuza mgogoro."

Anasema ni bora Iran ilichagua kujibu moja kwa moja badala ya kupitia Hezbollah. Baadhi ya Waisraeli wametoa wito kwa jeshi kupanua makabiliano yake na kundi lenye silaha la Lebanon ili kulirudisha nyuma kutoka mpakani.

Sanam Vakil kutoka Chatham House anasema shambulio hilo limekuwa na mafanikio kutoka mtazamo wa Iran.

"Mashambulio hayo kwa hakika yalipangwa na yalielekezwa kwenye vituo vya kijeshi kwa lengo la kutoleta uharibifu mkubwa au kumuumiza mtu yeyote."