Tunachojua kuhusu Mohammad Reza Zahedi, Jenerali wa Iran aliyeuawa Syria

 Mohammad Reza Zahedi

Chanzo cha picha, IRANIAN WORLD WEBSITE

Saa tano usiku wa Jumatatu, jengo la ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus lilikumbwa na mashambulio ya anga ya Israel, na kusababisha vifo na majeruhi, kulingana na Wizara ya Habari ya Syria, ambayo iliishutumu Israel kwa "kuanzisha mashambulizi ya angani kutoka upande wa Golan."

Balozi wa Iran nchini Syria anasema kuwa ndege za F-16 - 35 zilitumiwa kushambulia jengo la ubalozi.

Shambulio hilo lilisababisha vifo vya maafisa saba wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, kwa mujibu wa takwimu zake za hivi punde, ikiwa ni pamoja na kiongozi mashuhuri wa Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, Mohammad Reza Zahedi.

Televisheni ya taifa ya Iran ilitangaza kuwa "lengo la shambulio la Israel dhidi ya jengo la ubalozi mjini Damascus lilikuwa kumuua kamanda mkuu wa Kikosi cha Quds, Mohammad Reza Zahedi.

Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari alikataa kuzungumzia shambulio hilo, lakini katika mkutano na waandishi wa habari alisema , "Tunaangazia malengo ya vita, na tutaendelea kufanya chochote kitakachochangia kufikia malengo hayo."

Brigedia Jenerali Mohammad Reza Zahedi ni nani?

xx

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mashambulio hayo kwenye ubalozi mdogo wa Iran yalisababisha vifo vya wanachama saba wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran

Brigedia Jenerali Mohammad Reza Zahedi alikuwa kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi kwa Syria na Lebanon, kwa mujibu wa idhaa ya Iran ya Al-Alam.

Zahedi amehudumu katika nyadhifa tofauti za kijeshi ndani ya Kikosi cha Ulinzi wa Mapinduzi ya Iran kwa zaidi ya miaka 40.

Alizaliwa Novemba 2, 1960 huko Isfahan. Alijiunga na " Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu" mwaka 1980 na alikuwa mmoja wa makamanda katika jeshi hilo wakati wa Vita vya Iran na Iraq.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati wa miaka minane ya vita, Zahedi alishikilia nyadhifa mbalimbali za kijeshi ndani ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi.

Aliongoza Kitengo cha 14 cha Imam Hussein katika miaka kati ya 1983 na 1986, kisha akawa kamanda wa Vikosi vya Ardhi vya Walinzi wa Mapinduzi mwaka 1986, kwa mujibu wa amri iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ayatullah Seyyed Ali Khamenei.

Wakati wa uteuzi huo Ayatullah Seyyed Ali Khamenei alimuambia Zahedi: “Kwa kuzingatia rekodi yako angavu ya utumishi wa kijeshi katika Jamhuri ya Kiislamu, katika kipindi cha ulinzi mtakatifu, nakuteua wewe kama kamanda wa Jeshi la Ardhini la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu,” kulingana na tovuti ya kibinafsi ya Khamenei.

Mnamo mwaka wa 2005, Zahedi alichukua uongozi wa kituo cha "Thar Allah" hadi 2008, ambayo ni kituo kinachofanya kazi kama gavana wa kijeshi wa Tehran, kulingana na kile kilichoripotiwa na Taasisi ya Washington ya Sera ya Mashariki ya Kati, ambapo ilielezea kuwa " Makao makuu ya Thar Allah” yana jukumu la kusimamia shughuli za kijamii na kitamaduni huko Tehran.

Mnamo 2008, Zahedi alihamia Kikosi cha Quds, na kuwa kamanda mkuu hadi 2016. Kisha akahudumu kama kamanda wa Kikosi cha Quds katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran nchini Syria na Lebanon. Pia alihudumu kama naibu wa operesheni katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu mnamo 2017 kwa miaka mitatu

xx

Chanzo cha picha, Reuters

Wizara ya Fedha ya Marekani ilimuweka Mohammad Reza Zahedi kwenye orodha ya vikwazo ambayo inalenga "kufungia mali za magaidi na wafuasi wao," kulingana na amri ya utendaji iliyotolewa mwaka 2010, ambapo ilisema kuwa orodha yake inalenga uungaji mkono wa Iran kwa kundi la mashirika ambayo iliyataja kuwa ya kigaidi, yakiwemo Hezbollah ya Lebanon, Hamas, na vuguvugu la Islamic Jihad.

Ilimtaja Zahedi pamoja na maafisa watatu waandamizi katika Kikosi cha Quds cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran kwa sababu ya kile ilichosema ni jukumu la "kuunga mkono ugaidi.

Mara tu baada ya kuuawa kwa Zahedi, balozi wa Iran mjini Damascus alitangaza kwamba Iran "itajibu kikamilifu mauaji yaliyofanywa na Wazayuni," kama alivyosema.

Kwa upande wake, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje alisema kuwa nchi yake ina haki ya kujibu na kuchukua hatua za kukabiliana na shambulio hilo na mauaji ya Zahedi, na itaamua aina ya majibu na kumuadhibu mvamizi, kama alivyoeleza.

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi