Kwa nini usitishaji vita huko Gaza umefikia kikomo?

Chanzo cha picha, EPA
Mapigano yalianza tena kati ya Israel na Hamas siku ya Ijumaa asubuhi, na kuhitimisha usitishaji mapigano wa siku saba kati ya pande hizo mbili ambazo zilishuhudia mateka na wafungwa wakiachiliwa huru na usaidizi unaohitajika sana wa kibinadamu kufikia Ukanda wa Gaza.
Hapa kuna baadhi ya maswali muhimu kuhusu maendeleo ya hivi karibuni.
Kwa nini mpango wa kusitisha mapigano ulikoma?
Saa moja kabla ya usitishwaji wa mapigano kukamilika saa 07:00 kwa saa za huko (05:00 GMT), Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) liliripoti kuwa ving'ora vilikuwa vikisikika kwenye maeneo ya jamii zilizo karibu na Ukanda wa Gaza, kisha wakasema kuwa wamenasa roketi.
Saa moja baadaye, jeshi la Israel lilisema mapigano yalianza tena, na kuwashutumu Hamas kwa kukiuka masharti ya makubaliano.
IDF kisha ilisema ndege zake za kivita zilikuwa zikishambulia maeneo ya Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Muda mfupi baadaye, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema Hamas "haijatimiza wajibu wake wa kuwaachilia mateka wanawake wote leo na imerusha makombora kwa raia wa Israel".
Hata hivyo, Hamas ililaumu Israel kwa kuanzisha tena mapigano, ikisema ilikataa "kukubali matoleo yote ya kuwaachilia mateka wengine".
"Uvamizi huo ulikuwa uamuzi wa awali wa kuanzisha tena mashambulizi," ilisema katika taarifa yake, ikimlaumu Rais wa Marekani Joe Biden kwa "kuendeleza uhalifu wa kivita wa Wazayuni katika Ukanda wa Gaza" na "kutoa uungwaji mkono kwa Israel".
Katika muda wote wa usitishaji mapigano wa wiki nzima, Bw Netanyahu amekuwa chini ya shinikizo, hasa kutoka kwa watetezi wa mrengo wa kulia katika serikali yake, kuanzisha upya vita, jambo ambalo Israel imekuwa ikiweka wazi kuwa inakusudia kufanya mara tu makubaliano hayo yatakapokamilika.
Licha ya hayo, bado kuna matumaini kuwa makubaliano mapya yanaweza kufikiwa. Qatar, ambayo imekuwa na jukumu muhimu hadi sasa katika mazungumzo ya kusitisha mapigano, ilithibitisha Ijumaa kwamba mazungumzo yalikuwa yanaendelea "kwa lengo la kurejea kwa usitishaji mapigano".
Je, hali ikoje huko Gaza?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ndani ya saa saba baada ya mapigano kuanza tena, wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas imesema zaidi ya watu 60 wameuawa, na kuongeza kuwa karibu Wapalestina 15,000 waliuawa kabla ya kusitishwa kwa mapigano.
James Elder kutoka Unicef, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, alizungumza na BBC kutoka hospitali ya kusini mwa Gaza baada ya mashambulizi ya bomu kuanza, akielezea hali kuwa "ya kutisha".
Alisema ilikuwa "ya kutisha kwa watu" na kwamba "unaona hofu kwenye nyuso zao", akiongeza kuwa shambulio lilipiga karibu na kituo alichokuwemo.
Alielezea mwisho wa usitishaji mapigano kama "ndoto ambayo kila mtu aliiogopa kabisa".
Kabla ya kusitishwa kwa mapigano, Ukanda wa Gaza ulikuwa umepitia uharibifu mkubwa wakati Israeli ikifanya kampeni yake ya kulipiza kisasi kujibu mashambulizi mabaya ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba.
Israel ilidai kutumia zaidi ya mabomu na makombora 10,000, na uchambuzi wa BBC uligundua kuwa karibu majengo 98,000 huko Gaza huenda yalipata uharibifu.
Mashambulizi pia yalikwamisha misaada ya kibinadamu. Mashirika ya misaada yaliweza kutumia mpango wa kusitisha mapigano ili kupata usaidizi muhimu, lakini waliripoti kuwepo uharibifu katika maeneo mengi waliyoyafikia.
Kitakachotokea baadaye
Ingawa mazungumzo yanaendelea kwa matumaini ya makubaliano mapya kufikiwa, kwa sasa ni wazi kwamba vita vimeanza tena.
Baada ya wiki kadhaa za mapigano makali kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, hasa karibu na mji wa Gaza, jeshi la Israeli sasa linaonekana kuelekeza umakini wake kusini, ambapo mashambulio mapya ya anga yameripotiwa.
IDF pia imeunda ramani ya Gaza iliyogawanywa katika kanda zaidi ya 2,000, ambayo ilisema itatumika kusaidia watu huko Gaza kuepuka mapigano ya baadaye. Ilisema ramani imegawanywa katika maeneo ili kuwezesha watu "kuhama kutoka sehemu maalumu kwa usalama wao ikiwa inahitajika".
Siku ya Ijumaa, ndege za Israel zilidondosha vipeperushi katika maeneo ya mashariki na kaskazini mwa Khan Younis, jiji kubwa zaidi kusini mwa Gaza,
Vipeperushi hivyo havikurejelea vitalu vyovyote vilivyo na nambari, lakini ujumbe kwa Kiarabu uliwaambia wakazi katika maeneo manne yaliyotajwa, lakini ambayo hayajahesabiwa, "kuhama mara moja na kwenda kwenye makazi huko Rafah".
Mapigano hayo mapya yanakuja baada ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken kukutana na maafisa wa Israel, ambapo alisisitiza kuwa hatua inayofuata ya vita lazima kuhakikisha raia wanalindwa.
Bw.Blinken alisema ameiambia serikali ya Israel kwamba ni lazima iepuke kuondolewa zaidi kwa Wapalestina na uharibifu wa miundombinu muhimu, kama vile hospitali, vituo vya nishati na vifaa vya maji.
Ni nini kilifanyika wakati wa kusitisha mapigano?
Wakati wa kusitisha mapigano kwa siku saba, Hamas ilikubali kuwaachilia watu 110 kutoka Gaza, wakiwemo wanawake 78 wa Israel na watoto.
Kama sehemu ya makubaliano hayo, Wapalestina 240 pia waliachiliwa kutoka jela za Israel. Walikuwa wameshtakiwa kwa makosa mbalimbali, kuanzia kurusha mawe hadi uchochezi na kujaribu kuua.
Wapalestina wengi walioachiliwa hawakuwa wametiwa hatiani kwa makosa ya jinai, na walikuwa wakishikiliwa rumande wakisubiri kufunguliwa mashtaka.
Wengine walisema wamedhulumiwa na kuadhibiwa pamoja baada ya mashambulizi ya Oktoba 7. Israel inasema wafungwa wake wote wanashikiliwa kwa mujibu wa sheria.
Inakadiriwa kuwa mateka wapatao 140 wa Israel wamesalia mateka huko Gaza.















