Rafah: Hifadhi ya Wapalestina ambayo Israel inatishia kuivamia kwa mashambulizi ya ardhini

Chanzo cha picha, Reuters
Kutakuwa na hali mbaya katika mji wa kusini wa Gaza wa Rafah ikiwa Israel itafanya operesheni kubwa ya kijeshi huko, Umoja wa Mataifa (UN) umeonya.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameliagiza jeshi kujiandaa kuwaondoa raia kutoka Rafah kabla ya kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya Hamas.
Israel ilifanya mashambulizi ya anga katika mji huo usiku wa kuamkia Februari 11, ambapo watu 67 waliuawa kwa mujibu wa wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas. Israel imesema kuwa " wimbi la mashambulizi" litaandamana na uvamizi, ambao unalenga kuwaalilia huru mateka wawili.
Israel inadai kuwa Rafah ni ngome ya mwisho iliyobaki kwa wapiganaji wa Hamas, lakini Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya nusu ya wakazi wa Gaza wamekimbilia huko na ndio kitovu muhimu cha operesheni za misaada.
Huku wengi katika jamii ya kimataifa wakitahadharidha kuhusu mashambulizi ya Rafah, tunaangalia mji huu, watu wanaohifadhiwa huko na historia yake.
Mji wa Rafah uko wapi?

Rafah ni mji wa kusini zaidi katika Gaza. Mkoa wa Rafah unapakana na Misri na Israel - mji wenyewe uko kwenye mpaka wa Gaza na Misri.
Kwa sasa idadi ya Wapalestina inakadiriwa kuwa milioni 1.5, idadi hiyo ikiwa ni mara tano zaidi ya ilivyokuwa kabla ya mashambulizi ya Israel katika ukanda huo kuanza.
Eneo la Rafah lina takriban kilomita za mraba 60, takriban ukubwa wa eneo la Manhattan mjini New York.
Mpaka pekee kati ya Ukanda wa Gaza na Misri uko Rafah, na umekuwa ukitumika kwa miongo kadhaa kwa ajili ya kupata misaada katika Ukanda wa Gaza. Kabla ya vita, mamia ya malori yalitumia njia hii kuingia katika Ukanda wa Gaza kila siku.
Katika siku za nyuma, kulikuwa na mahandaki kadhaa ya magendo chini ya mpaka, ambayo yalitumika kuzunguka kizuizi cha Israeli na Misri ambacho kilizuia mtiririko wa bidhaa kwenda Gaza. Hii iliifanya Rafah kuwa eneo muhimu katika masuala ya biashara na uchumi.
Haijulikani ni mahandaki mangapi yaliyosalia, ingawa jeshi la Misri linasema limemaliza magendo na kuharibu mahandaki hayo katika miaka ya hivi karibuni.
Historia ya Rafah

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Rafah ni moja ya miji ya kale ya kihistoria ya Gaza na ulitekwa na Farao, Waasiria, Wagiriki, na Warumi.
Ulikuwa chini ya utawala wa Uingereza kuanzia mwaka 1917 hadi 1948, wakati taifa la Israeli lilipotangazwa.
Vita na mataifa ya Kiarabu vilifuata, na wakati mapigano yalipomalizika, Rafah, pamoja na maeneo mengine ya Ukanda wa Gaza, yalidhibitiwa na Misri.
Kisha, katika vita vya 1967 - vinavyojulikana kama Vita vya Siku Sita - Israeli ilichukua udhibiti wa mji huo kama ilivyochukua rasi ya Gaza na Misri ya Sinai, pamoja na Ukingo wa Magharibi, milima ya Golan na Jerusalem Mashariki.
Mwaka 1979, Misri na Israel zilikubaliana mkataba wa amani, ambapo Sinai ilirudishwa kwa Misri. Rafah iligawika, na sehemu ya Misri na sehemu katika Gaza inayokaliwa na Israeli. Mpaka wa waya ulipita mjini, ukitenganisha familia.
Kama sehemu nyingine kadhaa za Gaza, Rafah ni makazi ya maelfu ya wakimbizi wa Kipalestina ambao walikimbia au kulazimishwa kutoka kwenye nyumba zao wakati wa vita vya 1948, na vizazi vyao.
Hali ikoje kwa sasa?

Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya nusu ya idadi ya watu wa Gaza wanakimbilia Rafah, huku Martin Griffiths, mratibu wa misaada wa Umoja wa Mataifa akielezea hali ya maisha kuwa mbaya.
"Wanakosa mahitaji ya msingi ya kuishi, kuandamwa na njaa, magonjwa na kifo," alisema.
Watu waliohamishwa wanaishi mitaani, katika shule na mahema. Uchambuzi wa picha za satelaiti na BBC (kama inavyoonekana hapo juu) unaonyesha ongezeko kubwa la idadi ya mahema mjini Rafah tangu vita vilipoanza.
Watu wengi hapa, kama Abu Rushdi Abu Daqin, wamekimbia mapigano kaskazini baada ya kuambiwa wahamie kusini na jeshi la Israeli.
"Tumeteseka," Abu Daqin aliiambia BBC. "Niliondoka Gaza City kwenda Hamad na kisha nikaenda Khan Younis, kutoka Khan Younis hadi Rafah. Lakini kwa muda gani?" anauliza, baada ya kusikia kuhusu tisho la Israel la mashambulizi ya ardhini.
Watu wengi waliohamishwa katika mji wa Rafah wanaiambia BBC kuwa wanapendelea kukaa katika eneo la magharibi mwa mji huo karibu na bahari ya Mediterania, kwa hofu ya kuvamiwa na "uvamizi" kutoka upande wa mashariki, karibu na mpaka na Israel.
Kuna hospitali chache tu zilizofunguliwa ikiwa ni pamoja na Hospitali Kuu ya Rafah, Hospitali Maalum ya Kuwait, na Hospitali ya Martyr Abu Youssef Al-Najjar, ambayo yote haina vifaa vya msingi vya matibabu na inakabiliana na uhaba wa umeme.
Wakati Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu akionya kuhusu mashambulizi ya ardhini mjini Rafah, licha ya kulaaniwa kimataifa, watu wengi katika mji huo wanauliza swali sawa na Abu Daqin: "Watu wote wa Gaza wako hapa. Tunaweza kwenda wapi?"
Israel inasema inataka kupunguza madhara kwa raia katika operesheni yake, ambayo ilianzishwa kujibu mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba ya Hamas ambapo watu zaidi ya 1,200 waliuawa na karibu 250 kuchukuliwa mateka.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi












