Jeshi la Israeli linajumuisha akina nani na ni jamii gani nyingine zinazohudumu katika jeshi hilo?

Mnamo Mei 26, 1948, karibu wiki mbili baada ya uanzishaji waJimbo la Israeli kutangazwa, jeshi la Israeli lilianza kufanya kazi rasmi kama shirika pekee la kijeshi la nchi hiyo.
Leo, jeshi la Israeli linashikilia nafasi ya 17 kwenye orodha ya majeshi yenye nguvu zaidi duniani, kulingana na takwimu kutoka kwa tovuti ya Marekani ya "Global Firepower".
Jeshi hilo linajumuisha askari 169,000 katika huduma ya kawaida ya kazi, na karibu 465,000 katika hifadhi, kulingana na Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati (IISS).
Madhehebu na dini mbalimbali hutumika katika jeshi la Israeli, ikiwa ni pamoja na, pamoja na Wayahudi, Wakristo, Waislamu wa Bedouin, na Druze, ambao wote wana uraia wa Israeli.
"Mayahudi ndio walio wengi"
Huduma ya kijeshi ni ya lazima kwa wanaume na wanawake wa Kiyahudi ambao wamefikia umri wa miaka 18. Wanaume hutumikia miezi 32, na wanawake hutumikia miezi 24. Yeyote anayekataa utumishi wa kijeshi atawajibika kisheria na anaweza kufungwa gerezani mara kwa mara, kabla ya kuachiliwa na Bodi ya Wanajeshi wa Akili.
Mwishoni mwa muda wa utumishi wa lazima, askari huachiliwa, isipokuwa wale wanaotaka kuchukua kazi ya kudumu katika jeshi, ambapo huteuliwa kwa vikosi vya kawaida. Ama wale walioachiliwa, wanaunda kiini cha jeshi la akiba katika Israeli. Askari wa akiba huitwa kila mwaka kwa kipindi maalum cha kupata mafunzo ya kijeshi ili kudumisha utayari wao.
Idadi kubwa katika jeshi ni Wayahudi, kwani idadi ya Wayahudi nchini Israeli ni watu milioni 7.145 kati ya watu milioni 9.727, kulingana na Ofisi Kuu ya Takwimu ya Israeli kwa mwaka wa 2023.
Wale wanaotumikia jeshi ni "Wayahudi wa kidini, na wa jadi," wakati Wayahudi wa Kiorthodoksi (Haredim) hawaruhusiwi kutoka kwa utumishi wa kijeshi ndani ya mfumo wa makubaliano ya kisiasa ya tangu kuanzishwa kwa serikali, ambapo wanajitolea muda wote kwa masomo ya kidini.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa miaka mingi, suala la kuwasamehe Haredim limeibua mjadala wa kisiasa unaoendelea katika duru za Israel, na mwezi Februari, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Galant, alitangaza kuwepo kwa pendekezo jipya la rasimu ya sheria ambayo ingemaliza kuachiliwa kwao kutoka kwa jeshi, kwa kuzingatia vita vinavyoendelea huko Gaza.
Kiongozi wa upinzani wa Israel Yair Lapid alisema kuwa jeshi linahitaji kuajiri Haredim, wakati vita huko Gaza vikiingia mwezi wake wa sita. Aliongeza, "Sote tunabeba mzigo sawa, na wale ambao hawataajiriwa hawatapokea pesa kutoka kwa serikali."
Mnamo tarehe kumi na nane mwezi wa Machi, mamia ya Waharedi walifanya maandamano huko Jerusalemu, wakikataa kujiunga na jeshi, wakiimba kauli mbiu zikiwemo, "Tunakufa na hatujiandikishi jeshini."
Msamaha wa Haredim kutoka katika utumishi wa kijeshi unatakiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu wa Machi, kwani Mahakama ya Juu zaidi iliipa serikali ya Israel hadi tarehe 31 mwezi huu, ili kufikia makubaliano kuhusu kuajiri na wajibu wao katika utumishi wa kijeshi.
Kulingana na jeshi la Israel, takriban vijana 66,000 wa Haredi walipata msamaha wa kujiunga na jeshi katika mwaka uliopita, ambayo ni rekodi ya muda wote.
Kulingana na Taasisi ya Demokrasia ya Israeli, idadi ya watu wa Haredi nchini Israeli ni takriban 1,335,000, au asilimia 13.6 ya jumla ya watu wote.

Chanzo cha picha, Getty
Katika miaka ya mapema ya Israeli, jeshi na serikali ilitawaliwa zaidi na watu wa kidini na wa mrengo wa kushoto, kwani ilikuwa kawaida kuweka dini nje ya majukumu ya kijeshi.
Lakini miongo ya hivi karibuni, kwa mujibu wa ripoti ya Reuters mwaka 2016, imeshuhudia kuongezeka kwa "Uzayuni wa kidini," na hii imesababisha ongezeko kubwa la idadi ya maafisa wa kidini wa Kizayuni.

Chanzo cha picha, Reuters
Uraia wa nchi mbili
Chini ya sheria za Israeli, raia wa Israeli ambao wana uraia wa nchi mbili na wanaoishi kwa kudumu nje ya nchi pia wanatakiwa kufanya kazi ya kijeshi nchini Israeli.
Pamoja na kuzuka kwa vita na Hamas kufuatia shambulio la Oktoba 7, jeshi la Israel liliita mamia ya maelfu ya wanajeshi wa akiba, wakiwemo wale wanaoishi nje ya nchi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wasiohudumu katika jeshi
Wanawake wanaweza kuachiliwa kutoka kwa utumishi wa kijeshi kwa sababu kadhaa, kama vile ndoa, ujauzito, uzazi, au sababu za kidini. Wanaume vijana wa Israeli ambao wana matatizo ya matibabu au kisaikolojia wanaweza pia kuachiliwa kutoka kwa huduma baada ya kuchunguzwa.
Waarabu ambao wenye uraia wa Israeli
Waarabu wenye uraia wa Israeli wanajumuisha takriban asilimia 21 ya wakazi wa Israeli, na wanaishi katika maeneo ya Negev, Triangle, na kaskazini mwa Israeli.
Israel inalazimisha uandikishaji wa lazima kwa wanaume wa Druze na Circassian, na Waarabu wengine wote ambao wana uraia wa Israeli hawajumuishwi katika utumishi wa lazima wa kijeshi, lakini baadhi yao wanachagua kwa hiari kujiunga na jeshi.
Druze
Israel imelazimisha kuajiriwa kwa vijana wa Druze tangu 1956, kama sehemu ya kile kinachojulikana kama "Mkataba wa Damu," wakati viongozi wa madhehebu waliahidi uaminifu kwa Taifa la Israeli na kutumika katika jeshi badala ya kuimarisha hali yao ya kijamii na kiuchumi. .
Kikosi cha Druze, au kile kinachojulikana kama kikosi cha "Harif" au "Upanga", kilianzishwa mnamo 1974, ambacho kwa kawaida kilikuwa kikifanya kazi kwenye mpaka na Lebanoni, na Druze walikuwa wengi sana ndani yake, pamoja na askari wa Kiyahudi. Mnamo mwaka wa 2015, Mkuu wa Wafanyikazi wa Israeli, Gadi Eisenkot, aliamua kuvunja kikosi hicho kutokana na hamu ya Druze kujiunga na vitengo mbali mbali vya jeshi.
Leo, Druze wanahudumu katika vitengo vyote vya jeshi, ikijumuisha vitengo vya mapigano na miundo ya kiteknolojia na kijasusi, na wanatofautishwa na ujuzi wao wa lugha ya Kiarabu na utamaduni wa jamii ya Waarabu.
Kulingana na makadirio ya Israeli, zaidi ya asilimia 80 ya jamii ya Druze wanahudumu katika jeshi, wengi wao katika vitengo vya mapigano.

Chanzo cha picha, Getty Images
Idadi ya Druze ni takriban watu 150,000, wanaowakilisha chini ya asilimia mbili ya jumla ya raia wa Israeli na karibu asilimia nane ya wakazi wa Kiarabu, kutoka katika mikoa mingi, hasa katika Galilaya, Karmeli, na Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu.
Licha ya kuandikishwa kwa lazima, mavuguvugu kadhaa ya kupinga kuajiriwa kwa lazima katika jeshi yamekuwa yakielimisha jamii ya Druze katika miongo kadhaa iliyopita, ya kwanza ikiwa ni "Kamati ya Mpango wa Druze Arab," ambayo ilianzishwa mnamo 1970.
Mwandishi na mkuu wa kamati ya Druze Arab Initiative Committee, Ghaleb Seif, anakanusha asilimia zilizotangazwa rasmi za vijana wa Druze kujiunga na jeshi, na kusema katika mahojiano yake na BBC, “Asilimia ya waajiri wa Druze Arab katika idara zote za usalama za Israel ni asilimia nane tu.”
Katika hotuba yake, Ghaleb Seif pia anarejelea utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Haifa mwaka 2017, ambao unasema kuwa asilimia 65 ya Waisraeli wa Druze wanakataa utumishi wa kijeshi.
Rai awa Druze ambaye anakataa utumishi wa kijeshi anakabiliwa na kifungo na kunyimwa ajira na baadhi ya mamlaka, jambo ambalo linaongeza shinikizo la kiuchumi kwa vijana wanaokataa kujiunga na jeshi, kulingana na Ghaleb Seif.
Mkuu wa Kamati ya Mpango wa Waarabu ya Druze, ambaye hapo awali alihudumu katika jeshi la Israel na baadaye akajiondoa, anaamini kwamba kuandikishwa kijeshi kwa lazima “hakukuleta usawa na haki kwa wanachama wa dhehebu hilo.”
Kwa upande wa jamii ya Druze katika Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu, mtazamo ni tofauti kabisa, kwani Druze wa Golan wanashikilia utambulisho wao wa taifa la Waarabu wa Syria na kususia utumishi wa kijeshi, na pia wanakataa uraia wa Israeli.
Circassian
Huduma ya kijeshi iliwekwa kwa wachache wa Circassian mnamo 1958, na ni wanaume pekee wanaohudumu katika vitengo vyote vya jeshi.
Idadi ya Waislamu wa Circassians katika Israeli ni takriban watu 5,000, na wanaishi katika vijiji viwili kaskazini mwa Israeli, cha kwanza ni kijiji cha "Kafr Kama" mashariki mwa Ziwa Tiberias na cha pili ni "Al-Rayhaniyah" karibu na mpaka wa Syria.

Wabedui
Ingawa sheria haiwalazimishi Waarabu wa Bedouin kutumikia jeshini, baadhi yao walichagua kujiunga na jeshi ili kubadilishana na marupurupu kadhaa.
Data za jeshi la Israel, zilizochapishwa na Jerusalem Post, zinaonyesha ongezeko kubwa la idadi ya Waislamu walioandikishwa, wengi wao wakiwa ni Wabedui.
Kulingana na gazeti hilo, "Waislamu wapatao 606 walijiunga na jeshi mnamo 2020, ikilinganishwa na 489 mnamo 2019 na 436 tu mnamo 2018." Sababu ya ongezeko hili ni kutokana na kampeni kubwa za kuajiri zinazoongozwa na jeshi, zenye lengo la "kuajiri vijana zaidi wa Kiarabu."
Katika ripoti nyingine kutoka gazeti hilohilo, Wabedui 1,500 hivi wanatumika katika jeshi. Wakati wa vita vya hivi majuzi kati ya Israel na Hamas, mauaji ya mwanajeshi wa Bedouin Ahmed Abu Latif kwa mara nyingine tena yalitoa mwanga juu ya nia ya baadhi ya Wabedui kujiunga na jeshi la Israel.
Mtafiti na mkulima wa utamaduni (kama anavyopenda kujijua), Kayed Abu Latif, kaka wa askari Ahmed, alisema wakati wa mahojiano na BBC kwamba "si ajabu kwa jamii ya Bedouin kuwa ndani ya mazingira ya kijeshi nchini humo, ambapo kuna ushirikiano katika hatima na siku zijazo." .
Abu Latif anaeleza kwamba miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa ongezeko la watu wa Kibedui wanaojiunga na jeshi, na sababu hiyo ni kutokana na “matatizo ya kiuchumi na ubaguzi dhidi ya wanachama wa Waarabu walio wachache.”
Aliongeza kwa BBC kwamba "asili ya kijeshi ya vijana inahakikisha kwamba wanapata mahitaji ya msingi ya maisha, kama vile nyumba, kazi, na fursa za elimu zisizo na kikomo." Inaweza kupatikana bila huduma ya kijeshi.
Abu Latif analaumu "viongozi wa Kiarabu ndani ya Israeli, ambao hawakutafuta kuboresha hali ya maisha ya vijana wa Kiarabu.
Wabedui wamegawanywa kati ya Israeli ya kaskazini huko Galilaya na kusini mwa nchi hiyo katika Jangwa la Negev, linalokaliwa na watu wapatao 300,000, na asilimia kubwa yao wanaishi katika umaskini uliokithiri katika vijiji visivyotambulika ambavyo havina miundombinu, umeme, maji, shule, na vyombo vya usafiri.
Mnamo 1987, "Kikosi cha Bedouin" au "Kikosi cha Upelelezi wa Jangwa" kilianzishwa, ambacho ni kitengo cha watoto wachanga kilichoundwa kimsingi na askari wa Bedouin, na baada ya muda kilijumuisha vikundi vingine.
Wanajeshi wengi wa Bedui wanatoka kaskazini mwa Israeli, na wengine wanaamini kwamba kuenea kwa "harakati za Kiislamu" huko Negev kulisababisha kuwashawishi Wabedui walio wengi huko wasitumikie, wakati wengine wanaamini kwamba ubaguzi unaoendelea dhidi ya Wabedui wa Negev, hata kama kutumikia, ndio sababu ya kutokutumikia.
Mtazamo wa kijamii wa waajiri wa Kiarabu katika jeshi la Israeli
Baadhi ya askari wa Kiarabu wanakabiliwa na pingamizi kutoka kwa jamii zao kutumikia jeshi, na wengine wanawashutumu kwa "uhaini."
Miaka ya nyuma, Harakati ya Kiislamu ya Kaskazini mwa Israel inayoongozwa na Sheikh Raed Salah ilitoa fatwa ya kuwakataza Waislamu kutumikia jeshi la Israel, na atakayefanya hivyo na kuuawa katika vita, ni haramu kumuombea dua katika misikiti ya harakati hiyo.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












