Lebanon: Mstari wa Buluu katikati ya mapambano ya Hezbollah na Israel

- Author, Nafiseh Kohnavard
- Nafasi, BBC
"Ukisikia king'ora kinalia, unapaswa kukimbilia kwenye handaki lililokaribu," anasema Kapteni Aódhan McGuinness tulipowasili katika kambi ya Shamrock.
McGuinness ni kapteni wa operesheni za wanajeshi wa Ireland katika kambi hii ya kulinda amani cha Umoja wa Mataifa (UN) karibu na mpaka wa Israel na Lebanon.
"Tunaweza kusikia sauti ya ndege zisizo na rubani za Israel. Kwa sasa zinapaa kila wakati, mchana na usiku, katika miji na vijiji vya kusini mwa Lebanon."
Wakati maelezo hayo yakiendelea, mlipuko mkubwa unasikika si mbali. Mlipuko huo ni ishara nyingine ya kuongezeka kwa mvutano katika eneo hili tangu kuanza kwa mzozo kati ya Israel na Hamas.
Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, unaojulikana kwa jina la UNIFIL, una jukumu la kulinda mstari wa buluu, mpaka usio rasmi kati ya Lebanon na Israel.
Katika kipindi cha miongo minne iliyopita, eneo hilo limekuwa la mapigano ya hapa na pale kati ya Hezbollah, kundi la Waislamu wa madhehebu ya Shia huko Lebanon na jeshi la Israel.
Hezbollah inatambuliwa kuwa shirika la kigaidi na Marekani, Uingereza na nchi nyingine za Ulaya, lakini nchini Lebanon ni chama cha kisiasa - kinachoongoza upinzani uliokaribia kushinda wingi wa viti katika uchaguzi wa kitaifa wa mwaka jana.
Katikati ya Mapigano

Tukiwa tumevaa vizibao na helmeti, tulijiunga na kikundi cha walinda amani wenye silaha nzito katika msafara wa magari ya kivita kwa safari ya dakika 20 hadi kituo kingine kilicho umbali wa mita 500 kutoka mstari wa buluu.
Kamanda wa kituo hicho, Luteni Dylan Cadogan, anasema mara nyingi wanalazimika kujificha kwenye mahandaki wakati wa mashambulizi, wakati mwingine kwa masaa.
"Tuliona nyumba zikiharibiwa na raia walionaswa katikati ya mapigano ambao wanahitaji msaada wetu," anasema Cadogan.
Tukiwa katika mnara wa kambi hiyo, Luteni Cadogan anatuonyesha nyumba iliyo mbali kidogo.
"Katika nyumba ile, ni umbali wa mita 200 tu, kulikuwa na mama na mtoto. Nyumba yao ililipuliwa na ikabidi wakimbilie hapa kutafuta hifadhi. Tuliwapa msaada wa matibabu na kisha kuwapeleka mahali salama."
Wanajeshi wa UNIFIL wamepata miili ya waliouawa katika mapigano yanayoendelea, lakini hawawezi kusema kati yao ni wanamgambo wangapi wa Hezbollah kutokana na unyeti wa kazi yao na haja ya kutoegemea upande wowote kati ya pande zinazopigana.
"Sio kazi yetu kutoa maoni. Tunachunguza tu, kufuatilia na kuripoti kile tunachokiona," anasema Cadogan.
Misheni ya miongo mingi

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi yake Gaza kufuatia mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba, Hezbollah imekuwa ikifanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora kutoka kusini mwa Lebanon.
Vikosi vya Israel vinajibu kwa mashambulizi makali ya angani na makombora. Kutokana na mapigano hayo, watu 60,000 yameyakimbia makazi yao kutoka eneo la mpakani upande wa Lebanon.
Makundi ya ufuatiliaji yanasema, wiki ya kwanza baada ya shambulio la Hamas mwezi Oktoba, takribani mashambulizi 70 yaliripotiwa karibu na mstari wa buluu. Kufikia katikati ya Novemba, idadi hiyo iliongezeka na kufikia mashambulizi 250 kwa wiki.
Kikosi cha kulinda amani cha Ireland kilitumwa kwa mara ya kwanza mwaka 1978 baada ya Israel kuvamia kusini mwa Lebanon kujibu mashambulizi ya Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO) kwenye mpaka.
Tangu wakati huo, wanajeshi 48 wa Ireland wameuawa. Hilo linawatia wasiwasi jamaa za wanajeshi hao.
Kapteni Tony Smith, 27, yuko kwenye misheni yake ya pili, anasema, “mama yangu anataka nirudi nyumbani, nitarudi kwa wakati ufaao, lakini anajua kwa nini niko hapa. Licha ya wasiwasi wake, anaunga mkono ninachofanya.”
Ali na Mke Wake

Tunapoukaribia mji wa Tibnine, mabango yenye picha ya kiongozi wa Hezbollah, Sheikh Hassan Nasrallah na wapiganaji wa kundi hilo yanaonekana barabarani.
Ni kilomita 10 kutoka mstari wa buluu na mji huo uliharibiwa vibaya katika migogoro ya hapo awali. Kama ilivyo katika miji mingi ya kusini mwa Lebanon, Hezbollah ina ushawishi mkubwa na inadhibiti usalama katika maeneo haya.
Mmoja wa wakazi wa mji huu ni, Ali Saad, 57 anayefanya kazi kama mtafsiri wa UNIFIL.

Chanzo cha picha, THE SAAD FAMILY.
Ali anawashukuru wanajeshi wa Ireland kwa kuokoa maisha yake walipomchukua kutoka shuleni na kumpeleka kwenye moja ya mahandaki yao wakati wa shambulio la anga akiwa mdogo.
Tangu wakati huo, amekuwa karibu na vikosi hivyo na kundi la askari wa Ireland walihudhuria harusi yake na mke wake, Bassima, ambaye pia husaidia walinda amani katika huduma za lugha.
Ali anashukuru uwepo wa wanajeshi hao lakini anasikitika kwamba mzozo bado unaendelea kwa muda mrefu.
"Kusema ukweli, hatukufikiria kamwe misheni hii ingedumu kwa zaidi ya miaka 44," anasema.
Hofu Yazidi

Kwa Bassima, mapigano ya sasa yanampa kumbukumbu chungu juu ya migogoro ya hapo awali, kama vile vita kati ya Israel na Hezbollah mwaka 2006.
Bassima anaamini kuishi katika migogoro kumeleta madhara kwa mtoto wake, ambaye sasa ana umri wa miaka 23. Huwa na wasiwasi wakati helikopta za UNIFIL zinaporuka karibu na nyumba yao.
Kamanda wa UNIFIL Luteni Kanali, Cathal Keohane ana wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa kiwango cha vurugu katika eneo hilo.
"Tumeshuhudia kukuwa na kuongezeka kwa mashambulizi ndani ya Lebanon, tumeona matumizi ya silaha mbali mbali," anasema, akihofia kuwa hali itazidi kuwa mbaya.
Anatumai kusitishwa kwa mapigano Gaza kutapelekea kupungua kwa mvutano katika eneo la mstari wa buluu.
Lakini anaamini inaweza kuchukua muda kwa watu waliokimbia makazi yao kurejea nyumbani, hata kama mapigano ya mpakani yatasitishwa.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












