Sababu za Waarabu kushindwa katika vita vya kwanza na Israel

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Tarehe 29 Novemba mwaka 1947. Wayahudi wanaoishi Palestina waliketi mbele ya redio – kusikiliza kura juu ya pendekezo muhimu katika Umoja wa Mataifa kuhusu eneo la Palestina.
Kura hiyo ilikuwa kuhusu pendekezo la kuigawanya Palestina na kuunda eneo kwa ajili ya Wayahudi. Waliposikia azimio hilo limepitishwa na Umoja wa Mataifa, kulikuwa na furaha kubwa katika maeneo ya Wayahudi.
Katika kitabu cha 'A History of the First Arab-Israel War', mwanahistoria wa Israel Benny Morris, anasema: ‘Sio mbali na pale Wayahudi walipokuwa wanashangilia, vijiji vya Waarabu vilijawa na kiza na kukata tamaa. Walikuwa na wasiwasi juu ya azimio hilo.’
Kuunda historia mpya

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kuanzia mwaka 1947 hadi 1949, majeshi yanayounga mkono Wazayuni yalishambulia miji na vijiji vya Palestina.
Zaidi ya vijiji 500,000 viliharibiwa na Wayahudi na Wapalestina 15,000 waliuawa. Baadhi yake yalikuwa kama mauaji ya kimbari.
Mauaji makubwa zaidi yalifanywa katika eneo la Deir Yassin Aprili 9, 1948. Wanamgambo wa Kizayuni walishiriki katika mauaji hayo.
Takriban wanawake na watoto 107 waliuawa huko. Deir Yassin lilikuwa eneo la Jerusalem Magharibi ya leo.
Katika kipindi hiki mazingira ya kisiasa ya Mashariki ya Kati yalibadilika. Palestina ilitoweka na taifa jipya la Israel lilizaliwa.
Pendekezo la Umoja wa Mataifa

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Palestina ilikuwa chini ya udhibiti wa Waingereza baada ya Dola la Ottman kuondolewa madarakani katika Vita vya Kwanza vya Dunia.
Tangu wakati huo, Waarabu na Wayahudi walikuwa katika migogoro. Ndiposa, Umoja wa Mataifa ulipendekeza kuigawanya Palestina katika sehemu mbili na kuanzisha mataifa mawili.
Novemba 29, 1947, pendekezo la kugawanya Palestina inayodhibitiwa na Waingereza lilikubaliwa katika Umoja wa Mataifa.
Huku kukiwa na pendekezo la kuiweka Jerusalem kama eneo la kimataifa chini ya Umoja wa Mataifa.
Nchi 33 zilipiga kura kuunga mkono pendekezo hili. Nchi 13 zilipiga kura kupinga pendekezo hilo na nchi 10 hazikupiga kura.
Azimio hilo lilipitishwa ingawa nchi za Kiarabu zilitoka nje ya kikao hicho kupinga azimio hilo.
Mwanzoni wa mzozo

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Migogoro kati ya Wapalestina na Wayahudi ilianza mara tu baada ya azimio hilo kupitishwa katika Umoja wa Mataifa.
Waarabu hawakuweza kulikubali tamko hili kwa njia yoyote ile. Kwa sababu, eneo lao linachukuliwa na serikali tofauti inawekwa kwa ajili ya Wayahudi.
Vita vya kwanza ya Waarabu na Israel vililipuka. Kwa Waisraeli ilikuwa ni kupigania uhuru na kwa Wapalestina ilikuwa siku ya maafa.
Vita vya Kwanza vya Waarabu na Israel vilikuwa na awamu mbili. Hatua ya kwanza ilikuwa mzozo kati ya Wayahudi na Wapalestina. Na katika hatua ya pili, nchi za Kiarabu ziliingia vitani dhidi ya Israel.
Ndani ya miezi sita baada ya kupitishwa kwa azimio hilo katika Umoja wa Mataifa, Mei 14, 1948, waziri mkuu mwanzilishi wa Israel, David Ben-Gurion, alizindua taifa huru kwa ajili ya Wayahudi.
Mzozo kati ya Wapalestina na Wayahudi. Makundi ya Kiyahudi yenye silaha yaliwashambulia Wapalestina katika maeneo mbalimbali.
Makundi yenye silaha ya Kizayuni yalifanya mauaji makubwa ya Wapalestina. Mashirika ya Kiyahudi yenye msimamo mkali yalianzishwa.
Kutokana na hali hiyo, Wapalestina wengi walikimbia makazi yao. Kwa upande mwingine, Wayahudi wengi zaidi na zaidi walikuja katika maeneo haya.
Ushiriki wa nchi za Kiarabu

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Baada ya kutangazwa kwa serikali ya Israel, mzozo huo uligeuka kuwa vita kamili vya kijeshi.
Vita vya Waarabu na Waisraeli vilianza baada ya kuanzishwa kwa Taifa la Israel. Siku hiyo bado inaadhimishwa na Wapalestina kama 'Nakba' au Siku ya Maafa. Mataifa matano ya Kiarabu yaliishambulia Israel kwa wakati mmoja.
Katika maeneo ambayo maeneo ya Israel yalitangazwa, Waarabu wengi walifukuzwa na majeshi ya Israel, au walikimbia.
Wapalestina milioni saba na nusu wakawa wakimbizi wakati wa vita vya Waarabu na Israel vya 1948-1949.
Israel ilipojitangaza kuwa taifa, majeshi ya Waarabu kutoka Misri, Jordan, Syria, Lebanon na Iraq yalisonga mbele kuelekea Palestina. Wanajeshi wa Kiarabu walianza kushambulia.
Ndani ya wiki waliyazingira majeshi ya Israel. Wanajeshi wa Israel walikabiliwa na uwezekano wa kushindwa.
Ndipo Umoja wa Mataifa ulipoingilia kati na vita vikasitishwa kwa wiki nne. Usitishaji vita kwa kweli uliinufaisha Israel.
Mivutano miongoni mwa Waarabu

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kwa kukiuka masharti ya uwekaji silaha chini, Israel iliingiza silaha nzito kutoka iliyokuwa Czechoslovakia. Wakati wa majuma haya manne Israel iliongeza nguvu na ikabadilisha mwenendo wa vita.
Mara tu baada ya kumalizika kwa usitishaji mapigano, Israel ilianzisha mashambulizi na kuyateka maeneo mawili yanayoshikiliwa na Waarabu.
Takriban Wapalestina 70,000 walilazimika kuondoka katika maeneo hayo. Kwa upande mwingine, Israel iliikalia kwa mabavu ardhi iliyogawiwa kwa Wapalestina.
Mwanahistoria wa Uingereza na Israel mzaliwa wa Iraq, Avi Shlaim anabainisha, jeshi la Waarabu lilipata ufanisi wakati wa vita vya mapema, lakini hawakupata ufanisi wakati Israel ilipoanzisha mashambulizi mapya.
Hakukuwa na ushirikiano wa kutosha kati ya majeshi ya nchi za Kiarabu. Nchi za Kiarabu zilizoshiriki katika vita hivyo ziliongozwa na jenerali wa Iraq.
Lakini hakuwa na udhibiti juu ya askari wa nchi nyingine. Mbali na hilo, operesheni za kijeshi za nchi za Kiarabu hazikwenda kulingana na mipango yao.
Nchi za Kiarabu zikiongozwa na Misri zilianzisha serikali ya Palestina huko Gaza. Mfalme Farouk wa Misri wa wakati huo aliongoza mpango huo kama suala la kimkakati kwa nchi yake.
Kwa upande mwingine, Mfalme Abdullah wa Jordan alitaka kuichukua sehemu ya Wapalestina ili kupanua zaidi mipaka ya Jordan.
Mfalme Farouk alitaka Mfalme Abdullah wa Jordan asichukue Palestina kama sehemu ya Jordan.
Israel, wakati huo huo, ilikuwa ikifuatilia mzozo kati ya mataifa ya Kiarabu na wakati huo huo kuimarisha msimamo wake.
Waarabu wazidi kushindwa
Israel ilililazimisha jeshi la Misri kurudi nyuma kupitia mashambulizi ya anga. Avi Shlam anasema Misri iliomba msaada, lakini nchi nyingine za Kiarabu hazikuisaidia.
Lebanon, Saudi Arabia na Yemen ziliahidi kutoa msaada lakini hazikufanya hivyo. Vikosi vya Iraq, vikisaidiwa na washirika, vilikuwa vinashambulia kwa mabomu vijiji kadhaa vya Israel.
"Nchi za Kiarabu ama ziliogopa kuingilia kati, au hazikuwa na nia," anaandika Avi Shlam.
Mwishoni mwa mwaka Wamisri walishindwa huko Gaza. Matokeo yake, ndoto ya kuwa na taifa la Palestina iliisha.
Hatimaye Misri ilizungumza na Uingereza ili kulinda mipaka yake. Ndiposa, Israel ilitia saini mikataba kadhaa na Misri na nchi zingine kadhaa za Kiarabu 1949.
Mikataba hiyo ilimaliza Vita vya Kwanza vya Waarabu na Israel. Wapalestina laki saba walitimuliwa katika vita hivyo.
Baada ya vita vya kwanza vya Waarabu na Israel, Waarabu walipoteza imani kwa watawala wao. Waarabu hawakuwa tayari kabisa kukubali kuwa wameshindwa.
Ndani ya miaka mitatu ya vita hivyo, mawaziri wakuu wa wakati huo wa Misri na Lebanon na mfalme wa wakati huo wa Jordan waliuawa.
Isitoshe, jeshi lilimpindua rais wa wakati huo wa Syria na mfalme wa Misri wa wakati huo.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












