'Waarabu na Waislamu wote wako wapi? Mumewaacha watu wa Palestina wateseke'

- Author, Adnan El-Bursh
- Nafasi, BBC Arabic
- Akiripoti kutoka, Deir al-Balah, Gaza
"Waarabu na Waislamu wote wako wapi? Wako wapi watetezi wote wa haki za binadamu? Mumewaacha watu wa Palestina wakiteseka, wakilala njaa na kuangamizwa."
Mwanamke mwenye umri wa makamo aishambulia dunia katika foleni ya gesi ya kupikia huko Gaza.
Anapiga kelele kwa hasira hewani, kukata tamaa na kuchanganyikiwa yakidhirika katika uso wake.
"Tumekuwa tukingoja kwenye foleni ili kujaza mtungi mmoja wa gesi tangu asubuhi na mapema. Nilifanya sala yangu ya asubuhi nikiwa nimesimama."

Chanzo cha picha, Hani Kali/BBC
Ananiambia amehamishwa kutoka Beit Hanoun kaskazini, kilomita 2 tu kutoka mpaka na Israeli.
"Siwezi kuelezea uharibifu. Familia nzima imefutwa kutoka kwa kumbukumbu za raia. Waliuawa chini ya nyumba zao.
"Gaza imeharibiwa kabisa. Utuhurumie."
Sasa anaishi na familia yake katika shule ya Umoja wa Mataifa katika mji wa Deir al-Balah katikati mwa Gaza.

Chanzo cha picha, Hani Kali/BBC
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baada ya Hamas kushambulia Israel tarehe 7 Oktoba, na kuua watu 1,200 na kuchukua mateka zaidi ya 200, Israel ilianza mashambulizi ya anga na kisha kufanya uvamizi wa ardhini.
Takriban Wapalestina 14,800 wameuawa kufikia sasa, kulingana na wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas.
Ukanda wa Gaza ni makazi ya watu 2.4m na Umoja wa Mataifa unasema 1.8m wamekimbia makazi yao baada ya Israeli kuwaamuru kuhamia kusini.
Kuna mamia kwenye foleni ya gesi ya kupikia. Vijana wameketi kwenye mitungi ya gesi huku wakisubiri. Hali ni ya wasiwasi. Watu wamechoka.
Tangu kusitishwa kwa mapigano tarehe 24 Novemba, hadi malori 200 ya misaada yamekuwa yakiingia Ukanda wa Gaza kwa siku, karibu nusu ya yale yaliyoingia kabla ya vita.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasema kuwa yameweza kupeleka baadhi ya misaada kaskazini ambapo jeshi la Israel lipo, lakini kuna uhaba mkubwa kila mahali.
Mwanaume mwingine kwenye foleni anakubali kuzungumza nami.
“Huwezi kukuta kikombe cha chai wala pakiti moja ya biskuti, juzi watu walikuwa wakigawana mkate wakiwa wamelala barabarani.
"Mvua tuliyoshuhudia jana na baridi tuliyopitia. Watu walilala hapa. Mungu atusaidie."

Chanzo cha picha, Hani Kali/BBC
Israel ilisitisha uwasilishaji wote wa mafuta mwanzoni mwa mzozo na kisha kuruhusu kwa kiasi kidogo, kwa sasa jumla ya lita 140,000 kila siku mbili, kulingana na afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
Serikali ya Israel inasema mafuta ya ziada yanaweza kutumiwa na Hamas, shirika la kigaidi lililopigwa marufuku katika Umoja wa Ulaya, Uingereza na Marekani.
Mohammed al-Qidrah anasubiri kwa utulivu kwenye foleni ya gesi ya kupikia.
"Tumekuwa hapa kwa siku tatu. Tulikuja hapa siku mbili zilizopita na kutoka 03:00 hadi sasa, hatujaweza kujaza mtungi wetu.
"Hatuwezi kupata mafuta, unga au kitu chochote. Unahitaji kusimama katika mstari kwa kila kitu na unahangaika kuipata."
Marekani inatuma ndege tatu za misaada nchini Misri zikiwa zimebeba vifaa vya matibabu, chakula cha msaada na bidhaa za majira ya baridi, ambazo zitasambazwa na Umoja wa Mataifa huko Gaza.

Chanzo cha picha, Reuters
Shirika la Afya Ulimwenguni linaonya kuwa watu wengi zaidi watakufa kutokana na magonjwa kuliko watakavyouawa katika shambulio la bomu ikiwa miundombinu ya afya haitarejeshwa.
Wakati huo huo, muungano wa misaada unaoongozwa na Umoja wa Mataifa unasema asilimia 60 ya majengo ya Gaza yameharibiwa .
Wakati muda wa usitishaji vita ukiendelea, kuna dalili kwamba maisha yanarejea Gaza ambako mabaki ya zao la mzeituni mwaka huu yanavunwa.
"Tunapaswa kutumia fursa hii, hakuna muda," mkulima wa Kipalestina Fathy Abu Salah ameliambia shirika la habari la Reuters. Anaishi Khan Younis kusini.
"Vita hivi vilituangamiza, hakuna uzalishaji wowote. Mavuno mengi yaliharibika," anaongeza.

Chanzo cha picha, Reuters
Ukosefu wa umeme umesababisha kutegemewa kwa mafuta kuendesha mitambo kwenye mashine ya mizeituni.
"Kutafuta mafuta ni shida ambayo kila mtu anakabiliwa nayo," anasema mkulima wa mizeituni na mfanyakazi wa vyombo vya habari Mohamed Wafy.
"Mara tu tulipopata mafuta, tuliweza kufungua mashine ya mizeituni, hata kama inafanya kazi kwa kiwango cha chini kabisa," anasema.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












